Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa hotuba yake nzuri ya bajeti. Pia niwapongeze Mawaziri Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi - Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu na Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete - Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa utendaji wao mzuri.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita kwenye kundi la vijana na maendeleo yao kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, Taifa kuwekeza kwenye maendeleo ya vijana ni muhimu sana. Uwekezaji huu unatakiwa upanuke zaidi ya kuwapatia vijana huduma za elimu ya kawaida kwa ngazi ya elimu ya sekondari na vyuo na kuwasaidia vijana wavinjari na kutambua vipaji vyao na kuvijengea mikakati ya kuvitekeleza kwa vitendo na hatimaye kufikia ndoto zao za maisha.

Mheshimiwa Spika, Tanzania inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa ajira kwa vijana. Hivyo basi, ni muhimu sana Serikali ichukue hatua za kimkakati ili kuondokana na tatizo hili kwani lina hatarisha kesho yetu kama Taifa. Katika kipindi hiki, kumekuwa na ongezeko la vijana wengi wanaomaliza elimu katika ngazi mbalimbali (sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu) kila mwaka na kuishia majumbani na mitaani kwani katika soko hakuna ajira za kuwachukua.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hii ya ukosefu wa ajira kwa vijana wetu, Serikali inapaswa kuanzisha programu zenye uhalisia kutatua changamoto za ajira kwa vijana. Ni muhimu sana Serikali ikaanzisha mpango maalumu wa kuwapa vijana ujuzi ili uweze kusaidia kwenye kuzalisha ajira za haraka katika kundi hili. Programu hizi zinatakiwa zilenge idadi kubwa ya vijana walioko mitaani bila ajira, wale walioko mashuleni na vyuoni na wale wanaotarajia kujiunga na masomo ya sekondari na vyuo vya kada zote.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Serikali imeanza kuweka mazingira rafiki ya kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, kujipatia ajira na kujikwamua kiuchumi, lakini juhudi hizo ni ndogo mno ukilinganisha na ukubwa wa hii changamoto.

Mheshimiwa Spika, niipongeze sana Serikali kwani kutokana na ukubwa wa tatizo hili, wameanzisha mitaala mipya ya elimu inayolenga kuwaandaa vijana kujitegemea na kupunguza tatizo la ajira. Katika hili, Serikali imeweka kipaumbele katika utoaji elimu ya kukuza ujuzi wa ujasiriamali kuanzia shule za msingi, sekondari hadi vyuoni. Kwa mfano, wameanzisha masomo ya stadi za kazi kwa shule za msingi na taasusi ya ujasiriamali ambayo ni hiyari katika vyuo mbalimbali. Mabadilko haya yanategemewa kuleta ukombozi wa kiuchumi na maendeleo katika Taifa letu. Hivyo basi, ni muhimu Serikali ikawekeza rasilimali fedha ya kutosha katika mipango hii.

Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huu, ni vyema Serikali ikahusisha na kuwashirikisha vijana kwenye mambo mbalimbali ya msingi ambayo yakizingatiwa yataleta mabadiliko makubwa. Ili kufanikisha hili, napendekeza Serikali ifanye yafuatayo kwani yanaweza kuwa muarobaini wa kuwakomboa vijana wa nchi hii dhidi ya janga la ukosefu wa ajira.

Kwanza, Serikali iwe na programu maalumu ya kuhamasisha ujasiriamali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo NGO'S zinazoshughulika na masuala ya vijana.

Mheshimiwa Spika, kuanzisha uhamasishaji wa ujasiriamali kwa vijana kutachochea ushiriki wa vijana kuanzisha shughuli za kuwapatia ajira na kipato. Serikali inaweza kutoa mafunzo ya ujasiriamali kupitia semina na mikutano mbalimbali kwa kushirikiana na NGO's zote zinazosaidia maendeleo ya vijana hapa nchini. Hii itachochea ushiriki wa vijana kutoka maeneo yote na kuwasaidia kujiajiri na kukuza uchumi wao na wa Taifa.

