Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Morogoro Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hoja ya Wizara ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ambayo inaongozwa na mdogo wangu Mheshimiwa Mchengerwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kwanza kumpongeza Mwenyekiti wa Chama chetu cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa Tanzania. Vilevile, kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika Jimbo la Morogoro Kusini na Halmashauri ya Morogoro Vijijini. Zaidi ya shilingi bilioni 180 zimepelekwa katika Halmashauri yetu kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mchengerwa na wasaidizi wake; Naibu, Dada yangu Mheshimiwa Katimba, na Mheshimiwa Dkt. Festo, Katibu Mkuu na watendaji wote katika taasisi ambazo ziko chini ya Wizara hiyo; TARURA na nyingine zote, kwa kazi kubwa ambazo wanazifanya katika kumsaidia Mheshimiwa Rais, kutimiza maono yake. Maana ukiangalia tu Wizara hii inaitwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ni kwamba imebeba mambo makubwa katika ustawi wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utaanza kwenye upande wa TARURA. Nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika kuipatia TARURA fedha za kusaidia kuleta maendeleo ya barabara katika majimbo yetu. Nikikumbuka kwamba wakati Mheshimiwa Rais anaingia, na wakati mimi naingia katika Bunge hili la pili, Halmashauri ya Morogoro Vijijini ambayo ina majimbo mawili; la kwangu na la mdogo wangu Mheshimiwa Tale, tulikuwa tunapata shilingi milioni 880 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunavyozungumza, kila Jimbo tunapata shilingi bilioni mbili na point. Hii ni kielelezo tosha kwamba kuna kazi kubwa imefanywa na kuna mambo makubwa yamefanyika. Ukiangalia barabara za wakati ule zilizokuwa zinatengenezwa na za sasa hivi zilizotengenezwa ndani ya kipindi cha miaka minne, kuna kazi kubwa imefanyika. Ukiangalia kule Bungu, Kibungo Juu, Kasanga, Kolelo, Tawa, na Kibogwa kuna mambo makubwa yamefanyika na yanastahili kupongezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali, Halmashauri ya Morogoro Vijijini, katika kilometa za barabara tulizokuwa nazo ni 700 kwa majimbo mawili. Jimbo langu tupu lina kilometa 305. Hata hivyo, katika jimbo langu kuna kata 17, kata tisa ziko milimani. Tunashukuru kwa kiasi hiki cha fedha tulizopewa, lakini naomba Serikali iangalie ni jinsi gani tunaweza tukaongezewa fedha hasa kwa kata hizi za pembezoni (milimani) ili tuweze kujenga barabara na wananchi wetu wakafikika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukijaribu kuangalia barabara za milimani, zinahitaji kujengwa kwa zege na zinahitaji kujengwa kwa mawe kama tulivyofanya kwenye barabara ya Dakawa, kama tulivyofanya kwenye barabara ya kwenda Bwakila Juu, barabara ya kwenda Kibogwa na barabara ya kwenda Kibungu Juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, hebu tusaidieni kutuongezea bajeti. Katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini, tunahitaji bajeti ya karibia shilingi bilioni saba mpaka shilingi bilioni nane. Sasa hivi tunapata shilingi bilioni nne, hebu tusaidieni kutuongezea walau tufike hata shilingi bilioni saba, pengine tunaweza tukatatua changamoto za watu na kuweza kusaidia kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, niipongeze TARURA kwa kazi zinazoendelea. Pia, niendelee kumwomba ndugu yangu Seff, nilikwenda ofisini kwake kuomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Konde – Kiswila ambapo kule kuna kiwanda kikubwa cha karafuu ambacho tunategemea kujenga. Sasa, tuliomba fedha kiasi kama cha shilingi bilioni moja, tupate ili tuweze kutengeneza barabara hiyo ijengeke ili kiwanda kile walau kijengeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakuomba kupitia Bunge lako, TARURA waangalie jinsi gani wanaweza kutupatia fedha hizo ili zikafanye kazi hiyo na kutusaidia kuondokana na changamoto ambazo wananchi wetu wanazipata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa barabara, naomba hebu tujaribu kuangalia, kila mwaka tunatenga fedha za kujenga barabara kwa kiwango cha changarawe. Sasa kuna wengine wamesema lami, lakini kwetu sisi wa milimani tungeomba tuongezewa fedha na twende tukatengeneze barabara zetu kwa kiwango cha zege na mawe ambazo zitakuwa zinapitika mwaka mzima na vilevile, wananchi wetu watakuwa wanafaidika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo langu la pili ambalo ningependa kuzungumzia ni kwenye suala la afya. Nina kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye upande wa afya nchi nzima. Wakati tunaingia Bungeni, kwenye Bunge hili la pili, kwenye halmashauri yetu ya Morogorogo Vijijini tulikuwa hatuna Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya. Hata hivyo, hivi tunavyozungumza tumepelekewa zaidi ya