Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa na kwa sababu umempa alert, ngoja tu tumwache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu mpaka tulipofikia leo ni mwaka wa 55 tangu tumepata Uhuru. Wakati tunapata Uhuru na mpaka Baba wa Taifa anatoka madarakani, nchi yetu ilikuwa na viwanda karibu 366 ambavyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi ilivibinafsisha, ikaviua kabisa na tuna mifano thabiti.
Kwa mfano, mpaka 1984 viwanda vya nguo vilikuwa 12 leo hakuna kiwanda cha nguo hata kimoja kinachozalisha. Tulikuwa na viwanda vya kubangua korosho 12 leo hakuna kiwanda hata kimoja kinachosimamiwa na Serikali kwenye kubangua korosho. Tulikuwa na viwanda vya sukari, mkonge, viwanda mbalimbali vilikuwa 366. Tulikuwa na Shirika la Ndege mwaka 1984 tulikuwa na ndege 12 au 11 leo Shirika letu la ATC halina ndege hata moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunasema tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda ni wazo jema, lakini Mpango wa miaka mitano uliopita ndiyo ulitakiwa uondoe vikwazo vya kuelekea kwenye uchumi wa kati wa viwanda. Ukipitia kwenye Mpango wa miaka mitano uliopita, viwanda vinahitaji umeme, tuliwaambia na tulilieleza Taifa kwamba ndani ya kipindi cha miaka mitano lazima tuzalishe megawatts 2,780. Leo tuna megawatts 1,247 ambazo zimetoka mwaka 2010 - 2015 yaani tumepata ongezeko la megawatts 347 kwa miaka mitano. Bado hatujafikia lengo la miaka mitano hapo tunakwenda kwenye uchumi wa kati wa viwanda ambao upo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, unaona kabisa kwamba kikwazo hiki bado hatujaondokana nacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliweka lengo la barabara zaidi ya kilomita 5,000 lakini mpaka sasa ni kilomita 2,773 sawa na asilimia 53 ndizo ambazo zimejengwa. Sasa unajiuliza kwamba huu uchumi wa viwanda ambao vikwazo vyake tulipaswa kuvitatua katika Mpango wa awali wa Miaka Mitano haujakamilika, je, tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda wa namna gani? Hayo ndiyo maswali ambayo Serikali inapaswa kutujibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaangalia tu focus ambayo Wizara imetuletea, inasema tuna matarajio mwaka huu wa fedha wa 2016/2017 kuwa na bajeti ya shilingi trilioni 22.9 bajeti ya mwaka jana ilikuwa ni shilingi trilioni 22.45 yaani tumeongeza shilingi bilioni 450 kutoka katika bajeti ya mwaka uliopita. Ukiangalia watu wa Kenya, jana na wenyewe walikuwa wanatoa Mpango wao wa Taifa, bajeti yao ni Kenyan money trillion 2.19 ambazo ni sawasawa na trilioni 44.5 za Kitanzania. Kenya wana bajeti ya trilioni 44.5 sisi Tanzania tuna bajeti ya trilioni 22 halafu unasema tunakwenda kwenye uchumi wa kati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine tukisema ni maagizo mtatulaumu lakini unaona kabisa haileti sense. Bajeti ya Maendeleo ya Kenya ni nusu, asilimia 47 ya bajeti ya Taifa, trilioni 20.195 ya Kenya ndiyo bajeti ya maendeleo sisi bajeti yetu ya maendeleo haifiki hata trilioni 10. Kila mwaka tukikaa ndani ya Bunge tunaishauri Serikali kwamba angalau bajeti ya maendeleo ifikie asilimia 35 ya bajeti husika ya nchi lakini hicho kiwango hatujawahi kufikia katika historia ya hili Taifa.
