Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Ally Mohamed Kassinge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilwa Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi, awali ya yote na mimi niungane na Wabunge wenzangu wote ambao wamemshukuru Mheshimiwa Rais na mimi kwa niaba ya Wana-Kilwa, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu ameweka alama kubwa kwenye sekta hii ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na changamoto ya mradi wa miji 28 kwa miaka kumi sasa, lakini mwaka huu Mheshimiwa Rais amesema mradi wa maji miji 28 Kilwa utekelezeke na Wana-Kilwa wapate maji, shilingi bilioni 44 tumepata sisi wana Kilwa kwa ajili ya mradi ule kutoka Mavuji kwa ajili ya Miji ya Kilwa Kivinje na Kilwa Masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza mradi huu umekamilika maeneo yote, treatment plant tayari, tegeo tayari, minara miwili imeshajengwa kilichobaki ni usambazaji wa mabomba tunaomba msukumo wa Wizara ili mkandarasi aweze kusambaza mabomba maji yapatikane Kilwa Kivinje, Kilwa Masoko, Singino, Nangurukuru pamoja na vijiji vyote vinavyopitiwa na mtandao huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishukuru kwa mradi wa maji Kilwa Kisiwani, zaidi ya shilingi bilioni 1.6 zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya mradi huu na umesuasua kwa muda mrefu. Mheshimiwa Waziri, tunashukuru sana Wizara yako kwa heshima ambayo umetupa, umeleta msukumo mradi huu unatekelezeka, kilichobaki sasa hivi tunahitaji shilingi milioni 377 kwa ajili ya kwenda kusimika nguzo kupitisha maji baharini na bomba baharini ili Wana-Kilwa Kisiwani wakapate maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tumenufaika na mradi ambao Wabunge wenzangu wote wamepata wa visima vitano vitano kila jimbo. Mimi nimepata katika Kijiji cha Makangaga, Rushungi, Kisongo, Mirumba pamoja na Mikoma. Ninavyozungumza ni kwamba Makangaga na Rushungi pamoja na Kisongo maji yameshapatikana, lakini Mirumba na Mikoma bado, tunaomba msukumo wa Wizara. Mheshimiwa Aweso, tunakusifia na tuna kuamini, hatukusifii kwa sababu tunapenda kukusifia, tunakusifia wewe na Engineer Kundo kwa sababu mnachapa kazi ambayo watanzania wanaiona. Tunaomba msukumo miradi hii ya visima vitano kila jimbo ikakamilike ili wananchi wetu wakapate maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na ule mradi wa mtambo wa maji katika mikoa yetu. Mimi katika Jimbo langu nilipata bahati ya kuchimbiwa baadhi ya visima katika vijiji kadhaa kikiwemo Kijiji cha Matandu, lakini maji hayajapatikana, Limaryao kule maji hayajapatikana. Mheshimiwa Aweso ninaamini kwa msukumo wako na nimeembiwa kwamba mtambo huu bado upo Kilwa, ninaomba mtambo huu usitoke Kilwa mpaka maji yapatikane katika vijiji nilivyovitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mradi wa kutoa maji Pande kupeleka Limaryao. Kata nzima ya Limaryao imekuwa na changamoto kubwa ya maji. Katika hili tulikuwa na commitment ya Shirika la Misaada la Kijerumani lakini tunaomba intervention ya Wizara katika hili ili tutoe maji Pande kupeleka Limaryao ambayo nimezungumza mara kadhaa hapa ni kata ambayo haijapata maji tangu izaliwe kwa maana ya maji yaliyo rasmi yanayopatikana katika utaratibu ule ambao umeratibiwa rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana Wizara pamoja na watendaji wake wote wa Wizara, ikiwa ni pamoja na Engineer Mwajuma, Katibu Mkuu wetu, lakini pia Meneja wangu wa RUWASA wa Mkoa, lakini pia Meneja wangu wa Wilaya, ninaomba waongezewe nguvu. Kuna changamoto kubwa ya usafiri pale wilayani Kilwa, gari inayotumika ni mbovu, imechakaa ya muda mrefu ina kilomita zaidi ya laki nne. Kupitia bajeti hii niombe Mheshimiwa Waziri aone umuhimu wa kuwasidia gari RUWASA Kilwa ili wakatekeleze miradi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho Wana-Kilwa tunaomba, ukatembelee miradi yetu hii, mradi wa miji 28 ukautembelee uone, mradi mkubwa wa kutoa maji Kilwa Masoko kupeleka Kilwa Kisiwani zaidi ya shilingi bilioni moja ukatembelee uone tunakualika sana na sisi tunasema tunakwenda na Mama Samia, naunga mkono hoja. (Makofi)