Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa nafasi ya kusimama ndani ya Bunge. Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mambo yote anayoyafanya kwa wananchi wa Jimbo la Buchosa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana wewe mwenyewe kwa namna unavyoongoza Bunge letu, Waziri wetu wa TAMISEMI, Manaibu wake, Makatibu Wakuu, Watalamu wote wa TAMISEMI kwa namna wanavyofanya kazi yao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mkuu wangu wa Mkoa wa Mwanza ambaye yuko ndani ya ukumbi huu kwa namna anavyofanya kazi, na binafsi kwa ushirikiano anaonipa. Namshukuru sana Mkuu wa Wilaya yangu, Senyi Ngaga ambaye tunafanya naye kazi vizuri. Nawashukuru sana Baraza la Madiwani, Mwenyekiti wangu wa Halmashauri, na Mkurugenzi wangu wa Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, nimshukuru sana Mkurugenzi wangu wa Halmashauri. Huko nyuma niliteseka sana, lakini Mheshimiwa Rais akanisikia, akaniletea kaka yangu Mihayo, tunafanya kazi vizuri na Buchosa imebadilika sana. Nakushukuru sana Mihayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shukrani zangu pia ziende kwa CEO wa TARURA. Lazima niseme sentensi chache. Nimeshakutana na watu wengi sana kwenye maisha yangu, lakini huyu bwana ni mtu wa tofauti. Anapokea simu wakati wowote na anakupatia kila msaada unaouhitaji. Mungu akubariki sana Seif, endelea kufanya kazi yako vizuri na Mungu ataendelea kukunyanyua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumnukuu mshairi mmoja maarufu duniani anaitwa Dante, aliishi mwaka 1265. Dante alisema maneno yafutayo, nami nitayanukuu. Alisema: “The hottest places in hell are reserved for the ones who chose neutrality during the times of moral crisis”. Maana yake ni kwamba, sehemu yenye joto kabisa kule jehanamu imeandaliwa kwa wale watu walioamua kunyamaza wakati mambo yanaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi binafsi Eric Shingongo, Mbunge wa Buchosa, sipo tayari kwenda kwenye sehemu yenye joto kali kule jehanamu. Ndiyo maana sasa nitazungumza kile ambacho mimi ninaamini kwamba ni ukweli.

Mheshimiwa Spika, wapo watu wanapita wanazungumza maneno ya kwamba hakuna kilichofanyika hapa Tanzania na hakuna kilichotendeka tangu Uhuru wa nchi yetu. Tunawasikia wanapita kwenye majukwaa yao mbalimbali wanazungumza maneno kama hayo ambayo ninaamini ni uongo, labda kwa mtoto wa mwaka 2000, lakini hata mtoto wa mwaka 2000 na yeye anajua kwamba huo ni uongo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimezaliwa, nimekulia na nimesomea hapa Tanzania. Mimi ni zao la familia masikini kabisa kwenye nchi hii. Nakumbuka kutembea kilometa tisa kwenda shule na kurudi kwa miguu nikiwa mtoto mdogo. Kwa hiyo, akitokea mtu leo akasema hakuna kilichofanyika, huo ni uongo wa mchana ambao Watanzania ni lazima waukatae. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitaka nitoe data chache tu kuthibitisha hicho nilichokiongea. Najua mtakubaliana nami, mwaka 1961 tulipopata Uhuru, infant mortality rate (watoto wanaofariki chini ya miaka mitano), ilikuwa ni watoto 141 kati ya watoto 1,000. Leo ninavyozungumza ni watoto 43 tu peke yake wanafariki kati ya watoto 1,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maternal mortality rate kwa mwaka 1961 tulipopata Uhuru wa nchi yetu, walikuwa wanafariki akinamama 453 wakati wa kujifungua kati ya akinamama 100,000. Leo ninavyozungumza ni akinamama 104 peke yake ndio wanafariki. Hii imemwezesha Rais wetu kupewa mpaka tuzo ya Goalkeepers na Bill Gates Foundation. Mtu yeyote akisema kwamba hakuna kilichofanyika, huo ni uongo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 1961, life expectancy, umri wa Mtanzania kuishi ilikuwa ni mika 43, leo Watanzania tunaishi miaka 67. Hayo mambo yametokea kwa sababu ya huduma bora za afya na elimu kwa watu wetu. Mtu yeyote akisema Tanzania haijapiga hatua, huyo ni muongo, anatakiwa kuzomewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 1961 tulikuwa na Chuo Kikuu kimoja tu Tanzania. Leo kwa taarifa ya TCU tuna vyuo vikuu 50 ndani ya nchi yetu. Mtu yeyote akisema kwamba hakuna kilichofanyika, huyo ni muongo, anatakiwa kulaaniwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 1961 tulivyopata Uhuru, Tanzania umeme tulikuwa na megawati chini ya 100. Nimesoma data asubuhi ya leo mwaka 1967 tulikuwa na megawati 27. Leo ninapozungumza tuna megawati 3,404. Mtu yeyote akisema hakuna kilichofanyika, huyo ni muongo lazima alaaniwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi nchi yetu katika Afrika ni nchi ya nane kwa wingi wa umeme. Nani anapuuza Tanzania na maendeleo yamefanyika? Mambo mazuri yanafanyika, lazima Tanzania iwe mfano kwa sababu ni Taifa linaloenda mbele kwa kasi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtandao wa barabara, mwaka 1961 tulikuwa na kilometa 1,200. Leo ninapozungumza, tuna kilometa 13,000 tunaenda kilometa 14,000. Mtu yeyote akisema hakuna kilichofanyika, huyo ni muongo, lazima alaaniwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa niseme, John Maxwell alisema kwenye kitabu chake, “Everything raises of falls on leadership”. Haya yote yanayotokea nchi yetu ya shule niliyoyasema na mengine yote ambayo sijayatamka, yametokea kwa sababu ya uongozi bora wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anafanya kazi kubwa sana. Sisi wote lazima tukubali ya kwamba ndani ya uongozi wake, pamoja na awamu nyingine zote zilizopita, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya kazi kubwa sana, anahitaji kupigiwa makofi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, nizungumzie Jimbo langu. Katika Jimbo la Buchosa, mimi peke yangu nimepokea shilingi bilioni 66.2 ndani ya miaka minne. Tumejenga shule, zahanati, mitandao ya barabara na miradi ya maji. Kila kona ukienda, ninavyozungumza hivi sasa, kutana na Mtu wa Buchosa leo muulize; Buchosa ya leo na zamani ipi ni bora? Atakwambia Buchosa ya leo ni bora kuliko ya zamani. Hakuna barabara ambayo wakati wa masika haipitiki. Ni kweli mvua ikinyesha inaezua barabara, lakini TARURA wanafanya kazi kubwa na barabara zinaendelea kuboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, naomba niseme bila kuficha, nitaendelea kumtetea Rais wangu, nitaendelea kuitetea nchi yangu, mpaka mwisho wa uhai wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua kuna watu wanaweza wasiamini ninachokisema, lakini Buchosa tumejenga shule tano za High School, tumejenga zahanati 24, tuna vituo vya afya vitano. Tuna Chuo cha Ufundi kwa mara ya kwanza, hatujawahi kuwa nacho tangu Uhuru wa nchi yetu. Leo tuna Chuo cha Ufundi kinakaribia kukamilika. Sasa, niseme nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwaambie wananchi wa Buchosa kwamba, wamenituma Bungeni, naendelea kuwawakilisha, na kama alivyozungumza kaka yangu Mheshimiwa Deo Sanga, jambo moja kubwa sana, naomba nikunukuu: “Bado nipo, nitaendelea kuwepo” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme jambo moja nikielekea kuhitimisha mazungumzo yangu mafupi, naomba Waheshimiwa Wabunge mnisikilize vizuri. Naweza nikakiri na wengi mtakiri, mimi huwa napenda nizungumze ukweli wakati wote. Wakati mwingine ukweli umeniletea madhara, lakini naomba niseme ukweli ambao ninaamini kwamba ni ukweli.

