Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba iliyoko mbele yetu. Awali ya yote, napenda sana kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Ukarimu anayejalia neema ndogo ndogo na kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuanza kwa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wetu Mama yetu kipenzi Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika Taifa lake la Tanzania. Mheshimiwa Rais amekuwa hatulii usiku na mchana ndani na nje ya Tanzania kwa ajili ya kuwatafutia neema wananchi wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuanza kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kukubali ama kuuteua Mkoa wetu wa Pwani unaoongozwa na Mkuu wa Mkoa wetu, Alhaji Musa Kunenge kupewa heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa uzinduzi wa Mbio za Mwenge Kitaifa ambapo tumezindua tarehe 02 Aprili, 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwani kupitia Mwenge wa Uhuru tumeukimbiza, tumemulika na tumekagua miradi yenye takribani thamani ya shilingi bilioni 45. Hivyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Mwenge unasimama kwa niaba yake na Mwenge ule umemulika na kukagua miradi yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pasi na shaka, mwaka huu Mkoa wa Pwani tutaongoza, na katika hizi Mbio za Mwenge ndiyo tutashika namba moja kwani miradi mikubwa imetekelezwa na imetekelezwa kwa umahiri wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza Mbunge wangu wa Jimbo la Rufiji na Waziri wetu wa TAMISEMI, Kaka yangu Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, kule kwa Wandengereko wanamwita a.k.a. MMK katika maana ya Mchengerwa Mtu Kazi, nampongeza sana, amepatiwa kazi kubwa ya kumsaidia Mheshimiwa Rais, na anafanya kazi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu ya TAMISEMI ndiyo Wizara ambayo inashughulika na maendeleo ya watu katika miji, vijiji na vitongoji, lakini Mheshimiwa Mchengerwa amekuwa akifanya kazi ya kumsaidia Mheshimiwa Rais, lakini bado amekuwa yuko bennet na wananchi wake wa Rufiji. Napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri wake kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kwamba namshukuru sana Mheshimiwa Spika kwa kuniteua na kuniweka kuwa Mjumbe wa Kamati ya LAAC kwa kipindi cha miaka miwili na nusu. Kupitia Ujumbe wangu wa Kamati hii ya LAAC, nimepata fursa na nafasi ya kutembea karibia nchi yote ya Tanzania. Nadhani nimetembea Halmashauri ama niseme mikoa yote, nilibakiza Mkoa wa Kigoma tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ziara za LAAC zimenipa nafasi ya kuwa shuhuda kujionea miradi mikubwa ya kimaendeleo ambayo imetekelezwa katika Halmashauri zetu, katika Wilaya zetu na katika Majimbo yetu. Nikisema nitolee mfano katika sekta ya elimu, sote ni mashuhuda, shule za wasichana zimejengwa ambazo zina thamani ya shilingi bilioni nne mpaka shilingi bilioni tano katika mikoa yote ya Tanzania. Kwa hiyo, tunaweza tukafanya hesabu kwamba shilingi bilioni nne mpaka shilingi bilioni tano tukizidisha mara mikoa yote ya Tanzania tutaona ni kiasi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu shule za wasichana, Mheshimiwa Rais kwa kuwa ni mama, kwa kuwa ni mlezi, kwa kuwa ni mvumbua vipaji, ameona ipo haja na tija ya kuanza na zoezi la kujenga shule za wavulana. Shule saba tayari za wavulana zimejengwa kila moja yenye thamani ya shilingi bilioni 4.450.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, shule 29 za amali zenye thamani ya shilingi bilioni 1.6 na zenyewe zimejengwa. Kwa wale watakaoshindwa kwenda kwenye mfumo rasmi, basi waende kwenye huu mfumo wa amali. Mwisho wa siku Mheshimiwa Rais hajamwacha kijana yeyote wa Kitanzania pembeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine wa mambo makubwa yaliyofanywa na Rais wetu katika sekta hii ya elimu ni Shule za Kata. Shule mpya za Kata takribani 734, zenye thamani ya shilingi milioni 470 kila moja zimejengwa katika hili Taifa letu la Tanzania. Hivyo napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwani elimu ndiyo ufunguo wa maisha na elimu itatusaidia Taifa na vijana wa Tanzania kuondoka gizani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Mwenyezi Mungu amlipe sana Mheshimiwa Rais wetu. Kwa hiyo, kazi kubwa aliyoifanya kuwafanya watoto waondokane na ujinga, katika Dini yetu ya Kiislamu tumeambiwa “Iqraibi-ismi rabbika allathee khalaq.” Katika maana ya kwamba, “Twende Tukasome kwa Jina la Mola.” Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais anafanya kazi ambayo ameamrishwa na Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija katika upande wa sekta ya afya, Mheshimiwa Rais wetu amefanya kazi kubwa na kazi nzuri, kwani hospitali, vituo vya afya na zahanati zimejengwa. Tunazo hospitali mpya takribani 129 katika halmashauri zetu 129. Kwa hiyo, hili ni jambo la kumshukuru sana Mheshimiwa Rais. Pia kama hiyo haitoshi, tunazo hospitali kongwe 48 ambazo zimefanyiwa ukarabati pamoja na vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Rais amegundua kwamba afya ndiyo msingi wa Taifa la Watanzania na afya ndiyo msingi wa maisha ya mwanadamu, ndiyo maana kwa makusudi ameamua kuwekeza katika hii sekta ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda katika Mkoa wangu wa Pwani, katika Mkoa wetu wa Pwani ni Mkoa wa kielelezo, Mkoa ambao una mifano tosha ya mambo makubwa na mazuri yaliyofanywa na Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu katika shule ya sayansi ya wasichana kule Wilayani Rufiji katika Kata ya Chemchem, tumepatiwa kiasi cha shilingi 4,800,000,000 kwa ajili ya kujenga shule nzuri, shule ya kisasa ili kuweza kuibua vipaji vya watoto wa kike ama vipaji vya wasichana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule hii ama hakika tumeipa jina la heshima Bibi Titi Mohamed. Ni shule ambayo itakuja kutoa mabinti ambao ni Marais wa baadaye, Wenyeviti wa baadaye, Maspika wa baadaye na Mawaziri wa baadaye. Hivyo tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili pia nampongeza sana Mbunge wa Jimbo la Rufiji, kwani mbali na kwamba Mheshimiwa Rais ametupatia fedha, tumejenga shule nzuri ya kisasa. Yeye hakusita kuwawekea mfumo wa gesi ili waweze kupikiwa chakula katika majiko ya kisasa na katika bwalo ambalo ni zuri. Nafikiri katika sehemu zote tulizotembea hakuna bwalo zuri kama bwalo la kule Wilayani Rufiji, bwalo lile limejengwa vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ningependa kusemea ni mikopo ya 10%. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, hii mikopo ya 10% ilifika mahali ilisitishwa, kwa sababu ya baadhi ya watumishi kutokuwa na nia njema na baadhi ya vikundi hewa ambavyo vililetea Taifa hasara. Mheshimiwa Rais alisitisha kwa nia ya kwamba vichakatwe upya, viangaliwe upya ili irejeshe mikopo ambayo ina tija na afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii mikopo iliyorudishwa ya mfumo wezeshi, naipongeza sana Wizara ya TAMISEMI. Hii mikopo, kwanza imewekwa katika category tatu, mwisho wa siku hakuna mjasiriamali, awe mdogo, awe wa kati, ama mkubwa ashindwe kunufaika na hii mikopo. Nikitolea mfano wa Halmashauri yangu ya Wilaya ya Kibaha, mkopo mdogo wameweka kati ya shilingi 500,000 mpaka shilingi 10,000,000 ili vijana, wanawake na watu wenye ulemavu waweze kukopa. Kwa sasa mtu mwenye ulemavu ameruhusiwa kwenda kuchukua mkopo huu pekee yake, lakini kwa wale watu ambao wanaweza wakakopa mkopo wa kati ni kati ya shilingi 10,000,000 mpaka shilingi 50,000,000 na mkopo mkubwa ni kati ya shilingi 50,000,000 mpaka shilingi 150,000,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake ni kwamba vijana wa Kitanzania, wanawake, akina mama, akina mamalishe, pamoja na wauza mboga mboga, neema imefunguliwa na Rais Samia. Kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri jambo hili kama kuna mambo madogo, madogo niliona katika halmashauri zetu kadhaa Mkoa wa Pwani walizindua hundi za kimfano kwa ajili ya kutoa hii mikopo kwa akina mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo lenye tija, ni jambo lenye afya, ambapo Wabunge wa Viti Maalum tunapata nafasi kubwa na nzuri ya kumsemea Rais wetu kwa namna alivyotenda kwa wanawake wenzie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kumpongeza Spika wetu Dkt. Tulia Ackson kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Wabunge wa Viti Maalum tunamshukuru kwa vile vikao vya kila Alhamisi, alikuwa anatuita vikao vya kila Alhamisi kutuandaa maandalizi ya 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemwelewa Mheshimiwa Spika, tumemfahamu, tutafuata ushauri na Bunge lijalo tutarudi kwa wingi, namba ya wanawake itaongezeka, vikao vya Alhamisi haviwezi kwenda hivi hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, licha ya kutuheshimisha wanawake wenziwe, Mheshimiwa Spika ameheshimisha Bara la Afrika. Hii ilijidhihirisha pale Mheshimiwa Spika alipowakatalia Wazungu kwa kuona bado tuko kwenye masuala ya ukoloni. Ni kwamba tumeshamalizana na ukoloni, Afrika ni huru, tunasonga mbele na tunachapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)