Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naanza na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai wa kufika siku ya leo na kuweza kushiriki shughuli hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, natumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri, pia kwa coordination ya shughuli za Serikali na kwa namna anavyoweza kutuongoza kwa ajili ya kufikia malengo tuliyopewa na Ilani ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi pamoja na malengo na matamanio ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Waziri wa Kilimo, kwa kipindi chote nikiwa Naibu Waziri ninayeshuhulikia masuala ya ushirika wakati huo na nikiwa Waziri mwenye dhamana ya kilimo, namshukuru kwa dhati Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa support ambayo amekuwa akinipa mimi na kusaidia sekta ya ushirika kuweza kusimama na kufikia hapa ilipofika. Namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo ya Mheshimiwa Rais ilikuwa ni kwamba, lazima Tanzania tuwe na benki ya ushirika. Tarehe 28 mwezi huu Mheshimiwa Rais atazindua Benki ya Ushirika Tanzania, ambayo inaanza na mtaji wa shilingi bilioni 55 na itakuwa na matawi manne ambayo yatakuwa Mkoa wa Kilimanjaro, Mtwara, Tabora na Makao Makuu Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari benki hiyo imeshaanza pale ambapo lilikuwa jengo la ushirika. Mpaka kufika mwisho wa mwaka huu, tunaamini kwamba benki hii itakuwa na matawi nane na mawakala 36. Vilevile, vyama vyote vikuu vya ushirika vitakuwa ni mawakala wa Benki ya Ushirika ambao watafanya kazi ya kufungua akaunti za wakulima, deposit na withdraw. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, benki hii kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais itakuwa ina dirisha maalumu la guarantee scheme na equity fund kwa ajili ya kuwasaidia wakulima ili waweze kuwekeza kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka niseme, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa dhati kwa sababu, unaweza ukawa na ilani na mipango, lakini pale ambapo kunakuwa hakuna political will kwenye ofisi kuu ya nchi, mambo mengi yanakuwa hayawezi kutokea. Namshukuru Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021 wakati Mheshimiwa Rais anahutubia ndani ya Bunge hili, ukuaji wa sekta yetu ya kilimo ulikuwa ni 2.7% na bajeti ya kilimo ilikuwa shilingi bilioni 290. Mwaka 2024/2025 ukuaji wa sekta umefika 4.2% na bajeti imefika shilingi trilioni 1.2. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyoongea, mauzo ya nje ya sekta ya kilimo; na ninapozungumzia kilimo sizungumzii kilimo kwa mapana, ninazungumzia kilimo mazao. Mwaka 2021 mauzo ya nje ya sekta ya kilimo yalikuwa ni wastani wa dola bilioni 1.2. mwaka 2024 tumefika dola bilioni 3.5, mauzo ya nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Rais anahutubia Bunge hili, eneo la umwagiliaji ambalo limekuwa ni jambo kubwa sana leo, nami ninawaelewa sana matarajio mliyonayo Waheshimiwa Wabunge. Hatuwezi kukaa tunalalamikia mabadiliko ya tabianchi wakati Mwenyezi Mungu anatupatia maji, lakini tunashindwa kuyavuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ilikuwa ni shilingi bilioni 55, lakini leo bajeti yetu ni shilingi bilioni 400 lakini tunatekeleza miradi 780 ndani ya kipindi cha miaka mitatu. Leo hii mtandao wetu umetoka hekta 560,000 umefika hekta 970,000. Lengo la ilani ni hekta milioni 1.2. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya upembuzi yakinifu wa mabwawa 100. Kati ya haya 100, mabwawa 27 tayari yana wakandarasi na kati ya haya 27, mabwawa 10 yako zaidi ya 80%. Hizi ni hatua ambazo Serikali hii imechukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki ndiyo inaongoza kuendesha skimu ya ruzuku kwa wakulima kuliko Serikali yoyote. Tunatumia karibu shilingi bilioni 300 kwa ajili ya wakulima wa mazao ya kawaida, kwa maana ya mazao 13 ya chakula ambayo yanatupatia food security. Nini matokeo yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021/2022 uzalishaji wetu wa mahindi ulikuwa tani milioni sita. Msimu uliopita tumefika tani milioni 12, tumekuwa ni nchi ya pili Afrika kwa uzalishaji wa mahindi. Tulikuwa tunazalisha wastani wa tani 1,200,000 mpaka 1,600,000 za mchele. Sasa tuko tani 3,500,000 za mchele. Sisi ndio exporter tunaoongoza katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii imelia sana kuhusu mazao yanayoitwa ya biashara kwa maana ya korosho, pamba, tumbaku na kahawa. Leo tunavyoongea, sisi kama nchi mwaka 2024 kwenye zao la korosho kwa wastani kwa kipindi cha