Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa, naomba nimshukuru Mungu ambaye ametupa neema kubwa, katika kipindi cha miaka minne tupo humu ndani tukiwa wazima na afya njema. Naomba nimshukuru sana Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo amewafanyia Watanzania katika Tanzania nzima hususan Mkoa wa Katavi pamoja na Jimbo la Nsimbo, amefanya kazi kubwa; ametuletea fedha nyingi na miradi mingi katika Jimbo la Nsimbo, Halmashauri ya Nsimbo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Mchengerwa pamoja na Manaibu wake wote wawili kwa kazi kubwa nzuri wanayoendelea kuifanya na usimamizi wa Wizara. Hongereni sana Mheshimiwa Waziri Mchengerwa. Nisimsahau Katibu Mkuu wa Wizara pamoja na Manaibu Katibu Wakuu wote ambao wanafanya kazi kubwa nzuri kwa ajili ya kuendeleza kutuletea fedha katika mikoa yetu tulipokuwa huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee sana naomba nimpongeze Mkuu wangu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko kwa kazi kubwa nzuri anayoifanya katika Mkoa wetu wa Katavi. Anahamasisha na ana maono. Mkoa wetu wa Katavi umetulia. Hongera sana Mkuu wetu wa Mkoa Mwanamvua Mrindoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nisimsahau Mkuu wetu wa Wilaya, Jamila Yusuph, kwa uhamasishaji wake anaoendelea kuufanya katika Mkoa wetu wa Katavi Wilaya ya Mpanda. Anafanya kazi nzuri, anahamasisha, ninaona anachukua kero mbalimbali. Naomba nimpongeze Mkuu wetu wa Wilaya, Jamila Yusuph. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiwasahau Chama cha Mapinduzi Mkoa, Kamati ya Siasa ya Mkoa, Kamati ya Siasa ya Wilaya ambao wanaendelea kusimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Naomba nimpongeze Mwenyekiti wa Mkoa wa Katavi wa Chama cha Mapinduzi na Mwenyekiti wa Wilaya yetu ya Mpanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nampongeza Mkurugenzi pamoja na watendaji wote kwa sababu fedha zote zinakwenda kwenye Halmashauri yangu. Wanafanya kazi vizuri na wanasimamia miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watendaji wote katika kata zote pamoja na Watendaji wa Vijiji wameendelea kusimamia miradi yote inayopelekwa katika maeneo yetu. Tusiwasahau Wenyeviti wa Vijiji pamoja na Wenyeviti wa Vitongoji kwa sababu wao ndio wahusika wakuu kwa kila kitu walichokuwa wanapelekewa katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiache kuwapongeza walimu, walipelekewa miradi mbalimbali wakaisimamia na leo tunawapongeza kwa kazi kubwa nzuri. Walimu wa shule za msingi, walimu wa shule za sekondari waliyabeba majukumu haya kwa kasi kubwa kwa ajili ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwapongeze Madiwani wangu 12 wa kata 12. Nimefanya nao kazi vizuri kwa kipindi chote cha miaka minne. Wote tumehakikisha kuwa miradi ambayo tuliiomba imefanikiwa kwa 100%. Naomba niwapongeze Madiwani wote na Mwenyekiti wa Halmashauri yangu ya Nsimbo kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kupitia mfumo wa manunuzi (NeST). Mfumo huu unasumbua wakandarasi sana, haujawa rafiki. Wakandarsi wengi sasa hivi wanashindwa kuingia kwenye mfumo huu kwa sababu unasumbua. Tender zinatangazwa, wanashindwa kuingia kwenye tender kutokana na usumbufu wa manunuzi jinsi ulivyo, na kwamba wengi sasa hivi wamekata tamaa. Naomba Mheshimiwa Waziri alitazame hili kwa kuwa mfumo wa sasa hivi siyo mzuri sana na siyo rafiki kwa ajili ya wakandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, naomba nipongeze kwa ajili ya fedha ambazo tumeletewa kwa ajili ukarabati wa maboma. Naomba tuendelee kufanya kazi hii kwa sababu wananchi wengi wamejenga maboma ya zahanati pamoja na shule za msingi. Naomba sana tupeleke fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa zile shule kongwe, kuna shule kongwe za siku nyingi, za miaka mingi, zimechoka, vyoo vinabomoka, vinatumbukia. Ukiangalia, walimu wanapata shida, nyumba za walimu zimechakaa, na nyingine zinabomoka. Nilikuwa naomba tuangalie kwa jicho la huruma zile nyumba ambazo zilijengwa zamani, kwamba zikarabatiwe ili walimu waweze kuishi katika maeneo hayo ili tuendelee na kazi ya kujenga Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Chief wa TARURA