Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makambako
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia.
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa miaka minne hii katika nchi hii; maendeleo tumeyaona kila jimbo, maendeleo ni makubwa haijapata kutokea, ni makubwa mno, kiasi kwamba tunampongeza pamoja na msaidizi wake Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. Kwa kweli maendeleo ya nchi hii yameonekana.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mchengerwa, Manaibu wake, pamoja na Katibu Mkuu. Kwa kweli kuna msemo unaosema, “Upele umempata mkunaji.” Kwa kweli, tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mchengerwa kwa kazi nzuri na timu yake wanayoifanya na wasaidizi wao katika hii Wizara ya TAMISEMI, wamesimamia vizuri na mambo yanakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Chama cha Mapinduzi kupitia Kamati Kuu, Halmashauri Kuu, na kupitia Mkutano Mkuu ukiunganisha pamoja na Wabunge hawa kazi waliyoifanya ya kumpitisha bila hiyana kwamba awe mgombea pekee wa Urais ndani ya Chama chetu, waliyaona mambo makubwa anayoyafanya.
Mheshimiwa Spika, vilevile, msaidizi wake, Dkt. Nchimbi kwa kweli sasa hii Ilani ya 2025 - 2030 sasa mambo yanakwenda kuwa ni makubwa zaidi. Vilevile tunampongeza Mheshimiwa Dkt. Mwinyi, kwani Chama cha Mapinduzi kimefanya kazi nzuri upande wa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nielezee mafanikio na changamoto. Nikianza na upande wa elimu, Makambako tumepata sekondari nyingi mpya. Tumepata madarasa upande wa shule za msingi na sekondari. Ombi langu kwa Wizara ya TAMISEMI, walitupatia fedha shilingi milioni 585 za kujenga shule ya ufundi na nina imani na wenzangu wamepata. Sasa mahali ambapo imefikia, tunaomba fedha zilizobaki, shilingi 1,100,000,000 ili iweze kukamilisha hii shule ya ufundi, iweze kuwahudumia Wanamakambako.
Mheshimiwa Spika, vilevile kwa upande wa afya, kuna Kituo cha Afya cha Kitandililo. Kituo hiki tulipata fedha kidogo. Tunaomba tupate fedha nyingine ili kituo hiki kiweze kukamilika, kiweze kufanya kazi iliyokusudiwa katika Kituo cha Afya cha Kitandililo.
Mheshimiwa Spika, pia, tulikuwa tumeahidiwa juu ya kituo kimoja kimoja kila Jimbo, ambapo nilipendekeza kituo hiki kijengwe katika Kata ya Kivavi. Wananchi wa Kivavi au wa Jimbo la Makambo wanaendelea kusubiri Kituo hiki. Tunaomba sana katika mpango huu tuweze kupata fedha kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kivavi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile tuna ombi kubwa, tuna maboma mengi yamejengwa kwa nguvu za wananchi, Waheshimiwa Wabunge hawa pia na Waheshimiwa Madiwani. Tunaomba katika bajeti hii kuhakikisha maboma haya yote ya zahanati, shule (madarasa) na kadhalika, yaweze kumaliziwa kupitia bajeti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna zahanati moja ambayo nimekuwa nikiizungumza sana. Zahanati hii iko katika Kijiji cha Mkolango ambapo Waziri alishaniahidi kwamba Wananchi wa Mkolango watapata fedha mwezi huu wa Nne, siyo kwenye bajeti hii, kwenye bajeti ambayo ilishapita.
Mheshimiwa Spika, naomba fedha hizi ziende kwa wakati, kwa sababu wananchi niliwaeleza kama ambavyo Mheshimiwa Waziri Mchengerwa aliniambia mwezi huu wa Nne watapata fedha kwa ajili ya zahanati hiyo, kwa sababu, wananchi wameshajenga, wameshaezeka kwa nguvu zao, bado sasa Serikali kuweza ku-support. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine pamoja na kwamba halipo katika Wizara hii, lakini kwa sababu ni Serikali, kuna suala la fidia la umeme wa upepo katika Mji wetu wa Makambako. Suala hili la fidia la umeme wa upepo, wananchi wamekaa wakisubiria zaidi ya miaka 15 hawajapata fidia, hawawezi kuendeleza wala kufanya jambo lolote.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Waziri Mkuu alipokuja alitoa maelekezo, naomba kupitia kikao hiki kuhakikisha Serikali inatenga fedha kwa ajili ya kuwapa fidia wananchi hao ili waweze kupisha ule mradi uweze kuendelea.
