Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, ningependa kutoa ufafanuzi kwenye sekta yetu. Kimsingi nianze kumshukuru kwanza yeye kwa uongozi thabiti wa sekta hii, kwa kuniamini mimi msaidizi wake niweze kutoa ufafanuzi wa hoja chache kwa niaba yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri na nitafafanua maeneo machache ambayo kimsingi yameonekana kwetu. Maelezo yangu yataanza kwanza kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu, ukisikiliza Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu unaona mambo mengi na makubwa yaliyofanyika kwenye Sekta ya Uchukuzi, ambayo pengine huko nyuma ilikuwa ni kama historia. Nitajikita kwenye maeneo machache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na bandari. Performance ya bandari yetu imeongezeka mara dufu, Watanzania wanakumbuka miaka minne nyuma mzigo uliokuwa unasafirishwa kwenda nje ya nchi ulikuwa ni tani 5,600,000, lakini ndani ya miaka michache hii umefika takribani tani 9,100,000. Hata mzigo kwa ujumla, wa nchi nzima, ulikuwa ni tani takribani 16,000,000, lakini leo umefika tani 27,000,000 unaweza ukaona ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inatokana na kazi kubwa ya maboresho ya bandari iliyofanyika katika nchi yetu, ukianza na Bandari yenyewe ya Dar es Salaam, uchimbaji wa kina na mradi wetu mkubwa zaidi ya dola milioni 421 na Bandari yetu ya Mtwara, ambapo takribani shilingi bilioni 429 zimeelekezwa, ambayo imesababisha hata performance ya bandari sasa kuongezeka kutoka mzigo uliokuwepo wa tani karibu 600,000/700,000 mpaka 1,600,000. Hivyo hivyo kwa Tanga, fedha takribani shilingi bilioni 157 zilielekezwa pale na performance imefikia karibu tani 1,000,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamezungumza juu ya maboresho ya bandari mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Ziwa Victoria. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, mpaka 2021 Serikali ilikuwa imerasimisha bandari karibu 86, sasa zimefika bandari 135 na zote hizo sasa zipo kuanzia Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika pamoja na Ziwa Nyasa. Kwa upande wa Ziwa Victoria tumeshaanza maboresho makubwa kwenye Bandari ya North Mwanza, Kemondo na Bukoba, hivyo niwaombe Mheshimiwa Mwijage, Mheshimiwa Engineer Ezra na wengine, hatua kwa hatua tutakwenda kufikia bandari zao pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi mnafahamu, kwenye Ziwa Nyasa tunajenga bandari kubwa kuliko bandari nyingine yoyote iliyowahi kujengwa hapo nyuma, Bandari ya Mbamba-Bay kule Nyasa, lakini pia, upande wa Ziwa Tanganyika tumeshafanya ujenzi mkubwa kuanzia Kalema – Kabwe mpaka na Kigoma kwenyewe. Hivyo, hata maeneo mengine niwape uhakika Waheshimiwa Wabunge, kwa niaba ya Serikali kwamba, tutakwenda kuzifikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa SGR. Kwanza, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa, nishukuru Wabunge wote kwa kutambua na kuthamini kazi kubwa ambayo Serikali, chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeifanya ya uwekezaji mkubwa kwenye SGR. Hili ni jambo ambalo halijawahi kutokea kwenye historia yetu, leo Watanzania wanasafiri kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma na kurudi kwa muda mfupi, kwa raha mustarehe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya tulizoea kuyaona kwa watu wengine, Ulaya, leo yapo hapa Tanzania na hivyo kuifanya nchi yetu kuwa ndio nchi inayojenga reli ndefu kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza mpaka Kigoma na sasa tunaelekea mpaka Burundi, takribani zaidi ya kilometa 2,400. reli ndefu kuliko zote za kisasa Barani Afrika ipo Tanzania inajengwa. Tunaipongeza Serikali, kama ambavyo imezungumzwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni kwenye upande wa miundombinu ya viwanja vya ndege. Hivi ninavyozungumza karibu kila kona ya nchi tunafanya maendelezo ya viwanja vya ndege. Ukianza na kule Iringa uwanja upo karibu 98%, ukienda Shinyanga, ukienda Mwanza, ukienda Musoma, ukienda Arusha, ukienda Moshi, Lindi, Mtwara, Tabora na Rukwa, karibu kila sehemu. Zaidi ya shilingi trilioni moja zimeelekezwa katika kuboresha miundombinu hii ya viwanja vya ndege na hili linakwenda sambamba na kuongeza ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wanafahamu, takribani miaka 10 nyuma tulikuwa na ndege moja tu, mwaka 2016, leo tuna ndege 16 ikiwa ni pamoja na ndege ya mizigo. Haya ni mambo ambayo kimsingi hayakuwepo