Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Kassim Majaliwa Majaliwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, ahsante sana, nawashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kutuwezesha kukutana katika siku hii muhimu ya kuhitimisha mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake na Mfuko muhimu wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2025/2026 tukiwa buheri wa afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siku ya tarehe tisa mwezi huu wa Nne nilipokuwa nawasilisha hoja hii, nilikupongeza sana ukiwa haupo. Nirudie leo kukupongeza sana wewe mwenyewe binafsi kwa kazi nzuri unayoifanya ya kuliongoza Bunge hili kwa weledi mkubwa na umahiri mkubwa. Watanzania wanajua, Wanambeya nao wanajua. Nakuombea kila la heri ili uendelee kutekeleza majukumu yako kwa tabia hiyo hiyo, weledi huo huo na umahiri ulionao.

Mheshimiwa Spika, wewe pamoja na Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge mmefanya kazi nzuri kwa kipindi chote cha miaka minne kuliongoza Bunge hili kwa umahiri mkubwa na weledi mkubwa. Wamesimamia mijadala kuhusu hoja mbalimbali na wamesimamia mjadala juu ya hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana ndugu yetu Komredi Baraka, Katibu wa Bunge na watumishi wote wa Bunge kwa kazi nzuri ya kutoa huduma zinazowezesha Bunge hili kutekeleza majukumu yake vizuri. Hongera sana na tunamkushukuru sana Komredi Baraka.

Mheshimiwa Spika, aidha, nawashukuru na kuwapongeza Wenyeviti na Wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kwa michango yao. Ni ukweli usiopingika kwamba, maoni pamoja na ushauri wao wakati wote umekuwa ukileta manufaa makubwa kwenye hoja ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Dotto Mashaka Biteko, Mbunge, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa usaidizi wake muhimu na mzuri. Hakika yeye pamoja na Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, Mbunge na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu; kwa pamoja na Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Mrisho Kikwete, Mbunge na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na Wenye ulemavu, wameendelea kutumikia vizuri Ofisi yetu ya Waziri Mkuu na ushauri wao umeendelea kuleta masilahi mapana.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuendelea kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Johari Hamza, Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushauri wake na miongozo yake ya kisheria ndani ya Serikali yetu. Hakika mpaka sasa tunaendelea vizuri.

Mheshimiwa Spika, vilevile namshukuru Mheshimiwa Ummy Nderiananga, Mbunge wa Viti Maalum na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulia Sera, Bunge na Uratibu kwa pamoja na Mheshimiwa Patrobas Katambi, Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mawaziri wote wa sekta, Naibu Mawaziri kwa kuchangia hoja ya Waziri Mkuu wakati wa mjadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika nawashukuru Makatibu Wakuu. Nianze na Mheshimiwa Dkt. Jim Jonas, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu; na Bi. Mary Maganga, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. Wameungana pamoja na Naibu Makatibu Wakuu akiwemo Dkt. James Kilabuko anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu na Bi. Zuhura Yunus anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu. Wakuu wote wa idara, taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Wakala wa Serikali kwa ushirikiano mkubwa na kujitoa kwao katika kufanikisha majibu ya hoja za Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, kipekee nawapongeza watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, watumishi wa taasisi zote na Ofisi ya Bunge kwa kujituma na kufanya kazi kwa weledi mkubwa kuanzia kipindi cha maandalizi ya hotuba ya bajeti hadi leo tunapohitimisha mjadala huu wa hoja ya Waziri Mkuu. Ahsanteni sana kwa kuifanya kazi yenu vizuri na kuufanya mwenendo shughuli za Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa mwepesi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa dhati ya moyo wangu, napenda kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote kwa michango yenu. Hoja na michango yenu imekuwa muhimu sana kwenye ofisi yetu na kwa hakika inaakisi maeneo yote muhimu yaliyohitaji kuimarishwa zaidi katika suala zima la kuhudumia wananchi na kufanya uboreshaji kwenye utendaji wa Serikali na namna ya kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali imezingatia michango yao na katika utekelezaji itatoa kipaumbele kama ambavyo imeainishwa katika Mpango wa Bajeti wa Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge 103 walichangia mjadala wa hoja ya Waziri Mkuu. Kati yao 100 walichangia kwa kuzungumza na watatu walichangia kwa maandishi. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja ya Waziri Mkuu. Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa muda, naomba uridhie nisiwataje moja kwa moja kwa majina yao na badala yake majina yao yaingizwe kwenye Hansard. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na mjadala wa hoja ya Waziri Mkuu, sote tumewasikia Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri, wakitoa majibu na ufafanuzi wa hoja nyingi zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa baadhi ya hoja zinaendelea kufanyiwa kazi na Waheshimiwa Mawaziri, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali itawasilisha majibu yote ya hoja ambazo zimekuja mbele yenu na wamezitoa kwa maandishi kwa wakati wote tutakapokuwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe pongezi za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwanza kwa kutimiza miaka minne ya kuiongoza nchi yetu kwa mafanikio makubwa. Pili, nyote ni mashahidi kuwa katika kipindi Cha miaka minne ya uongozi wake, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi imetekelezwa kwa kiwango kikubwa kama ilivyoelezwa wakati nikiwasilisha hoja ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa pamoja na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa kumsaidia vyema Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutekeleza majukumu yake na hasa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (Chama Tawala) ambacho kwa sasa kiko madarakani.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kukumbusha baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hiki cha miaka minne ya uongozi wake na mafanikio hayo ni pamoja na haya yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ni kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Sambamba na kudumisha hali ya amani, utulivu, pamoja na mshikamano wa wananchi wa Taifa hili, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amewezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, mafanikio makubwa yamepatikana katika utekelezaji wa miradi ya huduma za jamii na miradi ya kimkakati, hususan katika sekta za elimu, afya, maji, kilimo, ujenzi, nishati, mawasiliano na uchukuzi.

