Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nikushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia hoja iliyoko mbele yetu. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia uzima na afya njema na ameniwezesha kusimama hapa siku hii ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara namba moja wa kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani na hii imejihirisha kwa namna ambavyo amenunua mitambo 25 ya kuchimbia visima nchini kote na katika Mkoa wangu wa Singida. Mheshimiwa Rais tunakushukuru na tunakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitumie nafasi hii pia kumpongeza sana Waziri kaka yangu Mheshimiwa Aweso kwa kweli unafanya kazi nzuri sana wewe pamoja na Naibu Waziri kama yangu Engineer Kundo na timu nzima ya Wizara ya Maji mnafanya kazi nzuri sana, ninawapongezeni wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mimi leo hapa nasimama kutoa shukrani zangu nyingi kwa namna ambavyo tumepokea fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maji katika Mkoa wangu wa Singida. Katika mwaka huu wa fedha tumepokea shilingi bilioni 16 na miradi 43 imeweza kutekelezwa katika Mkoa wangu wa Singida. Kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amemtua ndoo Mwanamke wa Singida. Kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Singida ninasema ahsante sana na tunakushukuru Mheshimiwa Rais tuko pamoja na wewe bega kwa bega kuhakikisha kwamba ifikapo Oktoba, 2025 unapata kura zote za ndiyo katika Mkoa wangu wa Singida. Mheshimiwa Rais tunakushukuru na tunakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kushukuru kwa Mradi wa Maji Kintinku - Lusilile. Mradi huu wa maji ulikuwa ukisuasua kwa muda mrefu sana, lakini kwa sasa mradi huu umekamilika na Wananchi wa Wilaya ya Manyoni wanakunywa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wa Wilaya ya Manyoni wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuwatua ndoo kichwani kwa sababu ukanda wote wa miji ya Kintinku na Lusilile ulikuwa una changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama na maji yake ukichimba chini unakutana na chumvi, hayafai kwa matumizi ya binadamu lakini sasa mradi huo umekamilika, tunashukuru sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru miradi ya miji 28 ambapo katika Mkoa wangu wa Singida miradi hii inatekelezwa katika mji wa Kiomboi, Manyoni na Singida. Niombe sana mchakato wake uendelee kwa haraka kwa sababu miji hii ina uhaba mkubwa wa maji na imekuwa kwa kasi ukilinganisha na mahitaji yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishukuru sana kwa mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria. Mradi huu umeshafika katika Tarafa ya Shelui, Wilaya ya Iramba, lakini vipo vijiji ambavyo viliwekwa katika mpango na vijiji hivyo havina maji mpaka sasa hivi. Vijiji hivyo ni Mgongo, Mtoa, Mgela, Kibirigi, Mseko na Msai. Niombe sana kwa kuwa mchakato unaendelea na vijiji hivi viweze kupatiwa maji ya Ziwa Victoria, lakini kwa kuwa pia mradi huu wa maji wa Ziwa Victoria unapita katika Mkoa wangu wa Singida na usanifu unaendelea, niombe sana vijiji vyote, kata na wilaya maji haya yapite. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Katika Mkoa wangu wa Singida kuna changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa maji safi na salama na unategemea vyanzo vya visima. Sasa njia pekee ya kumkomboa mwanamke wa Mkoa wa Singida ni maji ya Ziwa Victoria na tumewaambia kwamba yatapita maji haya kwa kilometa 12 pale mradi unapopita. Kwa hiyo, niombe maji haya yapite katika maeneo yote ya Mkoa wa Singida kwani ndiyo mwarobaini pekee wa kuweza kumkomboa mwanamke wa Singida kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishukuru katika Wilaya yangu ya Mkalama tumepata maji katika Vijiji vya Malaja, Nkalakala, Mwangeza na Mbigigi, lakini pia yako maeneo katika Wilaya ya Mkalama ambayo yana changamoto kubwa sana ningeomba yaangaliwe kwa kina. Maeneo haya ni Mwangeza, Singa, Mpambala na Kijiji cha Nyahaa, lakini pia kwa Wilaya ya Ikungi pia tumepata maji ipo changamoto kubwa katika Wilaya yangu ya Ikungi, Mji wa Ikungi pale kuna changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa sababu mji huo tayari umeshakua. Niombe sana Mheshimiwa Waziri uangalie kwa kina jambo hili ili wananchi waweze kupata maji. (Makofi)