Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia jioni hii ya leo. Naomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu. Naomba katika mchango wangu tumwombee Mheshimiwa Rais kwa Zaburi ya 25, ningeisoma lakini kwa sababu ya muda, basi naomba kila mtu akaisome. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Hassan kwa mambo makubwa sana ambayo ameyafanya katika nchi yetu. Ameiaminisha dunia kwamba wanawake tunaweza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nampongeza sana Mheshimiwa Spika wetu Dkt. Tulia Ackson ambaye ni Rais wa Mabunge ya Dunia. Kwa kweli, tunawashukuru sana, Tanzania imetambulika kwamba kuna wanawake jasiri, wanawake ambao wanaweza wakaongoza nchi, wanawake ambao wanaweza wakafanya mambo makubwa katika hii dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna usemi wa Wanyamwezi ambao unasema kwamba “mzigo mzito, mpe Mnyamwezi” lakini tunaubadilisha usemi huu kwamba mzigo mzito sasa hivi apewe mwanamke, kwa sababu wanawake tunaweza na tumekuwa tukibeba mizigo mizito sana bila kuidondosha. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nikipongeze Chama cha Mapinduzi kwa kumteua Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mgombea wa Urais 2025, pamoja na Mgombea Mwenza Dkt. Emmanuel Nchimbi. Pia Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi, nawapongeza sana. Tuna imani nao sana kwamba wataweze tena kuiongoza nchi yetu kwa kipindi kijacho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niendelee kumpongeza Waziri wetu wa TAMISEMI Mheshimiwa Mchengerwa, nampongeza na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Dugange pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa Zainab Katimba, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri ambayo wameifanya katika hii Wizara ya TAMISEMI na kuhakikisha kwamba nchi yetu inakwenda vizuri katika miundombinu yote ya barabara, afya na elimu na mambo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nichukue pia nafasi hii kumpongeza Mkuu wangu wa Mkoa Mheshimiwa Peter Serukamba ambaye kwa kipindi kifupi ameweza kufanya kazi nzuri sana katika Mkoa wetu wa Iringa. Tunaamini kwamba tunamwombea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nampongeza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa, M-NEC wetu ASAS ambaye kwa kweli kwa kushirikiana na viongozi wetu wa Chama wamesimamia vizuri sana katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba nianze na uchangiaji wa barabara za TARURA. Niungane na wote waliompongeza Engineer Seff ambaye ni Mtendaji Mkuu wa TARURA kwa kazi nzuri sana ambayo amekuwa akiifanya, kwa kweli tunamwombea Mwenyezi Mungu aendelee kumweka na aendelee kufanya utumishi katika Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nipongeze uanzishwaji wa Hatifungani ambayo ni Samia Bond. Tunaamini kabisa bond hiyo sasa itasaidia malipo kwa Wakandarasi wetu nchini na barabara nyingi sasa zitaweza kupitika na uchumi sasa utaweza kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Iringa tumepokea fedha nyingi sana kwa ajili ya ujenzi wa barabara za TARURA, lakini sasa kutokana na mvua nyingi, barabara nyingi zimekuwa zinaharibika kwa kipindi kifupi tu na hazipitiki kabisa wakati wa mvua na kusababisha mazao kutofika kwa wakati katika masoko, lakini pia pembejeo kutofikishwa kwa wakati katika mashamba vilevile baadhi ya wagonjwa wengine kutofika kwa wakati katika vituo vya afya, pia gharama za usafiri zinakuwa kubwa sana kwa kipindi hicho, kwa sababu barabara nyingi sana zinakuwa mbovu na nyingine hazipitiki kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitaje tu baadhi ya barabara ambazo zinasumbua sana wakati wa mvua. Kuna barabara inayokwenda Idete – Itonya – Muhanga – Mgeta kilometa 18, barabara hii inaunganisha Mkoa wa Morogoro. Kuna barabara ile ya Ipalamwa – Naupwega – Kimara, ujenzi wake unasuasua. Tunaomba jitihada ili barabara ziweze kupitika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna ile barabara ya Kidabaga – Magome – Ndengisivili – Kimara. Katika barabara hii kuna maeneo kama mawili yanasumbua, tunaomba Serikali iangalie ili barabara iweze kupitika kwa sababu wananchi wanapata shida sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ile barabara ya Lulindi – Ukwega – Boma la Ng’ombe, pia kuna barabara nyingine ya Masisiwe – Isanga, kuna barabara ya Kihesa Mgagao – Mwatasi, kuna barabara ya Ihimbo – Itimbo – Kising’a, na kuna barabara ya Mtandika – Ilula kilometa 22.