Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kushukuru sana kwa kupata fursa ili niweze kuchangia Bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Pia nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wote wawili, pamoja na Katibu Mkuu na wataalam wote kwa kazi kubwa na nzuri sana wanayoifanya.

Mheshimiwa Spika, nitajielekeza kwenye mambo manne. Jambo la kwanza nitazungumzia Mradi wa TACTIC, mradi ambao Dkt. Samia Suluhu Hassan ametafuta fedha kupitia World Bank, tumezipata na unakwenda kubadilisha Jiji la Arusha. Barabara za Engosheraton pamoja na Barabara ya Olasiti zimekwishaanza. Ninaomba tu Mheshimiwa Waziri afahamu tu kwamba mkandarasi anasuasua, yuko very slow japokuwa fedha zipo. Kwa hiyo ningeomba ofisi yake ikaongeze nguvu kwenda kumsukuma ili matunda haya watu wa Arusha waweze kunufaika nayo.

Mheshimiwa Spika, pili, kupitia Mradi wa TACTIC pia tuliweza kupata component ya kujenga Stendi ya Kisasa Jiji la Arusha, kujenga Soko la Kilombero na Soko la Morombo na tarehe 19 Januari, 2024 tender ilitangazwa. Jana Mheshimiwa Naibu Waziri ametujibu hapa kwamba mchakato ule ulifutwa kwa sababu mtu aliyepatikana hakuwa na kigezo. Nimeona pale palikuwa na usimamizi hafifu wa wataalamu. Kama wametangaza mwezi Januari mpaka kufika mwezi Juni wangeshajua kama mtu hana kigezo na wakatangaza mtu mwingine aombe, wakasubiri mpaka mwaka mzima ukaisha wakaja kutangaza mwaka huu.

Mheshimiwa Spika, ningeomba Wizara yako ingekaa karibu sana na wale ambao wanasimamia mradi huu ili uweze kukamilika na kuanza kwa wakati na jana wametupa ahadi kwamba kufikia mwezi Mei, mkandarasi atakuwa site; na mimi Mheshimiwa Waziri sina mashaka na wewe kwa sababu alikuja pale Esolongido baada ya kuzungumza kipindi fulani hivi, tumeona yule mkandarasi yuko site na kazi inaendelea. Tunaomba na hili pia la stendi mkaliwekee nguvu ili mwezi Mei, 2025 mkataba usainiwe na tumeone mkandarasi akiwa site.

Mheshimiwa Spika, kwenye hili nina angalizo moja tu, kwenye Mradi wa TACTIC tunataka tujenge barabara ya lami kutoka eneo la Stendi kuja Barabara ya Mbauda, lakini TANROADS pia wamesaini mkataba wa kilometa 70 kutoka kona ya Mbauda kwenda mpaka Oljoro, eneo ambalo ni hilo hilo. Kwa hiyo ninaomba wakae na TANROADS waangalie ili kama wao wanajenga hizo fedha zikiokolewa ziende zikaondoe changamoto nyingine ya barabara kwenye maeneo mengine ya Jiji la Arusha.

Mheshimiwa Spika, tunatamani pia Barabara yetu ya Lemala ambayo ina TBL-TANESCO pia iingie kwenye Mradi wa TACTIC ili iweze kuondoa changamoto hiyo. Pia Barabara ya Kibo na yenyewe iweze kumaliziwa. Vile vile Barabara ya kutoka Engosheraton kwenda mpaka kule upande wa Daraja Mbili.

