Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Same Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kukushukuru kunifanya mchangiaji wa kwanza na nianze kwa kusema naunga mkono hoja kwa sababu, labda nitasahau baadaye. Hotuba yangu ya leo ambayo ni Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, na wote tunaelewa TAMISEMI ndiyo suluhisho la maisha ya Watanzania, Mheshimiwa Waziri amesema hivyo, ninaomba niigawe mara tatu.
Mheshimiwa Spika, nitaanza kwa shukurani kwa Serikali; pili, nitasema na Serikali kwa dhati kabisa na kwa unyenyekevu mkubwa. Tatu, kama nafasi itatosha nitamwambia Mheshimiwa Rais jambo fulani kubwa sana, akiwa ndiye kiongozi mkuu wa nchi hii.
Mheshimiwa Spika, nianze kwa shukurani kwa Serikali. Kwanza, Waheshimiwa Wabunge niwakumbushe kwamba, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliingia madarakani tarehe 19 Machi, 2021. Kwa hiyo, sasa hivi tunzungumza kwamba, Mheshimiwa Rais Samia amemaliza kipindi cha miaka minne. Hakuna Mbunge hata mmoja atakayesimama hapa ndani aseme Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Sita haikufanya kazi kubwa sana, hayupo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba niseme ukweli. Ninatoka Mkoa wa Kilimanjaro, una majimbo tisa na kila Mbunge wa Jimbo la Mkoa wa Kilimanjaro anajivunia kazi zilizofanywa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipoapishwa ile tarehe 19 Machi, alimtuma Waziri Mkuu jimboni kwangu baada ya mimi kulalamika sana kuhusu ubovu wa jimbo langu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alifika tarehe 24 mwezi wa tisa, mwaka 2021. Waheshimiwa Wabunge ukimuona Waziri Mkuu amekuja kwako, kama ni Mbunge wa Jimbo, ambaye uko makini ni lazima utachukua nafasi hiyo kusema matatizo ya wananchi wako wote. Yote utayasema, nilisema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati huo Waziri Mkuu amekuja jimboni kwangu nilikuwa nina kituo cha afya kimoja, Kituo cha Ndungu, kilikuwa hakina hata mortuary ya kuhifadhi maiti. Baada ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuingia madarakani naomba niwaambie ukweli, hapa niliposimama, upande wa afya, jimbo langu lina sura gani?
Mheshimiwa Spika, kwanza, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Serikali ya Awamu ya Sita walinijengea Kituo cha Afya cha Mamba Miamba, nikajengewa Kituo cha Afya cha Mtii. Hapa ninapozungumza ninajengewa Kituo cha Afya cha Vunta. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa mnione mimi ambaye Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipoingia sikuwa na kituo cha afya hata kimoja, leo nina vituo vya afya vitatu. Ameniletea ambulance tatu, ameniwekea mortuary kwenye Kituo cha Afya cha Ndugu. Hivi wananchi wanataka tusimsifu Mheshimiwa Rais Samia? Hapana, anastahili sifa. Waheshimiwa, wananchi huko nje na wote wanaotusikiliza ninaomba niseme kwa nguvu zote, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya makubwa sana kwa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ninaomba niseme na Serikali. Hii nchi ina majimbo korofi, lakini katika majimbo korofi, naomba nirudie, Jimbo la Same Mashariki ni jimbo korofi. Jimbo lina tarafa tatu; tarafa mbili ni za milimani mno Waheshimiwa Wabunge. Siyo miinuko, no, ni milimani. Wananchi hawa ni wakulima na wana bidii sana.
Mheshimiwa Spika, tena niwaambie Waheshimiwa Wabunge, mimi sina wananchi walevi, nina wananchi wakulima. Wanapoamua kunywa wanakunywa, kupumzika baada ya kazi, lakini siyo ulevi. Sasa tatizo langu kubwa, hili jimbo ni korofi na ukorofi wa jimbo langu ni barabara. Tarafa ya Gonja ina kata nne: Kata ya Vuje, Kata ya Bombo, Kata ya Mtii na Kata ya Luguru. Tarafa hii ina barabara sita. Barabara ya kwanza Maorevuje, barabara ya pili Ndungulugulu, barabara ya tatu Kisangaze – Vumbamtii, barabara ya nne Mpirani – Dispensary – Ridindimo, barabara ya tano Maore – Kalungoyo, barabara ya sita Mpirani – Bombo. Niliposimama hapa nikizungumza barabara zote hizi hazipitiki. Ninaishukuru Serikali tena naishukuru mno kwa sababu ilinipatia fedha nyingi sana za kujenga hizi barabara. Tulipewa fedha, lakini jimbo langu lina mvua kubwa sana, milimani kule, barabara hizi zote ninavyosema hapa sasa hivi zote hazipitiki, si kwa pikipiki wala si kwa magari, wananchi wanabeba mizigo kwa shida sana.
