Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbogwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nichangie hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mungu Muumba wa Mbingu na Nchi kwa kuniwezesha na kupata hii nafasi adimu kabisa ya kuweza kuzungumza na Watanzania wote kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi ambazo amezifanya ndani ya mwaka huu wa tano na sisi kama Wabunge wake washauri wake tunaenda vizuri kabisa, lakini pia hata hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, inatoa taswira kwamba tunapokwenda na tunapotoka ni jambo la kumshukuru Mungu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hakika tulipotoka ni mbali, nchi yetu imepita kwenye bonde la umauti, kupotelewa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano kila mmoja tulikuwa tunatazamana kwamba tutamalizaje safari, lakini sasa hivi tunashukuru miradi inazidi kukamilika, bwawa la Mwalimu Nyerere limekamilika, lakini pia feri ya Busisi imekamilika na mambo mengine mengi lukuki siwezi kuyataja yote yamekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze sasa kwa kusema, ninatokea Mbogwe na Mbogwe tumepata neema mwaka huu Wizara ya Madini tumepata leseni nyingi, tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Madini kwa leseni alizozitoa, japokuwa kila kitu kizuri huwa kinakuwa na changamoto, taarifa ambayo hapa sasa hivi inasumbua kwenye mkoa huu wa kimadini, watu wanahitaji zile Sheria za Misitu na Sheria za Madini ziweze kulegezwa kidogo ili kusudi watu waende wakachimbe kwenye leseni zao. Kwa hiyo, kupitia hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, niiombe sana Serikali na wahusika wote kwamba waone sasa kila sababu hawa watu waliyolipia leseni huko waende wakaanze uzalishaji ili kusudi nchi yetu tuweze kupata mapato mengi na kuweza kukamilisha hii miradi mingine ambayo bado tunaihitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu bado ina uhitaji mwingi, Majimbo yetu kila Mbunge hapa ukiongea naye ukimuuliza bado mahitaji yapo ni mengi pamoja na kwamba yaliyofanywa ni mengi, lakini shida na zenyewe bado zipo nyingi majimboni. Kupitia mkoa wa kimadini wa Mbogwe nina imani tuna trilioni nyingi tunaenda kuzipata, nikiangalia upande wa barabara kila Mbunge hapa ukimuuliza barabara zake hazipo sawa, lakini pia upande wa maboma wananchi walijenga miaka mingi huko maboma bado yana uhitaji wa pesa. Kwa hiyo, niiombe sasa Wizara ya Madini kwa vile tunaona kabisa kwamba dhahabu zipo nje nje hapo Mbogwe kwetu waweze kuwasiliana na watu wa TFS ili kusudi walegeze masharti hayo yaliyopo ili dhahabu ziweze kuchimbwa na kazi ziweze kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine hapa napenda nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu. Waziri Mkuu umekuwa msaada wetu mkubwa sana Wabunge wako, tulikuwa tukipata na matatizo mbalimbali tunakufuata unatuelekeza kwamba nini cha kufanya, Mungu akubariki sana. Mwaka huu ni mwaka wa 10 Mheshimiwa Waziri Mkuu na amefanya kazi na hayati John Pombe Joseph Magufuli pia alikuwa akitusikiliza, lakini vilevile hajaonesha ubaguzi wala kinyongo chochote kwa Mama ametusikiliza, hajabadilika kwa kweli abarikiwe sana Baba Mungu ambariki sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza pia wasaidizi wake kwa maana ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Doto Mashaka Biteko pamoja na wengine ndani ya ofisi yake, Mungu awasimamie na hii hotuba yenu inatupa dira kwamba kama Wabunge nini cha kuwashauri na nini cha kufanya ili kusudi watu wetu waweze kuneemeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie masuala ya mikopo hii ya 10%, eneo hili halijakaa vizuri, naiomba ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu waweze kufanya maboresho vizuri na kwenye suala la ajira hasa walemavu wanapohitimu elimu ya juu, wapewe kipaumbele ili kusudi kuweza kuingia kwenye mifumo kuweza kulitumikia Taifa hili, kwa sababu unakutana na mwenye ulemavu amesoma vizuri, ana kila kitu na kipo safi, lakini changamoto ni ajira. Kwa hiyo niiombe Serikali hii ya Awamu ya Sita watu wenye ulemavu iwape kipaumbele ikiwemo hiyo mikopo ya 10% pale inapotoka kwenye halmashauri zetu, lakini na wao kama wao kwa vile wamesoma, ni wasomi wazuri, waweze kuajiriwa na Serikali hii ili tubaki sisi wazima sasa tupambane, wale wengine kama ajira zitakuwa bado, lakini hawa wenye ulemavu waajiriwe kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine napenda kushauri hapa kwamba mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, ninapenda kuwashauri viongozi wenzangu wa vyama vyote na wachungaji wote pamoja na mashehe, huu mwaka ni mwaka wa kuomba sana, tunahitaji tupate viongozi waaminifu kwenye Taifa letu, kitakachotutoa kwenye umaskini ni uaminifu tu, lakini ni mbaya sana pale mnapompata kiongozi asiye mwaminifu, matokeo yake tena kuja kuanza kutukanana pale tunapoanza kuzijadili ripoti za CAG.