Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa fursa nami kuweza kuchangia katika Wizara hii muhimu ambayo ni Wizara inayogusa moja kwa moja maisha ya Watanzania. Kabla sijaenda kwenye mchangao wangu, uniruhusu nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposimama na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tueleweke kwamba, lengo ni kushukuru na kupongeza kutokana na matokeo tunayoyaona, tunayoyashuhudia ya kazi kubwa anayofanya katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natokea Mkoa wa Tanga. Miaka minne mitatu iliyopita, Wabunge wote wa Mkoa wa Tanga ilikuwa kila tukisimama hapa tunalalamikia maji, tunalalamikia afya, tunalalamikia barabara. Malalamiko yalikuwa mengi kuliko shukurani, lakini kila anayesimama leo kitu cha kwanza tunashukuru. Tunampongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu tayari tumeona ametutoa kwenye hatua moja ya maendeleo na ametupeleka kwenye hatua kubwa mpya ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuwashukuru viongozi wengine wote wanaomsaidia Mheshimiwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu, Waziri Mwenye dhamana na Naibu Mawaziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa namshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, kwa sisi Wabunge, tena mabinti ambao tumeingia kwenye Bunge hili tukiwa tunahitaji malezi ya hali ya juu, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson alijitolea. Leo tunasimama kifua mbele, tuna uwezo wa kujenga hoja tukaeleweka, tuna uwezo wa kusimamia taratibu mbalimbali kwa sababu ya mwongozo na malezi ya Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson. Kwa pamoja tunamwombea afya sana na Mwenyezi Mungu ambariki sana, na watu wa Mbeya Mjini waone hili ambalo sisi tunaliona ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimejikita kwenye hoja moja tu, Elimu ya Ufundi. Nakumbuka wakati tu tumeapa mwaka 2021, mimi ni moja ya Wabunge ambao tulijenga hoja, tulisikitishwa, tulilalamika juu ya mfumo na matokeo ya elimu Tanzania. Mwaka 2021 baada ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuapa, alikuja kuhutubia Bunge hapa. Moja ya eneo ambalo alizungumza na yeye kutoridhika, ni elimu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hotuba yake, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo mahsusi kwa Wizara zinazohusika kufanya mapitio ya elimu yetu na mwisho wa siku tukaletewa sera na mitaala mipya ya elimu. Tunampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona kama ambavyo Watanzania tunaona, anaziona changamoto kama Watanzania tunavyoziona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunavyozungumza, tuna mtaala mpya, tuna sera, lakini hapa tulipo tunahitaji kwenda sasa tukaone matokeo ya sera na mitaala mipya ambayo imeshapitishwa. Tuna mambo makubwa matatu ambayo tunapaswa kwenda kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni kuboresha miundombinu ya elimu ya ufundi katika mkondo wa amali, elimu ambayo kwa Tanzania Bara ni jambo jipya. Elimu ambayo kwa Tanzania Bara bado haijawa na ushawishi wa kutosha, elimu ambayo kwa Tanzania Bara, pamoja na kwamba bado haijawa kwenye mazingira mazuri sana, ni elimu ambayo ina uhitaji mkubwa, na pengine ndiyo njia ambayo Watanzania tunakwenda kutoka, kupitia elimu ya ufundi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokwenda ni lazima tukubaliane kama Taifa, tutengeneze vipaumbele. Kipaumbele cha kwanza ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na elimu inayomwandaa Mtanzania kujiajiri, na ndiyo malengo ya kuwa na elimu ya ufundi nchini. Katika malengo hayo, ili uwe na elimu ya ufundi, lazima ujiandae kukuza ujuzi, lazima ujiandae kupanua uzalishaji, lazima