Mheshimiwa Spika, mafanikio hayo tunayoyapata katika utekelezaji wa ilani, ni ya kupigiwa mfano. Bila shaka kila mwananchi ni shahidi wa jambo hili. Kila eneo katika nchi hii limefikiwa na wananchi wamekuwa mashahidi kwa miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao. Hakika Mheshimiwa Rais anastahili pongezi na tumpongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha sera na sheria mbalimbali ili kuweza kuweka mazingira bora ya kuwawezesha wananchi kiuchumi. Suala la sera na sheria limewezesha kutenga 30% ya manunuzi ya umma kwa wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu. Pia, kuratibu na kuweka mazingira bora kwa vikundi na huduma ndogo za kifedha pamoja na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji ikiwemo sekta ya madini, mafuta na gesi.

Mheshimiwa Spika, uanzishwaji wa mifuko ya programu mbalimbali za uwezeshaji wananchi unatokana na mahitaji ya kiuchumi kwa maendeleo ya nchi yetu. Mifuko iliyopo imeweza kutoa jumla ya shilingi trilioni 3.5 kwa wanufaika zaidi ya milioni 24. Kati ya wanufaika hao, wanawake ni zaidi ya milioni 11 na wanaume ni zaidi ya milioni 13.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya mifuko ya programu hizo ni pamoja na mikopo ya halmashauri ya 10% kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu. Pia, ipo Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora na Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kwa Vijana. Tunayo Programu za Kukuza Viwanda Vidogo na Kati, Programu ya Kuimarisha Uchumi na Mama Samia na Mfuko wa Dhamana wa Wajasiriamali Wadogo.

Mheshimiwa Spika, mifuko na programu za uwezeshaji wananchi zinazoratibiwa na Serikali zinatoa fursa ya mikopo kwa riba nafuu kwa mtu mmoja mmoja na vikundi na uzalishaji mali. Serikali itaendelea kutekeleza na kusimamia mikakati ya kutoa elimu kwa wananchi kupitia njia mbalimbali ikiwemo maonesho, makala, vyombo vya habari na vituo vya uwezeshaji ili kuongeza uelewa kuhusu fursa zilizopo kwenye mifuko na programu hizo.

Mheshimiwa Spika, la tatu ni mifumo ya utoaji haki. Kama nilivyoelekeza kwenye hotuba yangu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekuwa kinara katika kuboresha misingi ya utoaji haki hapa nchini. Aidha, ameimarisha mifumo ya utoaji haki hususan matumizi ya TEHAMA kwenye taasisi za hakijinai.

Mheshimiwa Spika, mifumo hii imerahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wakati, kupunguza gharama kwa wananchi wanyonge na wasiokuwa na uwezo wa kupata huduma za Kimahakama hasa waliopo kwenye maeneo ya pembezoni. Kwa wakati huu tunaendelea na mkakati wa huduma za kisheria zinazotolewa bure kwa Watanzania kote nchini.

