Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nami kupata nafasi ili niweze kuchangia kwenye hotuba hii nzuri sana ya ndugu yangu Mheshimiwa Mchengerwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza, ameweza kuisoma hotuba yake vizuri. Nina hakika Wizara hii wamejipanga vizuri, yeye pamoja na wasaidizi wake, kwa maana ya Manaibu Waziri lakini na Katibu Mkuu pamoja na timu yake yote kwa ujumla. Hakika wanaitendea haki hii Wizara. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitaendelea kuungana na wenzangu tuendelee kuweza kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo imeendelea kushusha miradi mingi ya kimikakati ya kimaendeleo kwenye kila sekta; wameweza kugusa takriban sekta zote. Hapa kila mmoja akisimama hapa siyo kwenye kata, siyo kwenye vijiji, hakuna mahali ambako mradi haujafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi kule Wilayani kwangu Chunya takribani kila kijiji, na kila kata, kila mahali miradi imeenda imetiririka. Tunampongeza Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hakika ameonesha kwamba yeye ni mama na ni mama mwenye shughuli. Ndiyo maana tunasema tunamwongezea mitano tena; na sisi, pamoja na kumwongezea yeye na sisi bado tumo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa afya, mimi niseme kwamba kila mmoja amezungumza hapa, lakini sisi kule kwetu Chunya kwenye upande wa afya hospitali ya wilaya tumepata zaidi ya shilingi bilioni 5.7. Leo ukifika pale, na wale ambao hawajafika zaidi ya miaka miwili wakifika pale leo wanapotea kwa namna ambavyo majengo yamejengwa ya kisasa, vifaa tiba vimewekwa pale ndani na huduma sasa zinatolewa za viwango vilevile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine wakifika pale mpaka wanashangaa, kwamba ni hii Chunya tunayoifahamu au nyingine! Sisi ndiyo kazi ambayo alitupatia na tumeendelea kuifanya vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haijaishia hapo, katika kipindi hiki hapa cha Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na miaka mitano ambayo sisi tulipewa ridhaa hii vituo zaidi ya zahanati 15 tumeweza kuvijenga na vinatoa huduma. Haya kwetu sisi ni mafanikio makubwa kwa sababu tunasema mtu ni afya ndiyo maana afya imekuwa kipaumbele cha kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kana kwamba haitoshi, kwenye upande wa vituo vya afya zaidi ya vituo vya afya vitano vimejengwa ndani ya hii miaka mitano. Kituo cha Afya cha Mamlaka ya Mji Mdogo wa Makongorosi ni kikubwa, kina hadhi ya hospitali ya wilaya. Kimejengwa, kinatoa huduma, kina facilities zote, na mpaka huduma ya mortuary pale inatolewa na majokofu yamewekwa pale. Wananchi wananufaika kwa huduma hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, hatujatosha hapo, Kituo cha Afya cha Matwiga tulipata fedha na juzi tu takribani kama wiki tatu zilizopita tumepata zaidi ya shilingi milioni 200. Kazi inaendelea pale na huduma zinaendelea kutolewa. Kituo cha Afya cha Mafyeko tulipata zaidi ya shilingi milioni 300, kazi inaendelea lakini pia na huduma zinaendelea kutolewa pale na fedha zinazidi kutiririka kuhakikisha kwamba vituo hivi vinakamilika. Kituo cha Afya Kambikatoto ambacho ni zaidi ya kilometa 260 kutoka Chunya Mjini; kimejengwa kituo kizuri, Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alitupatia hizi fedha wananchi wananufaika pale na gari la wagonjwa tumewapelekea kule. