Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026


MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii niliyoipata kwa ajili ya kuchangia bajeti hii kubwa kabisa ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa miradi mingi sana ambayo sitaitaja hapa ambayo imekuja Moshi Mjini. Ninachoweza kusema tu ni kwamba Mheshimiwa Rais kwa Moshi Mjini sisi hatumdai. Hata kwenye bajeti hii ninachoomba ni ile ya kujazia juu ya keki wanasema icing, lakini ambavyo vimeshakuja kule vinatosha kabisa kufanyia kazi na Mungu ambariki ampe afya ili tufikie Oktoba na tuweze kumu-endorse kwa kura nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Mawaziri na Watendaji wote. Napenda tu kusema, wengi wametaja timu nyingi nyingi lakini hiyo timu yao hapo ninavyoiona ni kama timu ya Barcelona vipindi viwili tofauti: kipindi alipokuwepo Messi, Neymar na Suarez na kipindi hiki ambacho yupo Lamine Yamal, Raphinha na Lewandowski. Kwa hiyo, nawapongeza sana, Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri wote wawili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa ushauri. Kule tulikotoka kwenye upungufu wa watumishi hasa kwenye kada mbalimbali, nina maoni hapa ambayo najua yanaweza yakasaidia. Upungufu wa watumishi kwa mfano nichukulie kada ya Watendaji wa Mtaa na wa Kata. Jambo la kwanza ambalo naliona, kwa sababu nilishawahi kufanya nao kikao, ni suala la mshahara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu mwenye Diploma ambaye ameajiriwa kama Mtendaji wa Mtaa mshahara wake ni karibu nusu ya mtu mwenye Diploma aliyeajiriwa kwenye kada nyingine kwa mfano pale uvuvi. Walinipa mfano unakuta mtu anaanza na shilingi 480,000/=, kule mtu anaanza na shilingi 700,000/= mpaka shilingi 900,000/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini sasa kunakuwa na upungufu kila mara kwetu, katika kada zote TAMISEMI? Kwa sababu mishahara iko chini, watu wanaomba kule hata kama ana vyeti vingi. Unakuta ana Masters, lakini anaomba kwa kutumia hiki cha Diploma ili aingie apate check number; akishaingia pale anapambana kutafuta maeneo mengine ya kuhamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wenzetu wa utumishi wakiweza kufanya msawazo kwamba mishahara ya kuanzia kama ni Diploma Serikalini waanzie kiasi labda ni hiki kwa wote. Hilo kwanza, litaanza kupunguza upungufu kule kwenye maeneo yetu hasa TAMISEMI. Kwa mfano Watendaji wa Mitaa na Watendaji wa Kata walikuwa na maombi specific.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huku nimeona mmeongelea masuala ya nyumba zao, wao wamesema angalau pikipiki kama usafiri wa kuwasaidia kuzunguka kwenye ile mitaa, vijiji na kata kama walivyofanyiwa wale wa Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nimeona linaweza kusaidia ni kuona namna ambavyo baada ya muda wale walioanzia kwenye kada hiyo wanapata promotion ikiwemo pamoja na teuzi mbalimbali. Kwa hiyo, yule mtu anaweza akaamua abaki, lakini asubiri kwamba kuna neema hapo juu lakini anapobaki halafu haoni kuna neema, wanakuwa wanaendelea kuomba maeneo mengine na unajua siku hizi watu wanajisomesha, akipata eneo lingine anaondoka. Kwa hiyo, kule tunaendelea kubaki na upungufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo nilikuwa ninafikiria hasa yale maeneo ya kijijini ambayo watu wamekuwa wakihama sana, tulikutana nalo kwenye Kamati ya LAAC, tulitoa ushauri, sasa hivi Tanzania nzima ina wasomi. Yale maeneo yenye shida sana, watu wanahama sana, kwa sababu huko nyuma kidogo tuangalie namna ya kuajiri wenyeji wa kule