Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Nicholaus George Ngassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, nami kupata nafasi ya kuchangia jioni Bajeti yetu ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii ambayo nimeipata jioni hii kuongea katika Bunge hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango yangu itakuwa itakuwa imejikita na sehemu tatu. Sehemu ya kwanza nitakuwa nikieleza mafanikio, upande wa pili nitakuwa nikieleza changamoto lakini pia upande wa tatu nitakuwa ninatoa ushauri nini kifanyike ili tuweze kusonga mbele; na ndiyo faida ya kuwa na Wabunge vijana ambao bado akili zinachemka vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo letu la Igunga tulipata bahati, kati ya mwaka 2021 mpaka 2025 tulipata ziara ya viongozi wakuu watatu wa nchi hii. Tarehe 17 Mwezi wa Kumi, 2023 Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya ziara kwenye jimbo letu. Mheshimiwa Rais alikuta umati mkubwa sana wa watu, walimpokea kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa kumi na mbili jioni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uwanja tulioutumia unaitwa Uwanja wa Barafu, historia inaonesha kwa mara ya mwisho ule uwanja ulijaa mwaka 1993 mimi nikiwa Darasa la Kwanza, kipindi hicho walikuja Wazungu kuonesha sinema zile. Waliweka pale sinema, tulijaa sana pale kipindi kile wakati wanatoa elimu ya mambo mbalimbali ya afya ya jamii. Uwanja ule ndiyo ulijaa kwa mara ya mwisho na ukajaa kuvunjwa rekodi alipokuja Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi walijitokeza kwa wingi ikiwa ni shukurani kwa Mheshimiwa Rais kwa miradi mikubwa ya maendeleo ambayo ametufanyia takribani shilingi bilioni 100 zimeingia kwenye Jimbo letu la Igunga. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, tarehe 8 Oktoba, 2024 Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Makamu wa Rais pia alipita Igunga; na tarehe 12 Machi, mwaka huu 2025 Mheshimiwa Waziri Mkuu alipita. Tunawashukuru sana viongozi wetu hawa wakuu kwa kutenga muda wao kufika katika Jimbo letu na Wilaya yetu ya Igunga ambapo waliweza kujionea kwa uhakika na kwa uhalisia yale ambayo tumekuwa tukiyasema kila mwaka wameyafanya makubwa katika kipindi hiki cha miaka mitano. Tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia hoja yangu ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, nina mambo kama manne au matano nitachangia. Jambo la kwanza ni sekta ya elimu, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mchengerwa pamoja na Manaibu wake, Makatibu Wakuu pamoja na Watumishi wote wa Wizara, wamekuwa wakifanya kazi vizuri sana usiku na mchana. Unapoongelea TAMISEMI, nadhani shughuli takribani 80% za menejimenti ya Serikali zipo chini ya mikono yao. Wamekuwa mkipambana sana usiku na mchana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa hongera sana Kaka yangu Mheshimiwa Mchengerwa, hongera dada yangu Mheshimiwa Zainab, Kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Dugange na wasaidizi wako wote mmetutendea haki. Kwa kweli siku hizi vijana wanasema, hamna baya. Nasi tunasema hamna baya kwa kweli, mlikuwa mnafikika muda wote. Pia, tunawatakia heri katika majukumu yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya elimu tumefanya makubwa sana, elimu msingi na elimu sekondari. Hakuna Jimbo nchi hii ambalo halijajengewa madarasa, hakuna Jimbo nchi hii ambalo halijajengewa maabara, hakuna Jimbo nchi hii ambalo halijajengewa shule shikizi, miundombinu ya kila aina kwenye elimu, elimu bila malipo, uendelezaji wa walimu, ajira za walimu lakini pia na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ya elimu, kujenga vyoo na kila kitu. Wamefanya makubwa sana katika sekta ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa ushauri, changamoto ambayo imebaki pamoja na kwamba tumejenga madarasa mengi, kuna changamoto kubwa ya ujenzi wa nyumba za walimu, vyoo vya wanafunzi na vyoo vya waalimu. Sasa hii changamoto mbele nafikiri Mheshimiwa Mchengerwa mnaweza mkaumiza vichwa. Mimi ninawapa ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mashirika ya ujenzi ambayo yapo chini ya majeshi yetu, tuna Police Cooperate Society, tuna SHIMA lipo chini ya Magereza lakini tuna SUMA JKT. Tengenezeni model mwingie nao mikataba hawa watu waweze kujenga nyumba za walimu nchini au vyoo, tuachane na tatizo la vyoo kwenye shule zetu nchini na nchi nzima kwa ujumla. Mnaweza mkawapa mkataba wa muda mrefu