Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Naomba nimshukuru Waziri wangu wa Nchi, Sera, Bunge na Uratibu kwa kunipa fursa ili nami niweze kuchangia bajeti yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nianze kwa kuungana na Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kumpongeza Mheshimiwa Spika wa Bunge letu kwa umahiri wake na uchapakazi wake mkubwa ambao umeliwezesha Bunge letu kwenda vizuri.
Mheshimiwa Mweyekiti, pia, tumemwona Mheshimiwa Spika duniani akiwakilisha nchi yetu na kutuletea heshima, pongezi sana kwake. Pia, nampongeza na Mheshimiwa Naibu Spika na ninyi Waheshimiwa Wenyeviti mnaomsaidia Mheshimiwa Spika kwa kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati ya moyo wangu naomba sasa nimpongeze na kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake mahiri wenye kujali utu na pia kwa kuniamini mimi Ummy Nderiananga kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais na hii heshima kwangu ni jambo kubwa sana kwenye historia ya maisha yangu. Mheshimiwa Rais, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kukipongeza Chama chetu cha Mapinduzi kwa kumpa ridhaa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini na mgombea wake mwenza Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi; na kwa upande wa Zanzibar, Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kazi za viongozi wetu. Nchi yetu imepata mafanikio makubwa chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kipindi cha miaka minne tu, Mheshimiwa Rais ameonyesha kazi kubwa sana na tumeona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru Waheshimiwa Mawaziri mliochangia sekta mbalimbali, mmeonyesha namna Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa. Kwa hiyo, nawaomba Watanzania wote wanaotufuatilia, waendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais, tumpe nafasi akafanye kazi nyingine kubwa zaidi kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunawaahidi viongozi wetu, tutaendelea kuwapa ushirikiano, na tutaendelea pia kuwaombea kura maeneo mbalimbali na Mwenyezi Mungu atawajaalia Insha’Allah, watashinda kwa kishindo mwezi wa Kumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe pongezi kwa wasaidizi wanaomsaidia hii kazi nzuri Mheshimiwa Rais. Kwanza Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango kwa uchapakazi wake imara na maelekezo yake ambayo yameendelea kutusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nampongeza pia Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa uongozi imara na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, naye tunampongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naungana na Waheshimiwa Wabunge kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uchapakazi wake, umahiri wake, unyenyekevu na upole. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ofisini kwake Mheshimiwa Waziri Mkuu ameendelea kutupatia maelekezo na miongozo mbalimbali. Tunampongeza na sisi tunaofanya naye kazi, tunashuhudia kwamba yote Waheshimiwa Wabunge waliyokuwa wanayasema, ni kweli, nami binafsi nimeingia Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2020. Mheshimiwa Waziri Mkuu amenilea vizuri, nimeweza kufanya kazi chini yake, nimejengeka kiuongozi na niko tayari na ninaendelea kulitumikia Taifa letu. Ahsante sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nampongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Mashaka Doto Biteko kwa uongozi wake mahiri na kutuongoza vyema. Sambamba na utendaji kazi wake mzuri kwenye Wizara ya Nishati, tumemwona anavyochapa kazi, pamoja na maelekezo yake ambayo yamesaidia Ofisi yetu. Hata leo mnavyotuona, mkisemea vizuri Ofisi ya Waziri Mkuu, ni kwa sababu viongozi wetu hawa wapo na wanatuongoza vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uniruhusu kwa dhati ya moyo wangu nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Sera, Bunge na Uratibu, Mheshimiwa William Lukuvi. Huyu ni mentor wetu, ni senior, ni mwalimu wetu, amekuwa kiongozi mahiri, mwenye upendo na mlezi. Binafsi nimepata bahati ya kufanya naye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lukuvi ni moja ya hazina pia ya uongozi kwa nchi yetu. Ninakushukuru sana Mheshimiwa Waziri, ninakuombea afya njema, Mwenyezi Mungu aendelee kukubariki. Muda ukifika Mheshimiwa Waziri, basi Wanaismani waendelee kutupatia burudani kwa kukupa ushindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwashukuru Watendaji wetu. Katibu Mkuu Dkt. Jim James Yonazi; Naibu Katibu Mkuu, James Henry Kilabuko; Wakurugenzi wote na Wakuu wa Idara na Vitengo kwa kumsaidia kazi Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Sera, Bunge na Uratibu, Mheshimiwa William Lukuvi na kufanikisha utekelezaji mzuri wa majukumu ya ofisi yetu na bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na usimamizi na uratibu mzuri wa shughuli zote