Pili, Serikali iwekeze kuwezesha vijana kujiajiri kwenye sekta isiyo rasmi. Ni vyema Serikali ikaboresha mazingira ya sekta hii kwa kutoa ruzuku na mafunzo ya kibiashara kwa vijana. Kufanya hivi kutasaidia sekta isiyo rasmi kuwa rasmi na kutoa fursa nyingi zaidi za ajira kwa vijana. Hili likifanyika, vijana wengi wasio na ajira wataingia kwenye sekta isiyo rasmi na kuboresha maisha yao.

Tatu, kuhamasisha makundi ya vijana kuwekeza kwenye kilimo, mifugo na uvuvi; kilimo, mifugo na uvuvi ni sekta zenye fursa nyingi na uwekezaji wa kimkakati kwenye maeneo haya kunaweza kuwakomboa vijana wengi. Kwa kuwa nchi yetu ina ardhi ya kutosha ya kilimo na mifugo na maji ya kufugia samaki, sekta hizi zina uwezo wa kutoa ajira nyingi mno iwapo vijana watafundishwa kilimo na ufugaji wa kibiashara. Programu za Jenga Kesho Bora (Build Better Tomorrow - BBT) zilizoanzishwa na Serikali ni mifano yenye nia nzuri ya kuwapatia vijana ajira katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi. Naishauri Serikali iendelee kuwekeza kwenye miradi hii muhimu na ipanue wigo kwa kuwashirikisha wadau wengine wa kutoka ndani na nje ya nchi.

Nne, uwezeshaji vijana kupata mitaji; ni vyema Serikali ikaja na mikatati kabambe ya kuwasaidia na kuwezesha vijana kupata mikopo kwa masharti nafuu. Mkakati huu ni vyema uambatanishwe na mafunzo na ushauri wa kibiashara na ujasiriamali kwa vijana wanaoanza miradi katika maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Serikali ina programu ya kuwapatia vijana mikopo isiyo na riba kupitia halmashauri za wilaya, ni kwamba hadi sasa haijakidhi mahitaji ya vijana wote wanaotaka kusaidiwa hapa nchini. Hivyo basi, ni vyema Serikali ikashirikiana na taasisi za fedha na kuja na mifumo rafiki ya mikopo isiyo na riba kubwa na inayojali changamoto za riba kubwa kwenye mabenki yetu. Mikopo nafuu itawezesha vijana kuwa na uwezo wa kuanzisha miradi na biashara mpya zitakazolipa kwa pande zote mbili.

Tano, kuwezesha vijana kwenye uwekezaji katika viwanda vidogo vidogo; vijana wa Kitanzania wanaweza kupata maendeleo ya haraka kwa kujiajiri wao binafsi au katika vikundi na kuanzisha viwanda vidogo na kuwatafutia soko lenye tija kwa bidhaa watakazozalisha. Kushirikisha vijana kwenye hili suala la ujenzi wa viwanda, kutasaidia Taifa kujenga uchumi imara na endelevu.

Sita, ushirikiano na Taasisi za Kimataifa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali; kwa kuleta mashirika mbalimbali, hasa yenye programu za maendeleo ya vijana, Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwa nchi zingine jinsi ya kutatua changamoto za ajira. Mashirika haya yanaweza pia kusaidia kutoa mafunzo na mitaji kwa biashara changa zinazomilikiwa na vijana. Wizara inatakiwa ichukue mifano ya nchi zilizofanikiwa kama China na kuwapekeka vijana kwenda kuiga miradi mbalimbali ya maendeleo.

Saba, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (Youth Development Fund –YDF) uongezewe fedha; katika mipango mipya ya maendeleo, Serikali itoe fedha ya kutosha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa lengo kuu la kuwawezesha vijana kupata mitaji ya kutosha ili wajitengenezee fursa nyingi za ajira. Kwa maoni yangu, pesa inayotolewa na Serikali kuendesha mfuko huu ni ndogo sana.

Mheshimiwa Spika, nimalizie mchango wangu kwa kushauri kwamba katika hili suala la vijana, ni muhimu kuwepo na ushirikiano kati ya sekta zote na Serikali, kwa kuhakikisha kuwa uwekezaji, elimu na sera zinazoimarisha ujasiriamali na kubuni mazingira rafiki ya ukuaji wa ajira yanapewa kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.