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo imeweza kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi letu moja, haya yameweza kufanyika na mambo mengine bado yanaendelea kufanyika; tunaomba tuzidi kuongeza kwenye upande wa vifaa tiba, tupate vifaa tiba vingi na vya kutosha zaidi. Kana kwamba hiyo haitoshi, tupate pia na wataalamu wa kutosha. Vifaa vipo vichache ilhali pia majengo yapo ya kutosha, lakini tuna upungufu wa wataalamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri alichukue hili, atuletee wataalamu wa tiba tukahakikishe kwamba huduma za afya zinakwenda vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa elimu, kila mmoja hapa amekuwa shahidi, ameweza kuzungumza namna ambavyo kwenye upande wa elimu Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoweza kuigusa elimu kwenye jamii yetu. Yamejengwa madarasa ya kutosha, zimejengwa shule shikizi na shule mpya zimejengwa. Tukianza kutaja hapa shule mpya moja moja hatutamaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama amewekeza kuhakikisha kwamba elimu ndiyo mkombozi wa Mtanzania, ndiyo maana amepeleka fedha nyingi sana kwenye elimu. Kana kwamba haitoshi, ndani ya miaka minne ya Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tumeweza kujenga sekondari mpya tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga Sekondari mpya Lupa ya Maheka Girls, tumejenga Lualaje Sekondari, tumejenga Mafyeko, tumejenga Kambikatoto na tumejenga na Kata ya Nkung’ungu. Hizi sekondari mpya tano zimejengwa na sekondari mpya nyingine mbili zinaendelea kujengwa kwenye Kata ya Upendo na Kata ya Matundasi, kwa maana ya Kijiji cha Itumbi, tunaendelea kujenga. Haya kwetu sisi ni mafanikio makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeendelea, mwaka huu tumeweza kusajili sekondari nyingine mbili kwenda Kidato cha Tano na cha Sita. Tunategemea kwamba kuanzia Julai zipokee wanafunzi hawa wa Kidato cha Tano na cha Sita. Haya kwetu ni mafanikio makubwa sana. Tunampongeza Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tunaomba tuongeze juhudi sana ili tuhakikishe kwamba kwenye upande wa elimu tutatafanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnavyofahamu, Wilaya yetu ya Chunya ni moja kati ya wilaya kongwe; ilikuwa nyuma kwenye upande wa elimu na ndiyo maana sasa hivi tunakwenda kwa kasi zaidi. Kutokana na ukongwe wake huu, shule zile ambazo zilijengwa zamani, tuna shule kongwe nyingi, zimechakaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kwenye mipango hii tunajua tumeanza kupata fedha kwa ajili ya shule chakavu, lakini kwa Wilaya yetu ya Chunya kutokana na ukongwe wake na shule nyingi kongwe tunaomba atuangalie kwa jicho la huruma ili tuweze kupata fedha nyingi zaidi ili zile shule nyingi kongwe ambazo tunazo ziweze kupata fedha hizi na tuweze kukarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba uchumi ili uweze kwenda vizuri zaidi, lazima tuwekeze kwenye miundombinu, hasa miundombinu ya barabara. Wakati Mama Mheshimiwa Dkt. Samia anaingia madarakani sisi Wilaya ya Chunya bajeti yetu ilikuwa shilingi milioni 750 kwa mwaka, lakini leo tunavyozungumza tumefika shilingi bilioni 2.3.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mafanikio makubwa sana. Ndiyo maana tunaposema Mama, Mheshimiwa Dkt. Samia mitano tena hatuongei tu kwa kumpamba, ni kwa sababu amefanya kazi na inaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingi zimejengwa na nyingi zimetengenezeka. Barabara ya kutoka Chunya Mjini kwenda Ifumbo imetengenezwa kwa kiwango ambacho hakina mfano wake. Imejengwa kwa moramu, inapitika vizuri. Walikuwa hawana usafiri kule, leo wanalala magari matatu ambayo kila siku yanatoka kuanzia Ifumbo yanaenda sehemu nyingine mbalimbali. Haya sisi kwetu ni mafanikio makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara kutoka Njiapanda kwenda Sangambi imetengenezwa vizuri, Barabara ya kutoka Lupa kwenda Lualaje, Barabara ya kutoka Lupa - Nkung’ungu na Kambikatoto Sifa na nyinginezo zimefanikiwa vizuri. Pia, madaraja yameendelea kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba haya yamepiga hatua, lakini kwa jiografia ya Wilaya ya Chunya na kwa ukubwa wa Wilaya ya Chunya, leo Wilaya ya Chunya kijiografia ina zaidi ya square meter 13,000, ambapo square meter 13,000 hizi ukizijumlisha Wilaya ya Kyela, Rungwe, Mbeya Mjini, Mbeya Vijijini bado haijafikia Wilaya ya Chunya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bado tunapata bajeti ndogo, hizi shilingi bilioni 2.3. Pamoja na kwamba tumeongezewa, na tunaishukuru Serikali, tunaomba sana tuangaliwe na jicho la huruma ili tuweze kuongezewa bajeti hii ili tuweze kutengeneza barabara nyingi zaidi. Kwa sababu kwa sasa hivi barabara za kwenda vitongojini, nyingi hazijasajiliwa. Ndiyo kazi tunayoifanya, tuzisajili, ziingie kwenye mtandao wa TARURA ili tuweze kuweza kuiombea fedha na hivyo tupate fedha nyingi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kusajili barabara kadhaa, na tunaendelea kuzisajili barabara nyingine kwa sababu kule sasa hivi ndiko kwenye uchumi mkubwa sana hasa kama mnavyofahamu sisi Wilaya yetu ya Chunya ndio wazalishaji wa pili wa dhahabu kwa wachimbaji wadogo kwa Tanzania. Kwa hiyo, muone namna gani ambavyo barabara hizi zinakwenda kule kwenye maeneo ambako uchumi unazidi kufunguka; na ukiufungua uchumi wa kule maana yake ni kwamba, Serikali pia itapata mapato mengi zaidi, wananchi wataweza kunufaika kiuchumi, nasi kwa ujumla wake tutaweza kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya, lakini kupitia mapato ya ndani tumeweza kujenga na tunaendelea ujenzi wa stendi mpya pale Halmashauri yetu ya Wilaya ya Chunya. Naishukuru Halmashauri yangu ya Wilaya ya Chunya, Baraza la Madiwani na Mkurugenzi wetu ndugu yangu Tamim Kambona, anafanya kazi kubwa sana. Tumepata zaidi shilingi bilioni tatu na stendi inajengwa; na inawezekana ndiyo itakayokuwa stendi ya kwanza nzuri ya kisasa kwa Mkoa wa Mbeya inayojengwa kwa kupitia mapato ya ndani ambayo sisi Chunya tunaendelea kuijenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kazi ambayo wananchi walituamini kuifanya, tumeifanya kwa ukubwa wake, tumetekeleza Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi kwa kuhakikisha kwamba haya na mengine yanakwenda vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa 10% ya zile fedha kutoka kwenye Halmashauri, tunamshukuru mama yetu, baada ya kuzirudisha fedha, leo vikundi vingi zaidi vimeweza kunufaika. Awamu ya kwanza zilitolewa zaidi ya shilingi milioni 840 kwa Wilaya yetu ya Chunya; awamu ya pili ambayo kuanzia mwezi ujao wiki ya kwanza au ya pili tutakwenda kuzikabidhi. Tuna fedha ambazo zipo tayari shilingi bilioni 1.2, hizi zinapokwenda kwa wananchi maana yake tunakwenda kuunyanyua uchumi wa akina mama, vijana na walemavu wa Wilaya yetu ya Chunya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, tunaomba sana haya mengineyo ndiyo sababu inayotufanya leo hii tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo inaweza kufanya kazi kubwa na nzuri zaidi. Huduma za kijamii zinaendelea kuboreshwa zaidi, na sisi Wanachunya tunaendelea kuwaambia Mama, Mheshimiwa Dkt. Samia yeye hatudai, ila sisi tuna deni kwake, na hili deni tutampatia mwezi Oktaba kwa kumpa kura nyingi za kishindo zaidi ili aendelee kutumikia na sisi ambao tumechaguliwa na wananchi tuendelee kutumikia zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)