Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Eng. Dr. Leonard Madaraka Chamuriho

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ENG. DKT. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniruhusu nami nichangie hoja hii muhimu ya Wizara yetu hii muhimu ambayo inashughulika na wananchi, hasa wa ngazi ya chini kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuongoza vizuri hasa kwa falsafa zake za 4R ambazo zinasababisha twende vizuri, kwa utulivu na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, napenda kumpongeza Rais wetu kwa kuhakikisha kwamba Wizara hii ambayo iko chini ya ofisi yake ina ufanisi mzuri; na vilevile kwa kuendelea kuitafutia rasilimali ya kuweza kuifanya Wizara hii ifanye kazi kama inavyotakiwa. Tunampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kumpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuiongoza Wizara kwa usimamizi wake mahiri, na kwa kuandaa bajeti nzuri ambayo inatia matumaini mazuri katika utekelezaji wa majukumu ya sekta hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kuwapongeza wasaidizi wa Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange na Mheshimiwa Zainab Katimba kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Waziri, na vilevile Katibu Mkuu wa Wizara hii, Ndugu Adolf Ndunguru na Naibu Makatibu Wakuu wote na wataalam wote kwani tunaamini kabisa kwamba kazi hii nzuri iliyofanywa inawajumuisha hao wote katika utendaji kazi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI ina majukumu mengi lakini mchango wangu wa leo utajikita kwenye usimamizi na uendelezaji wa miundombinu ya usafiri. Ningependa kutoa pongezi kwa Serikali kwa kuanzisha chombo mahsusi cha TARURA ambacho ndicho kinachosimamia miundombinu ya usafiri katika Wizara hiyo. Uamuzi huo umezaa matunda, hivyo pongezi hizo ni dhahiri inabidi zielekezwe huko. Chini ya uongozi wake Mhandisi Victor Seff kwa kweli TARURA imefanya kazi ya mfano wa kuigwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, napenda kusisitiza kwa Waziri kwamba chombo hiki ni budi tukiwezeshe ili kiweze kuendelea kutekeleza majukumu yake vizuri. Uendelevu wa matunda bora ya TARURA unahitaji vitu vitatu. Kwanza rasilimali ambayo ina watu na fedha; pili, ina ubunifu hasa huu wa teknolojia; na tatu, ningesema ni uzingatiaji wa bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kwenye rasilimali watu, mfano mzuri uko kwa kiongozi mwenyewe wa TARURA, Mhandisi Victor Seff ambaye ninamfahamu vizuri. Huyu amefanya uhandisi kuanzia Kidato cha Kwanza kule Moshi Technical akatoka pale akasoma Dar Technical kabla ya kujiunga na vyuo vikuu. Kwa hiyo, hakuna wasiwasi na umahiri na ujuzi alionao. Kwa hiyo, katika rasilimali watu, wamekaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile anayesimamia miundombinu ya ujenzi na usafiri, Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Rogatus Mativila, naye ni mhandisi mzuri ambaye anaaminika katika kazi hizo. Hivyo, tunaona kwamba kwenye upande wa rasilimali watu kinachotakiwa ni kuwaongezea watu wenye weledi ili mipango yao na utekelezaji viweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru na kumpongeza, kwa sababu nikiangalia katika ukurasa wa 164 wa hotuba yake ametenga shilingi bilioni 7.97 kwa ajili ya ajira mpya. Basi katika hili tunamwomba asisitize kuzingatia kwamba hao watakaoingizwa pale wawe ni wale wenye weledi wa kuweza kumsaidia katika kutekeleza jukumu hilo la kutunza miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye jambo la pili la rasilimali fedha, kwanza ningependa kumpongeza kwa kuongeza fedha kwenye mtiririko wa Wizara yake katika eneo hili. Kwa kweli kazi za ujenzi, ukarabati na matengenezo ni kubwa sana. Ni kweli kwamba hata siku moja hii bajeti haitatosha. Hivyo, inabidi tuzingatie kwamba vyanzo vya mapato vinavyoelekeza bajeti hiyo vinaongezwa na pia vinalindwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia randama ya Wizara hii ukurasa wa 15 kwenye maduhuli ambayo yanatokana na hifadhi za barabara, nimeona kwamba kufikia Februari mwaka huu ni asilimia 58.8 tu ndizo zimekusanywa, na sababu imetolewa pale, sababu ni kwamba tumeshusha ushuru wa kukodisha zile hifadhi za barabara kutoka dola 1,000 kwa kilometa hadi dola 200. Hiki kilikuwa chanzo muhimu. Tusipovilinda vyanzo hivi tunaweza kupata changamoto huko mbele za kupata fedha ya kuweza kuendesha miundombinu hii inayosimamiwa na TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, ukiangalia katika mipango, jedwali la pili ukurasa wa 41 utaona tena kwamba chanzo hicho hicho mwanzoni kilikuwa kimepangiwa shilingi bilioni 5.6, lakini kwa mwaka huu kimepangiwa shilingi bilioni 7.0. Sasa unajiuliza kwamba ikiwa kile chanzo kule kimepungua, mbona matarajio ya makusanyo yameongezeka? Kwa hiyo, tunapata changamoto hapo kwamba tusipokuwa makini kuangalia vyanzo hivi tunaweza kupata shida katika kutekeleza majukumu yaliyopangwa kwa TARURA. Hivyo, vyanzo tuvilinde na tutafute vyanzo vipya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tupongeze na kutoa hongera kwa Samia Infrastructure Bond ambayo imekuja kwa ajili ya kusaidia wakandarasi ili waweze kupata mitaji mikubwa. Shida kubwa ya hawa wakandarasi siyo mitaji. Shida kubwa ni cashflow, kwamba wanapofanya kazi, wanatakiwa walipwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii Samia Infrastructure Bond ukiiongeza ili vilevile ishughulikie na kulipa wakandarasi, itakuwa na manufaa makubwa zaidi kuliko kuwapatia mitaji tu. Shida kubwa zaidi ni kwamba wakishafanya kazi wanakuwa hawajalipwa. Kwa hiyo, hizi bonds kama zitatumika katika kuwalipa itakuwa imeleta tija kubwa sana katika kwenda kwenye hiyo miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo nilikuwa nataka nilizungumzie katika hiyo ni ubunifu. Fedha za ujenzi hazitoshi katika miundombinu hiyo, kwa hiyo, inatakiwa kuwe na ubunifu mkubwa sana katika kupunguza gharama. Kwenye level ya miradi tunasema ni value engineering. Kwa hiyo, hiyo ikikuzwa ikaenda hadi kwenye level ya mipango, utaona kwamba tunaweza tukafanya kazi kubwa zaidi kwa kutumia rasilimali chache tulizonazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia TARURA, imeshaanza na tunaipongeza, kwani imerudi kule nyuma kwenye kutumia teknolojia ya mawe. Tumeona imeanza kujenga madaraja ya mawe ili kupunguza gharama za ujenzi ili tuweze kupata miundombinu mingi zaidi kwa fedha iliyopo. Vilevile, tumeona, na ukiangalia ukurasa wa 29 wa bajeti ya Mheshimiwa Waziri inaonekana kwamba anatumia teknolojia mpya ya EcoRoads, Ecoenzyme na Polyster. Teknolojia hizi lengo lake ni kupunguza gharama za miradi. Hivyo, ubunifu huo tunaomba uendelee na wapate wafanyakazi wenye weledi wa kuweza kufanya hizo tafiti ili teknolojia hizi mpya ziweze kuwasidia katika kupunguza gharama kwenye miradi hiyo mbalimbali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. ENG. DKT. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)