kwa kazi kubwa nzuri anayoendelea kuifanya. Tumepata fedha nyingi, miradi mingi ya barabara imetekelezwa na madaraja yamejengwa. Sasa hivi kule kwenye maeneo yetu mvua mvua zinanyesha; ubovu wa barabara, na bajeti yetu imekuwa ndogo kwa Mkoa wetu wa Katavi. Halafu fedha za mwaka huu bado madeni wakandarasi wetu hawajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, kutokana na kazi kubwa ya wakandarasi wa Mkoa wa Katavi ambao ni wavumilivu, wanatengeneza barabara bila hata kulipwa, sasa wamekaa muda mrefu huku certificates zikiwa zimefika. Nilikuwa naomba wakandarasi hawa wanaotengeneza barabara na kujenga madaraja walipwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na madeni hayo na kwamba kazi haziendi kabisa sasa hivi, hivyo TARURA waruhusiwe kutangaza kazi kwa sababu kazi zote zimesimamishwa. Waruhusiwe kutangaza kazi zote za ukarabati maana barabara sasa hivi kule kwetu Katavi zimeshachimbuka na nyingine zimekatika. Naomba basi ule ukarabati utangazwe na maboresho yaweze kufanyika kutokana na uharibifu wa mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mvua tunaihitaji kwa sababu ndiyo maisha yetu. Tunahitaji kufanya kilimo, wananchi wanahitaji kilimo lakini na hapo hapo kuna upungufu ambao umesababishwa na changamoto zinazotokea. Naomba sasa tuongezewe bajeti kwa ajili ya ukarabati na matengenezo katika Mkoa wetu wa Katavi kwa ujumla wake. Hizi fedha ziende ili zikarekebishe barabara pamoja na madaraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uharibifu, sehemu nyingine madaraja yamekatika kabisa, na watoto hawaendi shuleni. Kuna Kata kama ya Sitalike watoto sasa hivi wana taribani mwezi mzima hawaendi shuleni kutokana na kukosekana kwa daraja, maji yamejaa. Naomba sana basi tupewe bajeti ya dharura kwa ajili ya kutengeneza barabara za Mkoa wa Katavi hususan Jimbo la Nsimbo ili watoto waweze kwenda shuleni na mambo ya kijamii yaweze kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa afya, naomba niishukuru Serikali kwani katika Halmashauri ya Nsimbo kuna Hospitali ya Wilaya ingawa bado haijakamilika, lakini hivi karibuni tumeletwa fedha. Tuna vituo vya afya vinne, lakini vile vituo vya afya bado havijakamilika, bado hatujapata wodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishukuru, hapa karibuni nilipata shilingi milioni tisini tisini katika vituo vya afya viwili. Naomba sana niongezewe fedha kwa ajili ya mahitaji makubwa katika vituo wiwili, Kituo cha Afya cha Ugalla na Kituo cha Afya cha Itenka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa, naomba nishukuru kwa kupatiwa ambulance mbili katika Halmashauri yetu ya Nsimbo, lakini kwa bahati mbaya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa walikuwa hawana gari, wakaazima ambulance kutoka katika Halmashauri ya Nsimbo katika Kituo cha Afya cha Ugalla. Bahati mbaya walivyoichukuwa ile ambulance ikaenda kuanguka, ikapinduka. Sasa matokeo yake tumebaki na ambulance moja ambayo inahudumia wilaya na vituo vinne vya afya pamoja na zahanati, ile ambulance imebaki moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, kwa sababu hatuiombei ajali hata kidogo, ni bahati mbaya, ile ajali ilitokea ikiwa na mgonjwa akikimbizwa Hospitali ya Rufaa Mbeya, na kwa bahati nzuri gari limeharibika, lakini watu walipata unafuu, walipona. Tumewaombea Mungu wamepona, lakini gari ndiyo hilo limeharibika kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ningepatiwa ambulance nyingine kupunguza kasi ya wagonjwa kutoka sehemu nyingine hususan Kata ya Ugalla, kilometa 100 kutoka kata mpaka Makao Makuu ya Wilaya, ndipo kuna Hospitali ya Wilaya. Naomba kupatiwa hiyo ambulance ili iweze kukidhi mahitaji ya Wanaugalla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana kazi kubwa inayofanyika na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na wasimamizi wake wote, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa anajitahidi kuhakikisha trilioni za fedha zinazokuja na anazisimamia vizuri. Nawapongeza sana kwa kazi kubwa, na pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Mungu awabariki na awasimamie mpite wote kwenye Majimbo yenu na wale Viti Maalum mpite. Amen. (Makofi)