Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ismani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana tena hapa katika Bunge lako Tukufu tunapoelekea kuhitimisha mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, vilevile, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kusimama mbele ya Bunge hili Tukufu, ili kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge walizotoa wakati wa kuchangia hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge. Kwa sababu hiyo, nafikiri utanipendelea kidogo maana hoja za Bunge ni ngumu hapa.
Mheshimiwa Spika, kipekee nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuniamini na kuniteua kuwa mshauri wake, lakini pia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu. Ni heshima kubwa kwangu kutumikia nafasi hizi, na ni dhamira yangu kuhakikisha kuwa, nafanya kazi kwa weledi, uadilifu, uaminifu na unyenyekevu mkubwa huku nikizingatia maslahi mapana ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kutolea ufafanuzi hoja za Waheshimiwa Wabunge, naomba nianze kwa kutoa salamu za pongezi na shukrani kwa viongozi wetu wakuu wa Kitaifa kwa namna wanavyoiongoza nchi yetu kwa ufanisi weledi na dhamira ya kweli ya kuwatumikia Watanzania. Nianze kwa kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Sukuhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kutuongoza kwa ustadi mkubwa na kutoa miongozo madhubuti katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2025.
Mheshimiwa Spika, tathmini ya utekelezaji wa Ilani katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inaonesha kuwa, ilani imetekelezwa kwa zaidi ya 90% katika sekta na nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii. Huu ni ushahidi wa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wake na dhamira yake ya dhati ya kuwatumikia Watanzania, ndiyo chachu iliyokifanya Chama cha Mapinduzi kumteua, Rais wetu mpendwa, kuwa mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uchaguzi wa Mwaka 2025. Tunaendelea kumwombea, Mwenyezi Mungu aendelee kumjalia afya njema, hekima na nguvu tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025.
Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wenzangu watakubaliana nami kuwa uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan umejikita katika mabadiliko chanya, dhamira ya dhati ya maridhiano yakiongozwa na falsafa ya 4R na maendeleo ya kweli, kwa kila Mtanzania. Kupitia uongozi wake, Taifa letu linaendelea kustawi, kuaminika na kusonga mbele kwa kasi, hivyo wote twendeni tukampe kura zote za ndiyo kwenye Uchaguzi Mkuu ujao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa utendaji kazi wake na kumsaidia Mheshimiwa Rais kutuletea wananchi maendeleo. Mheshimiwa Makamu wa Rais amekuwa kiongozi imara, mnyenyekevu, shupavu, mwenye busara na mchapakazi katika kutekeleza mikakati mbalimbali ya kisera inayolenga kuboresha ustawi wa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile, namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa juhudi zake za kudumisha Umoja wa Kitaifa na kuleta maendeleo endelevu kwa Wananchi wa Zanzibar. Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi ni kiongozi thabiti anayefanya kazi kwa bidii na kwa ushirikiano mkubwa.
Mheshimiwa Spika, natumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuendelea kuaminiwa na Chama cha Mapinduzi, kuwa mgombea wake kwa nafasi ya Urais wa Zanzibar kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Uteuzi huu ni ushahidi tosha kwamba ameitekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2025 kwa upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, naomba pia kumshukuru sana Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naungana na Waheshimiwa Wabunge wote ambao 80% mmempongeza humu ndani kwanza, kwa maelekezo na miongozo aliyonipa katika kutekeleza majukumu yangu ya kila siku. Pili, namshukuru na kumpongeza kwa kuongoza shughuli za Serikali hapa Bungeni kwa umahiri na kutoa miongozo yenye manufaa kwa Taifa.
Mheshimiwa Spika, aidha, namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ya bajeti ambayo ameiwasilisha kwa weledi na ufasaha mkubwa. Hotuba hiyo imebeba vipaumbele muhimu vinavyoakisi mahitaji ya Taifa letu na itaendelea kutupatia mwelekeo sahihi katika kutekeleza majukumu ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kutoa hotuba kama mnavyojua Mheshimiwa Waziri Mkuu alielekeza Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi iliyosomwa kwenye Mkutano Mkuu itolewe kwa wananchi kwa siku saba mfululizo. Taarifa hii imerushwa kwenye vyombo vyote vya habari ili wananchi waweze kuona na kusikia kabla yeye hajatoa taarifa hii.