Mheshimiwa Spika, vilevile, Mheshimiwa Rais ameongeza idadi ya Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu pamoja na Mahakama za Rufani. Ongezeko hilo linachangia moja kwa moja katika kupunguza mlundikano wa kesi, hivyo, kurahisisha utoaji haki. Hali kadhalika amefanya maboresho ya miundombinu ya Mahakama kuanzia ngazi ya Mahakama ya Mwanzo hadi Mahakama Kuu ikiwemo ujenzi wa Mahakama pamoja na nyumba za Majaji.

Mheshimiwa Spika, mtakumbuka mnamo tarehe 05 Aprili, mwaka huu 2025 Mheshimiwa Rais aliweka historia kwa kuzindua jengo la kwanza la Makao Makuu ya Mhimili wa Mahakama ya Tanzania kwa kipindi cha miaka 104 tangu kuanzishwa kwake. Uzinduzi huo ni mwendelezo wa dhamira yake njema ya kuboresha miundombinu ya Mahakama hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo la nne ni ukusanyaji wa mapato, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio yaliyopatikana katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuimarisha ukusanyaji wa mapato. Ukusanyaji huo umewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali hapa nchini. Mathalan, katika kipindi cha mwezi Julai hadi Machi mwaka wa fedha 2024/2025 Mamlaka ya Mapato Tanzania imekusanya kiasi cha shilingi trilioni 24.05, sawa na ufanisi wa 103.62% ya lengo letu.

Mheshimiwa Spika, aidha, makusanyo hayo ni ya kiwango cha juu kabisa kufikiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kipindi kama hicho tangu kuanzishwa kwake. Kiasi hicho ni sawa na ongezeko la 77% ikilinganishwa na kiasi cha shilingi trilioni 13.59 zilokusanywa katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

Mheshimiwa Spika, ufanisi katika makusanyo uliofikiwa ni matokeo chanya ya kutekeleza kwa vitendo maagizo na maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kuboresha mazingira ya ulipaji kodi. Serikali inawapongeza walipakodi nchini kwa kutimiza wajibu wenu, kwa kulipa kodi stahiki kwa wakati bila shuruti na kuendelea kuunga mkono kizalendo juhudi za Serikali za kuleta maendeleo nchini kwani kodi yetu ndiyo maendeleo yetu. Pongezi nyingi kwa wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa wafanyakazi wamekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu. Nitumie fursa hii kuwapongeza kwa dhati wafanyakazi wote nchini. Vilevile, nawapongeza waajiri, viongozi, vyama vya wafanyakazi na wadau wote kwa kuendelea kuheshimu haki na utu wa wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) katika kuhakikisha kuwa misingi ya haki ya wafanyakazi inazingatiwa. Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba wafanyakazi wataendelea kupata stahiki zao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Mheshimiwa Spika, hili ninalizungumza kwa sababu mafanikio yote ya Serikali yanatokana na kazi kubwa inayofanywa na wafanyakazi hawa kwenye sekta ya umma na sekta binafsi. Kwa sasa tunafanya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yatakayofanyika siku ya tarehe 01 Mei ambayo yanafanyika kila mwaka, na mwaka huu maadhimisho hayo Kitaifa yanatarajiwa kufanyika Mkoani Singida.

Mheshimiwa Spika, maadhimisho hayo siyo tu kielelezo cha mshikamano na heshima kwa wafanyakazi, bali pia yanadhihirisha dhamira ya dhati ya kuhamasisha utoaji haki za wafanyakazi, ustawi, mazingira bora ya wafanyakazi na kupokea changamoto za wafanyakazi kupitia maandamano yatakayopita mbele ya mgeni rasmi.

Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa wafanyakazi wote nchini kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi, maarifa, uadilifu na kwa moyo wa kujituma katika kuwapokea, kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi kwa wakati. Hivyo, nawatakia kila la heri katika kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani.

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie ajenda mbili zilizopo mbele yetu kwa sasa. Kwanza, matumizi ya nishati safi, sote tunafahamu kuwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa kinara kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. Jitihada zake na hatua mbalimbali anazochukua zimeongeza hamasa kwa nchi yetu katika matumizi ya nishati safi. Hakika anastahili pongezi kwa maono yake na sasa tuko kwenye kampeni ya kuhakikisha kwamba Watanzania wanabadilisha matumizi kutoka nishati chafu kwenda nishati safi ya kupikia.

