Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mungu kwa kutujaalia uhai na wasaa wa kuchangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Pili, nikushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia bajeti hii.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Dkt. Emmanuel Nchimbi, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuchaguliwa kuwa wagombea wa Urais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Pia nikupongeze Mheshmiwa Waziri Mkuu kwa kuendelea kuwa kiongozi mahiri na kuisimamia Serikali kwa umahiri mkubwa.

Mheshimiwa Spika, katika Ofisi ya Waziri Mkuu pia nawapongeza Mawaziri wote, Naibu Mawaziri na watendaji wote wa Wizara zilizopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kusimamia masuala mazima ya utumishi kwa umakini mkubwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia na kuhakikisha mazingira ya kufanyia kazi yanakuwa bora na watumishi wanakuwa salama katika utekelezaji wa majukumu yao. Naishauri Serikali iongeze kasi katika suala zima la kaguzi mahala pa kazi kupitia OSHA.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia masuala mazima ya utatu yaani usimamizi wa uhusiano mzuri kati ya wafanyakazi, waajiri na Serikali kwa kuwa na mahusiano mazuri na pia imeendelea kusimamia vyema vyama vya wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara inayosimamia Sera, Bunge na Uratibu chini ya Waziri Mkuu, imeendelea kuratibu masuala mazima ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya kupitia Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Mamlaka hii ilikuwa ikifanya kazi katika mazingira magumu kwa kuwa na bajeti ndogo ya matumizi ya kawaida, pili haikuwa na fungu la maendeleo katika Bunge hili Tukufu tumeishauri Serikali sikivu ilikubali na kuipatia mamlaka hii fungu la bajeti ya maendeleo. Kwa sababu hiyo tumeona sasa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya inafanya kazi kwa weledi na ufanisi mkubwa kwani iliweza angalau kwa kiasi kidogo kuongeza vitendea kazi mfano walinunua boti na wameongeza vituo vya matibabu (MAT- Clinic).

Mheshimiwa Spika, ni jambo lisilopingika kuwa watumishi hawa wanafanya kazi nyeti sana na kwa muda mrefu wamekuwa na bajeti ndogo sana ya Matumizi ya Kawaida (OC), watumishi wamekuwa hawalipwi maslahi yao mfano posho mbalimbali katika kazi hizo ngumu wanazofanya, lakini wameendelea kufanya kazi kwa uadilifu na uzalendo mkubwa.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2025/2026 tumeishauri Serikali iongezee bajeti mamlaka hii na Serikali sikivu inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekubali kuongeza bajeti ya shilingi 5,000,000,000 kwa ajili ya maslahi mbalimbali ya watumishi na kwa ajili ya ofisi za kanda, kwa hakika hii itaongeza sana tija.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali tuliishauri tuwe na Sera ya Taifa ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, kwa kuwa suala la dawa za kulevya ni suala mtambuka kuna haja ya mapambano haya kuhusisha wadau mbalimbali, tunaipongeza Serikali kwamba imekamilisha sera hiyo ambayo inaitwa Sera ya Taifa ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2024.

Naipongeza Serikali kwa kuwa mamlaka hii sasa imeweza kwanza kuanzisha Kituo cha Habari na Mawasiliano (call center) kupitia namba 119 ambapo Watanzania watapata elimu na maelekezo ya matibabu bure. Pili Serikali imeanzisha maabara ya uchunguzi wa awali wa sampuli za dawa za kulevya, tatu mamlaka na sasa imejidhatiti na imethubutu kufanya tafiti na kubaini matumizi ya dawa za kulevya kupitia shisha, mimea mbalimbali, hii inafanywa na watumishi na wanafunzi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kazi kubwa imefanyika, kwa muktadha huo nimpongeze sana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu na Kamishna Aretas Lyimo wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya pamoja na watumishi wa mamlaka kwa kufanya kazi kwa uzalendo mkubwa kwa muda mrefu pamoja na maslahi kuwa madogo bila ya kukata tamaa na ufanisi wa juu katika kazi hii njema ya kupambana na dawa za kulevya mpaka sasa Serikali imekubali ushauri wa Kamati na kuwaongezea bajeti ya Matumizi ya Kawaida (OC) kuboresha maslahi ya watumishi hao, hii ndiyo Serikali sikivu inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan na wafanyakazi tunasema Dkt. Samia mitano tena, na maslahi bora kwa wafanyakazi na huo ndiyo moyo wa Rais kwa watumishi.

Mheshimiwa Spika, pia ninaipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kukamilisha ujenzi wa kiwanda kipya cha Uchapaji wa Nyaraka za Serikali na kufungwa kwa mitambo ya kisasa hakika kazi kubwa imefanyika, sasa nyaraka zote za Serikali za siri na za wazi zitachapishwa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa ubora na usalama na kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.