Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa maoni yangu. Jambo la kwanza, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri alizofanya kwenye kipindi chake cha miaka minne. Kwa kweli mimi kama Mwakilishi wa Jimbo la Geita, mpaka sasa tunasubiri tu tarehe ya kupiga kura ili tuweze kumwekea kura zake, hatuna matatizo na kura zake. Kwa kazi alizozifanya Mheshimiwa Rais kwenye Jimbo langu, naomba nitumie podium hii kusema nami nipo bado kwenye kiti hiki, nitaendelea kwa sababu nimefanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana wewe kwa kipindi chote cha miaka mitano umetuongoza vizuri sana. Najua umepokea form one wengi, lakini mpaka leo naona wote wako sawa wamekuelewa. Tunakushukuru sana kwa kutuongoza vizuri, Mungu akubariki sana na kwa kweli Wanambeya hatutaki watuangushe.
Mheshimiwa Spika, katika watu tunaowaombea wa kwanza kuongoza kwa kura, ni wewe. Watu wa Mbeya wametuletea mtu sahihi. Najua kulikuwa na maigizo, lakini baada ya kuondoa maigizo, hii ndiyo faida ya kuchagua viongozi wenye busara, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, nampongeza sana Mkuu wangu wa Mkoa, nimemwona, Mheshimiwa Martine Shigela. Najua mimi pamoja na Wabunge wenzangu wa Mkoa wa Geita tuna mlinzi mzuri sana kwenye Majimbo yetu, hatuna mashaka, hatuna wasiwasi, na hivi nimemwona na rafiki yangu Chongolo, tunamkaribisha sana. Amecheka sana wakati mchangiaji akichangia hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nimweleze ndugu yangu, Mheshimiwa Mchengerwa, Mheshimiwa Waziri kwenye majimbo yetu tuliwaahidi watu vituo vya afya. Naomba sana, siyo kwamba vitatukosesha kura, lakini kwa sababu tuliahidi na Serikali yetu ni Sikivu, tunaomba zile fedha kwa ajili ya kujenga vituo vya kimkakati. Tulifanya mikutano tukaahidi, wananchi wangu wa Kata ya Rubanga wananiangalia hapa, niliwaambia tunajenga kituo, sasa naomba ufanye namna yoyote ili tuweze kujenga kile kituo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka nizungumze kidogo kwa upole, hapa najua Katiba inaruhusu, siyo dhambi, na Mheshimiwa Rais alitangaza juzi kwamba watumishi wote wanaotaka kuingia Bungeni wamwandikie barua. Nimeona kamsururu kidogo ni karefu, wengi wamemwandikia Waziri wa TAMISEMI na Mawaziri wengine, hatuwaogopi na tunawakaribisha kuja Bungeni. Nataka kushauri, hii nyumba ni nyumba kidogo ya watu wanatakiwa tuwe wasafi siyo kichaka cha watu kujificha.
Mheshimiwa Spika, naomba… (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Musukuma, nasikia kuna watu wanasema orodha hii umeiona wapi?
Waheshimiwa Wabunge, lakini wale ambao wanataka kujua nani kiongozi kwenye eneo lake anagombea, mtamwona Mheshimiwa Musukuma atawajuza.
Mheshimiwa Musukuma, endelea. (Kicheko)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, intelijensia inakua kwa baadhi ya watu, siyo kwa wote, nakushukuru. Nilikuwa nashauri wale ambao wameandika kuja kwa Mheshimiwa Mchengerwa kutaka kuingia kwenye hii game ya siasa, tunawakaribisha na ni suala la Kikatiba, lakini kabla hajawapa idhini ya kwenda kugombea, naomba Mheshimiwa Waziri na kupitia Bunge lako hebu wapelekewe special audit kwanza. Wawe clear kwanza, waje wakiwa wasafi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yaani naona kama tunajikaanga wenyewe, tunatoa kulia tunaweka kushoto na mtu akishaingia humu ameshavaa kinga, hawezi kuitwa. Kabla mtu hajaachia kiti chake kuja kugombea Ubunge, peleka special audit. Kichere nimemwona hapa, ili wakija kwako na ile barua kwamba huyu hana matatizo, ndio waje huku. Hawezi kukwapua huko halafu wakaja kugombea Ubunge, haiwezekani.