Mheshimiwa Spika, tulianza na taasisi na sasa tunaenda mtu mmoja mmoja. Kufikia mwaka 2033 ni matarajio yetu kwamba Watanzania wote watakuwa wanapikia nishati safi kwa 80%. Tumeshuhudia Waheshimiwa Wabunge mkishiriki katika kuhamasisha na kugawa mitungi ya gesi ya kupikia kwa wananchi kwenye maeneo yenu. Hongereni sana Waheshimiwa Wabunge kwa jitihada hizo za kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika ziara nilizozifanya maeneo mbalimbali nchini, nimeshuhudia baadhi ya taasisi zikitumia nishati safi ya kupikia kama ilivyoelekezwa na Serikali. Hata hivyo, taasisi nyingine hazijatekeleza maelekezo hayo. Hivyo, nitumie nafasi hii kusisitiza taasisi zote zenye kuandaa chakula cha watu zaidi ya 100 kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii ya Bunge lako Tukufu kuwakumbusha wadau wote ikiwemo Wizara za Kisekta, taasisi za umma, Tawala za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa, sekta binafsi na Watanzania wote kuendelea kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mheshimiwa Spika, vilevile, taasisi za Serikali zihakikishe matumizi ya mapato yanayotokana na uvunaji wa miti, usafirishaji na biashara misitu yanaelekezwa katika kufanikisha mkakati huu wa uhifadhi wa mazingira. Kwa upande mwingine, nitoe wito kwa wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi.

Mheshimiwa Spika, ajenda ya pili, maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ambapo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imeshakamilisha uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura awamu ya kwanza katika mikoa yote 31 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nitumie nafasi hii kuwapongeza Watanzania, hakika wamejitokeza kwa wingi kwenye zoezi hilo kwa ajili ya kujiandikisha na kufanya maboresho ya taarifa zao.

Mheshimiwa Spika, katika kuendelea na maandalizi hayo, Tume inatarajia kufanya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa awamu ya pili mwezi Mei. Hatua hiyo itaenda sambamba na zoezi la uwekaji wazi wa daftari kwa ajili ya kuwawezesha wapigakura ambao wameandikishwa kukagua taarifa zao kwenye kuta za matangazo.

Mheshimiwa Spika, hivyo basi, nitoe rai kwa Watanzania waliopitiwa na zoezi la awamu ya kwanza kutumia fursa hiyo kwenda kujiandikisha na kuboresha taarifa zao awamu ya pili pindi Tume itakapotangaza.

Mheshimiwa Spika, nawasisitiza wapigakura ambao tayari wameandikishwa waende kwenye vituo vya kuhakiki majina yao kwenye madaftari ambayo wamewekwa wazi. Tume imekamilisha maandalizi ya kanuni za uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka huu 2025.

Mheshimiwa Spika, Kanuni za Maadili ya Uchaguzi za Mwaka 2025 na maelekezo mbalimbali ya uchaguzi yametolewa. Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa kuna hali ya usalama, amani, utulivu, uwazi na haki katika kipindi chote cha uchaguzi mpaka siku ya upigaji kura.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nijibu hoja chache ambazo zimejitokeza na ambazo hazikuguswa na Waheshimiwa Mawaziri. Natambua kuwa Waheshimiwa Wabunge wametoa hoja nyingi na zote ni za muhimu kwa maslahi mapana ya Taifa letu. Hoja nyingi zimetolewa ufafanuzi na Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri wakati walipokuwa wanachangia hoja zao.

Mheshimiwa Spika, kutokana na ufinyu wa muda, baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge zitajibiwa kwa maandishi na nyingine zitatolewa ufafanuzi na Waheshimiwa Mawaziri wakati watakapokuwa wanawasilisha bajeti zao za Wizara zao, ambapo pia nao watawajibika kujibu hoja mbalimbali pamoja na zile ambazo hazikupata nafasi kujibiwa kupitia hotuba yangu hapa.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe maelezo juu ya utoaji wa fedha kwa wakati. Fedha ambazo zimeenda kufanya maendeleo na matumizi mengi na kuziwezesha Wizara, Taasisi na Idara za Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Serikali yetu imeendelea kutoa fedha ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na matumizi mengine. Sote tumeshuhudia utekelezaji wa miradi mbalimbali kutokana na fedha zilizotolewa kwenye maeneo yetu ya uwakilishi.

