Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, niungane na wenzangu kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nampongeza pia Mheshimiwa Waziri na timu yake. Nina imani kwa uadilifu na uchapaji kazi wake, sina mashaka kwenye Wizara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mkuu wangu wa Mkoa Mheshimiwa Halima Dendego kwa usimamizi mzuri wa miradi yetu yote ya maendeleo na tuwakaribishe Mei Mosi inafanyika Singida Kitaifa. Tutakuwa na Kuku Festival siku moja kabla. Kwa hiyo, tunawakaribisha sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Singida Mjini wamenituma nije nimshukuru Mheshimiwa Rais kwenye jukwaa hili ambalo kwa miaka yote minne nimekuwa nikiomba fedha za miradi. Sasa nitumie jukwaa hili kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sasa kabla sijaeleza hayo, naomba nifanye rejea kwenye vitabu vyetu viwili vitukufu. Nikianza na Quran, inasema, “Kiongozi mzuri ni yule anayewa-inspire watu wake kwa matendo mema.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kwenye Bibilia ukirejea hadithi ya Yohana Mbatizaji akiwa gerezani alipotembelewa na wafuasi wake, naye aliamini kwamba, kwa kuwa yuko gerezani na Yesu anaweza kila kitu, angeweza kutoka kwa miujiza, akawatuma, “Nendeni mkamwulize yeye ndiye au tumsubiri ajae?” Bwana Yesu akawaambia, “Nendeni mkamwambie wafu wanafufuka, viwete wanatembea na vipofu wanaona,” na akamalizia, “Heri yule asiyechukizwa nami.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini katika rejea hii? Ni kwamba, kiongozi anapimwa kwa matendo na siyo maneno. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi ya vitendo ambayo ameifanya na sisi Wanasingida Mjini tunafaidika nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Singida Mjini tumepokea fedha za miradi zaidi ya shilingi bilioni 182. Ni fedha nyingi sana. Hatukuwa na Hospitali ya Wilaya, leo tunayo. Tumebakisha tu jengo la OPD. Kwa heshima ya Mheshimiwa Rais Mheshimiwa Waziri tuletee fedha tutengeneze jengo letu la OPD. Tulikuwa na kituo cha afya kimoja, leo tunavyo vinne. Katika elimu tulikuwa na shule moja ya sekondari, Mwenge Sekondari ya Advanced Level. Leo tutakuwa na shule sita za Kidato cha Tano na Sita, hii haijawahi kutokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, leo tumejenga shule nne mpya za O’Level ambapo ilikuwa ni maajabu sana kujenga shule hizi. Jambo kubwa zaidi, tuna shule ya amali, Shule ya Sekondari ya Ufundi. Zimeletwa shilingi 1,600,000,000 katika Mkoa wa Singida. Lazima tumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miradi hiyo ambayo ametuletea Singida Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo nataka nishauri ni eneo la elimu, na nitafanya rejea ambayo Mheshimiwa Waziri amekuja nayo. Kwanza, amesema elimu yetu ni uhai wa Taifa letu. Hii ni according to Mheshimiwa Mchengerwa. Ni jambo jema sana. Pia, amekuja na rejea nyingine, “Education is the most powerful weapon which you can use to change the world.” Hii imetokana na Nelson Mandela. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukirejea hizi quotation kubwa mbili maana yake unauona umuhimu wa elimu kwenye Taifa lolote duniani. Sasa nataka kusema nini? Elimu peke yake tumeshatengeneza miundombinu ya kutosha. Hatuna deni kwenye jambo hili. Tayari tuna shule, madarasa na kila kitu. Changamoto tuliyobakinayo ni ajira kwa walimu na hapa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ametuambia vizuri, Serikali imeajiri walimu 45,803. Hili ni jambo jema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, mahitaji ya walimu mpaka sasa tunavyozungumza hayapungui 200,000, walimu wanaotakiwa kuwepo. Kama tunahitaji walimu 200,000 mpaka leo maana yake tuna-deficit ya walimu 200,000. Kwa hili, bado tuna kazi kubwa. Ni lazima Serikali ije na mkakati wa kuona namna ya ku-accommodate haya mahitaji ya walimu na wanafunzi wetu ama shule zetu ziweze kupata walimu wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kushauri nini hapa? Nataka niishauri Serikali vizuri sana kwamba, sasa