Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Ridhiwani Jakaya Kikwete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chalinze

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kufika siku ya leo tukihitimisha hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Mheshimiwa Spika, naomba kutumia nafasi hii kukushukuru kwa kunipa fursa ya kusimama mbele ya Bunge lako ili kuchangia hoja iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu na pia, kutoa maombi ya fedha nikiunga mkono.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kuunga mkono hoja, na pili, kwa kipekee kabisa, naomba uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, kwa kutimiza miaka minne tangu aapishwe kuliongoza Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi chake tumeshuhudia maendeleo makubwa sana ambayo Serikali imetekeleza chini ya uongozi wake. Hakika amethibitisha kuwa, yeye ni kiongozi bora, imara, shupavu na mahiri kuliongoza Taifa letu na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020. Kwa hakika anafaa kuongezewa muda kuliongoza Taifa letu kwa miaka mingine mitano tena. Namwombea Mwenyezi Mungu amjalie afya na siha njema ili aweze kutekeleza majukumu yake ya kuliongoza Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kipekee naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini na kuniteua kuwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya kazi, ajira na wenye ulemavu. Kwa kuwa, hii ni mara yangu ya kwanza nasimama nikiwa Waziri wa Wizara hii ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, nataka nitoe salamu kubwa za shukrani kwake yeye, lakini pia, na wote wanaomsaidia na kumshauri katika kufanya kazi hizi ambazo zimeendelea kufanyika katika Wizara yetu na miongozo mbalimbali anayotupa.

Mheshimiwa Spika, pia, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango, kwa miongozo mbalimbali anayotupa, na pili, kwa jinsi ambavyo anaendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Spika, vilevile, naomba kutumia nafasi hii kwa fursa ya kipekee, kumshukuru sana Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Mbunge, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye yeye pia ni kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni kwa ushirikiano mkubwa na miongozo anayonipa ambayo inatuwezesha mimi na wenzangu ndani ya Wizara kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ninaendelea kukuombea Mungu akujalie heri na Wanaruangwa wakusikie na wakuchague tena kwa kura nyingi kwa sababu, nchi na Bunge bado linaendelea kukuamini. Mheshimiwa Waziri Mkuu, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Dotto Mashaka Biteko, Mbunge, Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, naye kwa kuendelea kutuongoza vyema katika majukumu yetu tunayotekeleza.

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana kwa ushauri wake, namshukuru sana kwa miongozo yake. Kama ilivyo kwa Waziri Mkuu, naye ninamtakia kila la heri kwa Wanabukombe, kama ambavyo walimleta, naomba wamrudishe tena ili tuendelee kuchapa kazi ya kuendelea kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, niruhusu nikupongeze wewe binafsi, Spika wetu na Rais wa Mabunge Duniani. Kwa hakika, kwa lugha ya mtaani, wanasema mpira unaupiga mwingi sana. Mwenyezi Mungu akujalie heri katika kutekeleza majukumu yako, lakini pia, nataka nikuhakikishie, sisi kama Wabunge wenzako, tutaendelea kuhimizana na wewe kusimamia majukumu yetu na kuhakikisha kwamba, Mbeya inakupendekeza, haikuachi ukaelea.

Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu nimshukuru Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa namna ya pekee wanavyoendelea kuliongoza Bunge letu kwa umahiri mkubwa sana. Nawaombea afya njema, lakini pia, nao nawatakia heri katika hayo yanayokuja hapo mbele.
Mheshimiwa Spika, vilevile naomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana Waziri Mwenzangu, Senior Wiliam Vangimembe Lukuvi, Mbunge wa Jimbo la Ismani, Waziri wa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu.

Mheshimiwa Spika, naomba nimwahidi Mheshimiwa Lukuvi, ushirikiano mzuri wa kutosha katika kumsaidia yeye, na pia, kumsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu katika kutekeleza majukumu yake, naye pia namshukuru sana na nimtakie kila la heri mzee wa kazi huko jimboni na Wanaismani wajue kwamba, tunaendelea kumhitaji. Amekuwa mwongozo wetu, sisi wengine tumefaidika naye tukiwa umoja wa vijana, tukiwa chipukizi na hata leo tuko ndani ya Bunge tunaendelea kufaidika naye katika miongozo yake. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, vilevile naomba uniruhusu nimshukuru Mheshimiwa Patrobas Katambi, Mbunge wa Shinyanga Mjini na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu; yeye pamoja na Mheshimiwa Ummy Hamis Nderiananga, Mbunge wa Viti Maalum, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu kwa ushirikiano mkubwa wanaotupatia mimi na mwenzangu Mheshimiwa Lukuvi katika kutekeleza majukumu yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli, msaada wao ndiyo ambao unasimamisha mafanikio makubwa unayoyaona leo yanatokea katika ofisi chini ya uongozi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Tunawashukuru sana. Tunawatakia kila la heri katika michakato inayokuja, lakini sisi ndani ya Wizara tumeridhishwa, tunashukuru na tunaendelea kuwaombea heri wananchi wawarudishe pia, ili muweze kutekeleza majukumu ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, naomba kutumia nafasi hii kuwashukuru sana Mawaziri wenzangu wa Wizara mbalimbali kwa ushirikiano mkubwa wanaotupatia katika kutekeleza majukumu haya. Pia, nitumie fursa hii kwa kipekee kabisa kumshukuru Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Marry Maganga, pamoja na Dkt. Jimmy James Onazi, Katibu Mkuu Sera, Bunge na Uratibu na Naibu Makatibu wetu wawili; Bi. Zuhura Yunusi na Dkt. James Kilabuko pamoja na watumishi wote wa taasisi tunazozisimamia kwa ushirikiano mkubwa wanaotupa katika kutekeleza majukumu yetu.

