Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa fursa hii. Ninaomba nianze kwanza kwa kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Waheshimiwa Wabunge walio wengi wamepongeza kazi kubwa na nzuri ambayo imefanywa na Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi na ni kweli kwamba, Serikali hii ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa sana ya kimapinduzi, kazi kubwa ya kutukuka na ya kihistoria katika kuleta miradi ya maendeleo kwa wananchi. Sote tumekuwa ni mashahidi kwa hakika, tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais, lakini pia, tunamshukuru kwa kazi kubwa aliyofanya na tunamwombea afya njema, ili aendelee kulihudumia na kulitumikia Taifa letu la Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa. Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya kazi kubwa na nzuri ya kupigiwa mfano ya kumsaidia Mheshimiwa Rais, ya kuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali hapa Bungeni na pia, kama msimamizi wa shughuli za kila siku za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hakika ni kiongozi wa mfano; ni kiongozi rahimu, ni kiongozi mwema, ni mchapakazi, lakini pia, ni kiongozi mwema. Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakushukuru sana kwa uongozi wako na tunakuombea sana afya njema ili uendelee kulitumikia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, wametoa michango mingi, lakini kwa maana ya muda nitaongea katika maeneo makubwa matatu; nikianza na eneo la Barabara za Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA). Serikali inatambua umuhimu wa barabara; barabara ni uchumi, barabara inadumisha na kuboresha huduma za kijamii na ndio maana mwaka 2017 ilianzisha Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini ikiwa na lengo, kwanza kuhakikisha barabara zetu zote za vijijini na mijini zinaboreshwa kwa wakati, lakini pia, kuongeza mtandao wa barabara za vijijini na mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka minne ya Serikali hii ya Awamu ya Sita barabara za vijijini na mijini bajeti yake imeongezeka sana kwa zaidi ya mara tatu ya bajeti ya mwaka 2020/2021. Kwa mfano, mwaka 2020 na 2021 Bajeti ya TARURA ilikuwa ni shilingi bilioni 250 tu, leo mwaka 2024/2025 Bajeti ya TARURA imeongezeka mpaka kufikia shilingi bilioni 870.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imeendelea kuongeza mtandao wa barabara, mwaka 2020/2021 mtandao wa barabara za TARURA ilikuwa ni kilometa 108,946, lakini leo tunaongea mtandao umeongezeka mpaka kilometa 144,430. Hii ni kazi kubwa sana iliyofanywa na Serikali katika kuongeza mtandao wa barabara vijijini na mijini, kwa leo kusogeza huduma za usafiri bora kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TARURA imeendelea kujenga barabara za lami, na barabara hizi za lami zimeendelea kuongezeka. Kwa mfano, katika kipindi cha miaka minne iliyopita kilomita za barabara za lami zilikuwa 1,449, leo tunaongea, Serikali imeweka fedha za kutosha katika ujenzi wa barabara za lami na kiwango cha barabara kimeongezeka mpaka kilomita 3,467. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kuzi-upgrade barabara za udongo kwenda kuwa barabara za changarawe kwa sababu barabara hizi zinadumu zaidi lakini pia zinarahisisha zaidi usafiri. Mpaka sasa tumeongeza sana ujenzi wa barabara za changarawe kutoka kilometa 27,309 mpaka kilometa 44,372. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamechangia kwa kina eneo la TARURA; na moja ya eneo ambalo wamechangia ni namna ambavyo Serikali ina wajibu wa kuongeza upatikanaji wa fedha kwa wakati ili kuwalipa makandarasi. Kufuatia muktadha huo Serikali ilifanya ubunifu na kuanzisha Mfuko wa Hati Fungani za Samia (Samia Infrastructure Bond) ambapo, mwezi October mwaka 2024, mwaka jana Mfuko huo ulifunguliwa ukiwa na lengo la kukusanya shilingi bilioni 150.

