Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Bupe Nelson Mwakang'ata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Kwanza kabisa, namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima mpaka tukawepo hapa kuchangia hoja muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee, naomba nimpongeze Spika wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, kwa kazi nzuri anazofanya. Jinsi anavyoliendesha Bunge, kwa kweli anastahili pongezi, maana wakati mwingine tunajiuliza, ni wakati gani anapumzika? Unabaki kumshukuru Mungu, kwa ajili yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Waziri, kaka yangu, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa na Manaibu wake wote wawili kwa kazi nzuri. Kwanza kabisa, nampongeza kwa uchaguzi uliopita wa Serikali za Mitaa, ameweza kuendesha vizuri sana, nchi yetu ina amani, tumepata viongozi walio bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii pia kumpongeza Mkuu wangu wa Mkoa, ndugu yangu Makongoro, kwa kusimamia vizuri Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Pia, nakishukuru sana Chama changu cha Mapinduzi, Mkoa wa Rukwa, kimeweza kusimamia vizuri Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nampongeza sana Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anazozifanya katika kipindi chake cha miaka minne, amefanya mambo mengi makubwa na mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wetu wa Rukwa, tulikuwa tuna changamoto sana ya hospitali za Wilaya, lakini Mama katika kipindi chake ameweza kutupatia fedha za kujenga hospitali za wilaya, wilaya zote nne tumepata hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi kati hapa tumezindua Hospitali ya Isihofu iliyogharamiwa takribani shilingi 4,500,000,000, sasa hivi imeanza kutumika. Pia, Sumbawanga DC hospitali imefunguliwa, tulipokea fedha takribani shilingi 4,500,000,000, kwa ajili ya ile hospitali ya wilaya. Tumejengewa hospitali wilaya zote, hongera sana Mama, umeupiga mwingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, Mheshimiwa Rais ametujengea vituo vya afya vizuri. Kipo kituo cha mfano Sumbawanga Mjini. Kile kituo sisi akina mama zamani tulikuwa tuna hofu, ukiwa mjamzito ukiambiwa unafanyiwa operesheni, unajihesabia mawili, aidha kufa au kupona, lakini sasa hivi vituo vya afya vyote, hasa kituo kile, ukienda mjamzito, akina mama sisi tunaomba ufanyiwe operesheni badala ya kusukuma na kuchanika msamba. Sasa hivi hakuna tena kuchanika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madaktari wapo vizuri, ukifanyiwa operesheni siku ya kwanza, ya pili, ya tatu, umeshaamka. Kwa hiyo, mama ametuletea huduma nzuri sana katika vituo vyetu vya afya, lakini pia, huduma zimejitosheleza. Kwenye vituo vya afya majengo ya mama na mtoto yamejitosheleza kabisa, ukijifungua mtoto njiti, mtoto anawekwa vizuri anakua bila wasiwasi. Hongera sana Rais wetu mpendwa, kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie sasa kwenye hoja zangu za msingi, naanza na Kituo cha Afya cha Kirando. Kituo kile ni kikubwa sana, kinahudumia vijiji vingi sana na kata zaidi ya nane; Kata ya Korongwe, Kata ya Kipili, Kata ya Kitete, Kata ya Mkinga, Kata ya Ninde na Kata ya Kirando. Kile kituo cha afya kinahudumia vijiji vingi sana. Tulikuwa tunaomba kipandishwe hadhi iwe hata hospitali ya Wilaya, lakini kituo kile hakina mortuary, pa kulaza miili panakuwa na uhitaji. Tunaomba kituo kile kijengewe jengo la mortuary. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la barabara. Kwanza kabisa, nampongeza Mkurugenzi wa TARURA, anafanya kazi nzuri, lakini nilikuwa naomba kwenye TARURA bajeti iongezeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna barabara nyingi ambazo zinahitaji huduma. Kuna barabara inayotoka Mto Wisa kupitia Ng’ongo kuingia Kristo Mfalme, barabara ile ni muhimu sana. Tulikuwa tunaomba TARURA waongezewe fedha kusudi iweze kutengenezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la maboma. Tunaomba pia, bajeti ya elimu iongezwe kwa sababu tuna maboma mengi ambayo bado hayajakamilika. Kwenye Wilaya ya Sumbawanga kuna maboma mengi sana ambayo hayajaisha, nikianza na maboma ya zahanati, tuna boma pale Kifinga, Msia, Tululu, Kilando, Legeza, Ilemba, Kapewa, Mtetezi na Sikaungu. Tunaomba basi, bajeti ya safari hii haya maboma yaweze kupatiwa fedha na hatimaye yaishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee hoja nyingine ya akina mama. Kwanza kabisa, tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutupatia ile 10%, ambayo ni ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Kwa kweli, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kweli, ile huduma ni nzuri sana, akina mama wanapata mikopo na hiyo huduma inaendelea vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Jukwaa la Wanawake. Jukwaa hili lilianzishwa kwa ajili ya (Mheshimiwa Waziri naomba unisikilize) uwezeshaji kiuchumi wa akina mama, lakini jukwaa hili naona kama limetelekezwa. Akinamama, viongozi wa majukwaa haya ya uwezeshaji, wanapata tabu sana kwa sababu, hawana fungu, hawana bajeti. Kwa hiyo, inakuwa ni tabu tupu. Nilikuwa naomba Jukwaa la Wanawake la Uwezeshaji kiuchumi lipatiwe fungu na bajeti yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala lingine la mikopo ambayo ilikuwa inaitwa Imbeju. Wanawake waliitikia mwitikio mkubwa sana kupata mikopo inayoitwa Imbeju. Wakachangishwa fedha, wakaambiwa wafunge akaunti, wakaambiwa waandae mihtasari, lakini matokeo yake akina mama walifungua akaunti, wametoa fedha zao, wamepoteza muda, lakini hamna kinachoendelea kwenye suala zima la mikopo ya Imbeju.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba nayo waifanyie kazi ili akina mama hawa waweze kupata mikopo hiyo. Kama haipo, basi waambiwe kwamba mikopo ya Imbeju haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee pia suala la watumishi. Mama amejenga vituo vya afya, amejenga shule, lakini Mkoa wa Rukwa tuna upungufu wa watumishi kwa 75%. Tunaomba sasa watuongezee watumishi, na watumishi hao wajengewe nyumba; kwa sababu watumishi wengi wakiletwa katika mikoa yetu ya pembezoni na wakipelekwa vijijini wanahama tena kurudi mjini kwa sababu kule kunakuwa na changamoto pengine za nyumba za watumishi. Kwa hiyo, tunaomba watumishi wajengewe nyumba ili waweze kutulia kule. Endapo wanapokuwa wanawaajiri wawe wanawapa mikataba kwamba hakuna kuhama, ndani ya miaka tano hahami mpaka hapo atakapomaliza miaka mitano ndipo afikiriwe jinsi ya kuhama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)