Mheshimiwa Spika, jumatatu juzi tarehe 14 Aprili, 2025 wananchi wa Tarafa ya Gonja hapa Lugulu hapa waliamua nao sasa waingie kutengeneza Barabara ya Ndungu - Lugulu. Nimemletea video kwenye WhatsApp yake Mheshimiwa Waziri na ameisoma. Nimemletea picha zingine tatu za barabara. Wananchi wameamua kuingia watengeneze barabara wenyewe, vijana zaidi ya 180. Hili si jambo la kawaida kwa sababu Tarafa ya Gonja yote imefunga.
Mheshimiwa Spika, ninaomba nimwambie ukweli kuwa tunajua mimi na wananchi wangu wanajua kwamba wametupa fedha nyingi sana, lakini sasa wamekwama. Tarafa ya Gonja wote wanakaa kule Gonja wanalima tangawizi, wanalima ndizi hawawezi kupeleka mazao kwenye masoko madogo wala makubwa.
Mheshimiwa Spika, sasa nina ombi, Mheshimiwa Mchengerwa nina ombi kwa Serikali, nimeleta picha umeona ni kiasi gani wale wananchi wanahangaika pale Lugulu. Ninaomba ili hawa wananchi wa Tarafa ya Gonja japo wapate njia. Ninaomba uongee na TARURA mkoa, ongea na Victor, huyu Mkurugenzi wetu mzuri sana ambaye ameketi huko juu; wawapatie hawa wananchi msaada mdogo wawakomboe wananchi wangu wa Tarafa ya Gonja. Ninaona huruma, mimi ni Mbunge wao, ninahangaika nao. Ninaomba niseme ukweli TARURA Mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya ya Same wanafanya kazi sana, tatizo hakuna fedha sasa hivi. Narudi kwako Mchengerwa, kwa unyenyekevu waangalie hawa wananchi wa Lugulu kwa sababu nimekuletea picha.
Mheshimiwa Spika, nina Tarafa nyingine ya Mambavunda. Hii Tarafa ya Mambavunda Barabara inaanzia Hedaru – Vunda - Miamba mpaka Ndungu. Ninaomba niipongeze Serikali, ahsanteni sana. Ninapoongea sasa hivi mkandarasi yupo kazini anafanya kazi. Ombi langu kwa Mheshimiwa Mchengerwa ni kwamba hii barabara sasa tafadhali wapeleke fedha za kutosha ili iwekwe zege kwenye sehemu zote korofi. Hawa wananchi wa kata tano wamechoka kusafiri kwa pikipiki au na mafuso. Ile barabara waipelekee fedha ili wananchi wangu waweze kusafiri na magari.
Mheshimiwa Spika, ninaomba nimalizie lile nililoomba kumwambia Mheshimiwa Rais. Hili neno ninamwambia Mheshimiwa Rais wetu kama kiongozi wa nchi yetu. Mheshimiwa Rais Samia tarehe 17 Septemba, 2024, alikuja Mkoa wa Kilimanjaro…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ANNE K. MALECELA: Hii ni kengele ya mwisho? Namalizia mama.
SPIKA: Ndiyo ni ya mwisho, dakika moja.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alikuja Mkoa wa Kilimanjaro akasema neno kubwa sana, ninaomba kumnukuu: “Kule kwetu kuna watu wanaitwa Mahulukutabu, watu hawa hawapendi utulivu wala raha. Mheshimiwa Rais akaendelea kusema kwamba, “tutailinda amani na utulivu wa nchi yetu, tutailinda kwa gharama yoyote ile” (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, naomba sisi Wabunge wote tumwambie Mheshimiwa Rais tunamuunga mkono katika kulinda amani ya nchi yetu hatutalala tutashirikiana naye katika kuilinda amani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi