Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Samweli Xaday Hhayuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hanang'

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye bajeti yetu ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia uzima, afya na hatimaye tumeweza kuwatumikia wananchi wetu kwa nguvu zote.

Mheshimiwa Mwenyeiti, vilevile, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pia, namshukuru Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Mchengerwa na Naibu Mawaziri ambao siku zote tumekuwa tukishirikiana nao; Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange, pamoja na ndugu yetu Mheshimiwa Katimba; watumishi wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI wakiongozwa na Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na watumishi wote. Vile vile kwenye ngazi zetu za mikoa tumekuwa tukishirikiana nao vizuri katika kusimamia miradi ambayo tunapata fedha kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa maana ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya dada yangu Almishi, tunashirikiana naye vizuri, Mkurugenzi, Theresia Irafay anasimamia miradi na anasimamia watumishi wake vizuri. Pia nawashukuru sana Waheshimiwa Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji ambao mara zote tumekuwa tukishirikiana nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha mwaka 2025, hii ni bajeti ya tano ambayo sisi tunapitisha kwenye Bunge hili la Kumi na Mbili. Shughuli nyingi zimefanyika na ndiyo maana nawashukuru wote wakiongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kazi aliyoifanya ni kazi ya kupigiwa mfano na tunasema kwa kazi hii aliyoifanya yote ambayo sisi tunapaswa kulipa Oktoba wakati wa kurudisha change, tutarudisha change ya kutosha. Wanahanang wanaahidi kwa yote ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameyafanya, sisi tunalo deni na deni hilo tutalilipa kwa nguvu zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu niseme machache. Kwenye sekta ya afya, sisi tulikuwa na hospitali ya wilaya ambayo imechoka sana. Kwa sasa tumepeleka zaidi ya shilingi bilioni 2.5 ambapo tumeboresha majengo yaliyopo, tumejenga majengo mapya ikiwemo jengo la emergence, maternity complex na tumeweka vifaatiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga vituo vya afya vipya vitano kwenye kipindi hicho kifupi, lakini tumekamilisha zahanati ambazo tumeombea fedha; Zahanati ya Gabadaw, Garawja, Gisiyal, Garbapi, pamoja na Dang’aida. Hizi tukizijenga tunafikisha zahanati 15 ndani ya muda huo mfupi. Maana yake ni kazi kubwa imefanyika kwenye sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo kwenye sekta ya elimu tumeboresha Shule ya Nangwa High School; Mulbadaw Secondary majengo yaliyopo pale ni ya kisasa sana. Vilevile, Katesh ambayo ni Makao Makuu ya Wilaya hatukuwa na high school, lakini kwa sasa imepandishwa hadhi tuna high school. Ukizichanganya pamoja tuna high school nne na tunatarajia nyingine mbili zipande hadhi, baada ya hapo tutakuwa na high school sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajengewa VETA pale Nangwa, lakini tumejenga shule za sekondari mpya. Tukikamilisha shule inayojengwa Dawar, Jorodom na baada ya kujenga Shule Gendabi, ndani ya muda huo tutakuwa tumejenga jumla ya shule sita za sekondari. Vilevile, tumeboresha shule za msingi kwa maana ya kuongeza madarasa, shule mpya pamoja na kukarabati shule. Hii ni kazi kubwa ndani ya muda huo mfupi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Mji wa Katesh ambao ndiyo makao makuu ya wilaya, pale tunakamilisha ujenzi wa stendi mpya ya kisasa. Kanda nzima ya Kaskazini huwezi kuona stendi nzuri kama hiyo. Stendi ile pale Katesh Mjini imepewa jina la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Vilevile, tumeomba fedha kwa ajili ya kujenga jengo jipya la Halmashauri. Tumeidhinishiwa fedha za awali, tunachoomba tu ni fedha hizo zitolewe kwa wakati, ujenzi ule uanze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ukienda Katesh Mjini hatukuwa na kilometa hata moja ya lami inayoingia pembeni. Kwa sasa tumejenga zaidi ya kilometa 4.5 ndani ya muda huo mfupi. Pamoja na kwamba tuliomba kilometa 10, unaona kazi ikiendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa barabara tumefungua barabara mpya zaidi ya 10 kwa kipindi kifupi. Nitaje barabara chache ambazo kwa kweli kwa Wanahanang ilikuwa ni kilio kikubwa. Tuna barabara