Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niungane na Waheshimiwa Mawaziri wenzangu kutoa pongezi za dhati kabisa kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa na nzuri ambayo ameifanya na kwa wasilisho zuri la bajeti yake. Moja, ni bajeti ambayo imesheheni mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na vilevile imebeba matumaini ya kweli ya Watanzania katika kuhakikisha kuwa wanapata maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati ya moyo nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu. Moja ya jukumu kubwa ni kumsaidia Mheshimiwa Rais; amemsaidia kwa vitendo. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwa tumemwona maeneo mbalimbali akifanya kazi. Miongoni mwa maeneo ambayo aliona kuwa yanahitajika kuchukuliwa hatua ni hasa kwa watumishi wazembe. Huko amechukua hatua bila kuangalia pasi na shaka kabisa. Kwa dhati na kwa moyo tunajifunza mengi lakini kwa dhati kabisa nimpongeze kwa kazi kubwa na nzuri ambayo ameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine, nipongeze Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Waheshimiwa Wabunge, wamepata michango mbalimbali kupitia bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini eneo la maji wamethamini kazi kubwa ambayo imefanyika katika kipindi hiki cha miaka mitano. Tunashukuru kwa jitihada na pongezi ambazo Wabunge wametupa, lakini yapo maeneo ambayo wameweza kuyachangia na nitaweza kuyatolea ufafanuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maji tulipewa maelekezo mahususi na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan; alisema kwamba yeye ni mama na asilimia kubwa ya wanaoteseka juu ya adha ya maji ni akinamama, kwa sababu hiyo hataki kusikia na wala hataki kuona kuwa akina mama wa nchi hii wanateseka kutokana na adha ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa imefanyika katika eneo la maji. Miaka ya nyuma moja ya changamoto kubwa sana katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikija bajeti ya Wizara ya Maji ilikuwa hapatoshi, lakini leo tunaona katika kipindi hiki cha miaka mitano, bajeti ya maji tumepata ushirikiano mkubwa hasa kwa Waheshimiwa Wabunge, hasa chini ya michango yao, lakini juu ya usimamizi mzuri wa Kamati yetu ya Maji na Mazingira na Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yangu ninataka kusema kwamba; moja ya changamoto ilikuwa ni ufinyu wa bajeti. Miradi mingi imejengwa ilikuwa haikamiliki kwa sababu ya bajeti, lakini Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongeza fedha katika eneo hili la maji. Leo tunaona na tunashuhudia kuwa miradi ambayo imejegwa tangu mwaka 1974 ambayo ilikuwa haikamiliki imekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda zako kule Serengeti Mugumu ilikuwa ni mifano ya miradi dhahiri ambayo imejengwa kwa muda mrefu bila haikamiliki lakini leo imekamilika. Tulikuwa tunafahamu kabisa kuwa tulikuwa na miradi chechefu zaidi ya 177 ambayo imejengwa lakini ilikuwa haitoi maji. Chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan miradi yote 177 imekamilika na inatoa huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo tumeona uthubutu wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kwenye miradi mingi mikubwa ya kimkakati iliyokuwa ikijengwa kwa fedha za wafadhili. Kwa sasa, kupitia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tunaona uthubutu wake kwamba fedha za ndani ndizo zilizowezesha kujenga miradi mikubwa ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Longido utakuta tumejenga miradi mikubwa. Leo tunajenga Bwawa la Farqwa, vilevile tunajenga Bwawa la Kidunda kwa ajili ya kupeleka maji Dar es Salaam, bwawa ambalo limezungumzwa kwa muda mrefu sana, lakini chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia zaidi ya bilioni 335. Hivi ninavyozungumza mkandarasi yupo site na Mheshimiwa Waziri Mkuu amefika na ameweka jiwe la msingi. Hii ni miradi ambayo imezungumzwa na Bunge hili, yalikuwa ni maazimio ya Bunge kwa muda mrefu na chini ya Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tumeweza kujenga huu mradi. Ninaamini katika kipindi hiki kifupi tutaweza kukamilisha ili kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri zaidi na zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira yake ya dhati, ametupa malengo kuwa itakapofika mwaka 2025 kuwe na 85% ya upatikanaji wa maji vijijini na 95% ya upatikanaji wa maji mjini. Hivi ninavyozungumza mpaka hivi sasa leo vijijini tuna takribani 83% na mijini zaidi ya 91%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miradi ya kimkakati ambayo tunaendelea nayo zaidi ya 1,000. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, moja ya maelekezo yao na hoja ambazo wamezijenga ni kuhakikisha kwamba miradi ambayo tumeianza tunakwenda kuikamilisha. Ninataka niwahakikishie, jitihada ambazo tunazipata kupitia Wizara ya Fedha na supportive kubwa ya fedha, miradi yote ambayo tumeianza tutaikamilisha na Watanzania waishio vijijini watapata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ya Tanzania ina takribani vijiji 12,318. Mpaka sasa kupitia wakala wa maji vijijini RUWASA tumekwishafika kwenye vijiji zaidi ya 10,000 na zaidi, tumebakisha vijiji 2,000 tu. Mkakati wa Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha kuwa vijiji vyote vya Tanzania vinapata huduma ya maji safi na salama. Hii ni katika kutimiza dhamira yake ya kumtua mwanamama ndoo kichwani. Mheshimiwa Rais ametununulia mitambo ya uchimbaji wa visima, ametununulia mitambo ya uchimbaji wa mabwawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa vijiji vyote vya Tanzania vinapata huduma ya maji safi na salama tumeanzisha program ya visima 900. Tumeanza phase one ambapo tutahakikisha kwamba katika kila jimbo tunachimba visima vitano na tutahakikisha kwamba hivi vijiji 2,000 tunavikamilisha. Tumeanza phase one, tunakuja phase two; mkakati wetu ni kuhakikisha kwamba vijiji vyote vinapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamejenga hoja ya kuwatetea wananchi wao. Kwa dhamira na support hii kubwa ambayo tunaipata kutoka kwa Mheshimiwa Rais sina mashaka, ninaamini kwamba vijiji vyote vitapata huduma ya maji safi na salama. Tunajua, si maeneo yote ukichimba maji utapata maji, yapo baadhi ya maeneo ni lazima uchimbe mabwawa. Tumepewa seti za mitambo ya uchimbaji wa mabwawa na kwa hiyo Wizara ya Maji haina kisingizio. Tumejielekeza huko na tumeanza kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda Handeni kwenkambala tumejenga bwawa kubwa la kimkakati kupitia mitambo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan; ukienda Kizengi kule Tabora tumejenga bwawa la kimkakati na sasa leo wanapata huduma ya maji safi na salama. Ukienda zako Monduli, tumejenga Bwawa la Lepurko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wetu ni kwamba mvua isiwe maafa, iwe fursa, hasa juu ya uchimbaji wa mabwawa kwa kuhakikisha kwamba tunavuna maji kwa ajili ya kunywa, kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na maji kwa ajili ya kutumika kunyweshea pia mifugo yetu iliyokuwepo nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema ni kwamba, kumpata Rais aina ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan hapatikani kila mahali na hapatikani kila wakati. Tumempata na hivyo ni lazima tumtumie kwa maslahi ya Watanzania. Hapa ninachotaka kusema ni kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni suluhu ya matatizo ya Watanzania. Ahsante sana. (Makofi)