Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, na mimi nimshukuru Allah Subhanahu Wa Ta’ala kwa kutujalia uzima, uhai lakini halikadhalika, niwapongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake, lakini na timu nzima ya watendaji wa Wizara ya Maji ikiongozwa na Engineer Mwajuma, kwa kweli kwa utendaji wao uliyotukuka. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Maji nimeweza kuwa nao karibu na nimeona jinsi Mheshimiwa Waziri alivyotengeneza timu bora ya kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyozungumza Mwenyekiti wangu wa Kamati, kwa kweli kila mkoa unaokwenda unahisi kama kuna photocopy imechukuliwa halafu imekwenda kuwa-pasted sehemu fulani. Watendaji wanafanana nidhamu, wanafanana ubora na wanafanana uwezo. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri na timu yako hongera kwa kutengeneza ufanisi mzuri katika Wizara ya Maji na ndiyo maana hakuna mtu ambaye atashangaa kuyaona mafanikio haya ambayo wajumbe hapa wa Bunge hili Tukufu wameweza kuyazungumzia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, kwa kweli amechagua majembe, amechagua jembe Mheshimiwa Waziri, amechagua jembe Mheshimiwa Naibu Waziri, amechagua jembe Jemedari wetu Engineer Mwajuma, kwa kweli hii ni mihimili na Mwenyezi Mungu aiweke kwa sababu matumaini makubwa kwamba hawa ndiyo wataondosha changamoto ya maji kupitia Mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini halikadhalika Mheshimiwa Waziri unafanya kazi nzuri na una jicho kwa sababu kila unayemteua ana sadifu, kwa sababu nikiangalia juzi tu umechagua Mtendaji Mkuu wa RUWASA kwa kweli anafanya kazi nzuri, tumeshuhudia. Tumekwenda kule Manyara tumeona kazi yake nzuri aliyoifanya, sisi tulimuona, lakini nashangaa na wewe ukamuona ukamsogeza karibu afanye kazi kwa uzuri zaidi. Kwa hiyo, hongera sana na yeye tunamwombea heri azidi kuleta mabadiliko katika RUWASA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka minne katika Bunge lako hili Tukufu kwa kweli kipindi cha Mama Samia kimeshuhudia reforms nyingi za maji. Tumeona hapa, wenzangu wamezungumza, sera ya maji ambayo ilikuwa ina zaidi ya miaka kumi naa huko hivi sasa imebadilishwa imefanyiwa marekebisho na imeridhiwa na tuna toleo jipya la mwaka 2025, na lenyewe sera zaidi inaelekeza kwanza kuweza kuratibu vizuri, lakini vilevile kujumuisha taasisi mbalimbali na Wizara ziweze kufanya kazi kwa pamoja, pamoja na kuwajumuisha wenzetu wa private sectors ushiriki wao katika huduma za kuendeleza masuala ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetumia nafasi hii kuwaomba wadau wa maendeleo wakiwemo private sectors tusaidie Wizara ya Maji kwa sababu huku ni ucha Mungu, lakini halikadhalika ni kusaidia jitihada za nchi kuweza kuendeleza harakati za maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia pamoja na mafanikio makubwa ambayo yamekuja kwenye hii Wizara, mimi nina ushauri wa mambo mawili makubwa, haraka haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa kwanza, tunajua mama ameonesha utashi mkubwa kuongeza bajeti kutoka shilingi bilioni 680 hadi shilingi trilioni moja katika kipindi hiki cha mwaka huu wa fedha. Sasa fedha hizi kama tutakwenda kutumia zote kulipa madeni, tutabakiwa na fedha kidogo sana kuweza kuendeleza huduma za maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba sana tumuombe Waziri wa fedha afanye kila linalowezekana fedha za madeni zile shilingi bilioni 500 azitafute sehemu nyingine na hizi shilingi trilioni moja zikafanye kazi ya kwenda kuelekeza huduma za maji moja kwa moja ikiwemo miradi mipya kwa sababu kama tutatumia fedha hizi kwa viporo vya miradi basi fedha hizi hazitatosha kuendeleza miradi mipya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika nimpongeze Mheshimiwa Waziri ametengeneza huu Mfuko wa Maji katika hali nzuri zaidi hivi sasa na Mtendaji yule kijana Haji anafanya kazi vizuri. Sasa ningeomba tu Mheshimiwa Waziri wa Fedha akajitahidi fedha za makusanyo zinazopitia mfuko wa fedha yaani kwa huduma za maji zote zipelekwe kwenye Mfuko wa Maji bila kuwapatia asilimia fulani kwa sababu tukizi-portion kidogo basi tunapunguza ule umadhubuti wa kwenda kufanya kazi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna huu mchakato wa accreditation kwa ajili ya GCF. Mheshimiwa Waziri hongera umeanza mchakato huu, lakini ningeomba tu vijana wako ni mahiri huu kuuendeleza mwa haraka kwa sababu taasisi karibu tatu ambazo zipo TAMISEMI, Wizara ya Fedha pamoja na wenzetu wa NEMC wameshaanza huu mchakato, lakini sasa hivi ni mwaka wa kumi bado hatujafanikiwa kuweza kupata accreditation au usajili kwa ajili ya Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi wa GCF. Nategemea kwamba wewe utakuwa ni mdau wa kwanza katika Taasisi za Serikali ukiondosha Benki ya CRDB kuweza kwenda kuwa mdau wa GCF Insha’Allah. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)