Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Michael Constantino Mwakamo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nami kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye hotuba hii ya Bajeti ya Waziri ndugu yangu, kaka yangu Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni shukrani za pekee kwa Mwenyezi Mungu kutujalia afya, mimi binafsi na Wabunge wenzangu leo tumesimama tena kwenye Bunge hili tukiwa tunatimiza miaka ya kikanuni kabisa ya kuwahudumia wananchi waliotuagiza kuja hapa. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa afya njema na kutufanya tutekeleze majukumu yetu salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Serikali yake kama ambavyo wenzangu wote wamefanya hivyo. Kiukweli kabisa sisi Wabunge, hasa mimi wa Jimbo la Kibaha Vijijini nina kila sababu ya kushukuru kila nikisimama kwa namna ambavyo Mheshimiwa Rais analitendea Jimbo langu mambo mema na makubwa ambayo miaka kadhaa ya nyuma hayakuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, historia hii imeandikwa na Mheshimiwa Rais kwa sababu ya miradi mingi iliyokuja katika jimbo lile, lakini imenifanya nami Mbunge wa form one kuwa na historia ya pekee ambayo haijawahi kuvunjwa kwenye Jimbo letu. Miradi mingi ya kimkakati imetekelezwa, na imetekelezwa tofauti na waliokuwa wanafikiri wao ni ma-senior kwenye jambo hili, namshukuru sana, sana, sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yake yote ya TAMISEMI, kwa maana ya kuanzia yeye, Manaibu wake, Watendaji wake Wizarani mpaka kule mkoani, tena kule mkoani Mheshimiwa Waziri ile timu ya kuanzia mkoani mpaka kwenye ngazi ya halmashauri yangu, kwa maana ya Mkuu wa Mkoa kaka yangu Kunenge, ndugu yangu Nickson na Mkurugenzi, dada yangu Bieda, hakika ingekuwa ni forward ya timu ya mpira, basi ningesema ile ni sawasawa na timu ya Simba. Inashambulia kwa hatari, na ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri aitazame timu ile ibaki katika mikono salama, imalize shughuli tulizozianza bila kufanya lingine lolote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli kubwa ambayo Mheshimiwa Waziri ninakuomba sana kwa muda huu, tunakoelekea, acha wamalize kazi kubwa waliyofanya na mimi halafu kama yatatokea mengine mwezi wa Kumi itakuwa ni baadaye, kwa sababu kwa kweli ni timu ambayo inamsaidia Mheshimiwa Rais, inaungana na mawazo ya Mbunge, inasimamia miradi ya wananchi na miradi imekwenda kwa kasi ya ajabu sana. Kwa hiyo, nakushukuru sana wewe kwa sababu, ni imani yangu kwamba, siyo tu kwa sababu unatoka Pwani, ni kwa sababu ameikamata Wizara sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, sisi kule Pwani tuna vitu viwili vinafanana, na kaka yangu Mheshimiwa Mchengerwa na watu wengine wachache wanaweza wakavikumbuka nikiwatajia. Kwetu kuna kitu kinaitwa furu, ni tunda la porini ambalo Mwenyezi Mungu amelileta na sanasana nafikiri linapatikana Pwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kuna kitu kinaitwa sizi. Mbegu ya furu itakapokuwa inachanua ni ya kijani, hii ni ishara kabisa ya Chama cha Mapinduzi, lakini inapoiva ina tabia ya kujificha kwenye rangi nyeusi. Ukijificha kwenye rangi nyeusi inafanana na sizi. Sizi ni kipande cha mkaa. Sasa kule Pwani wanajua kwamba ukiiweka sizi hapa na ukiiweka furu hapa, kama mtu hatambui kati ya vitu hivi kipi kina ladha, wanaweza wakakimbilia sizi. Vilevile, kule Kibaha Vijijini wanafahamu sizi na wanafahamu furu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na utendaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan na uimara wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha niliyesimama hapa ninazungumza, wanafahamu wakati ukifika baada ya ratiba hii iliyobadilishwa juzi, watatambua sizi ni nini na furu ni nini? Mheshimiwa Waziri nibebe hizi kama salamu kwa Mheshimiwa Rais, zifike kwamba Wanakibaha Vijijini wanajua furu yao na wataijaza kwenye makapu yote na mapakacha ya Pwani mwezi Oktoba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kutoa pongezi, nimesema wakati naanza kuzungumza, wakati naingia hapa mwanzoni kabisa mwa Bunge la Kwanza nilipokuja kama Mbunge, nilijawa hofu kubwa sana, nilipokuwa naangalia awamu ya kwanza ya uendeshaji wa Bunge, lakini nampongeza sana Mheshimiwa Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maana yake ma-senior wa humu ndani akiwemo Kaka yangu, Mheshimiwa Kigua, alikuwa ananipa mashaka kwamba hivi nitapata nafasi ya kuuliza hata swali la nyongeza na jina langu halijulikani? Nampongeza sana Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Naibu Spika, na Wenyeviti, ninyi mliomsaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila niliposimama kwenye kona hii, jina langu lilitamkwa vizuri na niliwasilisha mawazo ya wananchi wa Jimbo la Kibaha. Uhodari wenu wa kuyashika majina yetu hata kama sio wazoefu ndani ya Bunge hili, nina kila sababu ya kupongeza uongozi wake Mheshimiwa Spika; na kwa sababu yupo ndani ya Bunge hili, naona aangalie kwa vitendo bila kusikia sauti yangu, makofi haya ni kwa ajili yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu waliotangulia kusema wamejaribu kueleza namna miradi mikubwa iliyofanyika Jimboni, sina tofauti nao. Ili nisiweze kula muda wangu katika kueleza kila mradi uliofanywa, nihitimishe maneno haya ya kupongeza miradi kwa kumwambia, yaliyofanywa Jimboni ni ya hatari, ni makubwa, ni mengi na wananchi wanatambua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa ninayotaka kuifanya hapa leo, kwanza ni kutoa mifano michache ya mambo makubwa ambayo hayajawahi kufanyika, lakini pia nitatoa maombi maalumu na ushauri kidogo Serikali ikafanye utekelezaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mifano michache ninayopenda kuitumia kwenye sekta ya elimu. Jimboni kwangu Kibaha kuna mabadiliko makubwa sana, miaka mitano hii, shule nane za sekondari zimejengwa na watoto wanaendelea kudahiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiichukua sekta ya afya na sekta ya elimu msingi na sekondari, kwa miradi yake iliyotekelezwa kwenye sekta hii imetumika shilingi bilioni 19.57. Ni kitu ambacho hakijawahi kufanyika kwenye Jimbo la Kibaha kwa muda mrefu, japo yapo maneno ya kufikiri kwamba watu hawaijui furu au sizi, wakidhihaki jitihada hizo wakiamini vitu hivi vinashuka tu. Nataka niwaambie, Wanajimbo la Kibaha, kila king’aacho basi ujue kimesafishwa na anayekitunza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kazi ya miradi hii iliyofanyika Jimboni, haina tofauti na haina kipingamizi kumwambia Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Mwakamo, Watendaji wa Serikali pamoja na Madiwani wa Jimbo hilo kwa awamu yetu, tumetekeleza wajibu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa shukrani hizi na kueleza michango hii ya miradi iliyotendeka kwa ufupi huo, naomba niseme, kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri leo amelizungumzia Jiji la Kwala. Kwanza naipongeza Serikali na kama Mheshimiwa Rais asingekuwa na utashi binafsi wa kutupendelea, asingekuwa na sababu kuifanya Kwala iwe