Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika hotuba hii ya TAMISEMI. Awali ya yote, napenda kusema kwamba, naunga mkono bajeti hii na ninaomba Waheshimiwa wenzangu waweze kuipitisha ili tuweze kuipatia Serikali nyenzo za kwenda kutuletea maendeleo ya haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeagizwa na wananchi wa Kinondoni nije nizungumze mambo mawili ya msingi. La kwanza ni kuipongeza Serikali na hapa ninapoipongeza Serikali, nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wakati nagombea Ubunge, nilikuwa na ndoto ya kutaka kuiona ile Kinondoni tunayoitaka, Kinondoni ya mjini, Kinondoni tunayoitaka. Mheshimiwa Rais ametutimizia ndoto yetu na hakika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi naweza nikasema imefikia zaidi ya 90% kwa ushahidi wa kile ambacho kilitakiwa kufanyika, kimefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, namshukuru sana ndugu yangu Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, yeye ni mwana Kinondoni mwenzangu. Kwa wale ambao hamjui, Mheshimiwa Mchengerwa ni mwana Kinondoni katika jimbo langu, hivyo namshukuru kwa sababu, umekuwa ni msaada mkubwa sana kwangu. Hivi ninavyozungumza, wananchi wenzake wa Kinondoni niliwapelekea taarifa kwamba, Mheshimiwa Mchengerwa baada ya kumaliza bajeti yake amesema nitaongozana naye kwenda Kinondoni, kuna kazi kubwa ambayo ameniahidi anakwenda kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kwanza ni kwenda kuzindua dispensary ya mfano ya mionzi kutokana na fedha za Mfuko wa Jimbo, shilingi milioni 129, tumewekeza katika hospitali ile ambayo tayari inafanya kazi, Ultrasound na X-Ray za kisasa. Hivyo, Mheshimiwa aje aone, kumbe fedha za Mfuko wa Jimbo zinaweza zikafanya maajabu kiasi gani? Vilevile ameniahidi na nikawaambia wananchi wa Tandale na Ndugumbi kwamba, Mheshimiwa Mchengerwa atakuja hapa kutafuta majawabu ya mto Mwangosi, mto ambao unafurika na kuwasumbua wananchi wa pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nikawaambia watu wa Kijitonyama, kule ambapo tuna Uwanja wa KMC kwamba, kuna mto unaitwa Mto Kijitonyama na umeahidi tutakwenda tukaangalie, uone ni kwa jinsi gani Serikali inakwenda kusaidia wananchi katika eneo hili na mwisho, pale Mwananyamala sehemu za Msisiri kwenye lile bonde. Bonde lile ma-engineer wengi sana wamefeli kutafuta majawabu. Najua Mheshimiwa Mchengerwa tukienda pamoja pale atajua ni kwa jinsi gani ma-engineer waliopo katika Wizara yake watakwenda kutusaidia. Hii ni pamoja na Mto Mzimuni katika Kata ya Mzimuni, pia, nitampeleka kule. Ni kazi ya siku moja au nusu ya siku, atatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetufanyia mambo makubwa. Bonde la Mto Msimbazi, hongera sana kwa Mheshimiwa Rais, ametufanyia kazi. Shilingi trilioni 1.3 zinakwenda bonde la Mto Msimbazi, pamoja na Daraja la kisasa la Jangwani linalokwenda kubadilisha maisha ya wananchi wa Magomeni na maisha ya wananchi wa Mzimuni. Hakika wale wakandarasi wapo mzigoni, na jana nilizungumza na Mheshimiwa Ulega, ameniambia hata fedha za kuanzia wameshapewa. Hivyo ndani ya miaka miwili Magomeni na Mzimuni patakwenda kubadilika pale, sijui tutakuwa kama nchi gani? Siwezi nikaielewa, lakini panaweza pakapendeza kama vile Young Africans ilivyo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisemee kidogo changamoto. Leo hii tulikuwa na changamoto ya elimu. Pale kwetu, huwezi ukaamini kwamba katika jimbo kubwa kama lile la mjini, lenye watu takribani laki nne, hawana high school, lakini kwa mara ya kwanza, tangu tupate uhuru Kinondoni tunakwenda kuwa na high school, ambayo Julai, 2025, keshokutwa, wanafunzi wa kwanza wanakwenda kusajiliwa pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hongera sana kwa Mheshimiwa Rais, amenifanya nijisikie, kila ninavyotembea nasema, naam. Mimi nipo sawa, na ndiyo maana wananchi wa Kinondoni watambue kwamba nami nimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunazungumzia shule za English Medium. Pale kwetu Dar es Salaam shule hizo unazikuta