Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JANEJELLY J. NTANTE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi, nami nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa uweza. Niungane na wote waliokupongeza Waziri wa Maji Jumaa Aweso, libarikiwe tumbo lililo kuzaa na niwaombe Wana-Pangani wasifanye makosa, wakurejeshe na jicho la Mheshimiwa Rais likuone umalizie kazi uliyoianza, lakini nikupongeze Naibu Waziri, mimi huwa nakuita simba mwenda pole, lakini mkali kama pilipili wakichezea miradi ya maji, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Bi. Mwajuma ambaye ni mtaalamu mbobezi wa maji mtiifu na mnyenyekevu tofauti na kazi anazozisimamia, lakini mna Naibu Katibu Mkuu ambaye ndiyo mtaalamu wa uchambuzi wa sera, Bi. Agnes Meena, yawezekana ndiyo imesababisha hata sera ya maji sasa mmeibadilisha, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha anataka kumtua mwanamke ndoo kichwani, pale alipoamua kuongeza bajeti kutoka shilingi bilioni 680 hadi shilingi trilioni moja, si kazi ndogo na kwenye hiyo bajeti lipo Bwawa la Kidunda, Bwawa la Kidunda ni mwiba unaoenda kumaliza shida ya maji Pwani, Morogoro na Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimefanya kazi maji, nilianza kazi nikakuta Bwawa la Kidunda, leo niko Bungeni nimeongelea Bwawa la Kidunda nikiwa kwenye Kamati, lakini Mama Samia ameweza kuvunja kitendawili kile na kukitegua sasa Kidunda inaenda kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri hapa kwenye Kidunda, Kidunda kwa Morogoro itaenda kumaliza mgogoro wa wakulima na wafugaji kama mkishirikiana na Wizara ya Mifugo kwa kuweka sehemu za unyweshaji ili mifugo sasa ipate mahali pa kunywa maji iache kupita kwenye mashimba ya wakulima, lakini mkiwasiliana na uvuvi mkapanda vifaranga tunaenda kumaliza shortage ya Samaki, lakini kwa ukame wa Dar es Salaam na Mto Ruvu kukosa maji Kidunda inaweza kumaliza hilo tatizo, niwapongeze sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze kwa namna mlivyokiendeleza Chuo cha Maji kutoka kwenye udahili wa wanafunzi 2,320 hadi 4,260 sawasawa na 84% si jambo dogo, lakini mmeanzisha consultancy bureau ambayo mmeamua kuwakumbuka wastaafu, kwa hili nikupongeze na Wizara zingine igeni, kustaafu kwa miaka 60 siyo kwamba akili imezeeka, ng’ombe hazeeki maini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkiwatumia hawa wastaafu, Mheshimiwa Aweso upo kwenye kundi la maji huwa unaona utaalamu unaotiririka pale kutoka kwa wataalamu walio staafu wa maji yawezekana hapo ndipo ulipompata hata CEO. Sasa Bwire uliyokuwa unatiririsha pale ukayafanye DAWASA. Wapo wataalamu wamebobea nani kushukuru jana nimeona umealika hata wastaafu, ni kazi nzuri sana Wizara zingine igeni, hawa wastaafu tukiwatumia, nchi itafika mahali ambapo ni pazuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze kwa kujenga Mradi wa Banguro, mnaenda kumtua mwanamke ndoo kichwani, wanawake wa Pugu station, wanawake wa Gongo la Mboto, Kivule, Kata zote za Ukonga, lakini unapeleka maji mpaka Kibamba, hii ni kazi kubwa sana mmefanya na mmeamua kutumia shilingi bilioni 36.8 kuhudumia wananchi 250 siyo kazi ndogo na pesa zimetiririka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nishauri, siasa za Dar es Salaam ni maji, niombe muendelee kutumia visima vya Kisarawe II vikasambaze maji maeneo ya Kariakoo, maeneo ya Mbagala na maeneo mengine ambayo yana ya shida ya maji kwa sababu mwanamke wa Dar es Salaam hatuombi ruzuku ya mbolea, hatuombi ruzuku ya pembejeo, sisi tunachoomba ni maji. Siasa ya Dar es Salaam ni maji, kura za Dar es Salaam zinapatikana kutokana na maji. Niombe muangalie upatikanaji wa maji wa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmenunua vifaa vya maji taka, Dar es Salaam shida yetu ni maji taka, hebu DAWASA waongeze speed ya kutoa maji taka kwenye mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga hoja mkono, ahsante sana. (Makofi)