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wananchi tunaowaongoza kwenye maeneo yetu kila mmoja wetu wanatujua kwamba huyu ana tabia gani na huyu ana tabia gani, kama kuna mtu ana tabia siyo nzuri siyo mwaminifu sana katika Serikali hii ya Awamu ya Sita na tunaenda kupigiwa kura wamalizane naye huko huko wananchi ili huku tunataka warudi wale wenye nguvu ya Mungu, wenye upendo na Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu tumelia na umaskini muda mrefu, tunahitaji sasa yatosha Waislamu na Wakristo waseme kwa Jina la Yesu tunatuma viongozi ambao ni waaminifu ili kusudi tupige hatua kwenye Taifa letu. Inauma sana wapo watu wanaolipa ushuru, wanalipa kodi wakitegemea maendeleo waone kwenye maeneo yao, inaumiza pale ripoti inapokuja kutoka CAG tena kuna baadhi ya watu wenzetu wamelihujumu Taifa, ukiangalia Mheshimiwa Rais, anavyopambana kutafuta miradi anajibana usiku na mchana anasafiri kuhakikisha kwamba Taifa lake lisikwame, miradi hii inatumwa kijijini, huko kijijini wanaenda kupokea watu wetu ambao ni wataalam wetu, kweli wapo wazuri, lakini wapo na wabaya. Wengi ni wazuri wabaya ni wachache, kwa hiyo wachache watolewe kwenye mfumo wabaki waaminifu ili Taifa letu liweze kupiga hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu zipo changamoto katika miradi hii mingi tunajisifia, kwa mfano mimi zaidi ya shilingi bilioni 74 nimepokea kwenye Jimbo langu la Mbogwe, lakini ipo miradi mingine wananchi walikuwa wakishirikishwa, mradi unakuja unakamilika kabisa, unajitosheleza mwananchi kwa vile hajui huko, Mbunge na wewe upo bize huku na vikao vya bajeti wanaambiwa wananchi tena kuchangishwa, kitu ambapo Serikali hii imeshatoa hela ya jengo zima bila mwananchi kugusa kitu chochote, lakini kwa kutokutambua wananchi wetu wanaambiwa tena walete matofali, walete nondo, walete kokoto, unajikuta pesa zilizotolewa kwa mradi mzima zinaishia kwenye mifuko ya watu wengine, sasa hao ndiyo nawaombea washindwe kwa Jina la Yesu na waweze kupotea kabisa kwenye Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mama tena kwa kufungua demokrasia na juzi nimeona vyama 18 vimesaini, kwa hiyo niwaombe vijana wenzangu wote tukachukue fomu kuanzia tarehe moja ili tuweze kupimwa na wananchi na tuweze kuingia kwenye michakato na wananchi waweze kuhakikisha kwamba wanabadilisha uongozi mbovu wanaweka mtu yule wanayemwamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala lingine la rushwa, niwaombe wananchi kupitia mkutano huu ama jukwaa hili la Bunge, mtoa rushwa ni cancer moja kubwa sana. Kwenye maandiko matakatifu rushwa imekataliwa mara tatu, lakini pia hata sheria zetu rushwa hazitakiwi, sasa wananchi unapopewa rushwa na mtu isiwe ndoa ya kufunga naye, wewe chukua rushwa kaa kimya halafu za kwako kwenye akili sasa kufikiria kwamba hii rushwa niliyopewa huyu hana mapenzi mazuri na mimi, mwisho wa siku usimpe kura kabisa ili kusudi ajue kabisa kwamba unajua na tunajielewa vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kukushukuru wewe, ninajua na wewe unaingia kwenye michakato hii ambayo tunategemea kuingia wote, Mungu akubariki, Mungu akusimamie sana na wewe ukavuke salama ni imani yangu tutarudi pamoja lakini cha msingi tumtangulize Mungu, hata faulo tutakazoanza kuzicheza huko baada ya Bunge letu Tukufu kuvunjwa tarehe 27 najua kila mtu atatoka na sura yake hapa. Kwa hiyo, tumwombe Mungu, pia vile vyombo ambavyo vimepewa kutusimamia kama marefarii wetu haki ndiyo kitu pekee ambacho kitatuvusha salama, kwa sababu hata vurugu huwa zinaanzia pale haki inapokuwa haipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hata jinsi vita zinavyotokea nchi zingine chanzo kabisa ukikuta haki imepindishwa lazima vurugu itakuja tu. Ndiyo maana mimi nasema kipaumbele changu mimi ni haki amani baadaye, mtu akivunja haki yangu lazima tuvurugane, mambo ya amani yatakuja baadaye. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa wito kwa wale wote viongozi waliyochaguliwa kutusimamia kwenye uchaguzi huu watende haki ile ya Mungu, mimi Maganga kama kura zangu hazitoshi ziache hivyo hivyo zikae hivyo, usiniongezee wala kuniibia kura. Nikiwa nimeshinda ziache hivyo tu hivyo kura zangu zikae hivyo kwa sababu mimi siamini katika haramu kwenye maisha yangu. Haramu mimi ni mtu wa halali, kwa maana hiyo na Wabunge wenzangu niwaombe tusiwe na ubaridi wala unyonge twendeni tukapambane na tuhakikishe tunatafuta haki ya Mungu na tukipata haki ina maana Taifa letu litazidi kuwa la haki, tukipata haramu ina maana na Taifa letu litakuwa haramu kwa sababu tulipatikana kiharamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nimshukuru Mungu, nikushukuru sana, niwashukuru watu wote walionisikiliza, ahsanteni sana na Bwana awabariki sana. (Makofi)