Upanga, lakini leo mpaka Uswahilini kwetu kule Kigogo kuna English Medium za kisasa, Magomeni za kisasa, Kijitonyama za kisasa, sasa tunataka nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa ambacho nawashukuru tena ni tatizo sugu la secondary school tulilokuwanalo katika Kata ya Tandale. Hili suala tulimfikishia mpaka Mheshimiwa Rais, akatupatia fedha, sasa hivi ninavyozungumza, Tandale wana secondary school ya kisasa na wapo form two. Nawashukuru sana Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, walitoa kibali shule ile iitwe Tarimba Abbas Secondary School, Alhamdulillah, nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye Kata ya Kinondoni, ambayo ndiyo kata ya nyuma kabisa, leo ina secondary school ya kisasa. Hivyo tumeondoa matatizo ambayo yalikuwepo katika jimbo langu, mambo yote, miundombinu ya elimu, yamekwisha hatudaiwi. Mheshimiwa Dkt. Samia hatumdai katika masuala ya elimu, Dkt. Samia hatumdai kwenye masuala ya afya, tumetimia. Tuna vituo vya afya, tuna dispensary tena za kisasa. Changamoto iliyopo ni pale Tandale peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Manispaa tumetenga shilingi milioni 600 kwa ajili ya upanuzi wa Kituo cha Afya kile ambacho hupokea zaidi ya watu 1,000 kwa siku. Ukumbuke pale tuna soko la kisasa kubwa la nafaka, hivyo wananchi wanaokuja pale kupata huduma ni wengi sana. Tumeweka shilingi milioni 600 kwa ajili ya kununua eneo, lakini tutaomba Serikali, na hii naomba iwekwe kwamba, tungependa tutanue kile kituo chetu kiweze kuwa kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie matatizo ambayo yapo kule Mwananyamala, yaliyopo Magomeni, Tandale, Makumbusho, ambayo Serikali ya Dkt. Mama Samia imekwenda kutuondolea aibu hii, kwamba, Mto Ng’ombe wakati unajengwa, ambao ndiyo unapitia maeneo mengi sana na kuleta athari kubwa ya mafuriko, alimtuma Mheshimiwa Waziri Mkuu, alikuja kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alipokuja Mheshimiwa Waziri Mkuu alihakikisha mkandarasi anarudi katika eneo lile, lakini wale ambao walikuwa wanatakiwa kulipwa fidia ili wapishe ule mradi, fedha zile zikatolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza, Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Mchengerwa, matatizo ya mafuriko Kata ya Tandale, Makumbusho, Ndugumbi, Magomeni na Mwananyamala, ambayo yalikuwa yanaletwa na ule Mto Ng’ombe yale yameisha. Inyeshe mpaka inyeshe, watu wana-enjoy na hata kuamka saa nne wanaweza wakaamka. Hongera sana, Mheshimiwa Rais ametusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda nizungumzie jambo ambalo kidogo lina matatizo, ingawa hili nalo limetuletea mafanikio makubwa. Hakuna kata katika Jimbo la Kinondoni, Mheshimiwa Mchengerwa, ambapo tumeshindwa kujenga barabara hata moja. Kata zote tumeweka miguu yetu. Kuna kata tumefanya barabara nyingi na tumefungua uchumi wa wananchi wa Kinondoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Kigogo kuna masoko ambayo yalikuwa hayafanyi kazi, lakini kuna barabara inaitwa Mapera, tumeijenga ile kwa lami. Sasa hivi wananchi wanaweza kufanya shughuli zao za kibiashara vizuri zaidi na kuwanyanyua kiuchumi. Kata ya Hananasif, ambayo ilikuwa haina mradi, juzi tumewapeleka wakandarasi kwenda kujenga barabara tatu katika kata ile, Kinondoni ambako ndiko kulikuwa kumesahauliwa Barabara ya Best Bite. Wengi mnakaa Kinondoni mnaweza mkaiona sasa hivi Kata ya Kinondoni ilivyobadilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijitonyama kule anapotoka Mheshimiwa Mwenyekiti wangu, wazawa wa Kamati ya Bajeti tumetengeneza pale Mabatini, palikuwa panatisha. Sasa hata sijui nichangie nini zaidi ya kuwaambia Serikali, ahsanteni sana, Mheshimiwa Mama Samia ahsante sana. Kilichobakia ni kitu kidogo sana na wala sitaki nimsumbue Mheshimiwa Mama Samia, namsumbua huyu Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, ndio nakwenda naye baada ya bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mungu awabariki sana TAMISEMI, wanafanya kazi vizuri sana, ahsante. (Makofi)