Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkuranga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema na mwingi wa ukarimu. Pili, nitumie fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika mjadala huu wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na timu nzima ya ofisi yake kwa namna ya uwasilishaji mahiri na mzuri sana wa bajeti hii iliyoleta mwelekeo wa utendaji kazi wa Serikali uliokwisha kufanyika na ule ambao tunauelekea. Ninaomba pia nimpongeze yeye binafsi kwa namna ambavyo amemsaidia sana kazi Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mheshimiwa Waziri Mkuu hongera sana kwa kazi kubwa na nzuri uliyoifanya wakati wote katika kumsaidia kazi Mheshimiwa Rais, kinara wetu na jemedari wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wametoa michango inayohusu ujenzi wa barabara katika maeneo mbalimbali nchini. Barabara na madaraja yanayoendelea kujengwa, lakini na yale maombi mapya vilevile ambayo tumekwishakuanza kuyapokea wakati huu ambapo tumekuwa tukijadili bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata zaidi ya Wabunge 20 waliochangia kwa namna ya kuzungumza hapa Bungeni, lakini vilevile kwa namna ya kuandika. Tunawashukuru sana kwa michango hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba uniruhusu nieleze machache sana juu ya mafanikio ambayo tayari pia yalikwishaanza kuelezwa katika risala na hotuba iliyosomwa hapa na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Miongoni mwa mambo makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na kinara na jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni pamoja na miradi ya kielelezo ya kimkakati, kama vile Daraja la Kigongo-Busisi, Daraja la Pangani, Daraja la Tanzanite pale Dar es Salaam na miradi mingine mikubwa inayoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka minne ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yetu ya Awamu ya Sita ya Chama Cha Mapinduzi, jumla ya kilomita za lami 1,365 zimekamilika nchini kote. Hili Daraja la Kigongo-Busisi sasa limekwishakufika mwisho. Tunafahamu ya kwamba ni kiu ya Watanzania kuona kwamba jambo hili sasa linafunguliwa na linaanza kutoa huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Naibu wangu, amekuwa akijibu maswali hapa na kueleza; na hata jambo la Kigongo – Busisi amelieleza. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu amelieleza pia. Ni matumaini yetu kuwa mwezi Mei, 2025, Daraja la Kigongo-Busisi panapo majaliwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atakwenda kulifungua; na huo ndio utakaokuwa mwanzo na mwisho wa kuandikwa na kuelezwa kwa historia ya matumizi ya vivuko na habari ya vivuko katika eneo hili. Tunavichukua vivuko vile tunavitafutia maeneo mengine ya kwenda kuvipeleka. Hayo ni mafanikio makubwa ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na ni mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia alilikuta daraja hili likiwa limefikia 20% tu ya utengenezwaji wake. Kazi kubwa ameisimamia, ameifanya na sasa kazi ile imekwenda kukamilika. Siku ya kulizindua daraja lile, tutawaalika Waheshimiwa Wabunge wote na wananchi wote wa Taifa hili kwa kuwa jambo hili ni kielelezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja lile lina urefu wa kilometa tatu. Katika Eneo la Afrika ya Mashariki na Kati, hakuna daraja lingine refu linalozidi Daraja la Kigongo Busisi la John Pombe Magufuli (JPM). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo, pia tunayo mafanikio ya ring road ya hapa Dodoma ambayo ina zaidi ya kilometa 104. Hii ni katika kuonesha namna tulivyojiandaa kama Serikali kuufanya Mji wa Dodoma kuwa ni Makao Makuu ya Taifa letu na namna ambavyo hatutaki kurejea makosa ya kuwa na misongamano tena hapa katika Jiji la Dodoma. Ndiyo maana tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuturidhia tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha huu mradi wa ring road ya Dodoma, tuna mradi mwingine mkubwa wa kutoka Chamwino kuingiza barabara sita mpaka Dodoma Mjini na nyingine zitatoka zitaelekea usawa wa Arusha na nyingine zitaelekea usawa wa Iringa. Hii ni programu ambayo sasa hivi tupo katika hatua za kimanunuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, naomba nieleze juu ya mambo mbalimbali yaliyoelezwa na Waheshimiwa Wabunge, ikiwa ni pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa Mikoa ya Kusini walivyoeleza namna ambavyo barabara hii imechakaa sana na namna ambavyo wanatamani kuona barabara hiyo inafumuliwa na kujengwa upya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaeleze kuwa Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo. Tuna hatua kubwa mbili; kwanza, ni hatua ambayo haijaiva ambayo tunaendelea nayo, tunaitafutia fedha barabara hii ili tuifumue yote na tuanze upya ukiacha haya madaraja ambayo yanaendelea kujengwa sasa hivi. Wakati tunasubiri hilo, tayari tunayo maelekezo ya kuanza kutengeneza vipande kwa vipande hasa katika yale maeneo yaliyoharibika sana. Kwa mfano, eneo la kutoka Ikwiriri – Chumbi – Marendego mpaka Somanga, hili ni eneo ambalo limeharibika sana. Kwa hiyo, tayari hilo tumeliweka katika mipango ya bajeti ya 2025/2026 ili kuhakikisha kwamba tunalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, mvua zimekuwa zikituathiri sana. Sisi Serikalini tumejipanga vyema na tunashukuru sana kwamba wakati wote zinapotokea dharura hizi, huwa tunachukua hatua ya haraka sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru Mameneja wetu wa Mikoa na viongozi wa mikoa na wilaya; Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama wamekuwa wakitusaidia sana juu ya kuhakikisha kuwa mambo yanakaa sawasawa. Hata hili la Somanga, tunaushukuru sana Uongozi wa Mkoa wa Lindi na Wilaya ya Kilwa kwa namna ambavyo tumesaidiana kwenye kuli-handle jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge, ipo taarifa ambayo imesambaa jana usiku mpaka leo asubuhi ya kuwa daraja la muda la Somanga limekatika. Ninalihakikishia Bunge, daraja halijakatika, daraja la muda bado liko sawasawa. Mvua zinazonyesha nchini kote hususan katika maeneo ya Morogoro na mengineyo ambayo haya maji yote yanakwenda katika Bahari ya Hindi, yamefanya maji yapite juu ya daraja lile la muda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa msingi huo, kwa ajili ya usalama wa watu, tukasema, tusubiri kwanza na hiki ni kitu ambacho tunakifanya sehemu nyingi ikiwa ni pamoja na kwenye Daraja la Jangwani na kwingineko ili kuangalia usalama wa watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, nasema tu, kazi inaendelea na kazi ni nzuri. Tunayo matarajio, tutakaposoma bajeti yetu tutaeleza kwa kina sana juu ya mipango kadha wa kadha tuliyonayo ya kuhakikisha barabara mbalimbali katika Taifa zinaendelea kujengwa, zinakamilika na zile mpya zinaenda kuanza pia vilevile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa hatua hii, na ninasema kwamba, Mheshimiwa Rais Samia aliidhinisha jumla ya fedha shilingi bilioni 840 kwa ajili ya kushughulika na mambo ya dharura peke yake nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, na ninaunga mkono hoja. (Makofi)