Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Oran Manase Njeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee ninaomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza vyema miaka minne kwa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususani barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii.

Mheshimiwa Spika, pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa uzoefu na weledi wake, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, nina imani kubwa kwa Mheshimiwa Nchimbi na kumtakia afya njema na kila la heri kwenye mchakato ujao.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb), Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kutekeleza majukumu ya kumsaidia Waziri Mkuu, ikiwa na pamoja na jukumu la kuendelea kuisimamia ipasavyo sekta ya nishati.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi na Naibu Spika na pia uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ya Ushindani wa Kimataifa (National Competitiveness). Bajeti hii ambayo ni ya mwisho, inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi chake akiwa Waziri Mkuu, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimazi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kupelekea Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2023, pato halisi la Taifa kwa bei za mwaka 2015 lilifikia shilingi billioni 148,399.76 kutoka shilingi billioni 141,247.19 mwaka 2022, sawa na ukuaji wa 5.1% ikilinganishwa na 4.7% mwaka 2022. Ukuaji huu ni wa kiwango kizuri sana ukilinganisha kikanda na hata kidunia. Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya mwezi Julai, 2024, kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia imeendelea kupungua hadi kufikia 3.3% mwaka 2023 ikilinganishwa na 3.5% mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, kiwango cha ukuaji wa pato la Taifa kwa nchi za ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ulikuwa kwa wastani wa 4.6% na 3.9% mwaka 2023 ikilinganishwa na wastani wa 4.2% na 5.0% mwaka 2022 mtawalia. Vilevile ukuaji wa uchumi wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ulipungua hadi kufikia wastani wa 3.4% mwaka 2023 ikilinganishwa na 4.0% mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mwendelezo huo mzuri wa kiuchumi, Kampuni ya Moody’s imechapisha matokeo Machi, 2024 ambapo Tanzania imepanda kutoka daraja la chini la B2 (with Positive Outlook) na kwenda ngazi ya juu ya B1 (with STABLE Outlook). Matokeo hayo ni ya juu kabisa katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki na hivyo hatuna budi kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake mahiri uliowezesha Taifa kupata mafanikio hayo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kukua hadhi kimataifa, bado kuna kigugumizi kwa baadhi ya Taasisi za Kifedha nchini kuelekeza mikopo kwenye sekta muhimu za kiuchumi ikiwemo kilimo. Serikali kupitia Benki Kuu (BoT), ilitenga shilingi trilioni moja kuwezesha mabenki kutumia dirisha hili kukopesha sekta ya kilimo kwa riba isiozidi 10%. Kwa muda mrefu sasa hilo dirisha halijaonesha mafanikio ya kuchochea mabenki kupunguza riba kwenye mikopo ya kilimo na hata Taasisi za Serikali zinazonunua mazao ya kilimo bado zinahangaikia kupata hiyo fursa na badala yake kulazimika kukopa kwa riba za juu.

Mheshimiwa Spika, kilimo kama ilivyo kwa madini na utalii, zinaliingizia Taifa asilimia kubwa ya fedha za kigeni, Serikali iweke mkakati wa kuvutia uwekezaji ikiwemo mikopo ya mabenki ili kuongeza tija na ushindani katika masoko ya kimataifa. Kutokana na kilimo kuajiri asilimia kubwa ya Watanzania, Serikali itenge bajeti ya kuongeza mtaji wa angalau shilingi bilioni 150 kwa Benki ya Kilimo (TADB).

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2024 mpaka Machi, 2025 Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kwa mafanikio makubwa sana na utekelezaji huu unaonekana mpaka kwenye ngazi ya halmashauri zetu. Mafanikio makubwa yamejikita kwenye uboreshaji wa miundombinu ya barabara, reli, bandari, mtandao wa mawasiliano na uboreshaji wa usafiri wa anga. Naipongeza Serikali kwa hatua nzuri za utekelezaji wa mradi wa kihistoria wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR na ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (megawati 2,115). Miradi hii miwili ya SGR na umeme ni nguzo imara ya kiushindani katika uchumi wetu na nchi za Maziwa Makuu na hata za Kusini mwa Afrika na Kati.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatakiwa kuendelea kuchukua hatua za kibajeti kukabiliana hasa na mfuko wa bei na kuporomoka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani na sarafu kuu zingine. Kwa kuzingatia kuyumba kwa uchumi wa dunia, bajeti hii ijielekeze kuchukua hatua za kuchochea uzalishaji wa ndani ili kupunguza nakisi ya urari wa biashara (balance of payment – BOP), kuimarisha pato la Taifa kupitia sekta za kilimo, madini, utalii na uchukuzi. Hatua hizi ziende sambamba na kuimarisha mazingira ya uwekezaji hasa kwenye sekta ya kilimo na madini. Pia Serikali iendelee kusimamia sera ya fedha na bajeti ikiwemo ukimarisha mifumo na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za Serikali. Kutokana na utekelezaji wa miradi ya kimkakati, kunapelekea mahitaji makubwa ya fedha za kigeni na hivyo msukumo uwepo kwenye kuongeza uzalishaji wa madini na mazao ya kilimo. Hatua hizi ni muhimu kuhakikisha utulivu wa thamani ya shilingi na pia kuimarisha uhimilivu wa deni la Taifa hasa kwenye kigezo za ulipaji wa deni la nje kwa kulinganisha na uuzaji wa bidhaa nje (mapato ya fedha za kigeni).

Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za tabianchi, bado kuna fursa kubwa kwa Tanzania kwenye uzalishaji wa ziada wa nafaka ukilinaganisha na nchi za ukanda huu. Serikali iimarishe upatikanaji wa pembejeo bora kwa bei nafuu na kuimarisha upatikanaji wa masoko ya uhakika kupitia NFRA and Soko la Bidhaa (TMX). Kutokana na ruzuku kwenye mbolea na jitihada walizofanya Wizara ya Kilimo kuwapatia vitendea kazi Maafisa Ugani, ichochee kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo kutoka uzalishaji wa sasa wa kilo 1,000 za mahindi kwa eka mpaka kilo 4,000 kwa eka ya mahindi. Tanzania ina fursa kubwa ya biashara ya hewa ukaa (carbon credit) ikiwa ni pamoja na kuwa chanzo cha uhakika wa fedha za kigeni.

Mheshimiwa Spika, pamoja na msukumo kwenye kilimo, madini na utalii, Serikali inatakiwa kuwekeza hasa kwenye miundombinu ya usafirishaji ikiwemo barabara, reli, bandari na usafiri wa anga hasa kwa mizigo. Kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha, zimesababisha uharibifu mkubwa kwenye miundombinu ya barabara na hata reli. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, barabara zinazohudumiwa na TARURA kwa zaidi ya 80% zipo kwenye hali mbaya sana kutokana na mvua kubwa na pia kwa kukosa matengenezo ya mara kwa mara. Maeneo mengi ya vijijini barabara hazipitiki kutokana na ufinyu wa bajeti ukilinganisha na mtandao wa barabara zinazohudumiwa na TARURA.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali ichukue hatua za haraka kunusuru hali hii ili wananchi waweze angalau kusafirisha mazao yao.

Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuidhisha ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia Nsalaga (Uyole) mpaka Ifisi jirani na uwanja wa ndege wa Songwe. Kipande hiki cha barabara ambacho ni sehemu ya barabara kuu ya TANZAM, ni muhimu sana kwa kuinua uchumi wa Tanzania na hata kupunguza ajali za mara kwa mara zinazotokea katika mteremko wa Mlima Iwambi kuelekea Mji wa Mbalizi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa usafirishaji wa mazao yetu kwa soko la ndani na nje ikiwemo fursa za biashara ukanda wa SADC na uzalishaji mkubwa kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, napendekeza mwendelezo wa uboreshaji wa barabara za TANZAM kipande cha Igawa - Tunduma; barabara ya bypass ya Uyole - Songwe; barabara ya Mbalizi – Shigamba – Isongole kutokana na uzalishaji wa mazao ya kilimo; barabara ya Mbalizi – Galula – Makongorosi kutokana na uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na madini; na pia barabara ya Isyonje – Kikondo – Makete.

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha ujenzi wa SGR unaendelea kwa kasi ile ile na pia napongeza jitihada za kuendelea kutafuta vyanzo vya fedha vya masharti nafuu kugharamia ujenzi huo. Pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa, Serikali imefanya maboresho makubwa ya miundombinu na huduma katika bandari zetu hususana Bandari ya Dar es Salaam ili kukabiliana na ushindani mkubwa wa bandari zingine za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika. Bandari ya Dar es Salaam inakumbana na ushindani mkubwa toka Bandari za Mombasa (Kenya), Beira (Msumbiji), Nacala (Msumbiji), Durban (Afrika Kusini), Lobito (Angola) na Walvis Bay (Namibia).