bilioni ambayo imeweza kujenga Hospitali ya Wilaya, lakini wameweza kukamilisha jengo la utawala la hospitali, tumeweza kufikia mpaka kuweka vifaatiba kama X-Ray na mambo mengine. Vilevile, tumeweza kujenga zahanati tano mpya: Zahanati ya Kisemu, Zahanati ya Kisaki, na Zahanati ya Kasanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, katika zile zahanati nyingine ambazo tulikuwa tumeambiwa tunaweza tukapata, ombi langu kwa Serikali, mtusaidie kujenga zahanati katika kata za milimani ikiwemo Kata ya Singisa, Kata ya Bwakila Juu, na Kata ya Kolero ili tuweze kuwafikishia huduma wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri kata zote hizo tayari nimeshazipeleka kwenye Ofisi ya Mheshimiwa Mchengerwa. Ni imani yangu kuwa muda ukifika katika vile vituo vya afya ambavyo kila Mbunge atapewa, basi fedha ziende na wananchi wakapate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili napongeza kwenye suala la afya. Tumeweza kujenga zahanati mpya Mwambani, Ngong’olo, Gozo, Kiswila na Mgata, zahanati ambazo wananchi walijenga na TAMISEMI ilipeleka shilingi milioni 50 ambapo tumekamilisha bila tatizo na zinatoa huduma kwa wananchi wetu. Tuna kila sababu ya kumpongeza Mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, tuna changamoto kwenye suala la afya, kwa upande wa watumishi. Tumekamilisha majengo, lakini tunahitaji kuwa na watumishi. Tatizo kubwa tulilokuwanalo katika Halmashauri yetu ya Morogoro Vijijini, tuna changamoto ya Madaktari wa Usingizi na Madaktari wa Meno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna changamoto ya ukarabati wa vituo vya afya ambavyo viko kwenye Jimbo langu ambavyo ni Kituo cha Afya cha Tawa, Kituo cha Afya cha Dutumi, Kituo cha Afya cha Ngerengere kwenye jimbo la pacha wangu na Kituo cha Afya cha Mkuyuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna changamoto ya magari. Tunahitaji gari jipya la ambulance katika Hospitali ya Wilaya. Nashukuru na ninatoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa ambulance ambayo ametupatia, ambayo kwangu niliipeleka kwenye Kituo cha Afya cha Dutumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa elimu, tuna kila sababu ya kumpongeza Mama Samia Suluhu Hassan. Ndani ya kipindi kifupi amefanya mambo makubwa. Kubwa zaidi ambalo nataka niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge wenzangu, mama huyu toka ameingia, miaka ya nyuma kila ilipofika mwezi Desemba, Madiwani tulikuwa na hangaiko la kuwachangisha wananchi wetu kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, ambapo kulikuwepo na watoto wanaingia kwa first selection na second selection, lakini ndani ya kipindi cha Mama Samia, hakuna jambo hili. Watoto wote walikuwa wanaingia kwa wakati mmoja na hivyo hata ufaulu ulikuwa unaweza kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga shule mpya tano za sekondari. Tumejenga katika Kata ya Bungu, Kata ya Kisaki, Kata ya Kongwa ambayo ni ya ufundi, lakini Dutumi tumeongeza shule maalum ya akina mama. Dakawa tumeongeza shule nyingine kwa ajili ya kupunguza watoto kutembea umbali mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali, pamoja na mafanikio haya, bado kuna changamoto. Mimi ninakotoka ni katika Jimbo ambalo lina changamoto kwa sababu liko milimani. Kule milimani hatuwezi kuongeza shule nyingine za sekondari kwa sababu watoto ni wachache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kutoka kwenye Makao Makuu ya Kata kwenda kwenye vijiji ni mbali. Ombi langu kwa TAMISEMI, katika yale majengo ambayo mnataka kuyajenga kwa ajili ya mabweni, tunaomba mtupatie mabweni kwenye Shule ya Sekondari ya Kibogwa, Shule ya Sekondari Kibungo Juu, Shule ya Sekondari Bwakila Juu na Shule ya Sekondari ya Singisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo napenda kulizungumzia na ambalo niliombe kwako Mheshimiwa Mchengerwa, kuna maboma mengi ambayo wananchi wameyajenga na wangependa Serikali itie nguvu. Kuna maboma kwa ajili ya madarasa, nyumba za walimu na maboma kwa ajili ya zahanati. Ombi langu kwako, naomba zile fedha ambazo zimetengwa zije katika Jimbo la Morogoro Kusini na katika Halmashauri ya Morogoro, tukakamilishe kazi ya wananchi ili wakati ukifika tufanye kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nina ombi moja lingine. Kuna wataalamu wa sekta mbalimbali kwenye halmashauri zetu na kata zetu. Sasa hivi TAMISEMI tunapeleka fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya ujenzi, na tunawakabidhi madaktari na walimu ambao hawana utaalamu huo. Ombi langu ni kwamba tuangalie uwezekano wa kuajiri vijana waliosomea fani ya uhandisi wakasaidie kusimamia fedha hiyo na matokeo yake yakaonekane kuwa mazuri.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninaunga mkono hoja. Nataka kusema tu kwamba, miaka mitano kwa Mama Samia, haina mjadala. (Makofi)