inayoanzia Waama, inakwenda Diloda inatokea Mureru, wananchi wale walikuwa wanapata shida sana wakitaka huduma za afya, wakitaka kusafirisha mazao yao changamoto ilikuwa kubwa kwa sababu ya barabara hii lakini sasa barabara hiyo imefunguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna barabara ya Masakta – Lambo – Ng’alda kwenda Masqaroda, wananchi wanafurahia huduma ya barabara kwenye eneo hilo. Hata hivyo, tuna Kata ya Mulbadaw na Kata Bassodesh, kabla mvua ilikuwa ikinyesha Kata ya Bassodesh inakuwa kama kisiwa, kwa sasa tumeunganisha na barabara. Barabara hizo zimeendelezwa na kuhudumiwa nazo ziko kwenye hali ambayo inaridhisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio haya kwenye eneo la barabara, tunayo changamoto kidogo ambayo Mheshimiwa Waziri Mchengerwa, yeye anaifahamu. Nimemwandikia barua mwenyewe kwa mkono wangu, nimempelekea ofisini kwake, tumekaa na kujadiliana. Tuliomba fedha kwa ajili ya kukarabati zile barabara ambazo ziliathirika na maporomoko ya Mlima Hanang. Barabara hizo ni Barabara ya Endasak– Dawar, Barabara ya Mogitu – Gendabi, Barabara ya Jorodom – Nangwa, Barabara Nangwa – Gitting, Barabara za Mji wa Katesh, Barabara ya kutoka Katesh – Dumbeta – Mureru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliomba fedha za barabara hizo na Mheshimiwa Waziri ulivyochakata akasema, basi tutawaidhinishia shilingi bilioni 4.7. Mpaka sasa hizo fedha tunazisubiri. Tunachoomba sisi Wanahanang, atuharakishie ili hatimaye tuweze kurekebisha hizo barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ambazo ziliharibika na mvua iliyonyesha kwenye msimu wa 2023/2024 na 2024/2025, kwa kweli tuliomba fedha za dharura. Barabara ya Mogitu – Balang’dalalu, tuliomba shilingi milioni 800; na Barabara ya Endagaw – Gidahababieg, tuliomba kama shilingi milioni 600. Barabara hizo kwa sasa hazipitiki kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huu ni wakati wa mavuno. Tunachoomba, zile fedha za dharura tulizoomba ukijumlisha kwa pamoja zinakuwa kama shilingi bilioni tisa hivi. Kwa sababu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameleta ubunifu wa kisasa wa bond ambazo mlitarajia kukusanya za shilingi bilioni 150, mmepata zaidi ya shilingi bilioni 350, hizo fedha zije ziwasaidie wananchi na kukarabati hizo barabara na hatimaye tupate raha ya kutumia Mji wetu wa Katesh na maeneo yale ambayo maporomoko yaliathiri barabara zake ziweze kutengenezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna changamoto kwenye upande wa sekta ya afya. Tumejenga, lakini tunazo kata kubwa kwa mfano Kata ya Gitting ambayo ina watu zaidi ya 17,000, inahitaji kujengewa kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija Kata ya Gendabi, pale kuna Kituo cha afya cha private. Wananchi wamelalamikia kwa muda mrefu kuhusu suala la gharama kubwa kwenye eneo hilo. Vilevile, ukija kwenye eneo la Balang’dalalu, hiyo ni kata kubwa kweli kweli na ina watu zaidi ya 19,000, na ni Makao Makuu ya Tarafa ya Balang’dalalu. Tunaomba kwenye eneo hilo tujengewe kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Hidet ambalo kwa kweli jiografia yake kwenda kwenye Makao Makuu ya Tarafa ya Simbay ni ngumu sana. Wakati tunafikiria kuendelea kujenga barabara, kabla ya hapo tujengewe kituo cha afya kwenye eneo la Kata ya Hidet.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha, kazi kubwa imefanyika. Namshukuru sana Chief wa TARURA, mara zote tukienda kwake amekuwa akitusaidia. Barabara tulizoomba za mwaka 2024/2025, barabara ziliidhinishwa kwa 60% tu zitangazwe. Nina barabara yangu moja muhimu ya kuunganisha Makao Makuu ya Tarafa na Kata ya Gehandu, barabara inayotoka Balang’da – Gidabwanja inakwenda Gehandu, barabara hiyo ilikuwa haijawekewa fedha. Nimekwenda nimeomba, na akawa ameahidi kwamba atatafuta fedha na nimepata taarifa kuwa zimepitishwa shilingi milioni 200 kwa ajili ya kujenga barabara hiyo. Naomba hizo fedha zipatikane kwa wakati ili ujenzi huo uanze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, nasema Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi ambayo amefanya, nimesema sisi tuna deni naye na Wanahanang kwa yale mazuri aliyotufanyia wakati ule wa maafa. Wanahanang wameniambia, nenda ukamshukuru na sisi tutamshukuru vizuri zaidi Oktoba na wakati ule atakapotutembelea kudai change yake ambayo kwa kweli change sisi tunayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja.