Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026


MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nichangie hotuba ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambazo anaendelea kuzifanya katika Taifa letu. Kama ambavyo wenzangu wameshasema, hakika kuna miradi mingi sana iliyopatikana kwenye maeneo yetu. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi, tunapongeza kwa uimara wake kama ambavyo wenzangu wameshasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niungane nao kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi anazofanya katika nchi yetu. Leo wana Busega wamenituma nije nimshukuru sana kwa miradi mkubwa ya maendeleo, ambapo tumepata zaidi ya shilingi bilioni 67 katika miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan. Hakika haya ni mafanikio makubwa sana kwa wana Busega. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, mtani wangu, kaka yangu Mheshimiwa Mchengerwa kwa kazi kubwa anayoifanya. Hakika Wizara imepata mkunaji; na anafanya kazi nzuri pamoja na wasaidizi wake, Comred Dugange pamoja na dada yangu Zainabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tuwapongeze sana kwa kazi kubwa wanazozifanya katika Wizara yetu ya TAMISEMI. Pia kuna wasaidizi wao ambao ni Katibu Mkuu pamoja na timu yake. Tunawapongeza sana kwa kazi nzuri wanazozifanya kwenye hii Wizara yetu ya TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niungane na wengine ambao wamempongeza Mkurugenzi wa TARURA, kaka yangu Seff, na mimi nampongeza sana. Kwa kweli baba huyu amekuwa ni msikivu na anatusikiliza Waheshimiwa Wabunge. Hata ukienda kwake, hawezi kukukataa, atakwambia nipe muda nitafanyia kazi, na kweli anakuja kufanyia kazi. Hakika mtu huyu ni mtu sahihi, endeleeni kumshikilia ili alisaidie Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, nichukue nafasi hii kumpongeza sana kijana mwenzangu Mkuu wetu wa Mkoa wa Simiyu, kaka yangu Kenani Kihongosi, kwa kweli ni kijana ambaye ameendelea kuwa imara sana katika Mkoa wetu wa Simiyu, na ameendelea kuonesha vizuri kwamba mkuu huyu wa Mkoa ameamiwa akiwa kijana, kwamba kijana anaweza, na hata wengine wataendelea kuaminiwa kwa kuwa yeye ni moja ya sample ya vijana ambao wameaminiwa na wameweza kuhudumia Mkoa wetu wa Simiyu vizuri. Hakika amesimamia miradi mingi ya maendeleo katika Mkoa wetu wa Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nampongeza sana Mkuu wetu wa Wilaya, dada yangu Faiza Salim, hakika Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Mchengerwa ametuletea Mkuu wa Wilaya kwa wakati sahihi, na mtu sahihi. Hakika sisi kazi yetu ni kukaa hapa Bungeni, mambo ya usimamizi wa miradi ya maendeleo Mkuu wa Wilaya yupo kule Busega anafanya kazi vizuri. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri amwangalie kwa jicho la pili. Pale Busega bado tunaye na tunataka tutambe naye kwa kazi nzuri ambazo ameendelea kuzifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza Wakurugenzi, nimeona wamekuja kwa wingi hapa, wanaendelea kusimamia miradi yetu ya maendeleo, akiwemo na Mkurugenzi wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, nami nilete ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Rais aliwaahidi wana Lamadi stendi na soko, na ninaamini katika mpango wake ameviongelea. Kwanza nampongeza kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Rais angalau kuanza na fedha zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya miradi hii miwili. Sasa ametupa sisi tuchague. Sisi tunachagua kipaumbele cha kwanza kwenye miradi hii ya kimkakati, mradi wa stendi pale Lamadi kwa sababu hakuna kabisa stendi, na ni barabarani, watu wamekuwa wakigongwa na magari, wanakufa, wanapoteza maisha mahali pale. Sasa ni vizuri tukianza na stendi ili wananchi wetu waweze kuondokana na adha kubwa ambayo wanayo pale Lamadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza kwa sababu ameiweka kwenye mpango, nasi tunamshukuru sana, na tunamshukuru pia Mheshimiwa Rais. Watakapopata na fedha nyingine, basi tuangalie na hili soko ili tuweze kumaliza hii miradi ambayo ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, na stendi ambayo sasa inaenda kuanza katika mwaka wa fedha 2025/2026 kwa kuanza na hii shilingi bilioni moja ambayo nimeiona imewekwa kwenye mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Zainab kwa kuniletea memo ikionesha kabisa kwamba sasa Serikali na Wizara ya Fedha imetoa kibali kwa ajili ya stendi hii ya Lamadi. Wana-Lamadi tunawapongeza sana na wana-Lamadi wanasema wanatamba na Mheshimiwa Rais, wanaye na wanaendelea kumshikilia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, pale Lamadi tulileta andiko letu kwa ajili ya kituo cha afya. Ni imani yangu kwamba kwenye orodha ya vituo vya afya watatuletea fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya pale Kabita. Kata ya Kabita ina zaidi ya wananchi 36,000. Sasa ni muda muafaka wa kupatiwa kituo cha afya ili waweze kuwa na sehemu ambako wanapata matibabu kwa urahisi kuliko sasa ambapo wanakwenda kata nyingine, zaidi ya kilometa kumi, kwenda kutafuta matibabu. Tukiwapatia kituo cha afya litakuwa jambo la msingi na wananchi wa Kabita wataendelea kunufaika na suala zima la kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikiuzungumza hapa zaidi ya mara tatu nikimtania rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Dugange. Wakati akiwa RMO (Regional Medical Officer) kule Shimiyu; Mheshimiwa Mchengerwa kama ulikuwa hujui, huyu alikuwa Mganga Mkuu Mkoa wa Simiyu. Yeye mwenyewe kwa mwandiko wake alikipandisha hadhi Kituo cha Afya pale Lukungu Kata ya Lamadi. Akapandisha hadhi zahanati iliyokuwa pale Kiloleli na kuwa kituo cha afya, lakini bahati mbaya sana amepandisha kwa jina tu, lakini miundombinu haifanani na vituo vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine naendelea kumwomba, tuviangalie kwa mara ya pili, kwa sababu viliidhinishwa na Naibu Waziri mwenyewe; na kwa sababu yupo, basi aandike tu pale ili sasa tuweze kupata wodi mbalimbali ambazo zinahusika kwenye vituo vyetu vya afya, zikiwemo wodi za wazazi, akina mama, watoto, wodi ya wanaume na wodi nyingine ambazo zinatakiwa kuwa kwenye vituo vya afya. Hilo ni ombi langu sana. Kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Dugange hawezi kukwepa hapa, kwa sababu ni moja ya watu ambao walipandisha hadhi eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine la pili kwa Kata yetu ya Kabita, wametuletea ceiling ya ujenzi wa shule mpya shilingi milioni 584. Nawashukuru sana kwa ceiling hii kwa ajili ya bajeti ya mwaka 2025/2026.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Mheshimiwa Mchengerwa, kwenye Kata yetu hii ya Kabita tuna shule ambayo imeanzishwa na wananchi. Shule hii ina majengo machache. Sisi kama Wanabusega, kama Wanakabita, tunawasilisha andiko kwake, fedha hizi shilingi milioni 584 ziende zikaboreshe eneo hili ili shule hii ya Venance Mabeyo ambayo imepewa jina la CDF Mstaafu, iweze kupata miundombinu mingi na iweze kuhudumia wananchi ambao wako kwenye haya maeneo ya Kata yetu ya Kabita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kuhusu TARURA. Nawashukuru sana, jana yule mkandarasi ambaye alikuwa anadai shilingi milioni 133, yeye mwenyewe amenipigia simu kwamba amelipwa fedha zake, nami kwa mamlaka yangu ya kawaida nimemwambia kwamba siku mbili awe site, na tumekubaliana ndani ya siku mbili atakuwa site kwa ajili ya ujenzi wa daraja la wananchi wetu wa Kata yetu ya Rutubiga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nahukuru sana kwa ajili ya fedha hizi, shilingi milioni 133. Kwa kweli mkandarasi huyu atakapomaliza zoezi hili la ujenzi wa daraja, litakuwa mwarobaini wa Kata hii ya Rutubiga, hasa kwenda kwenye vijiji vya pale Rutubiga pamoja na Mwasamba. Daraja hili litaenda kuunganisha mawasiliano ya barabara. Pamoja na hapo, tutakapomaliza daraja hilo, tutatengeneza barabara ya kilometa 4.2, na wananchi wa kata yetu ya Rutubiga watafurahi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna barabara moja ambayo itabaki maeneo yale kutoka pale Rutubika kwenda pale Mwakiroba. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri ahakikishe kuwa barabara hii nayo inaingia kwenye mpango ili wananchi wa maeneo hayo nao wanufaike na barabara hii ambayo tayari daraja lake linakwenda kumalizwa kujengwa kwa fedha ambazo ametuletea na ambazo zimeidhinishwa na Mama Samia ambazo ni kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Busega.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna barabara nyingine za kimkakati. Barabara ya kutoka pale Ngasamo kwenda kule Kisesa nayo imeharibika sana kwa sababu ya mvua. Barabara hizi nazo zinatakiwa zitafutiwe fedha ya dharura ili tuweze kutengeneza kwa sababu zimeharibiwa sana na mvua. Barabara nyingine ni kutoka pale Ngasamo kwenda kule Sanga na yenyewe imeharibika. Hivyo, nayo itafutiwe fedha ya dharura ili wananchi wetu waweze kunufaika na barabara ambazo ni za kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. Nirudie maneno ambayo niliyasema katika bajeti iliyopita. Mama Samia tunaye na tunatamba naye. Hata maneno ya Biblia yako wazi. Ukisoma Ufunuo wa Yohana 3:11 iko wazi kabisa inasema, " Shika sana ulichonacho, adui asije akatwaa taji yako.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuendelea kumshikilia sana Mama Samia kwa sababu hata maandiko yameandika kwamba shika sana ulichonacho. Sisi Wanabusega tunamshikilia Mama Samia mpaka kieleweke. Tunaye na tunatamba naye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, naunga mkono hoja. (Makofi)