Mheshimiwa Spika, hivyo, nilihakikishie Bunge lako Tukufu kuwa kulingana na mpango kazi, Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na tumebaki na miezi mitatu ya kukamilisha bajeti yetu. Tutahakikisha robo hii ya mwaka iliyobaki tunamalizia kupeleka fedha kulingana na mahitaji ya Wizara hizo.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili juu ya uharibifu wa miundombinu iliyoharibika kutokana na mvua, kama nilivyoeleza kwenye hotuba yangu kuwa nchi yetu imepata athari kubwa kutokana na mvua kubwa za El-Nino na Kimbunga Hidaya, athari zilizojitokeza ni pamoja na vifo, majeruhi, upotevu na uharibifu wa mali pamoja na miundombinu hususan barabara, madaraja, ma-culvert.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilichukua hatua mbalimbali za kurejesha hali ya miundombinu hiyo iliyoharibika ili huduma nyingine ziweze kuendelea. Hatua hizo ni pamoja na kutafuta fedha za dharura, kuweka mfumo wa manunuzi na kutafuta wakandarasi na kuanza ujenzi wa miundombinu iliyoharibika katika mikoa yote hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa shilingi bilioni 72.15 kwa ajili ya kurejesha miundombinu ya dharura. Vilevile, imetoa shilingi bilioni 868.56 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kudumu kwenye wilaya 139 za Tanzania Bara ambapo miundombinu yake iliharibiwa kabisa. Miundombinu hiyo inajumuisha madaraja 63, barabara zenye urefu wa kilometa 827, mitaro yenye urefu wa kilometa 84, na ma-culvert 225 yamefanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tumeshuhudia mvua kubwa kwenye mikoa mbalimbali hapa nchini. Mvua hizo zimesababisha athari kwenye miundombinu ikiwemo Barabara ya Dar es Salaam hadi Lindi. Miundombinu hiyo ni pamoja na daraja la dharura lililopo kwenye barabara ya mchepuko katika eneo la Somanga ambapo daraja jipya linajengwa.

Mheshimiwa Spika, napenda niwafahamishe Watanzania na Waheshimiwa Wabunge wote wakiwemo Wabunge wa Mikoa ya Kusini kuwa ujenzi wa Daraja jipya la Somanga ambalo litakuwa na urefu wa meta 60 pamoja na barabara unganishi ya kilometa 1.7 unaendelea vizuri na haujaathirika. Hadi sasa mkandarasi amekamilisha ujenzi wa nguzo 27 kati ya 43 wa Daraja hilo na kwa ujumla mradi umefikia 38% ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba, 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa mkataba, madaraja mengine yanayopitiwa na mikondo ya maji kama vile Matandu, Mavuji, Nakiu na Mto Mbwemkuru yana wakandarasi, pindi mvua hizi zinazoendelea kunyesha kutoka Mkoani Morogoro na Misitu ya Selous zikishapungua ujenzi utaendelea kwa kasi. Kesho asubuhi saa mbili nitakuwa kule Somanga kukagua hali hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kukamilisha miundombinu iliyoharibiwa ili irejee katika hali yake ya kawaida na wananchi waendelee na huduma zao za kawaida. Vilevile, nitoe rai kwa wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya mvua zinazoendelea kunyesha ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza.

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie sherehe za Muungano. Tarehe 26 Aprili, 2025 tutaadhimisha miaka 61 ya Muungano wa nchi yetu ambao umeendelea kuwa chachu ya mafanikio tunayoyashuhudia leo. Nchi yetu iliungana pamoja na viongozi wetu shupavu, yaani Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume kuona haja ya kuliunganisha Taifa letu ili kuweza kuipata Tanzania yenye nguvu tunayotaka na tunayoiona leo.

Mheshimiwa Spika, maadhimisho ya mwaka huu yatakuwa na kauli mbiu, “Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Muungano wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa; Shiriki Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.” Hivyo, niungane na Watanzania wenzangu kuliombea heri na fanaka, Taifa letu huku nikiendelea kuwasihi kudumisha umoja, mshikamano na amani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, aidha, nawaomba Watanzania wote, kutumia sherehe hizi katika kukumbushana na kuelimishana juu ya umuhimu wa uwepo wa Muungano huu. Tuulinde na tuutetee. Muungano huu unaenda kulinda amani yetu, umoja na undugu wetu kwa pamoja na kufanya kazi kwa bidii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu michezo, nchi yetu imeendelea kupiga hatua katika medani za michezo kwa kuweza kufuzu katika mashindano mbalimbali ambayo yameijengea heshima nchi yetu. Kupitia uwekezaji uliofanywa na mwanamichezo nambari moja nchini, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, umeziwezesha timu zetu za Taifa kufuzu katika mashindano mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara yenye dhamana na michezo, Baraza la Michezo Tanzania na vyama vyote vya michezo nchini kwa kusimamia maono ya Mheshimiwa Rais. Maono hayo yamewezesha timu za Taifa kufuzu na kushiriki mashindano mbalimbali kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Taifa Stars imefuzu AFCON 2025, Taifa Stars hiyo hiyo imefuzu michezo ya CHAN 2025. Twiga Stars imefuzu mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake inayoitwa WAFCON. Ngorongoro Heroes chini ya miaka 20 wamefuzu AFCON 2025. Serengeti Boys chini ya miaka 17 wamefuzu AFCON mwaka 2024.

