Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Mohamed Lujuo Monni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia mjadala huu muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema ambaye ametujaalia afya njema, ametujaalia uhai na leo tupo hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais, amefanya kazi kubwa. Kila Mbunge ambaye anasimama hapa, anaeleza mazuri ambayo yametendwa kwenye majimbo yao, anaeleza namna gani Mheshimiwa Rais amewatendea haki Watanzania. Kwangu mimi yamefanyika mambo mengi, nami kipekee kabisa nachukua nafasi hii kumshukuru sana na ninaamini amefanya kazi ambayo Wanachemba wanajua wajibu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru pia Mheshimiwa Waziri, hotuba yake ilikuwa nzuri sana, amegusa maeneo yote. Nimefurahia kuchangia kwa sababu moja tu. Kila nilipoenda ofisini kwake lifanya kile ambacho kinahitajika kule Chemba, kwa hiyo, leo hapa nina jambo. Mheshimiwa Waziri nakushukuru kwa namna ambavyo unafanya kazi. Nawashukuru Naibu Mawaziri wote wawili pamoja na wataalam wote wakiongozwa na Katibu Mkuu, kwa kazi kubwa ambayo wanafanya. Nafahamu Wabunge wengi hapa wanaguswa na Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, natamani nikishukuru Chama cha Mapinduzi, hasa Mkoa wa Dodoma. Tumekuwa na Mwenyekiti mzuri sana, Alhaj Adam Kimbisa ambaye amekuwa akitekeleza na kusimamia vizuri Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Mkoa wa Dodoma kwa Chama cha Mapinduzi ni salama, uko kimya kwa sababu ya Mwenyekiti, anafanya kazi vizuri. Pia, namshukuru Katibu pamoja na wenzake wote ambao wanasimamia Ilani ya Chama cha Mapuinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaye Mkuu wa Mkoa ambaye anaratibu vizuri shughuli za Serikali kwenye Mkoa wa Dodoma, nampongeza sana. Pia nampongeza Mkuu wa Wilaya; vile vile tunaye Mkurugenzi wetu mpya wa Wilaya ya Chemba ambaye tunaona mwelekeo, sasa tunaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, namshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kazi, pamoja na kuwa ni wapya, lakini wanafanya kazi nzuri sana. Naomba nichangie kwenye maeneo matatu tu. Naomba nichangie kwenye elimu, afya, pia nichangie kwenye barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Serikali sana, kwa miaka minne hii ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tumejenga shule mpya saba za sekondari. Tumejenga shule maalum ya zaidi ya shilingi bilioni 4.1. Ninaamini shule ile inaenda kutatua changamoto na kutoa matokeo chanya kwa wanafunzi wetu ambao wamekuwa wakisoma kwenye shule za kutwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefungua shule mpya za msingi 13. Tumepokea zaidi ya shilingi bilioni 17 kwenye sekta ya elimu, Msingi na Sekondari. Tumejenga zaidi ya madarasa 145; tumemalizia maboma zaidi ya 60. Tumefanya kazi kubwa sana kwenye elimu, kazi kubwa sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa namna ya kipekee, mara zote ametoa fedha, lakini pia ametusaidia kwenye maeneo ambayo maboma yalikuwa na zaidi ya miaka 13, miaka 15. Nashukuru sana sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumepata kujengewa maabara. Pia, tumepata nyumba za walimu, lakini naishukuru sana Serikali, miaka minne iliyopopita, upungufu wa Walimu kwenye Halmashauri ya Chemba ulikuwa 22%. Leo tunaongea, kwenye primary school, tumefika 54%. Nakushukuru sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo ambalo nilitamani sana unisaidie zaidi, mwaka huu tumepata takribani walimu100. Walimu 54 kwa ajili ya sekondari, na walimu 40 kwa ajili ya primary school. Tuna upungufu wa zaidi ya walimu 756. Nakuomba sana sana Mheshimiwa Waziri, nilisimama hapa kwa sababu ya upungufu huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Chemba ni la kijijini, siyo kama Jimbo la Dodoma Mjini ambalo kukiwa hakuna walimu hapa unaweza ukapata tuition. Wapo jamii ya Kisandawe kule, kutoka shule ilipo mpaka kitongoji kilipo ni kilometa 42. Maana yake kama hakuna Mwalimu, hakuna alternative yoyote ya kupata masomo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, hebu tunapogawa walimu tuangalie na kipaumbele, ni namna gani tunaenda kugusa maisha ya watu wengi zaidi? Naomba katika hiyo changamoto tuweze kuitatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya pili kwenye elimu ni changamoto ya madawati. Kwa miaka minne hii tumejenga vyumba vya madarasa 147 vyenye madawati. Madarasa yatadumu kwa miaka 50, lakini madawati yatadumu kwa miaka saba. Ni bahati mbaya sana hatujawahi kuwa na mkakati wa moja kwa moja wa namna gani tunaenda kutibu, baada ya miaka saba yale madawati kuondoka, au madawati kwisha. Ni lazima, hakuna option, ni lazima Wizara iangalie namna bora ya kutibu hii changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa Mjumbe wa Kamati ya LAAC, wakati huo ukitembelea shule nyingi Tanzania nzima, kuna upungufu mkubwa. Kwangu upungufu wa madawati ni zaidi ya 70%. Ni lazima tuangalia ni namna gani tunaenda kutibu changamoto hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye sekta ya afya. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, tulikuwa hatuna hospitali ya Wilaya, lakini sasa hospitali ya Wilaya imekamilika. Tumejenga vituo vya afya, vizuri sana. Pia, tumefungua zahanati 11. Nasema hayo ni kazi kubwa sana ambazo zimefanywa na Mheshimiwa Rais Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, kuna changamoto kidogo. Kweli tunayo majengo mazuri, lakini kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi wa afya. Kwangu mahitaji ni makubwa sana, upungufu ni zaidi ya 71%. Nimesema hapa kwamba, jimbo langu ni la vijijini. Yapo maeneo kutoka kijiji kwenda kitongoji ni kilometa 40. Kijiji kwenda kitongoji! Yaani ili mtu atoke kwenye kitongoji kuja kwenye Kijiji, lazima afanye safari ya siku nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika mazingira ya namna hiyo, ni lazima tuangalie ni namna gani tunapeleka watumishi kwenye zahanati ambazo tumezijenga huko vijijini. Nakuomba sana, umekuwa ukifanya hivyo mara kwa mara, lakini nakuomba tena kwa mara nyingine, ajira za safari hii zizingatie maeneo ambayo yana mahitaji makubwa zaidi na ambao hawana alternative. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hivyo, wananchi wa kule kijijini hakuna dispensary ya mtu, hakuna private dispensary, hakuna hospitali ya private. Maana yake ni kwamba, kama zahanati yetu haina dawa, zahanati yetu haina mtumishi, maana yake yule mtu atabaki kuwa na tatizo lile lile bila alternative yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo ni la muhimu sana, kuna changamoto kubwa nimewahi kuisema huko nyuma, naomba kidogo Mheshimiwa Eng. Seff anisikilize. Hakuna uwiano ulio sawa, kati ya sealing zinazotolewa kutoka Halmashauri moja hadi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Chemba ina mtandao mkubwa wa barabara kwa sababu, jimbo ni kubwa sana. Wakati mwingine ukiangalia fedha inazopewa, sisi tuna zaidi ya kilometa 900, ukiangalia ceiling yetu ni ndogo kuliko watu ambao wana mtandao wa barabara wa kilometa 400, nami najua Engineer Seff ni Mhandisi, anajua ratio analysis, sijui ni kwa namna gani unaweza kutenga fedha kidogo kwa mtu mwenye barabara ndefu halafu ukaweka fedha nyingi kwa barabara fupi? Hili jambo linatakiwa liangaliwe upya, liratibiwe upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2024 tulipitisha bajeti hapa ya barabara. Zipo barabara ambazo tulizitengea fedha, moja ya barabara hizo ni Rufati – Muungano, Chemba – Soya, Donsee – Bugani – Kamaziwa, Baaba – Wavada, mpaka leo hazijatangazwa. Ukimwuliza Mhandisi mbona sisi tumepitisha bajeti? Anasema bado sijapata kibali cha kutangaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, zipo barabara ambazo zilitangazwa kama Mrijo Juu – Magasi zimesimama kwa sababu, TARURA hawajapewa fedha. Nina maombi mawili; kwanza naomba mruhusu hizi barabara zitangazwe kwa sababu, tayari tulishawaambia wananchi kwenye bajeti hii tunaenda kujenga barabara moja, mbili, tatu. Kutokuzijenga ni kutengeneza kutokuaminika wakati mwingine tunaposema tumepitisha bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wakandarasi waliopo kwenye barabara zile kwa mfano, huyu wa Mrijo Juu – Magasa ameondoka, ukimwuliza kwa nini umeondoka site? Anasema ni kwa sababu, hajapata fedha. Kwa hiyo, nawaomba, najua fedha zimeanza kutoka, na huyu mkandarasi wetu alipwe ili angalau barabara hii iweze kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna barabara muhimu sana, tangu nimekuwa Mbunge nimekuwa nikiongelea hapa. Nimeuliza maswali zaidi ya mara tatu, lakini nashangaa hujawahi kushituka kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna barabara ya kutoka kwa Mtoro – Sanzawa hadi Mpendo, ni barabara ndefu ya kilometa 54. Bajeti tunayopata ceiling ni shilingi bilioni 2.3, hakuna namna unaweza ukatengeneza barabara korofi vile kwa shilingi bilioni 2.5. Tumekuja na maombi maalumu mara kadhaa, namwomba Mheshimiwa Waziri, mimi najua yeye ni bingwa sana, jambo hili anaenda kulitatua. Hebu aangalie namna ambavyo anaweza kusaidia kwenda kutatua changamoto hii ya barabara.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naona unaniangalia. Muda wangu umeisha, lakini nikuombe Mheshimiwa Waziri, barabara hiyo ni muhimu sana, maana inaweza kutatua changamoto ya kata nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)