Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa ambayo umenipatia. Niungane na wenzangu kumpongeza sana, sana, sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi yake nzuri ambayo ameifanya ya mapinduzi makubwa na maendeleo makubwa ambayo ameipatia nchi yetu katika sekta zote. Tunashuhudia, vitu hivi vimefanyika kwa kipindi cha muda mfupi sana wa kipindi cha miaka minne. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza kwangu, namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kuturuzuku uhai, lakini pia kutuwezesha kufanya kazi kwa umahiri katika kumsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa imani yake kubwa ambayo ameiweka kwangu katika kipindi hiki ambacho ameniteua kuweza kumsaidia kuhudumu katika Ofisi ya Waziri Mkuu katika eneo la Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazidi kumshukuru Mheshimiwa Rais, lakini pia tunampongeza, kwani amekuwa ni kiongozi shupavu, mahiri, na ni Rais ambaye ameonyesha busara kubwa sana katika kuamua na kufanya maamuzi yake. Pia, ni Rais ambaye ameonyesha uwezo mkubwa wa uvumilivu na weledi. Vivyo hivyo ni Rais ambaye amekuwa na mapenzi makubwa sana kwa Watanzania bila kuwabagua na amepeleka maendeleo katika kila kona ya nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hatuna budi, na hatuna cha kumpa zaidi ya kumwombea sana kwa Mwenyezi Mungu ampe afya njema, umri, riziki na uwezo wa kuendelea kulihudumia Taifa letu, nasi tuzidi kumwombea na kumpigia kura nyingi sana katika uchaguzi ujao kwa ajili ya mafanikio ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili naomba nichukue fursa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ambaye ni Makamu wa Rais wetu kwa huduma nzuri anayoifanya kwa ajili ya Taifa hili na kumsaidia Mheshimiwa Rais. Sambamba naye yupo Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye sisi ndio Kiongozi wetu katika Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kweli ni kiongozi wa mfano wa aina yake. Ni mpole, mpenda watu, sijawahi kumwona amekasirika katika kipindi changu chote cha miaka minne ya kufanya kazi ofisini, lakini zaidi hata pale ilipotokea hali ambayo ina tafrani, amekuwa na utulivu lakini alilenga zaidi katika kutafuta suluhu kuliko kuongeza tatizo zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kustahimili maelekezo yake na uongozi wake bora katika ofisi hiyo Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kweli huna baya mbinguni na duniani tunayaona. Mungu akubariki sana, na sisi tutaendelea kuwa nawe katika kuhakikisha tunakusaidia katika majukumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameambukiza pia wema na upendo, lakini pia uchapakazi umemwambukiza msaidizi wake Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye naye pia kwa wema wake na maelekezo yao kwa pamoja wametusaidia sana katika kufanya kazi hizi kwa ubora na viwango ambavyo vinatakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wapo viongozi wetu Mheshimiwa Waziri Mzee Lukuvi, lakini pia yupo Mheshimiwa Ridhiwani. Hawa viongozi nao wanaambukizana wema, Mheshimiwa Lukuvi kwa kweli tangu nimfahamu amekuwa msaada mkubwa sana kwetu sisi vijana na kuiga aina ya uongozi kwake, vivyo hivyo katika maelekezo ambayo amekuwa akiyatoa amefanya kazi kubwa na nzuri nasi kwa kweli tunakushukuru Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yupo Mheshimiwa Waziri wangu Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, wananchi wa Chalinze tunawashukuru sana kwa kweli, sisi tunasema tumelamba dume, kwani wametuletea kiongozi huyu kijana shupavu ambaye sisi tunamwita kaka mkubwa ofisini, amekuwa mchapakazi, amekuwa kiongozi bora, mzuri lakini ni muungwana sana. Huyu mzee naye pia ni kama vile anaambukizwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, kila wakati ana-smile, sijawahi kuona amechukia na anarahisisha sana kazi kwa kweli. Katika ofisi yetu ameweza kufanya kazi vizuri na amekuwa pia akitoa miongozo na maelekezo inayopelekea kupata mafanikio katika ofisi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri weledi wake, maarifa, ujuzi na ubobevu wake kwenye maeneo mbalimbali. Mimi hapa mdogo wake huwa nateleza tu kwenye majukumu, kwa sababu njia anazonionyesha ni sahihi na tunafanya kazi kwa ukamilifu zaidi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru pia ofisi yetu, Makatibu Wakuu, Ndugu Jim Yonazi lakini Mama yetu Mary Maganga pamoja na Naibu Katibu Mkuu Zuhura Yunus na viongozi wengine ambao wapo kwenye hii ofisi. Mama huyu ni shupavu, mwenye weledi mkubwa, ameongoza vizuri ofisi hii na ametusaidia sana katika kufikia mafanikio haya na ni mtu wa facts and figures na wakati wote ameongoza Ofisi ya Waziri Mkuu