huko nyuma, tumeyafanya. Hivyo basi, hata maeneo ambayo viwanja vya ndege pengine hatujaanza, ikiwa ni pamoja na Njombe, Simiyu na maeneo mengine, Serikali inaendelea na mchakato, itayafikia na itajenga viwanja vya ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo limezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge kwa hisia kubwa ni kwenye meli. Kama ambavyo nimezungumza, unapozungumzia uchukuzi unaanzia baharini ambako mzigo ndiko unafika, unakuja usafirishaji ambako ndiyo reli, SGR, pamoja na meter gauge na pili, unakwenda kwenye upande wa pili kwenye maziwa makuu. Serikali imefanya kazi kubwa sana katika miaka hii minne na hasa katika mwaka huu wa fedha ambao tunauzungumzia, ambao Mheshimiwa Waziri Mkuu ameuzungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kuainisha kwa ufupi; kwenye Ziwa Victoria tayari meli yetu ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu, ambayo ilianza kujengwa miaka michache iliyopita ipo 98%. Ninataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, ndani ya miezi hii michache itakuwa imekamilika na itaanza kutumika. Kama hiyo haitoshi, Serikali imefanya maamuzi ya kujenga meli nyingine mpya ya tani 3,000 katika Ziwa Victoria, meli hii haijawahi kujengwa, lakini pamoja na hiyo tunaendelea na ukarabati, tumesaini mikataba ya Mt Ukerewe, Nyangumi, Clarias na Butiama na wiki ijayo meli yetu ya Butiama itaanza kufanya kazi tena baada ya kusimama hapo katikati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, Ziwa Tanganyika ambalo limekuwa likizungumzwa na wenzetu, Wabunge wa Mikoa hii ya Kigoma, Rukwa na Katavi kwa muda mrefu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelewa umuhimu na ameamua kufanya mambo mengi na makubwa katika ziwa hilo. Jambo la kwanza ni, ukarabati wa meli yetu ya MV Liemba iliyojengwa Mwaka 1913 ikasimama mwaka 2019, tumeenza ukarabati rasmi mwaka jana, fedha tumeshalipa na hivi ninavyozungumza tupo 19%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni meli yetu ya Mwongozo iliyojengwa mwaka 1982 ikasimama mwaka 2006 kufanya kazi, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kuanza kuikarabati. Tumesaini mkataba tarehe 8 mwezi uliopita, wa miezi kama tisa hivi ili ikarabatiwe irudi kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, meli yetu ya Mt. Sangara ambayo na yenyewe ilijengwa mwaka 1981 ikasimama kufanya kazi mwaka 2018 na yenyewe ipo 98% ya ukarabati. Tunachosubiri kwa sasa hivi ni ifanyiwe majaribio, siyo muda mrefu itaanza kufanya kazi. Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelewa kwamba, Ziwa Tanganyika ni uchumi, hivyo anajenga meli nyingine kubwa ya mizigo ya tani 3,500; meli hii haijawahi kuwepo katika mwambao wetu wa maziwa makuu. Meli hii, itakuwa na uwezo kama nilivyozungumza, itakuwa ina urefu wa mita 124, yaani kiwanja cha mpira uongeze na mita nyingine 24.

Mheshimiwa Mwenyekiti, meli hii itakuwa na uwezo wa kubeba mzigo sawa na malori marefu 25 au mabehewa 25 ya SGR, behewa moja likiwa na uzito wa tani 140 kwenye sakafu moja. Sakafu ya chini itakuwa na uwezo wa kubeba magari madogo 65, haijawahi kutokea katika historia ya nchi yetu. Watanzania tuungane kumshukuru kiongozi wetu kwa maono, uthubutu na utayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza, kutoa mzigo Dar es Salaam mpaka ufike Kalemie unahitaji kutumia siku saba, meli hii ikamilika pamoja na SGR, ndani ya saa 24 utakuwa umeutoa mzigo Dar es Salaam na kuufikisha Kalemie, Kongo. Tuna kila sababu ya kuendelea kushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili tunakwenda kujenga kiwanda kikubwa cha kujenga meli ambacho kitakuwa na uwezo wa kuweka meli mbili za tani 5,000 kwa wakati mmoja, nacho hakijawahi kiwepo katika historia yetu. Kiwanda hiki ambacho nakizungumza kinajengwa Katabe, Kigoma, kitasaidia nchi jirani zote za Zambia, Kongo na Burundi kujenga meli mpya na kukarabati zilizokuwepo. Hivi ninavyozungumza tayari mkandarasi ameshalipwa pesa za awali, advance payment, ili aanze maboresha na pia, tumeshalipa shilingi 1,000,000,000, kwa ajili ya ujenzi wa barabara pale Katabe na wenzetu wa TANESCO wanaanza kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea miundombinu hii ya ujenzi wa meli ikiungana na SGR na maboresho ya baharini, vyote kwa pamoja vinakwenda kufanya mapinduzi makubwa ya sekta ya uchukuzi katika nchi yetu ya Tanzania. Baada ya maelezo hayo, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)