Mheshimiwa Spika, vilevile, nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Dotto Mashaka Biteko, Mb, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, kwa maelekezo na miongozo anayonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Ninyi nyote ni mashahidi, Mheshimiwa Dkt. Dotto Biteko ni kiongozi mpole, mpenda ushirikiano na mnyenyekevu. Waheshimiwa Wabunge wote tunamjua vizuri, Mungu ambariki.
Mheshimiwa Spika, kipekee, nakupongeza wewe binafsi kwa uongozi imara usioyumba wa Bunge letu, pia kwa ufanisi mkubwa unaouonesha katika nafasi ya Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). Nakupongeza na kushukuru sana kwa sababu hata u-chief whip wangu bila ushirikiano wako hauna maana. Kwa hiyo, mafanikio yangu yanatokana na ushujaa wako wa kukaa kwenye kiti. Nakushukuru sana, wewe ni Spika bora kabisa.
Mheshimiwa Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Mussa Azan Zungu kwa style yake maalum ya kuliongoza Bunge. Pongezi kwa Mheshimiwa Naibu Spika wa Bunge kwa namna anavyokusaidia ipasavyo katika kuliongoza Bunge letu Tukufu na style yake, uongozi wenu unahakikisha kuwa majukumu ya Bunge yanafanyika kwa ufanisi na majadiliano yanakuwa ya manufaa kwa maendeleo ya Taifa letu. Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kuwajalia afya njema, nguvu na hekima ili mwendelee kulitumikia Taifa letu
Mheshimiwa Spika, aidha, nampongeza sana Ndugu Baraka Leonard, huyu Katibu wa Bunge hana maneno mengi, lakini Bunge limetulia. Pongezi kwa Katibu wa Bunge kwa usimamizi bora wa utendaji wa Bunge, anasimamia vizuri utendaji na Bunge letu limetulia, na ninyi wote ni mashahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nawapongeza pia Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge pamoja na Kamati ya Uongozi kwa kazi kubwa ya kumsaidia Mheshimiwa Spika katika kuongoza Bunge hili. Nikisema Kamati ya Uongozi, maana yake ni Wenyeviti wote wa Kamati na Wajumbe wao.
Mheshimiwa Spika, sambamba na salamu hizo za pongezi kwenu viongozi wetu wa Serikali na Bunge, naomba pia nitumie fursa hii adhimu kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Steven Masatu Wassira, mkongwe wa siasa kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, pamoja na Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi kwa kuidhinishwa na Mkutano Mkuu wa CCM kuwa Mgombea Mwenza wa Kiti cha Urais katika uchaguzi Mkuu ujao. Namwomba Mwenyezi Mungu aendelee kuwabariki viongozi wetu na wagombea hawa.
Mheshimiwa Spika, naungana na Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwashukuru Wajumbe wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Utawala, Katiba na Sheria; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi; na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa michango yao ambayo imekuwa na msaada mkubwa katika kuboresha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, pamoja na bajeti ya Mfuko wa Bunge. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote walioshiriki katika jambo hili.
Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa nawashukuru viongozi wenzangu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu. Napenda kumpongeza sana Mheshimiwa mdogo wangu Ridhiwani Jakaya Kikwete, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, kwa kazi nzuri anayoifanya. Ni mdogo wangu sana, na ninyi watu wa Chalinze mjue kwamba huyu kijana anafanya kazi kubwa sana. Msije mkauza bunduki mkanunua rungu.
Mheshimiwa Spika, vilevile Mheshimiwa Ummy Hamis Nderiananga, Naibu Waziri wangu katika Ofisi yangu ya Sera, Bunge na Uratibu, pamoja Mheshimiwa Patrobas Paschal Katambi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Sote tunatoa ushirikiano mkubwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Jim Jonas, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu; Mary Maganga, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu; Dkt. James Kilabuko, Naibu Katibu Mkuu na Ndugu Zuhura Yunus Abdallah, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira; Wakurugenzi na Wakuu wa Idara wote wanaotusaidia katika kutekeleza majukumu chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru na wadau mbalimbali ambao wanatusaidia na wanashiriki na sisi katika kutekeleza majuku yetu katika ofisi zetu.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Ismani na Watanzania kwa ujumla kwa imani kubwa wanayoendelea kuwa nayo kwangu na kwa Chama cha Mapinduzi. Pia, nawashukuru kwa kuendelea kuniamini kuwa mwakilishi wao na kuniunga mkono katika utekelezaji wa majukumu yangu ya kila siku. Naomba ushirikiano huo uendelee.