katika mafanikio kwa kutekeleza maelekezo na maagizo mahususi ambayo yanatolewa na viongozi wetu hawa wa juu ambao nimewataja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru pia viongozi katika Mifuko yetu ya Hifadhi ya jamii ambayo wamekuwa wakisimamia vizuri sana Wakurugenzi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii NSSSF, PSSSF, WCF, OSHA, CMA na taasisi nyingine zote zilizo chini ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwa kweli uwezo wao ni mkubwa, wamekuwa mahiri na hii inathibitisha uteuzi wa Mheshimiwa Rais, ni wa jicho la mwewe lisilokosea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwapongeze sana kwa kweli viongozi hawa, wamekuwa wakifanya kazi kubwa. Pia, Wakuu wa Idara na Taasisi na Vitengo chini ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wamekuwa wakifanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pongezi kubwa kwa Mheshimiwa Spika wetu Dkt. Tulia Ackson. Daktari huyu mahiri, mmbobevu wa Sheria na Mzamivu kwenye maeneo mengi ya kiutawala na uongozi, amekuwa kiongozi wa mfano siyo tu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bali pia ndiye Rais wa Mabunge yote Duniani ambayo kazi yake ameifanya kwa umahiri mkubwa. Sisi tunaiga wema wake, lakini pia umahiri wake katika kufanya kazi hii. Vivyo hivyo Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Wenyeviti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Mheshimiwa Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Mheshimiwa Mama Fatma Toufiq pamoja na Waheshimiwa Wajumbe wote kwa miongozo yao na shughuli kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya. Kwa sababu ya muda natambua, lakini pia nashukuru upande wa Chama cha Mapinduzi, hapa tunao Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini. Hawa ndio zao, mimi ni mtoto wao na tunda, nimetokana nao, nawashukuru sana kwa kunifikisha hapa. Nashukuru familia yangu kama ilivyotajwa, lakini kwa sababu ya muda, naona nina hoja ambazo napaswa kuzijibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye hoja kwa haraka na kwa sababu ya muda, naomba hotuba yangu au maelezo yangu ya kujibu hoja kama jinsi ambavyo tumewasilisha yote yaingie katika Kumbukumbu za Bunge (Hansard).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja ya kwanza ilihusu zaidi kuhusu Serikali itoe vitendea kazi kwa vijana wanaomaliza mafunzo ya uanagenzi. Serikali imekwishafanya hivyo na tutaendelea kufanya hivyo. Tumeshatoa tayari vifaa vyenye thamani ya shilingi 1,000,900,000 ambavyo vimeenda kununua vifaa hivi vilivyonufaisha vikundi zaidi ya 2,700, ambapo vijana 1,977 wamekuwa wanufaika. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026 tunatarajia kupata fedha tena shilingi milioni 637 ambazo zitaenda kuwasaidia vijana ambao wanafuzu mafunzo haya ya uanagenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ilihusiana na programu ya ukuzaji ujuzi katika programu hii. Hoja ilikuwa inasema, tutoe elimu. Tunayo furaha Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na maelekezo ya utekelezaji wa Mheshimiwa Waziri Mkuu tumeendelea kutoa elimu katika vyombo vya habari kupitia platform zote za media na social media na matangazo yamekuwa yakifanyika na tumekuwa tukitenga fedha zaidi shilingi 138.1 kwa ajili ya utoaji wa elimu kwa umma na pia zaidi kutoa taarifa ya mafunzo haya yanayofanyika chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa kuna hoja ya Serikali iongeze vyuo vya mafunzo ya uanagenzi. Moja ya hatua ambazo Serikali imefanya ni pamoja na kuongeza Vyuo vya VETA ambavyo vinatumika nchini kote, vinajengwa katika Halmashauri zetu za Wilaya, lakini hivyo hivyo vyuo vya maendeleo ya jamii tayari vimeshajengwa na vinafanyiwa maboresho hata pale kwangu Shinyanga tulipata shilingi milioni 650 kwa ajili ya maboresho ya chuo chetu cha maendeleo ya jamii. Vyuo binafsi navyo pia vimekuwa ni sehemu ya kuhakikisha kwamba mpango huu wa Serikali unatimizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika upande wa pili wa mafunzo mwaka wa fedha 2025/2026 tutaenda kuwafikia zaidi ya wanafunzi 8,000 ambao wataenda kwenye vyuo 52 hapa nchini kwa ajili ya kupata mafunzo katika Wilaya 48. Hii ni hatua kubwa ambayo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuonyesha. Pia katika maeneo mengine kwa haraka nikienda hata masuala ya ajira kwa ujumla, kwenye masuala ya ajira ni mjumuiko, ni pamoja na mpango wa utoaji wa mikopo, ajira za vijana zimeendelea kutolewa katika sekta ya umma hata katika sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya upanuzi wa maeneo mengi ya ajira, kwa mfano, uwekezaji umeongezwa nchini na kufanya maboresho ya sheria ili kuvutia uwekezaji; na