Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia hoja ya Wizara hii ya TAMISEMI ambapo na mimi ni Mjumbe katika Kamati hii ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kunijaalia afya, nimeweza kusimama katika Bajeti hii ya TAMISEMI ambayo ni bajeti ya mwisho katika Bunge hili la Kumi na Mbili.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, nakushukuru sana kwa kazi kubwa unayoifanya katika Bunge letu. Umekuwa mlezi wetu wakati wote. Katika hii miaka mitano ya misukosuko mikubwa, majina ya ajabu na matusi mengi umesimama pamoja na sisi. Pamoja na matusi yote na nini, lakini umeonesha ukomavu wako, umeweza kusimama pamoja nasi wanawake wenzako na kusema kwamba hili litafanyika kama sheria zitaonesha kwamba tumelifanya kimakosa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mwenyezi Mungu akubariki na tunakuombea kila la heri katika uchaguzi tunaokwenda kuomba tena ridhaa ya Wanambeya, basi Mwenyezi Mungu akufayie wepesi na uweze kuvuka salama salmini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya. Yeye pia amekuwa ni sehemu ya wale ambao walikuwa wakimwongeza kwa sisi hapa katika kuwepo kwetu Bungeni.

Mheshimiwa Spika, lakini mama huyu ameendelea kusimamia msimamo wake na amesema kwamba, hawa wanawake wataendelea kuwa Wabunge na tumeendelea mpaka leo tunasimama hapa na kumaliza katika Bunge hili la Kumi na Mbili, tunamalizia bajeti yetu ya mwisho. Tunamshukuru sana kwa kweli kwa uvumilivu wote ambao ameuonesha kipindi chote hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na yote wanayoyafanya na mimi niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI Mohamed Mchengerwa pamoja na Naibu Mawaziri wake. Pia, wasaidizi wao Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu kwa kweli wamekuwa ni viongozi ambao wameshirikiana vizuri na Bunge hili kupitia Kamati yako ya TAMISEMI, tumeweza kufanya majukumu yetu na kutekeleza kwa ufanisi na uadilifu mkubwa sana wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee lakini siyo kwa umuhimu namshukuru sana Engineer Seff wa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umeona makofi yamekuwa mengi hapa, siyo kwa sababu nyingine yoyote, lakini niseme tu na mimi kama Mjumbe wa Kamati, Engineer huyu amekuwa ni mtu msikivu, anayesikiliza na hata kama fedha hana kwenye eneo ambalo umelisema, lakini yale maneno anayokupatia ukitoka pale unasema kweli Serikali ya Awamu ya Sita inafanya kazi yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ninaendelea kumwombea kwa Mwenyezi Mungu, Engineer Seff Mungu ambariki aendelee kutekeleza makujumu yake vizuri. Pamoja na changamoto tulizonazo za barabara, lakini amekuwa akijitahidi kwenye maeneo yetu kufanya kile ambacho kinawezekana ili wananchi wetu waweze kuendelea na shughuli zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimekuwa ni sehemu ya sisi Wanakamati kukagua miradi mbalimbali na haya ninayoyasema kwa bahati nzuri nimeyaona kwa macho. Serikali hii ya Awamu ya Sita imeongoza kwa ujenzi wa madarasa mengi nchini. Pia, imeongoza kwa ujenzi wa zahanati na vituo vya afya pamoja na Hospitali za Wilaya kwenye maeneo yetu mbalimbali. Haya siyo kwa sababu nimeambiwa na mtu ama kwenye makaratasi, lakini mengi nimejionea mwenyewe na watu wanaweza kuiona thamani ya fedha yao ikiwa huko kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, binafsi nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa dhati kabisa kwa imani yake kubwa kwa wakandarasi wetu ambao ni wazawa. Wakati Mheshimiwa Rais anazungumzia kuhusu wakandarasi wazawa, wengi tulidhani na tulifikiri kwamba itakuwa ni kazi kubwa sana wakandarasi hawa kuweza kutekeleza majukumu yao, aidha kutokana na fedha kidogo walizonazo ama kwa hali nyingine yoyote. Mheshimiwa Rais aliweza kuwatengenezea mazingira bora na akawapa nafasi na wakandarasi wazawa kwa kweli wameonesha wanaweza wakapewa nafasi na wakafanya mambo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekwenda kukagua miradi mbalimbali ya stendi na masoko. Kuna baadhi ya miradi imejengwa na wakandarasi wazawa, na ukiambiwa kwamba miradi hii imejengwa na wakandarasi wazawa, huwezi kuamini hata kidogo.

Mheshimiwa Spika, pia, kuna maeneo tumekwenda ni wakandarasi wa nje na unaona kabisa kuna changamoto nyingi sana. Juzi tulikuwa Kahama, tumejionea kati ya mkandarasi mzawa na wa nje; mzawa amefanya kazi nzuri na kubwa kweli kweli kiasi kwamba tulivyoambiwa huyu ni mkandarasi mzawa, tukasema kweli Mheshimiwa Rais alifanya jambo zuri kuwaona hawa wakandarasi wazawa na kuweza kuwatengenezea mazingira mazuri ya kutekeleza majukumu yao.