Mheshimiwa Spika, suala la pili Mheshimiwa Waziri na hili nitaomba anivumilie kidogo, kwa sababu ninaamini mtu ukiwa mnafiki ukiwa kijana, ukizeeka ni lazima utakuwa mchawi na uchawi siyo sifa nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, Arusha wanajenga jengo la utawala, jengo ambalo baadhi ya viongozi wake wanalipigia debe sana. Ninataka nimwombe atume timu yake ikakae pale ikaangalie kinachoendelea pale ndani. Katika jengo la utawala kwanza gharama zake za jumla hazipungui shilingi bilioni tisa; jengo la floor nane unajenga kwa shilingi bilioni tisa maana yake ni kwamba kila floor moja ni bilioni moja na ushee, kitu ambacho kwa akili ya kawaida hakiwezekani.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia wameingia mkataba juzi juzi hapa wa shilingi bilioni 6.2. Katika mkataba ule kuna baadhi ya vipimo walivyoandika kwenye BOQ na kwenye utekelezaji ni tofauti. Wameandika kwenye BOQ wana vipimo vyao ni 1128-meter square, mkandarasi ame-quote kwa 1128 cubic meter ambayo imeongeza gharama ya shilingi milioni 252. Wameandika vipimo vyao ni hiyo 7,034-meter square, mkandarasi ame-quote kwa 7,034-meter square gharama zimeongezeka kwa shilingi bilioni 1.5.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo wameingia mkataba wa shilingi bilioni 6.2 gharama halisi zilitakiwa ziwe shilingi bilioni 3.4, kuna ziada ya zaidi ya shilingi bilioni nane. Leo wananchi wa pale Arusha wanapata tabu, vivuko ni shida, barabara za ndani ni shida, watu wanachezea fedha namna hii. Badala viongozi waliowaamini kusimamia na wao wanakwenda kushabikia.

Mheshimiwa Spika, mimi nimemwambia Mheshimiwa Waziri mara nyingi, kwamba sijawahi kuwa na mashaka na usimamizi wake tangu akiwa Wizara ya Michezo, Utumishi na alivyokuja TAMISEMI. Ninaomba aongeze jicho la ziada kwenye usimamizi wa miradi; kwa sababu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatafuta fedha dunia nzima kwa ajili ya Watanzania. Badala ya kuzisimamia vizuri zinakwenda kuliwa na watu wachache, hilo jambo halikubaliki. Utasikia Mbunge anagombana na kila mtu, ni kwa sababu ujinga wa namna hii, ninaachaje kugombana na kila mtu? Kwa sababu nimechaguliwa pale kulinda maslahi ya watu, hasa watu wanyonge. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri atusaidie kwa sababu hili jambo ni jambo very serious. Kwa mfano hawa wenzetu wa PPRA wana evidence ya hili jambo ninalolizungumza, lakini hatua hazichukuliwi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuliwaambia kuwa kuna wizi ulifanyika pale CAG akaleta timu pakawa na special audit, madudu ya kufa mtu, hakuna watu waliochukuliwa hatua, wanafanya kuzugazuga tu, wanasimamishwa kidogo, utapigwa siku ngapi, lakini hatua serious hakuna. Zile ni fedha za walipa kodi, ni fedha za Watanzania. Kwa hiyo, hili jambo namwomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu nasisitiza kwamba sina mashaka naye, ni imani yangu kwamba atakwenda kuhangaika nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la tatu ni kuhusu TARURA. TARURA bajeti yake Jiji la Arusha ni shilingi bilioni 4.39, ndiyo bajeti ya TARURA. Hapa tunaona watu wanachezea shilingi bilioni tisa kujenga jengo moja tu, hizi fedha zingekwenda kwenye barabara na kwenye vivuko haya makelele unayoyasikia Arusha leo yasingekuwepo. Wanataka zije huku kwa sababu wanajua ni rahisi kuzila na wanashirikiana, ni team work kwenye kulimaliza lile Jiji la Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina ushauri kwamba mapato ambayo yanapatikana kwenye majiji yetu, hasa haya makubwa, kama Arusha, Mbeya, Dar es Salaam na Mwanza, hebu wakae na watu wa halmashauri wasipange bajeti ki-traditionally, wapange bajeti kulingana na changamoto za watu. Leo kule kuna shida ya vivuko, leo kuna shida ya barabara, wanakwenda kutenga fedha shilingi bilioni 1.6 kwa Jiji la Arusha eti kwa ajili ya kwenda kubomoa eneo la stendi ndogo, eneo ambalo linaiingizia mapato halmashauri shilingi milioni 800 kwa mwezi, leo wanakwenda kulibomoa eti wajenge jengo lingine ambalo tayari kuna mapato wanayapata pale. Kwa nini hii shilingi bilioni 1.6 isingekwenda kujenga barabara? Kwa nini hii shilingi bilioni 1.6 isingekwenda kujenga vivuko ili tuondoe changamoto kwenye maeneo yetu?
Mheshimiwa Spika, wanafanya hivyo kwa sababu wanajua wakibomoa pale wakijenga kila mtu atapata kibanda kimoja kimoja au atapata vitu vingine; maslahi binafsi, hawaweki maslahi ya umma kwenye eneo hili. Jambo hili nilisema kwenye Kamati ya Mheshimiwa Waziri na maeneo mengine. Kwa hiyo wanakwenda kubomoa majengo pale na wanatumia shilingi bilioni 1.6, kitu ambacho kiko ndani ya uwezo wa wa Mheshimiwa Waziri; na Mheshimiwa Waziri anaweza akatusaidia kwenye jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, wanataka pia kujenga ukumbi kwa zaidi ya shilingi bilioni tatu. Pale wana AICC, ndiyo kazi yao, kwenye masuala ya ukumbi na vitu vingine. Sisi tumejenga jengo letu la halmashauri pale, kuna kumbi zetu za mikutano na vitu vingine. Badala ya sisi kujielekeza kwenye shughuli za maendeleo tunataka tena shughuli nyingine huku za ukumbi na nini; kwa sababu gani? Wanajua tu kwamba shilingi bilioni 3.4 ambayo wamemsainisha mtu watakula mle ndani. Si kwamba wanabuni na kwamba wanalipenda jiji. Maeneo ambayo yanatatua shida za watu fedha hazipelekwi.

