Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii. Awali ya yote, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameifanya ya kuleta fedha nyingi ndani ya Halmashauri yetu ya Wilaya ya Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais, ndani ya kipindi cha miaka minne halmashauri yangu imepata fedha nyingi sana za maendeleo. Zaidi ya shilingi bilioni 400 zimepatikana kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, ni hatua nzuri sana ambazo zimefanyika kwenye maendeleo, kwenye maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri, nawapongeza Waheshimiwa Manaibu Waziri wote wawili ambao wanafanya kazi ya kumsaidia Mheshimiwa Waziri kufanya shughuli za maendeleo ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali kwenye upande wa elimu. Kwenye sekta ya elimu tumepata fedha nyingi za maendeleo, ndani ya kipindi kifupi ambacho Mheshimiwa Rais amekuwa na dhamana tumepata fedha za kujenga shule nyingi za msingi, shule za sekondari, tuna zaidi ya shule mpya 33 zimejengwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, na vyumba vya madarasa zaidi ya 150 vimejengwa kwenye Wilaya hiyo ya Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na sekondari ambazo zimejengwa karibu kila kata, sasa tuna sekondari kinyume na ilivyokuwa huko nyuma, tumepata ujenzi wa Chuo cha VETA kwenye eneo la Wilaya ya Tanganyika, ambapo tulikuwa hatuna kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni maendeleo makubwa sana ambayo yamefanywa na Serikali ndani ya kipindi hiki ambacho Mheshimiwa Rais amepewa dhamana. Eneo hili tungependa kuishauri Serikali na kuomba msisitizo suala zima la kukamilisha maboma ambayo yameanzishwa na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi wamejitolea, tunayo maboma mengi ndani ya Wilaya ya Tanganyika ambayo yameanzishwa kwa ajili ya kujenga Shule za Msingi na kuongeza madarasa kwenye Shule za Sekondari. Naiomba Serikali kupitia kwako Mheshimiwa Waziri, uweze kufanya jitihada kwenye bajeti hii, uweze kuleta fedha kukamilisha hayo maboma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo Serikali imefanya kazi kubwa sana ni sekta ya afya. Kwenye afya tuna Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika, hospitali nzuri sana, vifaatiba tumeanza kuvipata na tunavyo vituo vya afya. Kabla ya hapo, tulikuwa na vituo vya afya vitatu, lakini tunavyoongea, sasa hivi tulishakuwa na vituo vya afya 10. Kati ya hivyo, saba vinafanya kazi na vitatu vinahitaji kumaliziwa ili viweze kutoa huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hapo, wananchi wengi wamejitolea sana kujenga zahanati kwenye vijiji mbalimbali. Eneo hili tunaomba Serikali iweze kubeba yale maboma. Tumeanzisha ujenzi wa zahanati Kijiji cha Mgamsa, Kijiji cha Kisubangala, Kijiji cha Kabanga na vijiji vinginevyo ambavyo vimejenga zahanati bado kuna hatua ya mwisho ambayo inahitaji kusaidiwa na Serikali. Matumaini yangu ni kwenye bajeti hii yale maboma yote ambayo yapo kwenye eneo la sekta ya afya mtayafanyia kazi, ili wananchi waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeleta huduma ya vitendeakazi, hasa vifaatiba, kwenye vituo vya afya. Bado tuna tatizo kubwa sana la Watumishi wa Serikali Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika. Mfano tu ni kwamba, baada ya kuleta X-Ray, Ultra Sound na vifaa vingine vyote ambavyo vinahitajika hatuna mtaalamu, ambaye anaviendesha vile vifaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaweza tukafanya mazuri tukashindwa kutekeleza kwenye eneo ambalo linasimamia huduma ambayo kimsingi ndiyo inayohitajika. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, tunahitaji sana watumishi waje kwenye eneo la Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kwa sababu, vile vifaa tunavyovipeleka vinaenda kulundikwa na havifanyi kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaye mtaalamu mmoja tu ambaye anashindwa kugawanyika aende kwenye vituo vyote hivyo vya afya akasimamie na afanye kazi kwenye hospitali ya Wilaya, kitu ambacho hakiwezekani kufanyika. Naombe eneo hili lifanyiwe kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala zima la watumishi kuna wimbi ambalo lipo kwenye Ofisi ya TAMISEMI, watumishi mnaowaleta wakishafika kwenye vituo vyao vya kazi mnatoa vibali tena kuwarudisha kwenye maeneo mengine. Hili ni tatizo kubwa sana na tunaomba Mheshimiwa Waziri alisimamie kwa sababu, wale watumishi wanaowapelekwa kule ni sehemu ya kwenda kutoa huduma kwa Watanzania. Hivyo, tunasisitiza eneo hili lifanyiwe kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuzungumzia ni suala la TARURA. Kwanza nawapongeza sana wasimamizi wote ambao wamesimamia suala zima la kupeleka miundombinu kupitia TARURA. Nawapongeza sana Manaibu Katibu Wakuu, akiwemo ndugu yangu Matibila, kwa kazi kubwa sana ambayo ameifanya kusukuma miradi ya maendeleo, lakini bila kumsahau Engineer Seff, ambaye ametusaidia sana kwenye eneo hili la kupeleka miradi ya maendeleo, hasa ya miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Engineer Seff alikuja Mkoa wa Katavi, amekuja kwenye eneo ambalo kulikuwa hakujafunguliwa barabara, alijionea na pale alitusaidia akatupa fedha za kujenga daraja, shilingi bilioni 1.5 na ile barabara kwa sasa kutoka Kambanga kuja Infisi, Infisi kwenda Bugwe imefunguliwa na inapitika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo ambalo ni la faraja na tumeokoa maisha ya Watanzania walio wengi kwenye maeneo haya, lakini alienda kule ukanda wa ziwa, ameenda kuangalia daraja kwenye Kijiji cha Kapalamsenga kwenda Itunya, lile daraja nalo limekamilika. Sasa kazi kubwa ambayo inahitajika kufanywa, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, ipo ahadi ambayo iliahidiwa na Serikali ya kuunganisha Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Kigoma kupitia Wilaya ya Tanganyika na Wilaya ya Uvinza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya kutoka Kapanga kwenda Bujombe - Bujombe kwenda Kalya, hii barabara iliahidiwa kipindi kile na Mheshimiwa Waziri Ummy, yenye thamani ya shilingi bilioni 1.5. Naomba Mheshimiwa Waziri, ahadi ambayo ilitolewa na Serikali aifanyie kazi na ni kiungo muhimu sana kwenye barabara inayounganisha Wilaya ya Tanganyika na Wilaya ya Uvinza. Eneo hili ni muhimu na mawasiliano hayapo kwa sasa, ikifika masika wananchi hawafanyi kazi. Kwa hiyo, tunaomba maeneo haya yafanyiwe kazi na mtoe fedha, kwa ajili ya kukamilisha hii barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie kuwapongeza sana Serikali, hasa kwenye kufungua barabara. Barabara zimefunguliwa nyingi sana. Jimboni kwangu tunazo barabara nyingi, lakini tatizo lililopo kwa sasa ni wakandarasi waliofanya kazi hawajalipwa. Tunaomba Serikali iwalipe wale wakandarasi, mwatie moyo ili waweze kufanya kazi na kukamilisha ile miradi waliyoianzisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine ambalo...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaomba wakaangalie maeneo ya kufanya maboresho hasa kwa upande wa madaraja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nawashukuru na kuwapongeza wote ambao wamefanya kazi nzuri, ahsanteni sana. (Makofi)