Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Tecla Mohamedi Ungele

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uzima, lakini nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa za kuwapatia Watanzania maji safi na salama. Tunaona miradi kote nchini inaendelea kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri Aweso na Naibu wake Engineer Kundo. Waziri Aweso huyu anatekeleza yale maono ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani. Ninampongeza sana, ni kijana mwenye juhudi kubwa muda wake mwingi anautumia kwa kazi hakika Mwenyezi Mungu ambariki sana. Pia nampongeza Katibu Mkuu wa Wizara hii ya Maji na watendaji wote wa Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza pia hata mameneja kwenye mikoa. Mkoa wa Lindi - Engineer Lubasa na Ma-engineer wake wale mameneja wa wilaya zote za Mkoa wa Lindi wanafanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi na usimamizi mkubwa wa miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mingi, lakini baadhi tu ya miradi mimi ni Mbunge wa Mkoa mzima wa Lindi, lakini nasema miradi mikubwa ya miji 28, mradi ule wa Mavuji kupeleka maji Nangurukuru, Masoko na Kivunje shilingi bilioni 44 umeshakuwa na tenki tayari pale Singino lakini bado sasa kusambaza mabomba tu kupeleka Kivinje na kule Nangurukuru na pia tenki lingine la kupeleka maji kule Masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna Mradi wa Nyangao kupeleka maji Ruangwa na vijiji 21 za Wilaya ya Nachingwea ni kazi kubwa inafanyika kwa Wizara hii. Mheshimiwa Waziri sisi Wana-Lindi tunakushukuruni sana kwa kazi yenu mnayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nashukuru kwa Wilaya ya Nachingwea kupeleka maji kule Kata ya Ngunichile. Wana-Ngunichile wameishi kwa maji ya kuokotaokota tangu misingi ya dunia hii iwekwe, lakini sasa hivi wanaenda kupata maji safi na salama. Tunawashukuruni sana Wizara, tunamshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan, haya mambo hatujawahi kuyaona ndiyo uongozi huu wa Dkt. Samia Suluhu Hassan lakini hata pia wa Mchinga wanapata maji safi na salama sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo kadhaa, tunaposhukuru namna hii Mheshimiwa Waziri, lakini pia tunavyoshukuru hatuachi kuomba tena. Kuna changamoto kubwa, naona ukurasa wa 29 wa hotuba yako Mheshimiwa Waziri umesema kwamba kuna uchunguzi unaendelea ufuatiliaji wa maji ya matumizi ya majumbani. Tumeona Mkoa wa Lindi na Mtwara kumeonekana maji yake yana madini ya chumvi, chuma na manganese. Sasa ndiyo maana sisi Wanalindi tunaomba ule mradi wa kutoa maji kutoka Rufiji kuleta Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rufiji siyo mbali kutoka Rufiji kuja Kilwa, halafu unakuja Lindi na ukitoka Mto Ruvuma unakuja pale Mangaka halafu unavuka tu unakuja Wilaya ya Nachingwea unaenda Wilaya ya Ruangwa. Kwa hiyo, maji yale yatakuwa maji salama lakini maji ya uhakika kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naamini kwa uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kama kwingine kunafanyika miradi mikubwa kutoa maji kwenye maziwa makuu kupeleka sehemu mbalimbali nchini Tanzania atashindwa kweli kutoka Rufiji kuleta hapo Lindi? Kutoka Ruvuma kuleta Lindi Nachingwea na Liwale? Nafikiri jambo hili kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni rahisi sana na ndiyo maana ameongeza bajeti ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna wale watendaji wetu wa Mkoa wa Lindi wana magari machakavu, hayawezi hata kwenda huko mbali tunakofikiria. Magari ni machakavu, Mheshimiwa Waziri mimi ninaomba utakapopata bajeti yako na kufanya mkakati wa kununua magari, basi naomba uwapelekee watendaji wetu wa Idara hii ya Maji kule Mkoa wa Lindi ili wafanye kazi ya ufuatiliaji na usimamizi wa miradi hii mizuri kwa wakati muafaka. Fikiri mtu yuko Kilwa – Masoko, Engineer Sultan yuko pale Kilwa Masoko anataka afuatilie mradi kule Kandawale zaidi ya kilometa 100, unafikiri anafikaje na gari chakavu namna ile. Hebu fikiria Engineer Musiba yupo pale Nachingwea anafuatilia mradi wa maji kule Kiegei au Kilimarondo zaidi ya kilometa 100 anafikaje na mle njiani kuna wanyama wale wakali, tembo. Ni hatari sana, chonde chonde tunaomba magari utakapo magari mapya basi naomba uwakumbuke maengineer wetu wa Mkoa wa Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipatia na nampongeza Mheshimiwa Rais, naunga mkono hoja. (Makofi)