Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie katika bajeti hii muhimu ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia, napenda kuanza kwa kunukuu kauli ya Mheshimiwa Waziri aliyeitoa kwenye ukurasa wa 138 wa hotuba yake akisema, “Naomba tusimame pamoja, siyo tu kama viongozi wa leo, bali kama warithi wa kesho tunaojenga Tanzania mpya kwa misingi ya uwajibikaji, ushirikishwaji na maendeleo yanayogusa maisha ya kila Mtanzania kuanzia mijini hadi vijijini.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri tangu mwanzo mpaka mwisho unaona kabisa dhamira ya dhati ya Wizara ya TAMISEMI kutaka kuunganisha Taifa, kuwatumikia Watanzania na kuhakikisha kwamba katika kuliunganisha Taifa, kila mtu atashiriki katika zoezi hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitayaunganisha hayo maneno yangu na mifano michache ambayo nimeiona katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Ninaanza na namna ambavyo Wizara hii imeanzisha mfuko maalum kwa ajili ya kuwasaidia fedha za mitaji wakandarasi wazawa wa Kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko huu uliopewa jina la Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan, unaitwa Mfuko wa Samia Infrastructure Bond. Mfuko huu walitegemea kuuza hisa zenye thamani ya shilingi bilioni 150. Hisa hizi zimenunuliwa na Watanzania. Mwitikio mkubwa waliouonesha Wananchi wa Kitanzania wa kawaida sana, lengo lilikuwa ni shilingi bilioni 150, lakini mpaka tunavyozungumza hivi leo, tumekusanya zaidi ya shilingi bilioni 300 katika Samia Infrastructure Bond. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushiriki wa wananchi katika kununua hisa za Mfuko wa Samia Infrastructure Bond unaonesha ushirikishwaji wa Watanzania wa kawaida katika kuchangia kwenye maendeleo ya nchi na ndiyo maana nilianza na ile quotation. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili limekuwa na kelele nyingi sana zikihusisha na namna ambavyo wakandarasi wazawa wamekuwa wanarudi nyuma kwa kukosa mitaji, wanarudi nyuma kwa kutokulipwa kwa wakati na wanarudi nyuma kwa kukosa uwezo au kutokujengewa uwezo wa kifedha ambao utawafanya watekeleze majukumu yao katika miradi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya TAMISEMI ambayo kimsingi mimi ninahudumu kama Mjumbe wa Kamati, jambo hili lilikuwa linatuumiza vichwa sana, lakini leo wakandarasi wetu wazawa watapata fursa ya kupata mitaji, tena ambayo haina ukiritimba, kwa sababu wataweza kuomba mitaji hii kupitia mtandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani mkandarasi ataomba then fomu ile itakwenda moja kwa moja TARURA kupitia mtandao. TARURA watathibitisha, itatoka pale itakwenda moja kwa moja kwenye Benki ya CRDB na Benki ya CRDB baada ya ku-assess watampatia mkandarasi mtaji bila ya kuwa na haja ya kuonana naye uso kwa uso. Jambo hili siyo la kubeza. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Wizara ya TAMISEMI kwa kazi nzuri waliyoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kujua dhamira ya dhati ya mtu, utaiona kwenye matendo yake. Katika kipindi hiki kifupi ambacho nimehudumu katika Kamati ya TAMISEMI, tumekagua shule za sekondari za wasichana za sayansi nchi nzima zenye thamani ya kuanzia shilingi bilioni nne mpaka shilingi bilioni tano na kitu ambazo kimsingi Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan amejitoa kwa hali na mali kuhakikisha watoto wa kike wanaweza kushiriki na kusoma masomo ya sayansi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama mwanamke kusema ukweli, niseme kazi kubwa imefanyika. Hivi tunavyozungumza leo, watoto wetu wa kike wako shuleni katika shule ambazo ni za kisasa zenye mabweni, mabwalo, maabara na maktaba za kisasa wanasoma masomo ya sayansi. Shule hizi zinafanya kazi sasa hivi nchi nzima. Hili ni jambo la kupongeza na ninasema ukweli, iko haja ya Waheshimiwa Wabunge wote hapa kupata fursa ya kuzishuhudia shule hizi ili tuweze kujua kazi kubwa iliyofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Manispaa yangu ya Shinyanga kuna shule inaitwa Rajani Sekondari. Ile shule iko jirani sana na ninapoishi mimi. Ile shule ilikuwa ina changamoto kubwa sana ya miundombinu. Kilio kikubwa cha Mheshimiwa Mbunge wa jimbo ilikuwa ni kupandisha hadhi ile shule. Leo tunavyozungumza, mabweni yameshajengwa, miundombinu ya madarasa imeshajengwa, wanamalizia kuweka maabara na shule ile wanaipandisha hadhi iende kuwa shule ya Kidato cha Tano na Sita. Haya ni mambo makubwa ambayo hatuwezi kuyabeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali hasa kwenye Sekta ya Elimu, kwanza shule hizi za sayansi zipelekewe vifaa vya kisasa vya maabara badala ya kutegemea kununua vifaa hivi kwa kutumia fedha za ndani za halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu moja tu, tayari wanafunzi wako shuleni, lakini vifaa vilivyopelekwa havitoshi na watoto hawa wamekaribia kuanza kufanya mitihani na ni lazima wafanye mitihani ya practical. Naishauri Serikali wapeleke vifaa vya maabara kwa haraka ili watoto waweze kufanya mafunzo kwa vitendo tayari kwa kujiandaa na mitihani yao ya kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, umuhimu wa kupeleka vifaa vya maabara kwa haraka, hizi shule zote ni mpya na mwisho wa siku unavyoanza ndivyo watu watakavyokuchukulia. Shule hizi zisipokuwa na ufaulu mzuri, zitashusha lile lengo kuu la Serikali la kutaka kuzifanya shule hizi ziwe special na la kutaka kufanya shule hizi zionekane ni za mfano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kuishauri Serikali ihakikishe inapeleka vifaa vya maabara vya kutosha ili watoto wafanye experiment ili wale best students ambao tumewachagua katika maeneo yale waweze kuonesha uwezo wao katika mitihani yao ya Kidato cha Tano, Kidato cha Sita na Kidato cha Nne. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri, katika eneo la mikopo ya 10%, mwaka 2024 wakati Mheshimiwa Waziri anawasilisha bajeti yake, hapa alitupa ahadi nzuri sana kwamba sasa wanakwenda kutoa mikopo ya 10% na akatuahidi kwamba kuna baadhi ya maeneo watatoa mikopo hiyo kwa kutumia benki na maeneo mengine watatoa mikopo hiyo kwa kutumia halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi hili linasuasua sana na mpaka sasa tunavyozungumza huu ni mwaka wa mwisho katika Bunge hili la Kumi na Mbili. Nadhani kama kuna jambo kubwa ambalo Wizara ya TAMISEMI inaweza kulifanya na kuacha alama baada ya bajeti hii ya mwisho, ni kuhakikisha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanapata mikopo ya 10%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi ni nyingi sana. Takribani shilingi bilioni 123 ziko kwenye akaunti zimezuiliwa, zinasubiri wanawake, vijana na watu wenye ulemavu waweze kufaidika. Nadhani ipo haja ya TAMISEMI kuchukua hatua madhubuti ya haraka. Nimeona katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri anasema tunakwenda kuanza kutoa mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumebakiza mwezi mmoja hapa, utasikia mara mifumo haifunguki, mara sijui NeST imefanyaje. Hebu waharakishe hili zoezi la kutoa mikopo ya 10% ili tuweze kuyasaidia haya makundi maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, nataka nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wangu wa Shinyanga. Pale Shinyanga, Manispaa ya Shinyanga Mjini ndiyo imeongoza kwa usafi, na kitaifa imekuwa ya pili kwa usafi. Sasa hili halitokei hivi hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo adha kubwa sana ya miundombinu. Juzi nilimwona Mheshimiwa DC Mboni kule Kahama anahangaika kukagua miundombinu ya barabara baada ya kukuta barabara nyingi zimeharibiwa na mvua. Hebu fikiria kwa 11% ya bajeti ambayo TARURA wamepelekewa, wamefanya kazi kubwa na leo humu ndani kila mtu anampongeza Engineer Seff. Je, wangepelekewa kwa asilimia ambazo zinatakiwa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, ipeleke fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo yetu kwa sababu hali siyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho, siyo kwa umuhimu, napenda kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Spika Dkt. Tulia Ackson. Daktari huyu siyo tu kwamba ni Daktari wa Sheria, maana ni mwalimu wangu, nina-declare. Siyo tu Daktari wa Sheria, lakini ameweza kumudu kuwa Daktari wa Siasa Kitaifa na Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ambao tunajifunza kutoka kwake, tuna mengi ya kuendelea kujifunza. Niseme ukweli, mwanzoni tulikuwa tunamwona kama mkali hivi, lakini sasa hivi tunaiona tija. Kwa sisi ambao tunawakilisha Bunge ndani na nje ya nchi, tunaonekana namna ambavyo tumenyooka kwenye namna tunavyojenga hoja na tumenyooka kwenye namna ambavyo tunaweza kutetea Taifa letu Kitaifa na Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kazi kubwa aliyoifanya, mimi ninamwombea sana aendelee kuwa Spika wetu hata katika Bunge la 13. Mwenyezi Mungu akubariki sana. (Makofi)