za Serikali. Tunawashukuru sana Watendaji wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uniruhusu niseme kwamba, mimi natokana na Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT). Naomba nitumie fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza viongozi wetu UWT kuanzia ngazi ya Taifa, Tanzania Bara na Zanzibar chini ya Mwenyekiti wetu mahiri, Mama Mary Chatanda na Makamu wake Mama Shomari; Katibu Mkuu, Dada Suzan Kunambi na Manaibu wao, wanawake wote wa UWT Mikoa, Wilaya, ngazi zote mpaka ngazi ya Mashina kwa kazi nzuri ambazo tumeendelea kushirikiana pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru pia kwa heshima mliyonipa binti yenu, na kwa kazi nzuri nyingi ambazo tumefanya pamoja katika maeneo mbalimbali kwa kipindi cha miaka mitano. Nawaomba kwa unyenyekevu mwendelee kuniunga mkono binti yenu muda utakapofika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wetu wa Nchi, Sera, Bunge na Uratibu, naomba niwashukuru pia na ninyi Kamati. Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge, Utawala, Katiba na Sheria inayoongozwa na wewe Mwenyekiti, Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama na Wajumbe wote wa Kamati kwa ushirikiano, ushauri na namna ambavyo mmeisimamia Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naishukuru Kamati yetu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI chini ya Mheshimiwa Mwenyekiti Elibariki Kingu na Wajumbe wote, tunawashukuru sana. Tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote, uchangiaji wao umetupatia faraja na msukumo wa kuendelea kumsaidia kazi Mheshimiwa Rais, ahsanteni sana, Mungu awabariki. Pia, nawashukuru Waheshimiwa Naibu Mawaziri na Mawaziri wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu hoja chache, nyingine Mheshimiwa Waziri wangu atakuja kuzimalizia. Kwanza ni kufikia malengo ya kidunia kupambana na UKIMWI hadi mwaka 2030, Serikali tunajipangaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa maelezo ya utangulizi ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha ambayo yametuwekea msingi wa kuonyesha kwamba nchi yetu hakuna litakaloshindikana, tutaenda vizuri. Kulikuwa kuna maneno hapa katikati kwamba sasa UKIMWI watu hivi na vile, lakini tunaenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia tuliandaa mpango wa uendelevu na uhimilivu wa kupambana na UKIMWI. Mpango huu tuliuzindua mwaka 2024 kwenye Siku ya UKIMWI kule Ruvuma na Mheshimiwa Makamu wa Rais ndiye aliyetuzindulia mpango ambao kidunia wanaita, sustainability roadmap ambayo lazima kila nchi itengeneze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi Tanzania tumefanya vizuri, tumeshauandaa, lakini tumeona mwelekeo mzuri. Wadau sasa wanaendelea kujitokeza kutuunga mkono kwenye hili eneo. Mheshimiwa Waziri wetu ameendelea kuturatibu na kutuambia hata kwenye mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI, mambo mengine ambayo siyo ya lazima tuyaahirishe, tufanye yale ambayo ni ya ulazima zaidi ili tuendelee kuhakikisha kwamba tunabana matumizi, lakini tunaenda vizuri. Kwa hiyo, nawahakikishia kwamba, kufikia 2030 nchi yetu tutakuwa tuko vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko hoja ya kuendelea kuwapatia dawa wafungwa walioko Magerezani. Tunaendelea vizuri na nakushukuru wewe na Kamati yako, tumeendelea kutembelea maeneo mbalimbali kuona afua za UKIMWI zinavyotekelezwa Magerezani. Hakuna mfungwa atakayekosa dawa chini ya Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tutaendelea kuwapa dawa, kuwapa huduma za kinga, kuwapa lishe na kadhalika ili waendelee vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la ufuatiliaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, tumeambiwa kufanya mambo ya monitoring and evaluation. Ofisi yetu chini ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi tumeendelea kufanya vizuri na ndiyo maana leo tunaripoti. Mheshimiwa Waziri Mkuu anasema, miradi imekamilika, reli ya SGR (Dar es Salaam – Dodoma) wote tumepanda tumeona. Pia, Mji wa Serikali tumefika 89%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tunaendelea kumalizia mfumo wetu wa ufuatiliaji na tathmini chini ya Mheshimiwa Waziri wa Sera, Bunge na Uratibu pamoja na e-GA ili kuwa na kitu kikubwa zaidi kitakachotuongoza kama nchi kwenye mambo ya ufuatiliaji na tathmini ya miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, hapa hapa kwenye monitoring and evaluation, tunakuja na application maalum. Tunatengeneza mfumo ambao utaitwa Kiongozi App, ambao utawafanya Waheshimiwa Mawaziri, Makatibu Wakuu, viongozi wote ndani ya Serikali kuweza kusomana na kuwa na information kiganjani wawe na taarifa. Unapoongelea mradi fulani, umefikia asilimia ngapi, tutakuja na hiyo na tunamshukuru Mheshimiwa Waziri wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, nawashukuru sana, Mwenyezi Mungu atubariki. (Makofi)