hata wa miaka mitatu kwa sababu ni mashirika yaliyo chini ya Serikali yetu, mtakuwa mnaenda mnalipana taratibu kutokana na makusanyo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuachane na habari ya kuja huku tunasema tunaomba vyoo au tunafika kule kwenye ziara za viongozi tunaanza kusema hakuna vyoo. Haya mashirika ni ya wazalendo, na yapo chini ya majeshi yetu. Mnaweza mkaingia mkataba mkubwa hata kama ni wa miaka mitano, lakini mna-assurance kwamba mtakuwa mnawalipa kidogo kidogo kutokana na makusanyo ya nchi. Itakuwa ni mfumo mwingine wa Force Account ambao uta-deliver kwa uhakika katika nchi nzima kwa wakati mmoja. Hilo ni jambo moja kwenye sekta ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kwenye suala la barabara za mijini na vijijini. Nawapongeza kiukweli TAMISEMI, mmesimamia vizuri sana TARURA. Moja ya eneo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais hata alipokuja Igunga nilimwambia na kumshukuru, alipofanya uamuzi wa kuamua fedha za barabara kila jimbo lipatiwe na liamue linaenda kutengeneza barabara za aina gani, Mheshimiwa Rais alifanya uamuzi mkubwa sana na hili jambo limetusaidia kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga madaraja mengi kwenye mito ya msimu na mito ya wakati wote na tumetengeneza barabara za lami. Kwa mfano, sisi pale Igunga kwa sasa tuna mtandao wa barabara za lami pale mjini takribani kilometa 20 wakati zamani lami ilikuwa historia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mtandao wa barabara za mataa. Barabara za vijijini tumetengeneza za changarawe na kila eneo tumegusa. Kuna madaraja ya kwenye mito yalikuwa yameshindikana kwa muda mrefu, lakini tumeweza kuyatengeneza kutokana na huu uamuzi makini wa Mheshimiwa Rais wetu wa kuhakikisha kwamba tunapatiwa fedha kwenye jimbo, tunakaa na wataalamu na tunaamua nini cha kufanya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ambayo nimeiona bado ipo kwenye huu utaratibu ambayo nadhani Mheshimiwa Waziri anaweza akaumiza vichwa na wataalamu wake wakalitafutia ufumbuzi, ni michakato ya kupata wakandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba kuna utaratibu wa Sheria ya Manunuzi, lakini kwa upande wa TARURA imekuwa ni ya muda mrefu sana. Wamekuwa na changamoto, wakipata wakandarasi baadaye wanarudi wanasema mkandarasi hakukidhi vigezo. Tumejikuta jambo dogo linatumia muda mrefu sana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri na wataalamu wake kwenye hili waumize vichwa ili kutatua hili tatizo kwa sababu linatukwamisha kwa muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza kutoa mfano, Mheshimiwa Rais alipotoa zile fedha za dharura kutengeneza zile barabara, zilichukua muda mrefu sana mpaka zikaanza kuleta kelele humu Bungeni mwaka 2024, lakini ni kutokana na huu mfumo wa upatikanaji wa wakandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalieni hili mlitatue ili tuweze kutatua changamoto. Barabara inapokatika, tunahakikisha ndani ya miezi miwili au mitatu tunakuwa tumeweza kuimaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nashauri, mnaweza mkatengeneza mwongozo na component ambayo baadaye mnaweza mkaiweka kwenye regulations. Tunapopeleka fedha za barabara, kuwe na percentage fulani, kwenye kila shilingi tunaweza tukakubaliana 10% au 30% ibaki kwa ajili ya maintenance.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia sana inaponyesha mvua kwa dharura, kwa sababu tunaelewa mvua za nchi hii nyingi ni za ukanda, na ni za muda mfupi. Inaponyesha mvua ya dharura, ikitokea changamoto kwenye barabara tusisubiri tena financial year inayofuata ndiyo waje watatue tatizo la ile barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajikuta tumengeneza barabara kilometa 20, imekatika kipande cha mita 100 na barabara inaacha kupitika mwaka mzima. Mheshimiwa Waziri, hii inakuwa haina value for money, hivyo mtengeneze mwongozo ambao utakuja kutusaidia, zinapotokea changamoto tunazimaliza kwa wakati na haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine unakuta linatokea tu eneo korofi dogo, lakini TARURA Wilaya, TARURA Mkoa hawana fedha ya kutengeneza maeneo korofi. Sasa mkiweka, kutakuwa na kile kikapu pembeni cha fedha ya uhakika. Kama barabara imetoboka au imetoka shimo, itakuwa siyo mpaka kusubiri financial year inayofuata ili iweze kutengenezwa. Hilo ni kwa upande wa eneo la barabara vijijini na mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kwenye ujenzi wa