Mheshimiwa Spika, naelewa kuwa dhamana waliyonikabidhi ni kuwahudumia na kuwatumikia kwa moyo na uaminifu, uwazi na uwajibikaji. Ninaahidi kuendelea kushirikiana nao kwa karibu kama walivyonizoea kusikiliza changamoto zao na kuzitatua kwa bidii na hekima. Ombi langu kwao ni lile lile, kwamba mwezi Oktoba mwaka huu 2025 tumpatie kura nyingi za “ndiyo” Mgombea Urais aliyedhaminiwa na Chama cha Mapinduzi. Kwa sababu hata mimi Mbunge wao bila yeye nisingesimama hapa.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani zangu kwa familia yangu ambayo imekuwa nguzo imara katika maisha yangu binafsi na safari yangu ya kisiasa inayoongozwa na mke wangu mpendwa Germina Lukuvi. Natambua kwamba mafanikio yangu yasingewezekana bila uvumilivu, maombi na support yao ya hali ya juu.
Mheshimiwa Spika, naomba niungane na Mheshimiwa Waziri Mkuu kutoa pole kwa wananchi walioathirika na majanga mbalimbali, ikiwemo mafuriko yanayotokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini kote.
Mheshimiwa Spika, vilevile nawashukuru wananchi na wadau wote ambao wanashirikiana Serikali katika kukabiliana na majanga hayo na kutoa misaada kwa waathirika. Moja ya eneo lililopata majanga haya hivi karibuni, ni Jimbo la Ismani. Tarafa ya Pawaga, ambapo Mheshimiwa Waziri Mkuu alielekeza Ofisi yangu itoe msaada na iende ikashirikiane na wananchi wa Pawaga.
Mheshimiwa Spika, nadhani mliwaona wasaidizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu wakifika huko na kutoa msaada. Hiyo ndiyo Ofisi inayosimamiwa na Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa. Tumekwenda pia sehemu mbalimbali kama vile Musoma, Hanang na sehemu nyingine.
Mheshimiwa Spika, baada ya salamu hizo, naomba nitoe ufafanuzi kidogo katika maeneo machache. Kwa Tume ya kudhibiti UKIMWI, TACAIDS, kulikuwa na hoja ambazo zimeulizwa na Waheshimiwa Wabunge juu ya Serikali kuongeza kasi ya elimu na kuhamasisha wananchi kupima ili kujua hali zao za maambukizi. Ushauri umepokelewa.
Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ilisema kwamba Serikali iendelee kutoa elimu kuhusu upimaji wa virusi vya UKIMWI na kuhamasisha matumizi ya dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI hususani kwa vijana.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua Madhubuti za kueleimisha jamii hususan vijana kuhusu VVU na UKIMWI pamoja na matumizi ya dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI. Hizo hatua nadhani wote kwa sasa tunazijua.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Joseph Mhagama (Mwenyekiti), Kamati ilitoa hoja kwamba Serikali ijiwekee malengo ya ukusanyaji maduhuli ambayo yanaakisi uwezo wa ukusanyaji wa hali halisi ya vyanzo vya mapato. Ufafanuzi wa hoja; Ofisi ya Waziri Mkuu ilikadiriwa kukusanya mapato ya shilingi bilioni 12 kwa mwaka huu unaoishia mwezi Juni. Makusanyo hayo yamezingatia uhalisia na uwezo wa vyanzo vilivyopo ikilinganishwa na makadirio ya shilingi bilioni 19 kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Zakaria na Waheshimiwa Wabunge wengine wametoa hoja kuwa, Serikali ihakikishe kwamba fedha za miradi namba 4.4.2.9 (Programu ya Kilimo na Uvuvi unatekelezwa kikamilifu ili kuwa na tija kwa Taifa. Tumetoa semina kwa Kamati, lakini tunakubaliana na hoja hii. Tutaendelea kusimamia hili jambo ili liwe na tija.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hoja hizi zilizotolewa kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, sisi wote kama Bunge tunajua kuwa moja ya kazi kubwa tunayoifanya hasa ofisi yangu katika kumsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu ni uratibu wa shughuli za Serikali na Bunge.