miaka mitatu, Serikali hii imetoa ruzuku ya zaidi ya shilingi bilioni 400 kwenye zao la korosho peke yake. Kwa kipindi cha miaka mitatu! Tumetoka wastani wa tani 180,000, leo tumefika tani 520,000 kwa msimu uliopita wa zao la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wastani wa bei ya mkulima kwa mara ya kwanza tumefikia kuuza zaidi ya shilingi 4,200/= wastani wa bei ya mkulima katika mfumo wa TMX. Vyama vyetu vya ushirika vimekusanya mazao na kuyauza kupitia Mfumo wa Stakabadhi ya Ghala na Ushirika kwa zaidi ya shilingi trilioni nne. Hili jambo halijawahi kufanyika katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tulikuwa kwenye kundi linaloitwa others kwenye uzalishaji wa tumbaku. Yaani wanatajwa wa kwanza, wa pili, wa kumi, halafu sisi tumewekwa kwenye kundi la wengineo; lakini leo hii Tanzania ni nchi ya pili Afrika kwa uzalishaji wa zao la tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mauzo yetu ya tumbaku yamefika zaidi ya dola milioni 400. Serikali hii inagawa ruzuku ya mbolea kwa wakulima wa kahawa pamoja na miche bure. Pia, kwa mwaka tunagawa zaidi ya miche milioni 22 kwa wakulima wa kahawa bure. Humu ndani ya Bunge wapo Waheshimiwa Wabunge ambao ni wakulima wa kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bei ya kahawa, kwa upande wa Kagera ilikuwa inanunuliwa kwa shilingi 700 mpaka shilingi 1,100. Msimu uliopita kahawa imefika zaidi ya shilingi 5,000 kwa wakulima katika Mkoa ya Kagera. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye tumbaku kulikuwa kuna madaraja 65, na kuna daraja linaitwa reject kwenye nchi hii. Yaani mkulima atalima, atavuna halafu inaitwa reject, inatupwa. Leo hakuna reject kwenye tumbaku. Leo mkulima aliyekuwa anapata Dola 0.5 kwa kilo, msimu umelioisha juzi Serengeti bei ya wastani ni Dola 2.5 kwa wakulima wa tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo moja ambalo nataka nilisemee kidogo. Kwa nini tunatoa ruzuku? Huu umekuwa mjadala na taasisi nyingine za Kimataifa zinatuonesha sisi kwetu ruzuku kwa wakulima ni wastage of resources, siyo sahihi. Ruzuku kwa wakulima ni njia mojawapo ya stabilization na kupunguza gharama ya uzalishaji. La pili, kama ambavyo Serikali inatoa ruzuku kujenga daraja au kutoa fedha kwenye kodi kujenga Barabara, ni sawasawa na kumsaidia mkulima, na ni sehemu ya facilitation kwenye shughuli za uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mheshimiwa Rehema amesema hapa, kwa nini tunasainisha fomu? Nawaomba wakulima wa tumbaku, najua kilio cha ruzuku yenu. Serikali imeshatoa shilingi bilioni 13. Tunachokifanya ni kwenda kujiridhisha, huyu Hussein Mohamed Bashe wa Ulyankulu, hii akaunti ni ya kwake? Asaini mwenyewe kwamba hii akaunti ni ya kwake. Sasa mnataka tuzipeleke hizi fedha za wananchi mitaani bure?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho, niongelee wakulima wa miwa. Kumekuwa na kilio kwa wakulima na nimeshongea na ndugu yangu Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Bunge hili halijapitisha sheria ya kuwataka wakulima wa nchi hii wawe na EFD receipts na EFD machine. Hatukupitisha humu na haya siyo maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi, wala siyo maelekezo ya chama kilichoko madarakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotakiwa, vyombo vyetu vya ukusanyaji wa kodi viende vikakusanye kodi kwenye eneo la formalization ambako tumewataka traders wawe na business license. Anayenunua mazao, lazima awe na TIN na atatoa risiti ya EFD na siyo mkulima wa kijijini kufuatwa na kuambiwa leta risiti ya EFD. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitumie Bunge hili kuwatangazia wakulima, hamwajibiki kwenda kutafuta EFD machine kwa ajili ya ku-produce risiti za EFD. Hiyo siyo shughuli ya wakulima wala vyama vya ushirika. Hii siyo genesis ya sheria iliyopitishwa na Bunge hili. Tunamfahamu ambaye anatakiwa ku-produce risiti za EFD. Tushirikiane ku-formalize kwenye sekta ya kilimo kwa kuwarasimisha wafanyabiashara wawe na leseni, wawe na TIN, na waingie kwenye tax base.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niingie on record ndani ya Bunge hili, kwamba tukifanya hivi, vyama vyote vya ushirika vitaacha ku-formalize na kuwa aggregated, na tutaua aggregation system tunayoijenga kwa jasho katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba TRA huko waliko wawaache wakulima wafanye kazi ya uzalishaji. Nendeni mkachukue kodi kwa traders ambao wanafanya biashara. Kipato cha mkulima ni kimoja tu kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)