Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kutoa mchango wangu kwenye hotuba hii ya Waziri Mkuu ya mwaka huu wa 2025. Nampongeza sana Waziri Mkuu kwa usimamizi wake katika majukumu ya kazi zake. Kwa umuhimu mkubwa nasema kwa sauti kumpongeza sana Rais Dkt. Samia kwa juhudi zake na usimamizi mahiri wa kuiongoza nchi yetu na hivyo kuhakikisha kwamba Ilani yetu ya Uchaguzi inaendelea kutekelezwa kwa ufanisi wa hali juu.
Mheshimiwa Spika, napongeza sana Makamu wa Rais kwa jinsi anavyomsaidia Rais katika majukumu ya shughuli za uendeshaji nchi yetu. Pongezi pia kwa Naibu Waziri Mkuu kwa jinsi anavyowajibika kwa kiwango cha juu kabisa.
Mheshimiwa Spika, tunathamini dhana nzima ya Rais wetu falsafa za R4 zinavyoweza kuchangia ustahimilivu, maridhiano na mabadiliko ya pamoja na kuijenga nchi ikiwa imara na tulivu. Kwa dhana hii Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia anatuweka kwenye njia sahihi.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya juhudi sana kuzalisha fursa za kuongeza ajira kutokana na kuanzishwa miradi mikubwa ya maendeleo, mfano ujenzi wa bomba la mafuta, bwawa la kufua umeme pia ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato ambao unakwenda kuwa lango muhimu la kuinua uchumi wa Tanzania. Usafiri na kuunganisha ulimwengu itakuwa jambo lenye tija sana.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa SGR; reli muhimu sana ambayo imewaondelea wananchi wa Tanzania wakijikomboa na dhiki ya usafiri, kupata usafiri wa hakika na wa haraka, haya ni mafanikio makubwa. Kwa sasa reli imekamilika Dar es Salaam-Dodoma na mradi unasonga mbele kuelekea kukamilisha kipande cha kufikia Mwanza na Kigoma.
Mheshimiwa Spika, kwenye sekta ya kilimo juhudi kubwa zimeelekezwa kwenye miradi ya umwagiliaji. Tunatambua kwamba sekta hii ya umwagiliaji ndio uti wa mgongo wa kilimo na Serikali imetenga bajeti kubwa kwa eneo hili. Wakulima wameendelea kuandaliwa kulima kwa tija, napongeza sana kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Spika, kuna jambo la faida na maana sana kwa Serikali kutia nguvu ya ziada kuanzisha shule za sayansi za wasichana katika mikoa 26 ujenzi ambao umeigharimu Serikali shilingi bilioni 121.55 na wanafunzi 10,274 wanakwenda kupata elimu ambayo inahitajika kwa ustawi wa nchi kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, wanafunzi wa vyuo vya kati na elimu ya juu wamefaidika sana na fursa ya Samia Scholarship Program kuwanufaisha wasomi kwenye nyanja za sayansi, teknolojia, ubunifu, uhandisi na tiba. Jambo la kutia moyo ni kwamba shilingi bilioni 6.63 zimeelekezwa na tayari wanufaika 1,313 wamehusika. Pia wanafunzi wa vyuo wa stashhada wamenufaika kwenye fani za ufundi, kuwahusisha wanafunzi 7,732 kwa mafanikio hayo inaashiria tunakwenda kupata ufanisi mkubwa kuelekea kuinua viwanda vyetu.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.