Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Magu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kukushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais ambaye kwa kweli ndiye mwenye hii Wizara, kwa namna ya pekee ambavyo anaendelea kutupatia fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi yetu. Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri na kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Mheshimiwa Mchengerwa, tangu aingie kwenye hii Wizara, mabadiliko makubwa ya kiutendaji tumeyaona. Tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na wasaidizi wake, Naibu Mawaziri hao wawili wanamsaidia sana. Kuna mambo hatufiki kwake, yanamalizwa na Naibu Mawaziri wake, hasa mimi nikiwa nimekaa hapa wakipita wananiuliza Magu kuna tatizo gani? Naweka mambo yangu hapo. Tunampongeza yeye pamoja na Naibu Mawaziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza Katibu wake Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, nao wanamsaidia sana kwa kweli, kwa sababu wakati wote siyo lazima tufike kwake, tunaishia kwa Watendaji mambo yanakwenda vizuri. Katibu Mkuu, pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Ndugu Mativila anayekusaidia kwenye miundombinu kwa kweli wakati wote ninamsumbua sana. Nimewahi kumpigia simu akasema, niko nje ya nchi, lakini akatoa maelekezo ya mipango ikaenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunampongeza Ndugu Seff? Ni kwa sababu anajali Wabunge wote. Hakuna Mbunge ambaye ameenda kwa Ndugu Seff akashindwa kusaidiwa na hata kushauriwa kwa ajili ya barabara. Kwa hiyo, nilitaka nipongeze hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Magu tumepata stendi na soko, nami nawapongeza sana TAMISEMI pamoja na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, akiwemo Mheshimiwa Tax pamoja na Mheshimiwa Mary Masanja, haya yote tumeyasukuma kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa kweli, niombe sasa maelekezo, TAMISEMI itoe hili jambo la manunuzi kwa stendi ya Magu Mjini na soko lianze mara moja kwa sababu, umeshatoa idhini na maelekezo tu ya manunuzi ili stendi na soko la Magu yaweze kujengwa. Kwa kweli, wananchi watakuwa wamepata stendi ya muda mrefu, ni stendi ambayo kwa kweli imechakaa, ni stendi ambayo ina madimbwi. Kwa hiyo, kwa fedha ambazo mmetupa kwa bajeti hii tunayomalizia, zitakwenda kusaidia sana maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunacho Kituo cha Afya cha Lutale, ni kati ya vituo ambavyo mlituambia Waheshimiwa Wabunge tutafute vya mkakati, ni Kituo cha Lutale. Nashukuru kwamba, mmeshakubali kutoa fedha, naomba sasa na Waheshimiwa Wabunge wengine kwa sababu mmesema kwamba, fedha mmepata, pelekeni fedha, ili hivyo vituo vianze kujengwa na vianze kusaidia wananchi wetu. Tunayo imani na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ukiiongoza wewe Mheshimiwa Mchengerwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, mahitaji tunayo, ni mengi. Maboma ya zahanati zetu bado hayajakamilika, nayo tuombe kama kuna namna ya kupata fedha, kwa ajili ya maboma ndugu yangu Mheshimiwa Mchengerwa, hebu tupatie fedha Waheshimiwa Wabunge tukakamilishe maboma ambayo yameanzishwa na wananchi pamoja na halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa niwapongeze Waheshimiwa Madiwani wa Wilaya ya Magu wakiongozwa na Mwenyekiti, pamoja na Mkurugenzi na Wataalamu wake, kwa namna fedha za mapato ya ndani zinavyofanya kazi kwenye miradi ya maendeleo. Kwa namna ya pekee nawapongeza kwa sababu, fedha za miradi ya maendeleo wanazipeleka kama ambavyo zimekusudiwa. Hebu sasa zile fedha shilingi milioni 50, 50 kila boma, nami nimeleta maboma 20 tu, yakipata shilingi bilioni moja tunamaliza, na wananchi wanapata huduma ya msingi huko. Kwa hiyo, naombe sana hili jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba, tangu Mwenyezi Mungu aumbe dunia, kuna maeneo yalikuwa hayajawahi kupata barabara na sasa hii kwenye Serikali ya Awamu ya Sita yamepata barabara. Kwa hiyo, tunapompongeza Mheshimiwa Rais, tunamaanisha, tunapokupongeza Mheshimiwa Mchengerwa na Waheshimiwa Manaibu wake, tunamaanisha, hata tunapowapongeza Makatibu Wakuu pamoja na Ndugu Seff, tunamaanisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Kabale – Jijimidi tangu Mungu aumbe ulimwengu, haijawahi kujengwa. Sasa barabara ipo, na wananchi wanaona. Barabara ya Nkumbulu – Kayenze B tangu Mungu aumbe ulimwengu haijawahi kutokea, sasa ipo na Barabara ya Mwamanga – Kisesa B, hasa pale Inolelwa ambapo kuna daraja, niombe fedha; wakandarasi wameshaleta certificate, wapewe ili waweze kumalizia hizo kazi ambazo wamebakiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, ni kazi kubwa imefanyika, lakini tunayo mahitaji. Barabara ya Kabila – Nobola – Kabale – Mahaha – Nyasato ni barabara muhimu sana. Mwaka 