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba sana hilo, vyombo vyote mlizingatie na Mheshimiwa Waziri kabla hajawaruhusu kuja kugombea, wawe na barua zinazotuonesha hawa watu ni safi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bahati moja nzuri mimi kwenye Jimbo langu nikiletewa kiongozi kama Mkurugenzi, wa kwanza kwenda ofisini kwake huwa ni mimi. Namwambia, nipe plan yako ya baadaye. Unataka kwenda kwenu kugombea Ubunge au unataka Ukurugenzi? Bahati nzuri huwa naletewa watu wanaokaribia kustaafu, hakuna anayesumbua watu kwenye Ubunge, kwa sababu ninajua mimi kahalmashauri kangu ni kachanga, ukianza kukakwapua tena kwenda kutunza za Ubunge utanimaliza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana, hili suala kwa manufaa ya Wabunge wote, hizi barua za special audit zitembee ili tupate viongozi safi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine nilitaka kutoa ushauri kwenye TASAF. TASAF iko Utumishi, lakini ukiangalia kazi za TASAF nyingi tunazifanya halmashauri. Nilikuwa nadhani, ikiwapendeza TASAF irudi TAMISEMI ili tu-deal nao moja kwa moja. Kuna kitu wenzangu mnaotoka vijijini mnafahamu, familia maskini zilizokuwa zinapewa fedha na TASAF shilingi 30,000 yaani yamekuja masharti unajiuliza, hawa watu waliotengeneza haya masharti wao wanakaa dunia gani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zile familia maskini, wale wazee, ili wapewe zile fedha walizokuwa wanapewa mwanzo, lazima wakalime barabara. Mbunge unafanya ziara, unakutana na bibi wa miaka 70, 65 amepewa hatua 10 za kupalilia. Utaendelea na ziara au inabidi umsaidie! Unajua tuko tofauti, mtu aliyekulia boflo na siagi huwezi kulinganisha na mtu amekulia uji wa muhogo halafu unalima mpaka saa kumi na moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ehee, haya mawazo yanafanyika kwa watu ambao hawafanyi research vizuri vijijini. Kule vijijini ukikuta mtu ameshakuwa mzee, kwanza amezaa watoto 16, halafu unaenda kumpimia hatua 10 ili umpe shilingi 30,000. Serikali hii ni tajiri sana. Nilikuwa nadhani haya majukumu yarudi moja kwa moja kwa Wakurugenzi ili tu-deal nao.
Mheshimiwa Spika, hawa waliotengeneza huu utaratibu siyo sahihi kabisa. Familia maskini, mtu mzee aliyekimbiwa na watoto wake, amewasomesha wapo mjini wameniga tai, mama analima vibarua, tena vya kulipwa shilingi 30,000. Hili nadhani pia tunahitaji kuliangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshukuru pia Mheshimiwa Waziri, amezungumza suala la mwendokasi. Kwanza, nashukuru kwa kuwa anachukua maeneo machache machache ya ushauri wetu sisi wazoefu. Mheshimiwa bado tatizo sidhani kama tutalitibu. Kama Serikali, wewe ndiyo unanunua magari halafu unampa mtu kuendesha, kila mtu anatafuta faida. Mimi siwezi kufanya kazi ya bure, lazima nitachukua change, tuje tukutane kwenye makaratasi, kwenye matatizo.
Mheshimiwa Spika, nadhani kama tumeweza kujenga miundombinu ile, jukumu la uendeshaji tuwape sekta binafsi, yeye mwenyewe na kila kitu cha kwake. Hii kazi siyo lazima tuwape wageni, siyo lazima. Wapo watu ambao ni Watanzania kabisa wanaoweza kufanya hizo kazi kupeleka mabasi Mbagala, kama mtu ana gari mia anapeleka mpaka Rungwe. Yaani kwenda Mbagala, tunahitaji kuleta Wazungu kweli!
Mheshimiwa Spika, hao wanaokuja hawana uchungu na Watanzania, wao wanakuja kuchuma ili waende kwao. Kwa hiyo, hizi kazi ambazo tunaweza kuzifanya wenyewe nadhani kuna umuhimu wa kuwapa watu wazawa ili waweze kufanya hizo kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, tunaenda kwenye uchaguzi na ninashukuru kwanza chama changu kwa kale kameseji kalikotoka jana usiku, kwamba tutachukua tarehe 28. Nakishukuru sana chama changu, Sekretarieti pamoja na waliotoa hayo maamuzi, Wabunge sasa tu-concentrate na Bunge. Tufanye kazi ya Kibunge, tukutane hiyo tarehe 28. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka kuwaambia kwa niaba ya sisi Wabunge tunaotokana na Chama cha Mapinduzi, sisi Sera yetu tunasonga mbele. Hawa wanaosema no reform, mimi nashauri kama kuna namna yoyote hata ya kuwapitisha mlango wa nyuma waruhusuni wasaini tukutane nao, hawana cha kutuambia. Kama walitafuta mlango wa kutokea, kutokwenda kusaini, wapeni hata kwa ziada ili tukakutane nao majukwaani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kazi zilizofanywa na Serikali ya Mama yangu Samia, mimi sioni hoja. Hata ukizunguka huko mtaani unawaambia watu tuzuie uchaguzi, leta hoja. Mwanzoni kulikuwa na hoja ya Escrow, EPA, watu wengi walitoka hata walioenda shule wasomi, lakini leo tunaenda kuzuia uchaguzi kwa sababu ya Madaraka, hapana. Wasitupe jezi tunawasubiri, wasitukimbie tarehe 28 likiachiwa tukutane kitaa wote tunajua kuongea.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)