hivi kwa walimu hawa tulionaonao, vyuo bado vinaendelea kuzalisha na kuleta walimu. Bado tutakuwa na gap kubwa sana. Wakati inaendelea na utaratibu wake wa kuajiri, inaweza kutoa maelekezo, mwongozo au waraka kwenye halmashauri zetu, wakatoa ajira ya muda kwa walimu ambao wanahitaji kufanya hii kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoa ajira ya muda kwa walimu hawa, utakuwa umepunguza hili gap ambalo tunalo na watoto wetu wanaweza kufundishwa kwa kile ambacho wanastahili. Tutatoa wanafunzi wazuri kuliko ambavyo sasa hivi tunasubiri ajira ambayo tunaitoa kidogo kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza education ni powerful weapon ambayo inaweza kubadilisha dunia kuipeleka kwenye mwelekeo mzuri na chanya, tukiacha hivi maana yake hii silaha inaweza kuwa bomu la nyuklia ambapo baadaye litakuwa ni hatari zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuishauri Serikali itoe waraka. Waraka huu utafanya nini? Huku chini tuchukulie mathalan tu Manispaa ya Singida, sasa hivi kwa mwaka mzima tunakusanya kama shilingi bilioni sita. Katika shilingi bilioni sita, category yetu sasa hivi ni 60% fedha za maendeleo; tumetoka kwenye 40%. Maana yake kila mwezi tunakusanya shilingi milioni 500 na 60% yake ni shilingi milioni 300.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi tunahitaji 20% tu kwa sababu tayari miundombinu imejengwa ya kutosha, 40% inatosha unaweza kuajiri walimu wa muda 200 ambao wanahitaji shilingi milioni 40. Wewe tayari kwa mwezi unapata shilingi milioni 60. Jambo hili litakuwa limetusaidia na hapa nimechukua category ya Manispaa. Sijagusa majiji mengine ambayo inawezekana kufanya zaidi ya hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nimwombe Mheshimiwa Waziri, wala hapa hahitaji kutumia nguvu. Sisi tayari tumeshajenga shule. Mheshimiwa Rais kajenga shule, kajenga madarasa na yote yana madawati, hivyo kashamaliza kazi yake. Siyo tu madawati, watoto leo wanasoma kwenye tiles. Maana yake kila kitu kiko vizuri. Tunahitaji walimu, na hao walimu wapo wala hatuendi kuwatafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutoe tu mwongozo wa kuzitaka halmashauri zetu kuweka utaratibu wa kutenga fedha kwa ajili ya ajira ya muda ambapo pia inawezekana kwa mapato ya ndani. Hoja yangu nilikuwa nataka nisimamie hapo, na niwaombe sana tufike mahali tuone umuhimu wa kupunguza hili gap.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unapunguza kwenye eneo la walimu maana yake unaweza kupunguza pia kwenye eneo la afya na watumishi wengine ili kuweza kuleta ufanisi wa kazi kwenye maendeleo ambayo tunayatarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunalo soko moja kubwa sana Soko la Ipembe. Ndiyo tumebaki hapo. Mheshimiwa Waziri mimi nina jambo moja tu limebaki ambapo Soko hili la Ipembe nakumbuka mwaka 2024, Naibu Waziri kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Dugange alijibu swali akasema wakandarasi wataingia Desemba kwa ajili ya kuanza ujenzi wa soko hilo. Mpaka sasa hawajaingia, na sasa tumeingia kwenye bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, tumebakiza soko tu ili mji huu sasa, kesho tukuombe uwe jiji. Maana yake Soko hili la Ipembe lijengwe kuwa soko la kisasa. Tunahitaji fedha tu kwa ajili ya kujenga Soko hili la Ipembe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tumebakiza kituo kimoja cha afya ambacho tayari kuna kata kama nne zinaizunguka kata moja, na katika vile vituo vya afya vya kimkakati tuliweka Kituo cha Afya cha Kata ya Kisaki. Hapa tayari tuna Kata ya Mwankoko ambayo ina zahanati, Kata ya Unyanga ina zahanati pamoja na Kata ya Unyamikumbi ina zahanati. Hii ukijenga kituo cha afya ita-accommodate hizi kata nyingine nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na wananchi wangu tumeshafanya juhudi za kutosha. Tumeshajenga jengo la OPD na Serikali ilituletea shilingi milioni 50. Tumebaki kwenye suala la umaliziaji ili tuwe na kituo cha afya. Naiomba Serikali iweze kutusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)