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mtandika – Msosa kilometa 16, Barabara ya Ihimbo – Kitelewasi, barabara ya Mtandika – Nyanzwa, barabara ya Ilula – Image – Ibumu, hii barabara ingepewa heshima kabisa ya Engineer Mfugale kwa sababu ni sehemu ambapo amejenga makazi yake pale, ingesaidia ikajengwa hata kwa lami, lakini sasa hivi haipitiki ni mbovu. Pia kuna barabara ya Mahenge – Ilindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu sasa tunaomba barabara hizi Serikali ingefanya upembuzi yakinifu, maeneo yale ambayo ni korofi, yaweze kujengwa ili hizi barabara ziweze kupitika wakati wote wa mwaka ili kutokuleta usumbufu ambao umekuwa ukijitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye sekta ya afya. Naomba niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa tuzo aliyoipata ya kupunguza vifo kwa akina mama nchini, kwa kuleta fedha nyingi sana katika ujenzi wa hospitali zetu za Wilaya, vituo vya afya na zahanati zilizosheheni kila kitu. Sera ya Serikali ni ujenzi wa vituo vya afya kila Kata, lakini naiomba Serikali kuleta fedha katika baadhi ya Kata ambazo hazina vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, naweza nikataja Kata chache za Wilaya ya Kilolo ambazo hazina vituo vya afya. Kata ya Ukumbi, Kata ya Ihimbo, Kata ya Udekwa, Kata ya Ibumu, Kata ya Image, Kata ya Idete, Kata ya Ilole, Kata ya Lugalo, Kata ya Ng’ang’ange, Kata ya Boma la Ng’ombe, Kata ya Masisiwe, Kata ya Kising’a, Kata ya Mlafu, Kata ya Wambingeto, na Mahenge. Hivi vituo havijajengwa pia barabara zake hazifikiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa wakati mwingine zinasababisha hata akina mama wajawazito kwenda katika vituo vya afya kwa shida sana. Hata pikipiki hazifiki, zinabebwa mgongoni kwa sababu hazipiti wakati wa mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba maboma ya vituo vya afya na zahanati ambazo zimejengwa kwa nguvu za wananchi, basi angalau Serikali ilete fedha ili kuweza kumalizia, pia nyumba za madaktari na watumishi. Watumishi bado hawatoshelezi katika vituo vya afya na zahanati na katika hospitali zetu za Wilaya. Tunaiomba Serikali izingatie hilo ili tuweze kuboresha afya na kuondoa kabisa vifo vya akina mama na watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya elimu, naomba niwapongeze walimu wote nchini, bila kuwasahau walimu wetu waliopo katika Mkoa wetu wa Iringa, wamefanya kazi nzuri sana. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa ujenzi wa shule za watoto wa kike ambazo zipo 26 nchini ikiwepo katika Mkoa wetu wa Iringa ambayo imejengwa katika Wilaya ya Kilolo, Shule ya Lugalo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nalipongeza Bunge letu kwa kujenga shule za shule za sekondari za watoto wa kike na wa kiume kwa kuleta ubunifu, nao pia wameweza kuongeza juhudi nawapongeza sana. Hata juzi tulikuwa kwenye Marathon ya Bunge kwa ajili ya ujenzi wa shule zetu za watoto wa kike na wa kiume. Hii tumetoa alama Wabunge, kwamba na sisi tunaweza tukajenga shule za watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo changamoto nyingi sana kwa shule zetu za msingi. Shule zetu za msingi nyingi ni kongwe sana, unakuta watoto wanasoma kwenye mazingira magumu. Mkoa wetu wa Iringa ni Mkoa wenye baridi sana, unakuta shule nyingi hazina madirisha, hazina milango, hazina ceiling board, hazina floor. Kwa hiyo, watoto wetu wanasoma kwenye mazingira magumu sana, ni nyingi hata kuzitaja siwezi. Sasa ningeiomba Serikali iangalie na itoe uzito shule hizi ziweze kukarabatiwa ili vijana wetu waweze kusoma katika mazingira mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naomba kuchukua nafasi hii kushukuru Chama changu cha Mapinduzi kupitia Jumuiya ya UWT inayoongozwa na Mheshimiwa Mary Chatanda. Pia katika Mkoa wangu, Zainab Mwamwindi ambao kwa kweli wamenilea, wamenifunza mpaka leo hii naweza kufanya kazi vizuri. Nawaomba wananchi wa Iringa, nikienda kuomba tena, kwa maana tunamaliza, tuna-graduate, nikienda tena waniamini kwamba ninaweza na sitawaangusha, nitafanya kazi kwa uaminifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)