kwa sababu sasa hivi watu wenye Diploma na Degree sasa hivi Tanzania nzima wapo. Inaweza kupunguza ile morali ya kutaka kutoka hapo kwenda sehemu nyingine kwa sababu ameajiriwa eneo la nyumbani na cost yake ya maisha inaweza ikawa ni ndogo. Kwa hiyo, nimeona kwa watumishi nianze na hilo, linaweza likatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Waziri, sisi tuna hospitali ya wilaya, namshukuru sana Mheshimiwa Rais Mama Samia. Pia, naishukuru Wizara wanaendelea kutupatia fedha. Tofauti yetu na maeneo mengine yote Tanzania, hospitali yetu ya wilaya hatukuwa na eneo. Tumelijenga eneo la ekari sita, kwa hiyo, tumejenga kwa ghorofa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipatiwa portion ile ile kwa mwaka, kazi ambayo unakuta tumeifanya kwa fedha ambayo wenzetu watakuwa wameenda mbali, sisi inakuwa kazi ndogo. Kwa hiyo, tunaomba ile lumpsum ya kuja kwa kila mwaka watuongozee au ikiwezekana watuhamishie kabisa Hazina tulipwe kwa certificate, itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, tumeshakwenda Wizarani pale, mimi Mstahiki Meya, Mkurugenzi, Afisa Mipango wetu, tukakutana na Cheyo. Nilishawahi kumfuata yeye binafsi zaidi ya mara moja na Naibu Waziri kuhusu Stendi ya Nganga Mfumuni wale CRJE imekwama kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale CRJE wana kazi nyingine maeneo mengine. Mkiwapa commitment na kwa sababu Wizara ya Fedha imeshakubali kulipa, watarudi site. Lile ni eneo letu la muhimu, Serikali imeshaingiza shilingi bilioni saba na ni chanzo cha mapato. Tunaomba sana mliangalie ili tuweze kuli-jump start limalizike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine, kipindi ambacho tuliunguliwa na Soko la Mbuyuni, nilimfuata Waziri tukiwa hapa kwa sababu liliungua tukiwa hapa, nikamwomba atusaidie fedha kwa ajili ya kwenda kulijenga upya lile soko na akaniahidi kwamba atanipatia, lakini tuliporudi kule, Mkurugenzi, Mstahiki Meya pamoja na Madiwani tukajibana tukatafuta fedha pale tukalijenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu tulilijenga kwa fedha zile za ndani, ile fedha iliyokuwa atupatie namwomba sana atusaidie iende kwenye Soko la Manyema ambalo lilikuwa ni ahadi ya viongozi wawili wakubwa. Alikuja Mheshimiwa Chongolo wakamlilia akasema atakuja kuomba na ameshaleta hayo maombi na alipokuja Dkt. Nchimbi pale Moshi pia walimwomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huyu Mheshimiwa Dkt. Nchimbi ni Makamu wa Rais ajaye, na ni Mgombea Mwenza. Sasa ahadi yake isipotekelezwa inaweza ikatuletea ugumu kidogo. Haitatuzuia kwa chochote, lakini kama ile fedha ambayo ilikuwa tupatiwe kwa ajili ya soko la Mbuyuni tutapatiwa, itatusaidia sana pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, option ya pili ambayo naweza kuomba, kama bado hamjapata fedha, mtupe commitment ya fedha kwa sababu ilikuwa ni karibu shilingi milioni 600, kwamba mtaleta pale ili fedha ambayo itajenga vibanda Mbuyuni, tukae na halmashauri tuibadilishe iende ijenge Manyema. Hiyo fedha ambayo anatupatia ije kwenye vibanda kwa sababu pale Manyema tutakuwa tumefanya kazi kubwa zaidi kwa sababu wafanyabiashara pale ni kama 1,400.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukijenga vibanda 50 kwa shilingi milioni 500 tunaenda kuweka wafanyabiashara 50 tu pamoja na kwamba ni chanzo cha mapato. Kwa hiyo, hizo option mbili mojawapo akiweza kuifanya, atakuwa ametusaidia sana na soko letu la Manyema litakuwa linafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi niliuliza swali kuhusiana na Barabara ya YMCA – KCMC. Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye maadhimisho ya miaka 51 ya Hospitali ya KCMC aliombwa barabara mbili na alikubali zote na barabara moja ilikuwa imeshakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka YMCA kwenda KCMC ilikuwa imetengewa fedha, yalipotokea mafuriko ya El-Nino ikaondolewa. Barabara ile hatuwezi kuijenga kwa mapato ya ndani kwa sababu inajengwa kwa double road na itahitaji fedha nyingi. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba sana kama inawezekana kwa sababu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, basi tutafutiwe ile fedha ili tuijenge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema ni muhimu kwa sababu gani? Kwa sasa hivi barabara ya Moshi – Arusha inajengwa kwa double road, barabara ya kuingia mjini kuanzia YMCA kwenda roundabout ya NBC inajengwa kwa double road. Kwa hiyo, kinakuwa kimebaki kipande hicho cha YMCA – KCMC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ile ni muhimu kwa sababu ina taasisi zaidi ya 10. Ina CCP, Chuo cha Ushirika, Chuo cha Mwenge, Uru Seminary, Old Moshi Secondary, Hospitali ya Kibosho, Kibosho Girls, Mweka Wild Life College na kadhalika. Ni barabara ya muhimu sana kwetu sisi Moshi Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo wenzangu wengi wameshalitaja ni vile vituo vya afya. Nilikuwa naomba sana, vile vituo vya afya vya kimkakati Moshi Mjini niliomba kwa ajili Kiborloni. Nimeshawaambia na wanasubiri, na Kiborloni ni eneo lenye watu wengi. Naomba sana Mheshimiwa Waziri afanye hima ili tuipate ile, Kituo cha Afya kiende Kiborloni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa vile vituo vya afya vya mapato ya ndani, naomba mtusaidie vikamilike kwa haraka kwa sababu sisi tulienda kujenga kule kwenye Kata ya Msaranga pale Mandaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la muda mrefu na nimeona kwenye ukurasa wa 119 kuhusiana na majiji. Nilishaleta maombi haya mara nyingi na bahati nzuri wakati wa mchakato wa Moshi Mjini kupanua mipaka yake au kuwa jiji, nilikuwa Diwani na nilishiriki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimtumia Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri GN number 219 ya tarehe 25 mwezi wa Sita mwaka 2016 ambayo ilisainiwa na Mheshimiwa Lukuvi. Kwa hiyo, sisi tulikuwa tumeshamaliza hatua zote. Hatua ile ilisimamishwa hivyo, tunaomba sasa turejeshewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoomba hili, Moshi Mjini hatuombi kwa ajili ya prestige. Makaburi yamejaa, hatuna mahali pa kuweka makaburi mengine. Madampo yamejaa, tumeenda kununua Moshi vijijini zaidi ya kilometa 16, hatuna maeneo ya uwekezaji. Tuna uhitaji huo sana. Mheshimiwa Mchengerwa naomba sana hili la Moshi kuwa Jiji na kupanua kwenye ile mipaka ambayo tumeshamaliza hatua zote, utupe baraka tulikamilishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa ni kuhusiana na ushauri kwa TARURA. TARURA imekuwa very efficient, lakini kuna eneo moja lina changamoto ambalo ni eneo la ku-repair. Sasa unakuta wanatoa tender ya repair labda kipindi cha mwanzo wa mwaka. Mtu anachukua tender baadaye unakuta kuna repair ndogo ndogo hawawezi ku-repair kwa sababu wanahitaji mpaka watoe tender.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tutafute mechanism aidha ya kuwa na mtu ambaye atakuwa ni responsible mwaka mzima au TARURA wawezeshwe kwa vifaa vidogo vidogo ili waweze kufanya hizo repair wenyewe.

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na ninaunga mkono hoja.