Mheshimiwa Spika, pia, naomba kuwashukuru wadau wote wa maendeleo tunaoshirikiananao katika kutekeleza majukumu yetu. Hapa naomba niwataje kwa uchache. Kwanza ni Mashirikisho ya Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Baraza la Taifa la Ushauri wa Watu Wenye Ulemavu, Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), NGOs za ndani na za Kimataifa bila kuwasahau wadau wakubwa ILO, UN Women, UNICEF na UNFPA kwa kuwataja kwa ufupi.

Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa na kipekee naomba nitumie nafasi hii kuishukuru sana familia yangu, wazazi wangu na hasa mke wangu kipenzi, Mama Aziza, watoto wetu na wananchi wa Jimbo la Chalinze ambao kwa kweli, ushirikiano wao mkubwa wanaotupa umetuwezesha kutimiza majukumu haya vizuri. Nataka tu nitambue uongozi bila kuwataja kwa majina, watu wa Chalinze ambao wapo upande wako wa kushoto pale juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu hoja za Kamati na Waheshimiwa Wabunge, nami naomba niungane na Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi wa Maendeleo ya Jamii, ikiongozwa na Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum na Mwenyekiti wa Kamati yetu, kwa ushauri na ushirikiano mkubwa aliotupatia wakati wa kuchambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Mheshimiwa Spika, pia, nataka niipongeze Timu ya Simba Sports kwa kufanikiwa kuingia nusu Fainali ya Kombe la Washindi Afrika. Naomba nitumie nafasi hii tu kuwakumbusha, wenzenu walicheza fainali, ninyi mjipange mkachukue kombe. Mpira ni ushindani, mpira ni uwekezaji, lakini mwisho wa siku mpira ni furaha na mpira ni burudani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuwahakikishia kuwa, maoni na ushauri uliotolewa kwa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Fungu 65 na Fungu 15 kwa mwaka 2025/2026 yote tumeyazingatia. Pia, naomba kutoa shukrani za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango na ushauri wao ambao kwa kiasi kikubwa umelenga kuboresha utekelezaji wa majukumu ya ofisi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee, naomba kuwatambua na kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hotuba ya Waziri Mkuu kwa kuongea na kwa maandishi. Naomba orodha yao iingie kwenye Hansard kama ilivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 118(2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Juni, 2020 inayohusu kujadili utekelezaji wa Bajeti ya Wizara, naomba sasa kwa heshima na taadhima uniruhusu nitoe ufafanuzi wa baadhi ya hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge walizichangia na kutaka ufafanuzi, na hoja nyingine zitafafanuliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu atakapokuwa anahitimisha hoja yake.

Mheshimiwa Spika, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii ilikuwa na hoja saba zilizotolewa kwa niaba yao na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati yetu. Nataka kutumia nafasi hii kwanza kuishukuru Kamati, kama nilivyoeleza mwanzo kwa michango yao mizuri, na pili, kwa kumbukumbu na maelekezo ambayo sisi kama Wizara, tumeyachukua. Nataka kulihakikishia Bunge na Kamati yako kuwa, michango yao yote imechukuliwa na itafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, maelezo mengine yalishatolewa mwanzo na Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna maeneo naomba uniruhusu niweze kujazia nyama na mengine kutoa ufafanuzi zaidi ili Bunge lako lisiwe na muda mrefu wa kusikiliza repetition ya maeneo hayo badala ya kuendelea mbele kujadili hotuba ya bajeti iliyo mbele yako.

Mheshimiwa Spika, katika maeneo ya kuhakikisha kwamba, Watanzania wanapata fursa ya kupewa nafasi ya kufanya kazi nje ya nchi; pamoja na maelezo mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri nataka kuelezea kwamba, Serikali imekamilisha mfumo wa ESMIS ambao unasaidia kuunganisha taarifa za wenzetu wanaokwenda kufanya kazi nje, ili waweze kuunganishwa na mifumo ya kibenki, ikiwezekana hapa Tanzania, ili zile remittances zinazokuja ziweze kujulikana.

Mheshimiwa Spika, leo hii katika moja ya jambo kubwa ambalo Bunge lako katika michango yao limeelezwa kwa sauti ya juu sana ni hesabu ndogo ya marejesho ambayo yanaletwa nchini kwetu. Nataka niwahakikishie, moja ya kipengele ambacho kimekuwa ni changamoto kwetu ni kukosekana kwa mfumo sahihi ambao tunaweza tukapata taarifa ya fedha kiasi gani zinaletwa, na watu wangapi wanafanya nini na kiasi gani kinapatikana?

Mheshimiwa Spika, nataka tuendelee kulihakikishia Bunge lako kwamba, mfumo huu ambao nimeusema hapa utaanza kufanya kazi katika mwaka huu wa fedha. Tumeshakamilisha mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya kuendesha mashtaka na kuweka kumbukumbu kwa migogoro ya wafanyakazi. Yaani hapa nazungumzia OCMS, ambayo kwa lugha ya Kiingereza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa, dakika mbili, malizia. Kengele ya pili imeshagonga.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Dakika kumi?

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa, dakika mbili.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Dakika mbili! Dakika kumi zimekwisha!
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, nimekuongeza dakika mbili kwa sababu, mbili nilishakupa. Yaani muda wako ulikuwa umekwisha, nikakuongeza dakika mbili na sasa nimekuongeza mbili umalizie.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, sawa. Kwa niaba ya Serikali, naomba yale majibu yetu yote tuliyokuwa tumeyaandaa, yaingie kwenye Hansard, ili tusije tukaacha ombwe kwa yale maswali au michango mizuri iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba niseme tena kwamba, naunga mkono hoja iliyotolewa. Baada ya hapo, kwa ruhusa yako, naomba sasa nikae. (Makofi)