Mheshimiwa Spika, alipoingia madarakani Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, inawezekana mimi na Watanzania wengine wengi hasa kabila langu hawa Wasukuma, ambao hawajazoea kuongozwa na wanawake walikuwa na mashaka kwamba, ataweza? Kwa sababu kwanza kafiwa na Rais madarakani, uchumi wa dunia umeharibika na amekuta miradi mingi, lakini yaliyotendeka na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan yamebadilisha kabisa mtazamo wangu mimi na Watanzania wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi Watanzania wana imani kubwa sana na wanawake kuliko ilivyokuwa huko nyuma, kwa kazi ambayo ameifanya. Watanzania wana imani kubwa sana na wanawake kwa kazi ambayo wewe Mheshimiwa Spika, umeifanya.

Mheshimiwa Spika, wewe na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mmeinua sana heshima ya wanawake katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo bila kudanganya na kupindisha maneno, nataka niseme wazi, leo hii akiibuka mwanamke mwingine anataka Urais, hakuna mtu atakuwa na mashaka, hayupo. Najua wanaume watasema na wanaweza wakasema, mwanamke tena. Kwani tangu 1961 mbona ilikuwa wanaume tu.

Mheshimiwa Spika, kwa kazi iliyofanyika akitokea mwanamke mwingine anataka Urais leo, Watanzania tumpe bila mashaka kwa sababu Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya jambo moja kubwa, ambalo hakika…

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

TAARIFA

SPIKA: Mheshimiwa Shigongo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kunti Majala.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nataka tu nimpatie taarifa mzungumzaji Mheshimiwa Shigongo kwamba siyo Urais tu, sasa hivi Watanzania hata kwenye Majimbo na Kata hawana shida na wanawake kwa kazi kubwa iliyofanyika. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Shigongo, kengele imegonga, lakini nakupatia nafasi, unaipokea taarifa hiyo? (Vicheko)

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo kutoka kwa shemeji yangu, Mheshimiwa Kunti Majala. Kwa kweli ni kweli kabisa Watanzania hatukuwa na uzoefu wa kuongozwa na mwanamke.

SPIKA: Sekunde 30.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, kwa yaliyofanyika wala wanawake msisite sasa hivi, gombeeni nafasi yoyote na tutawaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa kusema jambo moja tu la muhimu ambalo mimi ninaamini…

SPIKA: Kengele ilishagonga.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, ilishagonga? Ahsante kwa nafasi hii. Naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)