ujiandae kupanua soko la ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana umechangia, moja ya eneo ambalo nilikusikia ulisema, hakuna nchi duniani ambayo inaweza kumaliza changamoto ya ajira. Naungana nawe, ni kweli kabisa, lakini ipo namna kama Taifa. Nitakupa mfano, Switzerland, Ujerumani, China, India, Korea, ni Mataifa ambayo yamekuwa na maendeleo makubwa kiuchumi kwa sababu waliwekeza kwenye elimu ya ufundi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia enrolment ya Ujerumani tunavyozungumza sasa, nusu ya wanafunzi wake wanapelekwa kwenye Elimu ya Ufundi. Ukiangalia Switzerland, tunavyozungumza sasa 90% ya wanafunzi wake wanapelekwa kwenye elimu ya ufundi. Lengo ni nini? Lengo ni kukuza uzalishaji, lengo ni kukuza ujuzi, lengo ni kupanua mazingira kwa ajili ya soko la ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 141, Serikali imeshajenga shule 100 za ufundi nchini. Hili ni jambo kubwa sana na tunaipongeza sana. Jambo ambalo sijaliona ni hizi shule zimeshajengwa, lengo ni kutoa elimu ya ufundi, ziko wapi karakana? Wako wapi walimu wa ufundi? Viko wapi vifaa vya kufundishia vitakavyokidhi elimu ya ufundi tunayoihitaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshakuwa na elimu ya ufundi kwa kipindi kirefu kidogo. Tumekuwa na elimu ya ufundi lakini tuepuke kwenda kwa mazoea. Elimu ya ufundi tuliyokuwanayo, tumefundisha watu kwa nadharia kwa kipindi kirefu. Elimu ya ufundi tunayotamani kuiona sasa ni elimu ya watu kwenda kupewa ujuzi au kufundishwa kazi wanazokwenda kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu akitoka kwenye chuo cha ufundi, awe na uwezo wa kwenda kujiajiri, awe na uwezo wa kwenda kufanya kazi bila kupewa elimu nyingine tofauti na ile ambayo ametoka nayo kule chuoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tungependa kuona hizi shule zilizojengwa kwa elimu ya amali, vyuo vya ufundi vinavyojengwa, VETA na maeneo mengine, walimu wenye ujuzi wawepo wa kutosha ili tudhamirie kwa pamoja kutoka kwenye hatua tuliyonayo kwenda kwenye hatua nyingine ambayo itatuletea ule uzalishaji na kupanua soko la ajira, kama ambayo nimesema hapo mwanzoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumzia elimu ya ufundi, ukiboresha elimu ya ufundi, maana yake unaiandaa nchi kuwa nchi ya viwanda. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alitembelea Mkoa wa Tanga, alifanya ziara kwa wiki nzima kwenye Mkoa wa Tanga. Moja ya wimbo wake katika maono yake, maelezo aliyotoa, alitamani kuirejesha Tanga ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga ya viwanda haiwezi kupatikana bila malighafi. Ni lazima tuwaandae vijana leo kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda ambavyo vinadhamiriwa. Ni lazima tuandae vijana leo kwa ajili ya kwenda kuajiriwa kwenye viwanda vinavyotegemewa kuanzishwa. Sasa, haya yote yanahitaji uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ni gharama na ndiyo sababu wakasema, kama ukiona elimu ni gharama, jaribu ujinga. Elimu ya ufundi ni gharama kuliko ambavyo tunategemea kuona. Elimu ya ufundi peke yake kwa shule ambazo zipo sasa hivi, zinahitaji shilingi bilioni 135.5 ili ziweze kupata vifaa. Walimu waliopo sasa hivi ni nusu, 50% peke yake, kati ya Walimu ya zaidi ya 2,000 waliopo ni zaidi ya 1,000, nusu ya walimu hatuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama tuna dhamira ya dhati ya kwenda kwenye elimu ya kujitegemea itakayoleta manufaa kwa Watanzania kuepuka kupigiwa simu za mara kwa mara kuombwa ajira, ni lazima tujikite kwenye elimu yenye tija kwa kupeleka vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika shule ambazo tumeziandaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)