Mheshimiwa Spika, Timu ya Taifa ya Mpira Ufukweni imefuzu BSFCON 2024. Kushiriki mashindano ya Futsal ya wanawake yanayofanyika nchini Morocco na kufuzu kwa Timu ya Taifa ya Cricket chini ya miaka 19 katika mashindano ya Kombe la Dunia. Tujipongeze wenyewe kwa matokeo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya ni mafanikio makubwa sana kwa nchi yetu. Sote tunapaswa kujivunia hatua hii na kuendelea kumuunga mkono Rais wetu ambaye ameonesha nia thabiti ya kuhakikisha kwamba Taifa letu linapata heshima kupitia michezo.

Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu kama ambavyo uliniruhusu siku ya tarehe 9 Aprili, 2025 nilipokuwa nasoma Hotuba ya Bajeti na ilikuwa ndiyo siku Timu ya Simba ilikuwa inacheza mchezo wa robo fainali na niliitakia heri kwenye mchezo wao. Nitumie nafasi hii sasa niwapongeze wawakilishi pekee wa nchi yetu na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati waliosalia kwenye michuano mikubwa ya Kimataifa Barani Afrika, (CAF - Confederation Cup) timu ya Simba Sports Club toka Mtaa wa Msimbazi Jijini Dar es Salaam kwa kufuzu hatua ya nusu fainali kwa kuiondosha timu ngumu ya Al-Masry kutoka nchini Misri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa, naomba nimpongeze mlinda mlango wa Simba Moussa Pinpin Camara kwa kuokoa mikwaju miwili mizito ya penati iliyoiwezesha Simba kushinda. Naipongeza sana Timu ya Simba kwa ushindi huu na tunawatakia heri katika mechi inayofuata ya nusu fainali, na nina imani watafika hatua ya fainali na hatimaye kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza kwa kaulimbiu iliyosema, “Hii Tutavuka” na sasa kauli ya kuingia nayo kwenye mashindano ya nusu inasema, “Hatuishii Hapa.” Hiyo ndiyo kaulimbiu mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, nitoe shukrani kwa Bunge lako Tukufu. Ninapoelekea kuhitimisha niendelee kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuturuzuku rehema ambayo tumeipata ya kujenga utulivu, kusikilizana na kuweza kujadiliana kwa misingi iliyozingatia umoja, mshikamano na kuheshimiana.

Mheshimiwa Spika, Bunge hili limetia fora, limejenga heshima na limejijengea historia kubwa ya kuweza kujadili masuala mbalimbali ya Kitaifa kwa ushauriano mkubwa kwa heshima ya hali ya juu na kuhakikisha kwamba Taifa letu linasonga mbele.

Mheshimiwa Spika, kipekee narudia tena kukushukuru na kukupongeza wewe mwenyewe, Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa kusimamia vema majadiliano na hoja hii. Pia namshukuru Katibu wa Bunge na Watumishi wa Bunge kwa huduma nzuri pia na Waheshimiwa Wabunge wenyewe kwa michango yenu kwa kuishauri Serikali na Serikali pia kupitia Mawaziri, Naibu Mawaziri na Watendaji wetu ndani ya Serikali kwa kupokea ushauri na kuutekeleza vilivyo na hatimaye kuifanya Serikali kuwa Serikali pendwa. Hakika usimamizi wa miongozo yenu imeweza kuhitimisha mjadala huu.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru kwa dhati ya moyo wangu tena Wabunge wenzangu wote kwa namna ambavyo mmeweza kuijadili hoja hii na kujitoa kwenu katika kuishauri Serikali. Maoni na ushauri mlioutoa umepokelewa kwa uzito mkubwa kabisa na Serikali itayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba Bunge lako Tukufu liridhie na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zilizo chini yake na Mfuko wa Bunge kama nilivyowasilisha katika hoja yangu ya tarehe 09 Aprili, 2025.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)