masoko ya kimkakati. Ukiangalia katika maeneo mengi sana kumekuwa na utaratibu wa kujenga haya masoko ya kimkakati. Sasa mimi ninashauri kitu kimoja. Jambo la kwanza, ili nyie TAMISEMI muweze kushusha huu mzigo, toeni maelekezo kwa halmashauri inayohitaji kujenga soko la kimkakati, itafute eneo liwe katikati ya mji kabisa. Tuachane na ile biashara ya kujenga soko la kimkakati kilometa 15 kutoka mjini, mkijidanganya kwamba tunavuta mji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna kuvuta mji, mtajenga soko na litakosa biashara. Watafute eneo katikati ya mji na mwaambie waanzishe kama tulivyokuwa tunajenga maboma halafu wakifika kwenye lenta nyie TAMISEMI ndiyo muingie kumalizia. Tutajenga masoko yote na yatakuwa na ufanisi kabisa. Tutaachana na kujenga masoko nje ya mji, yanachosha wananchi. Matokeo yake wananchi wanaenda kwenye magenge na mmejenga soko la bilioni limekaa halina kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, waambie kama ni halmashauri itafute kiwanja katikati ya mji hata kama ni cha kununua kwa kulipa fidia. Maana yake katikati ya mji litakuwa na tija na kila mtu atakwenda. Hilo ni upande wa masoko ya kimkakati. Mheshimiwa Waziri, Mawazo yangu ni hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu Sekta ya Afya. Nawapongeza sana kwenye Sekta ya Afya. Tumejenga vituo vya afya vingi, zahanati nyingi, tumetoa ambulance, vifaatiba, na tumejenga mpaka hospitali zenye ICU.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Igunga zamani tulikuwa tunakwenda Bugando Mwanza. Sasa hivi tuna ICU ya maana kabisa na ya kisasa inayoweza kuhudumia wagonjwa 10 mahututi kwa wakati mmoja hata kama wamepata ajali. Tuna wodi za mama na mtoto za kila aina. Sisi tuna wodi ya mama na mtoto inayoweza kuhudumia akinamama 55 kwa wakati mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu. Ameweka commitment kubwa kwenye Sekta ya Afya. Unapoongelea ustawi wa nchi, maana yake unaanza na afya ndiyo inafuata elimu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa changamoto ambayo bado ninaiona kwenye Sekta ya Afya ni ndogo sana. Kwenye Sekta ya Afya changamoto ni customer care tu. Wale wahudumu wa afya bado maneno yao siyo mazuri kwa Watanzania na kwa wananchi hususan kwa akinamama wanaojifungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa ni suala tu la uwajibikaji na wasimamizi wanaowasimamia. Muwape miongozo na uwajibikaji uwe wa kiwango cha juu ili tuweze kupunguza. Wananchi wanapokuwa harassed, wanatukanwa na wanapewa maneno mazito mazito wanajikuta wanawachukia viongozi kwa sababu ya chuki na hasira za mtu mmoja ambaye unakuta amegombana na mume wake, lakini anaenda kutukana akinamama wanaojifungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano ni suala la mafunzo ya watumishi wa halmashauri. Hili linahusiana kidogo pia na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, lakini kwa kuwa asilimia kubwa ya watumishi ni wa kwenu, jitahidini sana kuweka mkazo katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifanya tathmini, watumishi wa umma wengi wanaosoma na kujiendeleza sasa hivi, wengi wanajisomesha kwa gharama zao wenyewe na wanajiendeleza kwa gharama zao wenyewe. Sasa Mheshimiwa Waziri mliangalie hili. Kama pale Wizarani mna kitengo au mna dawati linalohusiana na masuala ya mafunzo, basi muwape kipaumbele sana watumishi hususan kada za chini na kada za kati. Wasiwe wanasubiri mpaka Tume ya Uchaguzi wanakuja na shughuli zao, ndiyo wanarudi mjini wanafundishwa wanaondoka. Mwawekee elimu ambazo zinaendana na ujuzi, taaluma na kazi wanazozifanya ili kuweza kujenga capacity za watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kwa umuhimu mkubwa natoa shukurani na pongezi kwa Mheshimiwa Spika wetu Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson; Naibu Spika, Mheshimiwa Zungu; Wenyeviti na watumishi wa Bunge kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakitupatia katika kipindi chote hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoongea neno ‘Bunge’, inakuja picha ya Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson ambaye ni Spika mpenda haki sana. Mara nyingi unaposema neno ‘haki’ ukiwa katika viwanja hivi, basi unaona picha ya Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Spika alikuwa muungwana sana hususan kwa sisi Wabunge ambao ni vijana tunaokua, ametuvumilia lakini ametulea na amekuwa mlezi mwema.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)