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari njema ni kwamba mwitikio ulikuwa mkubwa na mzuri na mpaka sasa Serikali imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 320 kwa ajili ya Samia Infrastructure Bond. Mfuko huu utawawezesha sana makandarasi wazawa, kwanza kuhakikisha kwamba wanapata mkopo wa masharti nafuu ambao hauhitaji dhamana ili waweze kukamilisha miradi yetu ambayo inaendelea katika maeneo yetu ya miji na vijijini. Kwa hiyo nitumie nafasi hii kuwatia shime makandarasi wazawa wote wanaofanya kazi kupitia TARURA wahakikishe wanatumia fursa hii nzuri ya Samia Infrastructure Bond kwa ajili ya kukwamua ile miradi inayokwama ili miradi yetu ya barabara vijijini na mijini isikwame. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Sekta ya Elimu ya Msingi; tunafahamu kuwa elimu ndiyo nyenzo muhimu katika maendeleo ya Taifa lolote. Serikali hii ya Awamu ya Sita imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika Sekta ya Elimu ya Msingi na Sekondari. Katika kipindi cha miaka minne Serikali hii imefanya kazi kubwa ya kihistoria ya kujenga miundombinu ya huduma za elimu, kwa maana ya shule mpya za msingi, shule mpya za sekondari, pia ujenzi wa madarasa na miundombinu mingine muhimu ya elimu. Katika kipindi cha miaka hii minne, jumla ya shule mpya za msingi ambazo zimejengwa ni 1,580 na shule mpya za sekondari zilizojengwa ni 1,031. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haijawahi kutokea katika kipindi cha miaka minne Serikali ikajenga shule kwa wingi kwa kiasi ambacho kimefanyika katika kipindi cha miaka hii minne. Waheshimiwa Wabunge ni mashuhuda, katika maeneo yetu tumeona kazi kubwa ambayo imefanyika. Lengo la Serikali ni kuendelea kusogeza huduma za elimu karibu na watoto wetu, karibu na wananchi na pia kupunguza mdondoko wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuboresha na kuondoa changamoto ya mdondoko, Serikali imeendelea kujenga mabweni kwa ajili ya watoto wa shule za sekondari na hususani watoto wa kike. Jumla ya mabweni 1,000 yamejengwa katika kipindi cha miaka minne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeendelea kuboresha sana huduma za chakula katika shule zetu za msingi na sekondari. Katika eneo la sekondari tumeendelea kujenga pia mabwalo. Waheshimiwa Wabunge katika michango wamesisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu hiyo na mabwalo yameendelea kujengwa. Jumla ya mabwalo 133 yamejengwa na yanatumika katika shule zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii iliweka mpango kabambe wa kukarabati na kujenga madarasa kwenye shule zilizopo, ambazo zina upungufu mkubwa wa madarasa. Katika kipindi hiki cha miaka minne Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amejenga jumla ya madarasa 62,685 katika shule za msingi na sekondari kote nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii inatekeleza mpango wa elimu bila malipo ambapo Serikali inatoa zaidi ya shilingi bilioni 484 kila mwaka kwa ajili ya sekta ya elimu bila malipo. Ili elimu hii iwe bora, lazima tupate walimu. Serikali imeendelea kuajiri walimu kila mwaka wa fedha; na mpaka sasa tangu mwaka 2020/2021 jumla ya walimu 45,809 wameajiriwa na kati yao msisitizo mkubwa, kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge mmekuwa mkichangia, walimu wa sekondari wa masomo ya sayansi wameajiriwa 29,399. Wakati huo huo ufaulu wa elimu ya msingi na sekondari umeendelea kuongezeka kati ya 85% na 99.9%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Sekta ya Afya, Serikali hii ya Awamu ya Sita imevunja rekodi kwa kuwekeza kwa kiwango kikubwa sana katika Sekta ya Afya ya Msingi. Katika kipindi hiki cha miaka minne Serikali imewekeza zaidi ya shilingi trilioni moja na bilioni mia mbili tisini na saba katika Sekta ya Afya ya Msingi kwa kujenga hospitali za halmashauri 129, kwa kujenga vituo vya afya vipya 367 na kwa kujenga zahanati 980; kwa maana ya kuchangia nguvu za wananchi. Serikali itaendelea kuboresha sana miundombinu hii ya huduma za afya kwa kuhakikisha kwamba maboma yote yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi yanaendelea kukamilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kupeleka magari ya wagonjwa. Jumla ya magari 316 yamepelekwa, yakiwemo magari ya wagonjwa 382 na magari ya kusimamia huduma za afya msingi 210. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile eneo la muhimu sana ambalo Waheshimiwa Wabunge wamechangia ni eneo la vifaa tiba. Mheshimiwa Rais kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI ameanzisha utaratibu wa kununua vifaatiba bora na vya kisasa katika kila mwaka wa fedha; na katika kipindi hiki cha miaka minne Serikali imenunua vifaa vya kisasa zikiwemo digital x-rays, mashine za ultrasound, vifaa vya maabara na vimepelekwa kwenye zahanati zetu, kwenye vituo vya afya pia kwenye hospitali za halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma zetu za afya zimeendelea kuboreka sana ndiyo maana katika historia ya nchi yetu, mwaka huu Mheshimiwa Rais amepewa zawadi au tuzo ya The Global Goalkeeper Award, ambayo imetokana na mafanikio makubwa ya kihistoria ya kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kutoka 500,056 kati ya vizazi hai 100,000 mwaka 2016/2017 mpaka vifo 104 tu kati ya vizazi hai 100,000 mwaka 2023. Niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba mafanikio haya makubwa yataendelea kufanyiwa kazi, ikiwemo eneo la ajira kwa walimu 25,936. (Makofi)

Mheshimiwa Mwneyekiti, ninahitimisha kwanza kwa kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge; na kwamba mafanikio haya makubwa ya sekta hizi nilizozisema kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni mafanikio yetu sote; na mimi ninawaombea katika mchakato unaofuata kwa kazi hii kubwa ya kutukuka na ya kihistoria; wote Mwenyezi Mungu akatujalie tuweze kurejea kwa sababu, kwa hakika tumeweka alama kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)