Mheshimiwa Spika, vilevile, kuna soko la Kimataifa. Eneo hili lililotengwa kwa miaka mingi, tunaipongeza na tunaishukuru Serikali kwa kulipa fidia zaidi ya shilingi 3,200,000,000. Wapo wananchi 18 ambao bado hawajalipwa fidia, tunaiomba Serikali imalizie kuwalipa wananchi hawa 18 ili waweze kupisha huu mradi.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala la barabara. Tunaishukuru TARURA, TANROADS kwa Makambako Mjini, lakini TARURA wanafanya kazi nzuri sana. Ombi langu, fedha ziongezwe pamoja na kwamba fedha zimetengwa hapa kwenye taarifa ambayo imesomwa hapa. Barabara za kwenda vijijini, nina barabara hapa ya kutoka Makambako inaitwa Barabara ya Mgimba – Mlowa - Kifumbe, kwenda kutokea Nkitu mpaka pale Ikelu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii barabara ni kama ring road kwa Makambako, kutoka Makambako kwenda kwenye hospitali ya wilaya ni kilometa nane. Tunaishukuru Serikali imetupa fedha za kujenga lami kilometa mbili. Tunaiomba Serikali, barabara hii siyo nzuri hasa kwa akina mama wajawazito na akina mama wagonjwa wanapokwenda hospitali yetu ya halmashauri iweze kutengenezwa kwa wakati ili iweze kupitika kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile, kwenye hili suala la afya, nimeuliza swali la nyongeza asubuhi kuhusu suala la watumishi. Katika Kituo cha Afya hiki cha Kitandililo nilipofanya ziara hivi karibuni, wananchi wale waliomba angalau, kwa sababu kuna wahudumu wawili tu pale, waongezewe wahudumu ili waweze kuwahudumia wananchi wa Kituo cha Afya cha Kitandililo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaipongeza Serikali kwa kuhakikisha Jimbo letu limepata umeme kwenye vijiji vyote, sasa hivi Serikali imetupatia karibu vitongoji 18. Wakandarasi wanaendelea kupeleka nguzo na kadhalika, tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, lakini siyo kwa umuhimu, mtu anapofanya vizuri ni lazima apongezwe kama alivyosema Mheshimiwa Mama Kilango. Maono yangu na maono ya Wabunge hawa kwa kweli baada ya uchaguzi wa 2025 kila mahali tumejipanga kuhakikisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anapata kura za kutosha, na baada ya uchaguzi lazima afikiriwe tena kwa mambo mengine kwa sababu ana maono makubwa sana kwa nchi yetu na Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Makambako kwa namna wanavyoniunga mkono, wanavyokuwa nami, na mimi inawajali wananchi wangu. Nawaambia Mungu anipe uzima, 2025 nipo, na 2030 nipo ndugu zangu bila shida yoyote.
Mheshimiwa Spika, namwombea Mheshimiwa Waziri Mchengerwa kama ninavyosema, kwa kazi nzuri anayowatumikia Watanzania na Jimbo lake. Sisi Wabunge tunamwombea Mheshimiwa Mchengerwa kwenye Jimbo lake aweze kurudi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile na Naibu wake, ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Dugange, tunamwombea, kazi anayomsadia Waziri ni kazi nzuri sana…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa haya ahsante sana…
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, bila kukutaja wewe, wewe ni Rais wa Mabunge ya Dunia. Sisi wenzako wa kule Mbeya tunakuombea, tunakuombea Watanzania wa Mbeya wakurudishe tena kwa heshima tuliyopewa. Mungu akubariki, ahsante sana. (Makofi)