kwenye vinywa na mipango mikubwa ya Serikali kama ilivyo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa yapo maeneo mengine yana ardhi kubwa na yanaweza kufanya miradi ambayo Kwala imekusudiwa, lakini Mheshimiwa Rais ametupendelea na amesema lianzishwe jiji maalumu litakaloitwa Kwala litakalokwenda kuwa kongani la viwanda, na linalokwenda kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenye hili Jiji la Kwala, wakati Serikali inaendelea kuliandaa, nawaomba mliandae na miundombinu yake. Jiji la Kwala lipo pembezoni kidogo mwa barabara kubwa ya Dar es Salaam, lakini limepitiwa kabisa na reli zetu mbili; ipo reli ya SGR na ipo reli yetu ile ya zamani. Kwa hiyo, naomba sana, tutengeneze barabara kama ambavyo tumeanza kutengeneza barabara ya lami kutoka Vigwaza kwenda Kwala, zipo barabara kama ya kutoka Kwala kwenda Ruvu, ni muhimu ikashughulikiwa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo barabara ya kutoka Kwala kwenda Gumba kutokea Chalinze, ni muhimu ikashughulikiwa kwa wakati. Ipo barabara ya kutoka Kwala – Kimara Misale inakwenda Morogoro Vijijini. Hii ni muhimu ikashughulikiwa kwa wakati. Barabara hizi zikifunguka tafsiri ya kuitengeneza Jiji la Kwala linakwenda kuwa la kishindo kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, yapo maombi maalumu ambayo nayawasilisha hapa kwa ajili ya kuomba utekelezaji wake. Kwanza, kuna hii tafsiri tunaizungumza wengi, kwa sababu zile barabara hazikamiliki. Kwanza nampongeza Kiongozi wa TARURA ndugu yetu Seff kama ambavyo amepongezwa na wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nakataa kwamba siyo kweli kwamba TARURA ina bajeti ndogo sana. Nitatoa mfano mdogo sana. Kwa mwaka Mkoa wa Pwani, TARURA inapokea shilingi bilioni 32, hebu zidisha shilingi bilioni 32 mara idadi ya mikoa ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nina ushauri kidogo. Tunaziona fedha hizi ndogo kwa sababu ya namna tunavyozitumia. Kila mwaka mkoa unatumia shilingi bilioni 32 kufanya ukarabati kwenye barabara ambazo ikinyesha mvua moja ya masika, hujui kama umeifanyia ukarabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, tungeweza kutengeneza utaratibu, na kupanga ni kuchagua. Leo hii sisi SGR imefika Dodoma, tunafurahia kipande ambacho tunakitumia na watu walioko Katavi na walioko Mwanza wanaifurahia na wanaisubiri ifike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye TARURA tungekuwa na utaratibu kwa mfano, fedha zinazokwenda kwenye mkoa, tukatafakari katika fedha zile zisigawanywe katika mazingira ya kidogo kidogo, tuamue tunashambulia barabara ngapi za kimkakati kwa mkoa. Kama ni barabara mbili za Mkuranga, kama moja ya Kibaha Vijiji, lakini ni barabara ya kimkakati, tukiimaliza japo kwa lami nyepesi, maana yake miaka 10, miaka 15 tutakuwa haturudi hapa, tutakuwa tunakwenda kufanya kazi kwenye barabara nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivi, kwa mfano kwa hii shilingi bilioni 32 ya Mkoa wa Pwani, mimi na wewe na ndugu yangu yupo pale pembeni Bwana wa Kibiti, ninaamini kabisa tukikubaliana wenyewe kwenye mkoa wetu, tukazielekeza shilingi bilioni 32 za mwaka mmojawapo, tukashambulie kwangu mimi kwa mfano, halafu tukaja kwako ninaamini kabisa baada ya miaka mitano hizi kilometa zinazotajwa za mkoa, kilometa 5,172 zitakuwa zime… (Makofi/Kicheko)

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tulia kaka, muda umekwisha, naunga mkono hoja. Ahsanteni kwa kinisikiliza. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante kwa kunisikiliza.