Sasa unajiuliza tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda ama tunapiga propaganda za kuwaambia Watanzania kwamba matarajio yetu ni haya, maana tumekuwa ni watu wa kubadilisha slogan ili kuwateka wananchi katika mambo ambayo tunashindwa kuyafikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumekuwa ni watu wa kuwashauri tu, tumekuwa ni watu wa kuwaambia lakini mmeshindwa kuyatekeleza haya. Sasa leo tunawauliza kwenye hizo trilioni 22 bajeti ya maendeleo ina-reflect viwanda? Unakuta hai-reflect viwanda ambavyo tunatarajia kuwekeza. Kwa hiyo, mwakani Waziri wa Fedha atakuja na visingizio hivi hivi kwamba bajeti ilikuwa ndogo ndiyo maana tumeshindwa kufikia malengo. Tunahitaji kujenga reli ya kati, tunahitaji kujenga viwanja vya ndege na kununua ndege, nchi yetu haijawahi kuwa katika vikwazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Iran juzi wametoka kwenye vikwazo wamekwenda Ufaransa kwenye Shirika la Airbus wameagiza Boeing 108, hawa watu walikuwa kwenye vikwazo sisi ambao tumekuwa kwenye amani kwa kipindi chote tunazungumza stori za namna ileile. Unajiuliza hivi Watanzania tunayoyasema ndiyo tunayoyatekeleza? Tunaulizana kila siku kwa nini tunashindwa kutekeleza masuala ya msingi ambayo kama Taifa tumekuwa tukiyahitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuzungumze…
TAARIFA
MWENYEKITI: Kuna taarifa Mheshimiwa Silinde naomba uketi....
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, this is the fact ipo kwenye taarifa ya Wizara ya Fedha, taarifa yenyewe imesema kwamba mpaka 2010 tumezalisha megawatts 900, kutoka 2010 - 2015 tumeongeza megawatts 347 tu. Kama Wabunge ndiyo jukumu letu kuieleza Serikali. Kwa hiyo, hayo matarajio ambayo tulikuwa tumeyapanga tufikie 2,780 ifikapo 2015 ambayo bado hatujafikia. Kwa hiyo, that is the fact Mheshimiwa Waziri. Kwenye upande wa viwanda, the same applies, Taifa linaelewa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kumalizia, kama Taifa na Bunge nashauri katika bajeti ya mwaka 2016/2017, lazima tutunge sheria kwenye Sheria ya Bajeti tuingize provision ya kuhakikisha kwamba Serikali inaweka at least 40 percent ya bajeti ya nchi kuwa ya maendeleo, tuiwekee sheria. Hii asilimia 35 ambayo tumekuwa tukiizungumza haina sheria ndiyo maana utekelezaji wake haupatikani. Kwa hiyo, nalishauri Bunge na hata Wizara mnapotengeneza ile Finance Bill, moja ya provision ni kuhakikisha kwamba asilimia 40 ya fedha inayotokana na bajeti nzima inakwenda kwenye maendeleo na tunaitungia sheria ili utekelezaji wake upatikane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine bandari tumeeleza, Bunge hapa lilitunga Sheria ya Mawasiliano (Telecom Act) ya 2009 na kuna Sheria ya Madini ya 2010 ambayo zinaitaka Serikali kuhakikisha Makampuni ya Madini pamoja na Makampuni ya Simu yanajisajili kwenye Soko la Hisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiangalia Makampuni ya Simu yana mapato makubwa, angalia mzunguko wa Mpesa, angalia wateja ambao wako kule lakini angalia kodi wanayolipa kwenye Serikali! Makampuni ya Simu tangu 2009 mpaka leo miaka saba yameshindwa kujisajili. Kodi wanayopata Serikali siyo stahili kwa sababu tumewaambia kabisa mkiyasajili tutakuwa tunaona uendeshaji wao lakini Serikali miaka yote haifanyi. Sisi kama Wabunge jukumu letu ni kuwashauri na tumekuwa tukiwashauri lengo letu kuhakikisha Serikali inapata mapato sahihi na mkipata mapato maana yake haya yote tunayoyazungumza hatutayajadili tena kwa maana ya mdomo tutajadili utekelezaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapokuwa tunawashauri wakati mwingine muwe mnapoekea siyo mnabisha tu. Uwezo wa kujenga hoja tunao na uwezo wa kusema Tanzania ni mkubwa kweli kweli, tatizo la Tanzania ni utekelezaji wa yale ambayo tumekubaliana ndani ya Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri mnapokuja Mpango na mnajua kabisa haya mapendekezo ama mwongozo wa Mpango tunaoujadili leo ilitakiwa iwe ni extract kutoka kwenye Mpango wa Miaka Mitano kwa sababu hatuna ule Mpango wa jumla wa Miaka Kumi na Tano. Tunasema tuna Strategic Plan ya miaka kumi na tano lakini…
MWENYEKITI: Ahsante, muda wako umekwisha.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)