Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Maimuna Ahmad Pathan

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi siku ya leo kuchangia hoja ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai siku ya leo, pumzi yake kwa bei ya bure kabisa pia ninapenda nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambazo anazifanya, akishirikiana na Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, kazi zao wanazozifanya hakika zinaonekana. Tunashukuru sana viongozi wetu chini ya Chama cha Mapinduzi kwa kuwa wameitekeleza sana vizuri Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja iliyopo mbele yetu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba nichangie machache kwenye hoja hii. (Mkaofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuna reli yetu ya SGR, kuna treni ambayo tunaitumia sasa hivi, ndugu zangu hii reli ni ya kizalendo. Niwaombe Watanzania tuitunze, tuithamini na tuendeleze hii reli yetu ya SGR, hii ni reli ya kwanza Tanzania ya kizalendo ambayo imejengwa na Watanzania wenyewe. Kuna reli ile ya TAZARA ile ilijengwa na Wachina, kuna reli nyingine hii ya kati na yenyewe imejengwa na Wajerumani, kwa hiyo ni uthubutu mkubwa sana sisi Watanzania wenyewe whether kwa pesa zetu wenyewe au kwa kukopa, lakini ni uthubutu ambao tumeuanzisha Watanzania wenyewe, hakika ni tunu kubwa sana kuwa na SGR. Tunaona jinsi inavyopunguza muda wa kusafiri kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam, badala ya masaa tisa au 10 tunatumia masaa matatu na nusu hakika kweli tuwapongeze viongozi wetu kwa kazi kubwa waliyoifanya na maono makubwa waliyoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza hapo mwanzo kwamba reli hii ni ya kizalendo, hii tumetengeneza sisi wenyewe, tuitunze, tuithamini ili iende vizuri, tusiharibu cha kwetu. Najisikia fahari sana ninaposafiri nikitumia chombo hiki cha SGR, ninakuwa na amani kwa muda mfupi ninafika ninapokwenda bila wasiwasi wowote. Mungu awaongoze viongozi wetu waweze kuiendeleza mpaka pale walivyopanga ifike Nchi ya Congo, ifike Rwanda na kwingineko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana tuangalie mpango mbadala kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi, mpango mkakati wa kimaendeleo. Kama tunavyojua Serikali inafanya juhudi kubwa sana kuondoa wanyama wale tembo, inajitahidi kwa kweli na kazi zao zinaonekana, lakini pamoja na hayo tujue sasa hivi kwa Mkoa wa Lindi kutakuwa na njaa kubwa sana, kwa hiyo niombe sana Serikali kwa sababu mazao hayakai kule. Hivi juzi eneo la Kilimarondo kuna mtu alilima heka 30 zote zimevamiwa na wanyama, vyakula vyote vimeliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu na ninajua juhudi kubwa wanazozifanya Serikali, bado tuwaombe waendelee, lakini pia lile wazo langu ambalo nilishatoa mara nyingi la kuweka solar electric fence kwenye maeneo ambayo yamezungukwa na mbuga za Wanyama. Naomba Serikali bado iendelee kulitilia mkazo najua ni suala la muda mrefu siyo la haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kuliongelea ni Mradi mkubwa wa Maji wa kutoka Mwalimu Nyerere kuelekea Mkoa wa Lindi na Mtwara. Mkoa wa Lindi hatuna mradi mkubwa wa maji, tuna miradi midogo midogo ya maji, ombi langu kwa Serikali kuna maji ambayo yanaweza kutusaidia watu wa Mkoa wa Lindi na Mtwara yanayotokea kwenye bwawa la Mwalimu Nyerere. Huu mradi tukiunganishwa na sisi wananchi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara utatunufaisha sana, niiombe Serikali iweze kufikiria chanzo hicho cha maji, huo ni mradi mkubwa ili na sisi wananchi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara tuweze kufaidika na mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala la umeme kama alivyoongelea Mbunge mwenzangu pale Mheshimiwa Kuchauka, tunaomba wananchi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara tuungwe kwenye gridi ya Taifa. Tatizo tulilonalo la umeme ni kubwa sana lakini tatizo hili litakaa vizuri au litapungua pale tutakapoungwa na sisi kwenye gridi ya Taifa, niiombe sana Serikali ijitahidi kufanya hivyo ili nasi tufaidi matunda ya Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Serikali kwa matengenezo ya haraka ya madaraja kwa barabara ya Kusini ya kwenda Lindi na Mtwara ilipokatika kutokana na mvua, lakini wamejitahidi wamefanya kazi usiku na mchana, Mheshimiwa Waziri alikuwa pale, amerejesha barabara, usafiri tunasafiri vizuri tunaelekea Kusini, lakini bado niwaombe Serikali tuwe na barabara mbadala kumtoa mwananchi anayetoka Liwale apite Nachingwea aende Masasi, aende Tunduru apite Ruvuma aende Mbeya apite kule Njombe, Iringa aje Dar es Salaam, route ni ndefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali yetu sikivu itutengenezee barabara ile ya kufungua mkoa ya kutoka Lindi kwenda Morogoro. Barabara hii ya kupitia Liwale ikitengenezwa itasaidia sana inapotokea janga kama hilo, siyo tu inapotokea janga kama hilo itapunguza foleni na matatizo mengine kwenye kutumia barabara moja kwa sababu barabara hii itakuwa ni fupi sana itasaidia sana wananchi hasa kusafirisha mazao ya wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe pia, Serikali kuna wananchi ambao walipisha upanuzi wa viwanja vya ndege Wilaya ya Kilwa na Wilaya ya Nachingwea muda mrefu sana, ni zaidi ya miaka kumi tumekuwa tukilizungumzia hili. Niiombe Serikali yangu sikivu kwa kuwa, malipo hayo walisema yapo kwenye bajeti ya mwaka huu unaoisha mwezi wa Juni, niombe iweze kuwalipa wale wananchi kwa sababu, hawajui wafanye nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine maeneo yao yalikuwa ni yaleyale, hawana maeneo mengine ya kulima, hawana maeneo mengine ya kuishi, wamekaa hawaelewi wafanye nini. Niiombe Serikali yetu sikivu iweze kuwalipa wananchi wa Kilwa na Nachingwea, kwa ajili ya ku-compensate maeneo yao ili maisha yao yaweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ajira kwa walemavu. Ajira kwa walemavu kiukweli, kidogo wamesahaulika. Kuna kijana nilikuwa ninahangaika naye muda mrefu kweli, ni wa kule kwetu Mkoa wa Lindi; amesoma vizuri, ana degree yake, lakini ni mlemavu. Amekuja Dodoma mara nyingi sana, kuja kufanya interview, lakini inaonekana hawa walemavu nafasi zao zile bado hawazipati vizuri. Ninajua Serikali yetu ina nia nzuri sana, Serikali yetu ni sikivu, niiombe iendelee kusimamia ajira za walemavu, ili waweze kupata haki yao ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe pia Barabara ya kutoka Masasi kuelekea Nachingwea kwenda Liwale. Nimeona kuna mradi mpya ambao utatengeneza barabara kipande kidogo, lakini bado niendelee kuiomba Serikali, barabara hii ni ya msingi sana na ni ya kimkakati, iweze kutenga bajeti ili barabara hii iweze kutengenezwa kwa kuwa, barabara hii ni muhimu na ni ya mkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mikubwa imefanywa na Serikali kwa kweli, tumeiona. Miradi ya maji imemwagwa mingi sana, shule za sekondari, shule za msingi, zahanati, vituo vya afya na pale Kilwa sisi tumepata bandari ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Mama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa, ametoa miradi mingi kwa nchi nzima, amejitahidi, mama amefanya; sisi wananchi wa Lindi, Bandari ile ya Kilwa na miradi ambayo ameileta tunamshukuru sana. Niwaombe ndugu zangu Watanzania wote ambao mnanisikiliza sasa hivi, kazi alizozifanya mama zinaonekana, ni nyingi mno na kila sehemu kwenye Majimbo yote, si ndio ndugu zangu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana, mama huyu kwa kazi alizozifanya tunatakiwa tumwongezee miaka mingine mitano, ili aweze kumaliza miradi yake ambayo ameianzisha na miradi ambayo inaendelea, kama neno lake linavyosema, kazi inaendelea na yeye ataendeleza miradi yake. Ahsanteni sana ndugu zangu. Ninaunga mkono hoja. (Makofi)