Mheshimiwa Spika, maboresho ya bandari zetu iendane na kuondoa changamoto zingine ambazo zinasabisha gharama kubwa za usafirishaji kwa bandari zetu na kusababisha kupoteza biashara ya usafirishaji kwa bandari shindani. Ufanisi wa bandari unategemea pia maboresho ya barabara, reli ya kati (TRL), reli ya TAZARA, utendaji wenye tija wa wadau wote wa bandari na hata watumishi ili kupunguza gharama za usafirishaji kwa wateja wa bandari zetu.

Mheshimiwa Spika, kwa taarifa zilizopo, zaidi ya 70% ya mzigo wote wa nchi za nje unasafirishwa kwa kupitia Dar es Salaam Corridor inayohudumia cchi za DR Congo, Zambia na Malawi. Pamoja na fursa za kijiografia ya bandari zetu, mzigo unaopita sasa kwenye Bandari ya Dar es Salaam, ni 50% tu ya biashara yote ambayo kwa sasa inashikiliwa na bandari shindani. Kwa ajili ya kunusuru biashara hii inayopotea kwa bandari shindani, Serikali ichukue hatua za haraka kuboresha huduma za TAZARA ikiwa ni pamoja ya maboresho ya miundombinu ya reli, ununuzi wa vichwa vya reli, mabehewa na vitendea kazi vingine.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali kwa haraka ishughulikie maboresho ya mkataba wa TAZARA na kisha kutafuta mbia mwenye uwezo wa kifedha na uendeshaji. Katika kipindi hiki cha ushindani mkubwa usafirishaji wa reli ni mojawapo ya suluhisho kubwa la kupunguzo mzigo wa bei kubwa kwa wateja wa bandari zetu na hata wananchi. Pamoja na maboresha ya reli ya TAZARA, napendekeza kuendelea na ujenzi wa Bandari Kavu Mbeya ambayo ina fursa kubwa katika kipindi hiki katika kuwezesha kupunguza gharama za kusafirisha kwa wateja wa bandari na hata kupunguza bei za mafuta ya petroli, pembejeo na mazao ya kilimo. Bandari Kavu ya Mbeya ni njia panda kwa wateja wa nchi za Malawi, Zambia, DRC, Lubumbashi na hata kwa Zimbabwe na Msumbiji.

Mheshimiwa Spika, kwa lengo la kuvutia wawekezaji na kuongeza pato la fedha za kigeni, napendekeza Serikali kuchukua hatua kuharakisha uwekezaji kwenye mradi wa madini ya kimkakati kidunia, ikiwemo na gesi ya Helium na madini ya Niobium. Serikali iweke msukumo kuanza kwa uzalishaji wa gesi ya Helium na uzalishaji wa madini ya Niobium ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kiwanda cha Ferroniobium (FeNb) ambacho kitakuwa cha kwanza Afrika na cha nne duniani. Kutokana na mahitaji makubwa ya ujenzi wa reli, madaraja na reli ya SGR, kuna mahitaji makubwa ya vifaa vya chuma ambavyo ni imara, lakini vyepesi na vyenye ubora wa kimataifa. Kwa kutumia sheria zetu za uwekezaji, Serikali itumie fursa za kipindi hiki ili kuvutia wawekezaji kwenye madini ya viwandani ili yaongezwe thamani hapa kwetu na pia kuvutia malighafi ya madini toka nchi zingine ili yachakatwe hapo kwetu. Tanzania imebahatika kuwepo kwa madini ya Niobium ambayo inapatikana milima ya Pandahill Songwe, Wilaya ya Mbeya na mahitaji ya Ferroniobium (FeNb end product) ni makubwa duniani na hapa kwetu pia.

Mheshimiwa Spika, kwa kutumia rasilimali zetu za madini, Serikali inaweza kutengeneza fursa nyingi na kupitia Mradi wa Niobium na Kiwanda cha Ferroniobium, ajira 2,000 zitakazozalishwa wakati wa ujenzi na pia kutakuwepo ajira za kudumu zaidi ya 600 na indirect jobs 7,000. Mradi utazalisha mapato kila mwaka shilingi bilioni 500 (US$ 220 million) ambapo mapato kwa serikali kila mwaka shilingi bilioni 50 (US$ 22 million) uhai wa mgodi ni zaidi ya miaka 30. Hiki kitakuwa kiwanda cha kisasa cha kwanza Afrika (modern manufacturing plant and smelter). Pamoja na kuingiza teknolojia hii adimu na ujuzi (skills transfer) pia itakuwa itachangia huduma za kijamii (corporate social investment in community) na chanzo cha fedha ya kigeni.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.