Mheshimiwa Spika, wewe leo unaenda kwenye kivuko ambacho kinahitaji gharama ndogo tu, pengine shilingi milioni 50, fedha hazipatikani, lakini unachukua fedha hizo hizo unakwenda kubomoa sehemu ambayo inakupa shilingi milioni 800, stendi ndogo, unaweka shilingi bilioni 1.6 huku hujamaliza shida za wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninaomba kwa kweli tusaidiane kwa sababu tunayo dhamana na jukumu la kumaliza shida hiyo; kwa sababu kuna kama Kituo cha Afya Mkonoo, Mheshimiwa Rais Samia amepeleka pale zaidi ya shilingi milioni 800. Kilikuwa ni kizahanati leo ni kituo kikubwa, lakini kuna barabara mbovu. Tungeweza kuokoa hii 1.6 tungeweka lami pale kwenye kituo cha afya, watu wakaenda zao wakapata huduma na wakaendelea kula matunda ya Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa pia na changamoto barabara yetu ya AFCON ile Barabara ya Njolo, kule tunakojenga uwanja wetu wa kisasa wa mpira nako pia barabara ni mbovu. Ni imani yetu kwamba kupitia bajeti hii tutakwenda kuliangalia ili tuondokane na hizo changamoto.

Mheshimiwa Spika, kingine Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amepeleka shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga soko la wamachinga miaka miwili iliyopita, mpaka leo hazijatumika. Sasa unajiuliza Arusha hakuna Wamachinga? Kwa nini hela hazijatumika? Katika hali ya kawaida ukienda kwenye masoko, angalia soko la Mbauda pale matope matupu. Milioni 500 ipo Mheshimiwa Rais ameleta lakini imekaa tu. Nenda Soko la Machinga Namba 68 matope matupu, mapaa yale hayaeleweki, milioni 500 ipo ina miaka miwili Mheshimiwa Dkt. Samia ameleta lakini hakuna ambacho kinaendelea pale.

Mheshimiwa Spika, nenda Soko la Samunge hali ni mbaya, karibuni kila mahali. Sasa unajiuliza hao waliowapeleka kwenda kusimamia maendeleo kule wanafanya kazi yao ipasavyo au wana ajenda zao nyingine?

Mheshimiwa Spika, ninajua muda ni mchache masuala ni mengi, baada ya kusema hayo, ninakushukuru sana kwa fursa hii adhimu. (Makofi)