Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia hoja iliyoko Mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya, na kwa kweli Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweza kuivusha nchi katika kipindi ambacho dunia nzima ilikuwa inapita kwenye misukosuko. Ni kipindi ambacho kimeambatana na misukosuko mingi kutokea katika records za masuala ya kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi matukio haya ya kimisukosuko huwa linatokea moja, linahangaikiwa hilo hilo, linapita, watu wanarejea, lakini kwa kipindi hiki cha miaka minne kumekuwa na misukosuko mfululizo ambayo ilikuwa ikitokea katika masuala ya kiuchumi, lakini jemedari wetu amesimama imara na nchi imevuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na Covid ambayo ilipiga nchi zote za dunia hii, tukavuka. Likaja suala la mzozo Mashariki mwa Ulaya ambao ulichangia gharama za maisha kupanda, tukavuka. Yakaja masuala ya uhaba wa fedha za kigeni na kwenyewe tumevuka, tumerudi katika hali ya kawaida. Hata sasa limekuja suala la sera za nje za baadhi ya Mataifa na lenyewe kama ambavyo Mheshimiwa Rais wetu ameweza kusimama kwenye masuala mengine na Taifa letu, likavuka na hili tayari Serikali imeshaanza kuchukua hatua, na ninawahakikishia Waheshimiwa Wabunge hata hilo tutavuka na tayari kazi imeshaanza kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilijitokeza hoja, na nianzie hapo hapo kwamba kuna baadhi ya Mataifa yamebadilisha sera zao ambazo zinahusisha kupunguza fedha katika mataifa yanayoendelea ikiwemo Tanzania. Sitataja kwa ajili ya mahusiano ya Kimataifa, lakini nadhani mmeshapata hayo Mataifa ambayo yamefanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawahakikishia, Serikali yetu tayari ilishafanya tathmini na tayari kazi hiyo ya tathmini imeshafanyika na ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. Timu hiyo iliyosimamia kazi hiyo ilikuwa chini yake na tathmini ya sekta zote imeshafanyika na tayari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyoongea, tayari Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeshaanza kuchukua hatua. Kwa mfano, tulikuwa na mahitaji ya takribani shilingi bilioni 220 kwenye sekta ya afya kuweza kuziba pengo ambalo limetokana na fedha zile ambazo tulitarajia kutoka kwa wenzetu ambao wamebadilisha sera yao na kupunguza fedha zinazokuja kwenye Mataifa haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyoongea, tayari Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeshatoa shilingi bilioni 98 kwenda kwenye afya, kuweza kufidia zile fedha ambazo zingepatikana kutoka kwa wadau, wenzetu wale ambao walikuwa wanachangia katika hiyo sekta. Tathmini hiyo inaendelea katika maeneo mengine, lakini pia na utoaji wa fedha utaendelea katika maeneo mengine yale ambayo yalikuwa yanahitaji fedha hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Afya ndiyo iliyoguswa zaidi. Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa usimamizi wa shughuli za Serikali wa Mheshimiwa Waziri Mkuu, imeendelea kutekeleza na tutaenda hatua zaidi ikiwemo kuwekeza fedha kwenye uzalishaji wa dawa zile ambazo tulikuwa tunapata kupitia wale wabia wetu, ziweze kuzalishwa ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye mpango wa maendeleo utakaosomwa katika hili Bunge; na bajeti itakayosomwa katika Bunge hili, sehemu hiyo ya fedha itaelekezwa kwenye viwanda vinavyozalisha dawa ndani ya nchi ili tuweze kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu, umri wake, uwezo wake na uwekezaji uliofanyika kwenye afya tunaweza tukajitegemea kumaliza Malaria, tunaweza kujitegemea kwenye TB, tunaweza tukajitegemea kwenye vitendanishi, na tunaweza tukajitegemea katika madawa mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari shilingi bilioni 98 zimeshakwenda na nyingine zitakwenda kwenye MSD ili kuweza kuhakikisha kwamba MSD inajitegemea, na hili jambo linaendelea. Fedha nyingine tutakaposoma Mpango na Bajeti, zitakwenda kwenye Bima ya Afya kwa Wote ili tuweze kujitegemea katika Sekta ya Afya kama ambavyo Mheshimiwa Rais ametoa kwenye maelekezo yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata sekta nyingine ambazo zimeguswa, niwahakikishie Watanzania, hapatakuwa na sekta ambayo itakosa fedha eti kwa sababu kuna Taifa mojawapo limebadilisha sera ambalo lilitakiwa lisaidie Mataifa yanayoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumeshaingia uchumi wa kipato cha kati, na tunaendelea kusonga mbele tutoke uchumi wa kati wa chini, twende uchumi wa kati wa juu. Kwa hiyo, hakuna sekta itakosa fedha kwa sababu kuna Taifa limebadilisha sera yake ya kusaidia Mataifa yanayoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutatengeneza mkakati wa kubana matumizi, tuondoe matumizi kwenye maeneo ambayo yana uhitaji usio mkubwa sana, tupeleke fedha kwenye maeneo ambayo yana matumizi yenye ulazima ikiwemo miundombinu, afya, elimu, maji, umeme pamoja na sekta nyingine zote kwa ujumla ikiwemo sekta za uzalishaji. Tutafanya hivyo na kazi hiyo tayari imefanyika, timu ya wataalamu imeendelea kuyafanya hayo. Tutayafanya hayo na Taifa ni lazima lisonge mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania imeshaingia kwenye kumbukumbu za kupanga jambo kubwa na kutekeleza. Moja, tulipanga kuhusu kutekeleza Mradi wa Umeme wa Mwalimu Nyerere. Tuliupanga ulikuwa mkubwa, ulikuwa unatisha, ulikuwa ndani ya misukosuko, lakini tumetekeleza na umekamilika na sasa unafanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tulipanga kutekeleza Mradi wa Reli ya Kisasa kweli kweli ambayo hata Mataifa makubwa mengine hayana mradi kama huo, tumeutekeleza. Sasa hivi zaidi ya kilometa 722 kazi yake inaonekana, na sehemu kubwa imeshaanza kufanya kazi, Dar es Salaam mpaka hapa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi pande zote zilizosalia, zina wakandarasi, na makabidhiano ya fedha na utiaji saini tunamalizia hatua za mwisho, na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya vipande vyote vinavyosalia, ziko hatua ya mwisho. Kwa hiyo, kuanzia huu mwaka wa fedha, fedha zitaanza kumiminika katika hivyo vipande kwa uhakika ili kuweza kuhakikisha kwamba miradi hiyo inakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu lile daraja kubwa la kuunganisha sehemu moja ya nchi yetu na sehemu nyingine, Daraja la Kigongo – Busisi (Daraja la Magufuli). Tumepanga na tumetekeleza, limeshakamilika na leo hii Waziri akipita pale hahitaji Mabuti, anapita na suti yake, pameshakuwa tayari kwa ajili ya matumizi. Hii ni miradi mikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunatekeleza Bomba la Mafuta ambalo Tanzania imetekeleza wajibu wake, upande wake ambao unatakiwa utekelezwe kwenye hilo Bomba la Mafuta. Kwa hiyo, hii ni mifano kwamba hili ni Taifa linalojitegemea, lenye kiongozi makini na wasaidizi wake makini kama Mheshimiwa Waziri Mkuu hapa na shughuli anazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa maeneo mawili yaliyotajwa, maji na barabara tumeongea na Mawaziri wa Kisekta. TARURA tumeongea na Mawaziri wa Kisekta. TAMISEMI, Kilimo, pamoja na sekta nyingine zote tumeshaongea na Mawaziri wa Kisekta. Tayari tumeshatoa fedha za TARURA, tumeshatoa fedha za maboma, tumeshatoa fedha za vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedgha zote tumeshazitoa na tutaendelea kutoa nyingine zinazotakiwa ili hiyo kazi yote ambayo Waheshimiwa Wabunge makini kabisa, Wawakilishi wa wananchi wa uhakika, wasio na mbambamba, mmesema humu ndani ya Bunge ili hizo fedha ziweze kufika na hiyo miradi iweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji huu unahitaji mapato, kwa hiyo, tutaongeza mapato. Tumekubaliana na Mamlaka ya Mapato kuongeza elimu kwa mlipakodi ili kuongeza compliance, kulipakodi kwa hiari kama Mheshimiwa Rais alivyokuwa ameelekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi juzi tulisaini Mkataba na Shirikisho la Mpira wa Miguu ili tutumie michezo kutangaza elimu ya mlipakodi. Tuna fungu letu ambalo huwa tunalitumia kwa elimu ya mlipakodi, tutalisambaza kuanzia michezo ya mashuleni, ili wanafunzi wale kuanzia wako shuleni; shule za msingi na sekondari waanze kujifunza uzalendo wa kulipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnakumbuka wakati tuko shule tulikuwa tunaimbishwa Kaburu Matata na tukamchukia kweli Kaburu. Hivyo hivyo, na uvamizi ule tuliuimba tukauchukia sana. Hata mlipakodi akiandaliwa hivyo kwamba kukwepa kodi ni jambo baya, watakapofika kuwa walipakodi, itakuwa hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulisaini mkataba na Federation, tutatumia ile. Tutavitumia vilabu vya Simba na Yanga, vina walipakodi wengi na wafuasi wengi. Sisi tunahitaji kodi, wao wana walipakodi, ili viweze kutusaidia katika kutoa elimu pamoja na michezo yote itumike katika kutoa masuala ya kuelimisha watu kulipa kodi kwa hiari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hata hivi sasa nawapongeza sana Simba, bado wana michezo ya Kimataifa, nawapongeze sana. Mimi siyo shabiki wa Simba, lakini ni kiongozi wa Simba. Nawapongeza sana Simba na ... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, muda wako umeisha. (Kicheko/Makofi)
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana Simba kwa kuwa bado wana michezo, wao pamoja na Yanga waende Mamlaka ya Mapato Tanzania ili waendeleze ule mkataba tuliokubaliana wa kutumia mpira wa miguu kutangaza elimu ya mlipakodi, na hivi Simba wataenda kucheza South Africa, waweze kupata na fungu la kuweza kuhakikisha wanaenda kuwatoa wale wenzetu kule, liwasaidie kuwatoa wale wenzetu kule ili waweze kuendelea kutangaza vizuri Taifa letu pamoja na hii kazi ambayo tunataka tutumie pia michezo kuweza kuelimisha walipakodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata taasisi nyingine zenye matangazo, mpeleke pale Simba, halafu wasaidiwe mafuta, waende kule, watatangaza hizo shughuli zenu ili waweze kuhakikisha wanapeperusha vyema bendera yetu. Tukirudi humu ndani nami nakuwa na sehemu ninazoshabikia, basi huko tutaongea tukiwa humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi/ Vicheko)