2024 mvua ilinyesha kubwa, tulikuwa tumeijenga barabara vizuri, imeharibika. Nimeomba fedha za dharura, sikupewa; nimeomba tena mara ya pili, sikupewa; niombe sasa Mheshimiwa Mchengerwa, kama kuna mabakimabaki hapa yaliyobaki, hebu mwambie Ndugu Seff sasa aweze kurekebisha huko maneno yaweze kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Barabara ya Muhaha – Mwamnemba kwenda pale Itilima kwa rafiki yangu Mheshimiwa Njalu. Ni barabara ambayo inatuunganisha Wilaya ya Magu na Wilaya ya Itilima, nayo tumeiombea kwenye bajeti hii na kwa kweli, najua kwamba itapita iweze kujengwa ili angalau wananchi waweze kupata barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mahaha kwenda Bariadi kunahitajika daraja tu pale, hatuhitaji fedha za barabara kwa sababu, barabara imejengwa kutokea Magu mpaka Mahaha, tunakosa daraja la kuunganisha kwenda Bariadi kule Tubhukilo. Hebu tupatieni fedha ya daraja ili tuweze kuunganisha Bariadi na wananchi waweze hasa kufungua uchumi wa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikilia hapa kwamba, Mji wa Kisesa na Bujora ni miji mikubwa sana. Idadi ya wananchi kwa mujibu wa sensa ni takribani watu 63,000 ukiongeza ongezeko kwa sababu Mwanza na Ilemela yote inapumulia Kisesa na Bujora, hebu uangaliwe ule mji kwa fedha ambazo mnapata kutoka World Bank, TACTIC na mashirika mbalimbali yanayotoa fedha, tuuangalie ule miji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, Ndugu Seff alifika pale akatuma wataalamu wake wa ku-design waka-design barabara zote akatuambia tuanze na zipi? Tumeshaleta, tunahitaji fedha, ili angalau hizo barabara, hata kama siyo lami, zijengwe kwa kiwango cha mitaro na gravel, ili ziweze kupitika wakati wote kwa sababu, maji yote yanayokusanywa kwenye nyumba za bati yanamwagika na kukata barabara, niombe sana jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Magu ina miji mingi. Ukienda pale Nyambuge, ni mji unakua, ukienda pale Lugeni mji unakua, ukienda pale Ilumbu ni mji unakua na Mji wa Magu wenyewe, Mji wa Kabila na Mji wa Mahaha. Hebu wataalamu muitazame hii miji, wananchi wanatutangulia sana, sisi tunabaki nyuma kwamba, tuangalie mji ulivyo sasa na baada ya miaka 10 ijayo hiyo miji itakuwaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wananchi watakosa kabisa barabara kwa sababu, wanajenga holela na hakuna barabara, tunaomba hii miji itazamwe kwa namna. Tunapozungumza hapa, sisi tunaomba mtuelewe, tunajua TAMISEMI kazi kubwa imefanyika, lakini bado mahitaji ya Watanzania ni mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Barabara ya Matela – Nyakasenge. Barabara hii inaunganisha kutoka kwenye lami, trunk road, kwenda TANROADS. Kwa hiyo, tungeomba hizi barabara kwa kweli, ikiwezekana zipandishwe hadhi, zina sifa, inatoka trunk road kwenda TANROADS. Maana yake ni kwamba, ina sifa zote za kwenda TANROADS. Kama siyo hivyo, basi mtutengee fedha kwa sababu, zinapitika na watu wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Barabara ya Kisesa kwenda Kayenze, nayo ni trunk road, inaungana na TANROADS, barabara ambayo inatoka airport kuja Nyanguge. Hebu nayo muone namna ambavyo mnaweza kutusaidia kwa kweli. Barabara hizi ni muhimu sana kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri kwamba tunaweza kujipa muda, tunajua fedha hizi tunazopata ni kidogo, siyo nyingi sana, na mahitaji ya Watanzania ni makubwa, hebu tujipe muda kwamba, mwaka huu tunamaliza maeneo gani, hasa ambayo yanasaidia wananchi kiuchumi, ili kuhakikisha kwamba, tunawakomboa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nipongeze sana kwenye elimu. Kwa kweli, kazi kubwa imefanyika, kila Mbunge hapa ni shahidi. Sasa kinachohitajika hapa, nami niseme tu kwamba, kule Magu sasa tumeshatoka kwenye sekondari za kata, tumekwenda kwenye sekondari za vijiji na sekondari nyingi wakati wowote tutazifungua. Sasa walimu ni wa muhimu sana. Ajira mmetoa, lakini bado upungufu wa walimu ni mkubwa. Naomba hilo pia lifanyiwe kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya kazi kubwa kwenye afya, vituo vya afya tumejenga vingi na vifaatiba tumepeleka, lakini bado wataalamu wanahitajika. Serikali ya Awamu ya Sita imejitahidi kwa yote, imepeleka wataalamu, lakini bado wataalamu wanahitajika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie sasa kwa kusema kwamba, kwa kweli, Mheshimiwa Rais hakukosea kuiunda vizuri Wizara hii ya TAMISEMI kuanzia kwa Mheshimiwa Waziri, wasaidizi wake na watalaamu. Kule TAMISEMI kuna mtu anaitwa Ndugu Cheyo, mtaalamu mzuri wa mipango, hakuna asiyemjua, hakuna asiyemsikiliza. Kwa kweli, TAMISEMI ina watu waliobobea, watu makini, tuendelee kuwatumia, kwa ajili ya kutusaidia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niunge mkono hoja, japo nilikuwanayo mengi. Mungu akubariki sana. (Makofi)