Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuungana na Watanzania wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake katika nyanja mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuungana na wananchi wa jimbo langu la Mbulu Mjini kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali nzima ya Awamu ya Sita kwa jinsi wanavyoiongoza Taifa letu na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020-2025 Mwenyezi Mungu awabariki sana.
Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa - Waziri Mkuu, Mawaziri, Naibu Mawaziri wote walio chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa wanayoifanya toka mwaka 2020 hadi 2025, hakika mambo mengi yaliyoshindikana muda mrefu yamefanyika.
Mheshimiwa Spika, nazipongeza sana Kamati zetu zote za Kudumu zinazosimamia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara zilizoko chini ya ofisi yake.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa mchango wangu kupitia mapendekezo ya bajeti ya Wizara hii muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, kwanza tunaomba Serikali itoe fedha zote zinazoombwa katika kifungu hiki kwa 100% ili tuweze kutekeleza mambo yote yaliyokusudiwa.
Pili, Serikali ijitahidi kupeleka walimu wa elimu maalumu kwenye shule zote nchini ambazo tayari tumejenga miundombinu ya huduma kama madarasa, mabweni na kadhalika, lakini hakuna walimu na watumishi wasio walimu, mfano huu uko Shule ya Msingi Endagikort katika Halmashauri ya Mbulu Mjini.
Tatu, Serikali iangalie uwezekano wa kuongeza pensheni ya wastaafu wa zamani wanaolipwa shilingi 100,000 hadi shilingi 150,000 kwa kuwa kundi hili lina changamoto kubwa sana ya kugharamia huduma za afya na mahitaji mengine ya maisha.
Nne, Serikali ijitahidi kuongeza bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa kwa kuwa hali ya mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuleta majanga mengi sana bila kutarajiwa na kusababisha madhara makubwa ya maisha ya Watanzania na rasilimali zingine.
Tano, Serikali iangalie utaratibu wa kuweka mkakati wa kuzuia utengenezaji na uingizaji wa bidhaa zilizo chini ya kiwango kwani tunapata athari za kiafya na kiuchumi kwa kuwa ukaguzi unafanyika wakati wauzaji, wasambazaji na watumiaji tayari wameshaathirika.
Sita, Serikali iangalie upya kupitia blueprint tumefanikiwa kiasi gani na upande wa wadau wake wanasemaje kama upande wa pili ili kufanya tathmini na kuleta mafanikio na maaboresho zaidi.
Saba, tayari tumepata mafanikio makubwa sana katika dhana ya uwekezaji, Serikali ijikite kuwahamasisha na wawekezaji wenye fursa ya kuajirika kwa kundi kubwa la vijana nchini.
Mheshimiwa Spika, nane, kwa kuwa Serikali ilikuwa na nia njema ya kujenga barabara kilometa 2035 za EPC+F nchini na kwa kuwa sasa huenda mpango ule hatutaweza kutekeleza na wananchi wa maeneo hayo wanasubiri kwa hamu kubwa sana ujenzi wa miradi hiyo Serikali iangalie namna ya kujenga hizo barabara ili kujibu kiu ya wanufaika wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, sasa naunga mkono hoja 100% na naomba kuwasilisha.