kufanya maboresho ya sheria ya kuratibu ajira za wageni. Pia katika hatua nyingine katika eneo hilo kwenye suala la ajira tumeendelea kufanya na kukuza maeneo mbalimbali, kutenga maeneo ya uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetenga maeneo ya kuzalisha na kuuza bidhaa ndani na nje ya nchi, lakini pia punguzo la tozo kwenye maeneo ya baishara yanayoweza kutoa ajira zaidi, tumefanya kwenye maeneo ya mikopo ukiacha 4:4:2 zinazotolewa na Halmashauri zote nchini, tumeenda kwenye hatua nyingine ya kila Wizara ya Kisekta kwa maagizo ya Mheshimiwa Rais na maelekezo ya utekelezaji ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhakikisha kila Wizara inazalisha ajira nchini, kuweza kuhakikisha kwamba katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Wizara ya Miundombinu kwenye ujenzi kote unapofanyika hata maeneo yale ya miradi ya mkakati; Bwawa la Mwalimu Nyerere, SGR huko tulipata ajira na mafanikio, tulipata ajira zaidi ya milioni 8,084,000 zaidi hata ya lile takwa la ilani ambalo lilikuwa linahitajika kwamba tupate ajira milioni nane. Haya ni mapinduzi makubwa ambayo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya kilimo, tunao mpango wa Building a Better Tomorrow ambapo vijana wanapata mafunzo na tunawapa maeneo maalumu kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu. Wizara ya Bashe inafanya kazi hiyo, Wizara ya Madini napo pia tunatoa mafunzo kwa wachimbaji na pia tunawakopesha vifaa ambavyo vinawasaidia kwenye mpango wa Mining for Brighter Tomorrow kupitia Mheshimiwa Antony Mavunde Waziri mwenye dhamana husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, zaidi ya shilingi bilioni 10 zilitolewa kwa ajili ya kuwasaidia vijana hao, na pia boti zilitolewa na Mheshimiwa Rais zaidi ya 100, ufugaji wa samaki kupitia vizimba, lakini pia unenepeshaji mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara nyingine ambayo inafanya kazi hiyo, hata Wizara ya Michezo, ili kuongeza wigo wa ajira. Tunatambua michezo inaajiri zaidi, Mheshimiwa Rais anajenga viwanja karibia nchi nzima kwenye maeneo yale ambayo ni ya kimkakati. Arusha unajengwa uwanja utakaobeba zaidi ya watu 22,000. Pia ameanza kutoa fedha, ukiacha zile za Kapu la Mama, kuna fedha zaidi ya shilingi bilioni tano zinatolewa kwa ajili ya ukopeshaji wasanii na watu wengine ili kutoa fursa za vijana hao kwenye hayo maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna thamani ya fedha zaidi ya shilingi trilioni 2.7 zilitolewa kupitia Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ulionufaisha wananchi zaidi ya milioni 24 ikiwa ni kuwawezesha walio kwenye biashara na kwenye maeneo ya kukuza mitaji, na pia kuongeza fursa mbalimbali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Mikopo napo pia huko ni uwezeshaji wa vijana. Zaidi ya shilingi bilioni 788 zinatolewa Wizara ya Elimu kwa ajili ya kuwasaidia vijana ambao wapo kwenye mfuko wa mpango wa elimu. Pia kuna Samia Scholarship zinatolewa yoyote ambaye atafanya vizuri kwenye masomo ya sayansi. Mheshimiwa Rais ameweka mpango wa kuwafadhili bure ili vijana wetu waweze kusoma na kujipatia ajira ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kwenye ajira, tumefanya. Mheshimiwa Waziri wangu, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete ana mpango wa kuingia mikataba na nchi zaidi ya nane ya kupata ajira katika maeneo na Mataifa mbalimbali na tumeanza, mfano na nchi tatu; nchi za Uarabuni na Qatar na maeneo mengine ambapo zaidi ya vijana 500 wameshakwenda kwenye hatua ya kwanza ikiwa ni pamoja na mjumuisho wa mafunzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ni mengi, muda ni mchache, lakini tunatambua haya yote yamewezekana kwa sababu wapo watendaji wenye dhamira safi. Mheshimiwa Rais amekuwa akifanya hivyo na kuhakikisha anatuelekeza katika kuwahudumia Watanzania bila ajizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nizidi kushukuru nafasi yako wewe binafsi, na pia tuzidi kushukuru kwamba Mheshimiwa Rais ajenda za uchaguzi anazo kwa sababu amegusa maisha ya Watanzania, na pia yeye mwenyewe ni mgombea mahiri ambaye hana mshindani hapa nchini, ameji-organize vizuri kupitia Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo Mheshimiwa Rais ana-communication strategy za maana za kushinda uchaguzi; tatu, ana rasilimali mali za kusaidia kushinda uchaguzi; na nne, ana rasilimali watu ambao wanaweza, sisi tuweze kushinda uchaguzi. Wale majirani zetu kule ni nyumba ya njaa. Ukiona nyumba haina hata paka, ujue kuna njaa. Tuwape pole, na tutawashinda katika uchaguzi ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja na Mheshimiwa Rais tumpe kura za ndiyo, ndiyo. Mungu awabariki sana. (Makofi)