Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ningane na Wabunge wenzangu kuunga mkono hoja ya kupitisha shilingi 1,16,894,958,000 kwa ajili ya kwenda kumwezesha na kuziwezesha kazi za Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta hii ya maji, ninaunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mapinduzi makubwa sana ndani ya miaka hii minne kwenye sekta hii ya maji. Sisi Handeni Mjini tunampongeza sana tunamshukuru sana, lakini nitumie nafasi hii pia kukushukuru Waziri Mheshimiwa Aweso kaka yetu na mdogo wetu, sisi wenzako Wabunge tunaotoka Mkoa wa Tanga tunajivunia kujitambulisha kwamba Mheshimiwa Waziri wa Maji anatoka Mkoa wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu yangu Mheshimiwa Engineer Kundo, hongera sana kwa uchapakazi wako mapema sana ulifika Bwawa la Kwenkambala, mapema sana, maelekezo uliyoyaacha pale kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri na kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, yametekelezeka na ninataka niwajulishe kwamba bwawa lile kwa sasa imekamilika, Bwawa la Kwenkamba. Ombi langu kwenye bwawa hili ni kwamba tumemaliza awamu hii ya kwanza ya kulijenga bwawa sasa twende awamu ya pili ya kutenegeneza treatment plant na baadaye tuyapandishe maji juu ya kilele cha Mlima Mhandeni kwenye tenki la ukombozi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mkubwa ambao Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameufanya Jimbo langu la Handeni Mjini ni Mradi wa Maji wa HTM, mradi wa kitaifa, mradi wa shilingi bilioni 171, mradi ambao toka mwaka 1974 hatukuwahi kuwa na mradi mkubwa kama huo isipokuwa Awamu hii ya Sita. Kupitia mradi huu tunayatoa maji Mto Ruvu – Korogwe tunayaleta mpaka juu ya kilele cha Mlima Mhandeni mahali ambapo tumejenga tenki kubwa. Mheshimiwa Rais ametuwezesha kujenga tenki kubwa pale, tenki ambalo yeye mwenyewe Mheshimiwa Rais amefika kwenye kilele cha mlima huo na kuiweka alama ya kumaliza matatizo ya maji kwenye Mji wa Handeni. Maji yatatiririka kutoka juu ya kilele cha Mlima Mhandeni kwenye tenki la Ukombozi mpaka Kata ya Kwa Magome yataanzia pale Hedi, Kwa Magome yatakwenda Kwa Magome – Lusanga, Lolopili – Sasioni mpaka Kolubaka kata yote ya Kwa Magome maji yatatiririka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka juu ya kilele cha Mlima Mhandeni kwenye tenki la Ukombozi ambalo Mheshimiwa Rais amelizindua maji yatakwenda mpaka Kata ya Malesi, yataanzia Malesi penyewe yatakwenda mpaka Masampata, yatakwenda Kulukole, yatakwenda kwa Madule na yatafika viunga vyote vya Kata ya Malesi toka juu ya kilele cha Mlima Mhandeni maji yatatiririka. Maji yatatiririka kutoka tenki la Ukombozi mpaka Kata ya Konje yataanzia Kiturwe yatakwenda Masalanka, Mankinda yatafika mpaka Komnazi maji yatatiririka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji yatatiririka mpaka Kata ya Kwenjugo kuanzia Wandama, Kwedigongo, Ngugwini, Kwediswa mpaka Bwila kata yote ya Kwenjugo itapata maji kutoka juu ya kilele cha Mlima Mhandeni kwenye tenki la Ukombozi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji yatatiririka mpaka Kata ya Msasa, yataanzania Msasa shule yatapita Mazundu, maji yatakwenda mpaka Kwedeseni, yatakwenda Visenenzi na mpaka Mnazi mmoja maji yatatiririka, kazi za Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, maji yatatiririka mpaka Kata ya Mlimani, yataanzia Kwa Baya yatafika kwa Sindi maji yatakwenda mpaka kwa Sahasani pale Anitakaye, maji yataririka kutoka juu ya kilele cha Mlima Mhandeni kwenye tenki ambalo Mheshimiwa Waziri unalifahamu vyema tenki maarufu tenki ambalo tumekubaliana kulipa hilo jina la Ukombozi kwa sababu Handeni Mjini tumekuwa kwenye dhiki kubwa ya maji kwa miaka mingi mpaka hapa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyokuja kutukomboa Wana-Handeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji yatatiririka kutoka juu ya kilele cha Mlima Mhandeni mpaka Kata ya Kideleko, yataanzia vilima vya Bangurandekai yatashuka Lumbizi, yatashuka Kideleko yenyewe, Kampene mpaka maeneo yote ya Kata hiyo ya Kideleko maji yatatiririka. Maji yatatiririka kwenye viunga ya Kata ya Vibaoni, Chanika na Mdoe pale mjini pote soko la zamani kote maji yatatiririka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)