Mheshimiwa Spika, leo mchana tumeshuhudia Waheshimiwa Mawaziri wakitoa hoja na kujibu baadhi ya hoja za kisekta. Sisi kazi yetu ni kuratibu. Kwa hiyo, nawapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri wenzangu wote kwa michango yao yote waliyoitoa ambayo imepokelewa vizuri sana na Waheshimiwa Wabunge, wananchi na Watanzania. Michango ambayo imeboresha na kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge ambao walikuwa wanachangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, michango yao ndiyo michango yetu katika ofisi yetu kwa sababu sisi kazi yetu hatufanyi, wanafanya wao, lakini sisi tunafanya kazi ya uratibu, nataka kuwahakikishia kuwa mkiona yale mengine hayakujibiwa, watayajibu kwenye hotuba zao kwa sababu wote mtawasikiliza sasa. Baada ya Waziri Mkuu kutoa mwongozo leo, kila Waziri atasimama hapa kueleza sekta yake, na bado watajibu hoja zenu zilizobaki kutokana na hotuba zao.
Mheshimiwa Spika, nnaomba nishukuru sana ushirikiano wa idara mbalimbali; Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wanafanya kazi kubwa na ninyi mashahidi. Vilevile, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bunge, nimeshasema hapa, likiongozwa na Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wake, Wenyeviti wa Kamati na Sekretarieti yake ikiongozwa na bingwa kabisa Katibu wa Bunge, ndugu yetu Baraka. Nawapongeza sana kwa sababu mimi ni sehemu yao.
Mheshimiwa Spika, mimi ni Kamishina na ninajua Wajumbe wa Kamisheni tunavyofanya kazi, ninawashukuru sana. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Uongozi, najua tunavyowajibika kumsaidia Mheshimiwa Spika. Nawaomba tu tuendelee kumsaidia Mheshimiwa Spika, kama mnavyomjua ili aweze kutimiza majukumu yake, lakini pia tumwombee ili huku Mbeya waendelee kumwelewa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, naomba nihitimishe tu kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote na kuwatakia kila la heri. Huu ni mwanzo tu wa kusoma bajeti, na hii ni bajeti ya kwanza. Kwa hiyo, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge muwe wavumilivu, sasa kazi imeanza.
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa Wizara zitakuja kueleza mafanikio ya Dkt. Samia Suluhu Hassan katika miaka minne ya utekelezaji na kutoa taarifa kwa wananchi wa Tanzania kupitia kwenu. Mtapewa nafasi ya kutoa ushauri kwa Serikali pamoja na haya ambayo yamesemwa leo na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, huu ni mwanzo tu, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu amefungua mlango, na sasa ndiyo kazi imeanza, tunaanza kusikiliza hoja mbalimbali za Wizara. Waheshimiwa Wabunge, mtapata nafasi ya kusikiliza na kutoa michango yenu kwa niaba ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kurudia shukrani zangu tena kwa…
SPIKA: Dakika moja, malizia Mheshimiwa.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: …kwa Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na viongozi wote kitaifa pamoja na Waheshimiwa Wabunge. Nataka kuwahakikishia ushirikiano wenu mkubwa katika kutimiza majukumu yenu mkiwa hapa Bungeni na sehemu nyingine, kwa sababu kwa upande wa Serikali, mimi ndiye msaidizi wenu ninayefanya shughuli za Bunge pamoja na shughuli za Serikali.
Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa uvumilivu wa kutuvumilia sana sisi wasaidizi wake, na ninawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge. Shukrani mlizompatia Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni za kweli. Ni mtu msikivu, yuko hivyo hivyo. Huwa naona hapa hata akina Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, wanamuudhi hapa nyuma, lakini hakasiriki. Huwa wanakuja kumchokoza hapa…
SPIKA: Haya, ahsante sana Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, baada ya maelezo haya mafupi, nakushukuru sana na ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kuipokea vizuri hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja na kuunga mkono. (Makofi)