Mheshimiwa Spika, kuna miradi ya TACTIC inayoendelea nchi nzima sasa hivi, lakini miradi hii tumeona ambavyo Serikali imewaamini wakandarasi wazawa na wameweza kuifanya miradi hii kwa ukamilifu mkubwa. Pia, miradi mingine ambayo inaendelea, inafanywa vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi natokea Tabora. Sisi ni sehemu ambayo tumepata mradi mkubwa wa TACTIC ambao ni wa soko. Mradi huu tunaye Mkandarasi mzawa ambaye anaitwa Sihotech Engineering, anakwenda kwa speed ya hali ya juu, kiasi kwamba hatukutegemea kwamba kwa sasa angekuwa amefikia hatua hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huyu Sihotech ameweza kutengeneza miradi ya soko na stendi katika Mkoa wa Mbeya na Shinyanga. Tumekwenda na tumeona kazi nzuri iliyofanyika. Ni imani yangu hata pale Tabora katika soko lile, ule wakati ambao Mheshimiwa Waziri amesema kwamba soko hili litakuwa tayari na wafanyabiashara wetu wataenda kufanya kazi, naiona hiyo ahadi ya Mheshimiwa Waziri kwa jinsi ambavyo Mkandarasi huyu anafanya kazi nzuri kwa weledi na kwa kasi ya hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nami kwa kweli niungane na Mheshimiwa Rais kwa imani aliyoionesha kwa wakandarasi wetu wazawa, wanafanya kazi nzuri na hawa wakandarasi wazawa wengine waendelee kuonesha imani hiyo kwa Mheshimiwa Rais ili waweze kupewa kazi nyingi ambazo zinajitokeza katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, binafsi nizungumzie kwenye Sekta ya Elimu na niseme kidogo kwenye baadhi ya Miradi ya Elimu ambayo imekuja kwenye Mkoa wetu hususan kwenye Jimbo la Tabora Mjini ambalo ninatokea mimi.

Mheshimiwa Spika, tuliomba hapa kwamba kuna shule nyingi sana za msingi sasa ambazo zinahitaji ukarabati, zimeshakuwa za muda mrefu. Kipekee kabisa, naishukuru sana Serikali na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI amepeleka fedha kiasi cha shilingi milioni 316 katika Shule ya Msingi Town School. Shule hii ilikuwa ni ya mwaka 1940. Leo tumepewa shilingi milioni 316 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa kuongeza madarasa katika shule hii ambayo ipo katika Kata ya Gongoni ambapo mimi natokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kazi ya kukarabati imeanza kufanyika, majengo yale ya zamani yaliyochakaa, sasa wameshaanza ujenzi wa madarasa ambapo unaenda kukamilika na watoto wetu sasa wataanza kusoma katika shule hiyo, ikiwa ni shule inayoonekana mpya, na imefanyiwa ukarabati wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu, pia, tumeletewa shilingi milioni 170 katika Shule ya Msingi Kitete iliyo opposite kabisa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Leo ukipita katika shule ile, ilikuwa imechakaa kweli kweli, lakini sasa hivi ukipita kama shule mpya. Kwa kweli kwa ukarabati huo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ukarabati huo na shule zetu sasa zimeonekana zikiwa mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunavyo vituo vya afya, pia tunazo zahanati, na bado kuna ujenzi wa zahanati zinaendelea katika Jimbo letu la Tabora Mjini. Kwa hiyo, tuishukuru sana Wizara ya TAMISEMI kwa kupitia Waziri wake Mheshimiwa Mchengerwa kwa kutuletea fedha.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi sisi Jimbo letu ni kubwa sana, lina kata 29. Tumelalamikia sana kwamba hatuna huduma za afya za karibu. Leo tunapata huduma za afya za karibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mchengerwa kwa ahadi yake ya kutupelekea fedha kwa ajili ya kumalizia majengo katika Kituo cha Afya Maili Tano. Amesema kwamba fedha hizi zitakwenda baada ya kuanza kwa bajeti hii ili kujenga majengo ambayo yanakosekana katika Kituo cha Afya Ipuli.

Mheshimiwa Spika, wakituwekea majengo yale, yanaweza kutusaidia kuhudumia wananchi wengi wa maeneo ya mjini katika Jimbo la Tabora Mjini na kwenye kata ambazo zinazunguka kituo kile cha afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na haya, nashukuru pia kwa miradi ya barabara ambayo imekuwa ikiendelea. Tunayo miradi ya TACTIC ambayo inaendelea na ujenzi wake. Pia, tunayo miradi ya TARURA ambayo kwa kweli wamepata fedha kidogo, lakini wameanza kutekeleza miradi mbalimbali ambayo barabara zilikuwa zimechoka na zimeharibika.

Mheshimiwa Spika, vilevile, kipekee kabisa kabla sijamaliza, nisipomshukuru sana Mkuu wangu wa Mkoa, ndugu yangu Chacha Matiko, kwa kweli nitakuwa sijamtendea haki. Mkuu wa Mkoa huyu amenipatia amani wakati wote. Nimefanya kazi kwa ujasiri mkubwa sana, na kila ninapohitaji ushirikiano katika Ofisi ya Mkoa, kwa kweli Mheshimiwa Mkuu wangu wa Mkoa na RAS wake wamekuwa mstari wa mbele kuweza kunipatia ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata pale nilipokuwa nina changamoto yoyote, nikienda, kwa kweli wamekuwa wakinisaidia ili niweze kutekeleza majukumu yangu kama Mbunge wa Mkoa wa Tabora. Kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Mkuu wangu wa Mkoa na RAS wetu kwa kuniamini na kuona kwamba, mimi ni Mbunge na ninaweza kutekeleza majukumu yangu katika eneo langu la kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. (Makofi)